TAFAKURI MSIBANI: “Shujaa” kaanguka ili aliyozika yafufuke

Takribani mwaka mmoja uliopita, tarehe 8 Aprili 2020, niliandika neno fupi katika mjadala wa group moja lenye watu wa itikadi mchanganyiko liitwalo “Kanda ya Kaskazini.” Mjadala ulihusu agizo la rais dhidi ya watoto wa kike wanaopata mimba wakiwa shuleni, na kelele za utetezi wa watoto hao zilizopigwa na wadau wa elimu, zikiwemo taasisi za kimataifa ambazo wenzetu walidai kuwa ni za “mabeberu.” Niliandika hivi:

Ishu yenyewe ni ndogo na iko hivi:

Hakuna mtu timamu anayependa mabinti wapate mimba wakiwa shuleni – in fact, hata wasipokuwa shuleni.

Lakini pia, huko nyuma, serikali imekuwa na utaratibu mbovu wa kushughulikia suala hili.

Wasichana wamekuwa wakifukuzwa shule (kama adhabu), huku wavulana au wanaume wanaohusika na mimba hizo wakiendelea na masomo au maisha ya kama kawaida.

Au hata pale wanaume walipofungwa, hatima ya mtoto huyu aliye tumboni haikuzingatiwa; kwamba atakuwa mtoto wa mzazi mmoja asiye na elimu wala kipato.

Wanaoelewa wanajua faida ya kuemilisha mtoto wa kike. Na ipo mifano mizuri tu ya baadhi ya watoto wa kike waliopata mimba wakiwa shuleni, wakapatiwa fursa (kwa utaratibu usio wa kisera), na wakawa watu wa maana sana katika jamii.

Kuelekea mwishoni mwa serikali ya awamu ya nne, serikali, baada ya kusikiliza hoja za wadau, ilitengeneza sera ya kutafuta ufumbuzi wenye nafuu kwa watoto na kwa jamii nzima.

Katika baadhi ya maeneo, sera ilitamka bayana kuwa “wasichana watapewa fursa ya pili,” ili wasikose elimu kwa sababu ya mimba; na wanaume wanaohusika nazo watapewa adhabu wanayostahili.

Ni sera ya serikali. Na ni sera nzuri tu kijumla.

JPM alipoingia madarakani, sera hiyo ikawa imekamilika. Waziri anayehusika na masuala ya afya na jinsia, Ummy Mwalimu, akatangazia taifa kuhusu sera hiyo na faida zake kwa umma katika muktadha wa haki ya mtoto kupata elimu.

Na Makamu wa Rais, Samia Suluhu, akatangaza tena katika tukio jingine, kama njia ya kuandaa umma kisaikolojia, na akazungumzia umuhimu wa sera hiyo katika kuboresha haki ya elimu kwa mtoto wa kike.

Samia na Ummy ni akina mama. Waliongea kama viongozi, wazazi na wasomi.

Miezi kama miwili baadaye, ghafla Rais JPM akafoka jukwaani (nadhani alikuwa Bagamoyo kwenye ziara ya kiserikali), akatangaza “msimamo wake binafsi” ambao unapinga sera ya serikali.

Kwa kufanya hivyo, kimsingi, JPM alifanya makosa mawili ya kiuongozi:

Kwanza, alikuwa anawafokea waziri wa afya na makamu wa rais. Hawa ni wasaidizi wake wa karibu ambao hahitaji kuwajibu kupitia majukwaa ya kisiasa. Kwa bahati mbaya, kuna mazuzu yalishangilia tamko la rais.

Pili, rais alipingana na sera ya serikali yake. Kwa wanaoelewa, hii ilionyesha kuwa ama haijui, au haikubali. Lakini, hata kama haikubali, hivi sivyo viongozi wafanyavyo.

Yeye alisema “katika kipindi changu cha urais, hakuna msichana aliyebeba mimba ambaye ataendelea na masomo. Siwezi kusomesha wazazi,” kana kwamba ni pesa yake, na kwamba ataishi milele; au kuna Tanzania mbili – yake na ya Watanzania!

Tangu hapo zimekuwepo jitihada kitaifa na kimataifa kumkumbusha kuwa nchi si yake, bali ni ya Watanzania; na kwamba suala hili lilijadiliwa mno na wadau wa elimu na haki za mtoto. Msimamo wa pamoja ndio msimamo wa kitaifa.

Hiki alichofanya JPM dhidi ya makamu wa rais, waziri, watoto wa kike na wananchi wanaotetea haki ya mtoto kupata elimu, ni kielelezo cha “ubeberu wa Magufuli.”

Vile vile, ni ushahidi kuwa serikali haiwasiliani ipasavyo. Ni ushahidi pia kuwa Rais JPM hajali misingi wala kanuni za uongozi, bali hisia zake. Ni kielelezo pia cha ujinga wake kuhusu mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.

Ndiyo maana “mabeberu” wa nje wanamsumbua. Amevunja sera yake mwenyewe, na mikataba iliyoridhiwa na taifa lake chini ya viongozi wastaarabu wanaojua dunia inaelekea wapi na umuhimu wa kuelimisha mtoto wa kike.

Kwa ubeberu wake, yeye anawaza kukomoa mtoto wa kike. Sikiliza hata toni yake. Ni ya kibeberu.

Mabeberu wa nje wanamsumbua beberu wa ndani kwa sababu principle inambana. Taifa linasema hivi kwa maandishi, naye (mtu wa kupita tu aliyelewa madaraka) anatamka kinyume na msimamo rasmi wa Taifa analoongoza.

Kwa lugha nyepesi, kuna ushamba fulani unatokea ofisi kubwa, lakini unashangiliwa na kuenezwa na baadhi ya mazuzu tu kwa vile umevalishwa cheo na madaraka!

Ona sasa alikojifikisha. Benki ya Dunia imelazimisha serikali izingatie masharti ya mkataba wa kimataifa kuhusu haki ya mtoto.

Ni kwa sababu moja kuu: Magufuli atapita tu, Tanzania itabaki.

Zuieni ubeberu wa ndani, epusha maafa makubwa ya baadaye.

Neno hili liliandikwa Aprili 8, 2020

Ninapolitafakari leo Aprili 4, 2021 katika Sikukuu ya kuadhimisha Ufufuko wa Yesu, huku taifa likiendelea na maombolezo ya kuondokewa na Rais JohnPombe Magufuli, hapo hapo nikifuatilia mwenendo na mwelekeo mpya wa utawala wa nchi, naona kama “shujaa” ameanguka ili baadhi ya mambo mema aliyozika yapate kufufuka.

Nakutakieni Paska Njema!

Like
1