WANAZUONI, walimu na wachambuzi kadhaa wa masuala ya elimu wameonya kuhusu historia ya Tanzania kupotoshwa kwa malengo ya kisiasa.
Tayari Serikali ya Tanzania kupitia kwa Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalichako, imeeleza kuwa kuanzia Julai mwaka huu kutakuwa na somo la Historia “linalojitegemea,” ambalo litafundishwa kuanzia shule za awali hadi kidato cha sita.
Prof Ndalichako amesema hayo ndani ya miezi miwili tangu Rais John Magufuli alipoagiza somo la historia liwe la lazima kwa wanafunzi wote. Alitoa agizo hilo Desemba 9, 2020, Ikulu ya Chamino, Dodoma.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, somo hilo litajenga uzalendo kwa wanafunzi kuipenda nchi yao na kuwa tayari kuipigania na kulinda rasilimali zake.
Hata hivyo, baadhi ya walimu wa somo la Uraia waliohojiwa na SAUTI KUBWA wameonyesha wasiwasi juu ya msukumo huo wa kisiasa, kwa maelezo kuwa upo uwezekano wa kupotosha historia na kuficha ukweli wa hali halisi ili kutukuza watawala.
Walimu hao, ambao hatutawataja majina kwa sababu zinazoeleweka, wamesema kwamba shule zimekuwa na somo la historia kwa muda mrefu, na sehemu kubwa inafundishwa historia ya Tanzania.
Wanatilia shaka sababu ya agizo hili jipya, na hasa mitaala ya somo hilo ilivyoandaliwa kwa haraka haraka. Mmoja alihoji: “Kuna sababu ipi kulazimisha somo la historia ya Tanzania lisimame peke yake?”
Walimu hao wanahoji umakini wa waandaaji wa mitaala na uchapishaji wa vitabu ndani ya miezi miwili tu, wakidai kwamba “huu ni ulipuaji,” na kwamba utaligharimu taifa.
Miongoni mwa walioshangazwa na kasi hii ni mwanazuoni na mtafiti wa historia, kutoka Idara ya Historia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambaye naye ameomba jina lake lihifadhiwe.
Anasema kasi ya kuandaa mtaala wa somo hilo jipya ni sawa na mkakati wa “kuchakachua” historia ili kufurahisha watawala
“Hii spidi inaleta wasiwasi. Kazi ya kuandaa mitaala siyo ndogo na kamwe siyo ya kukimbizana. Nashangaa hawa wenzangu wanaweza kufanya kazi hiyo kwa muda wa mwezi mmoja hadi mwili. Hawa wametumia nini, yaani mtaala wa somo kuanzia msingi hadi elimu ya juu ya sekondari ndani ya mwezi mmoja, kweli?,” amehoji daktari huyo wa historia.
Mbali na wasiwasi wa wataalamu hao wa historia, wakili na mtetezi wa haki za binadamu, Tundu Lissu, jana alieleza hofu hiyohiyo akisema kwamba “serikali inaelekea kurudia makosa ya miaka ya nyuma kwenye suala hili la kufundisha historia ya Tanzania.”
Alisema Tanzania imekuwa na somo la historia kwenye mitaala yake kwa miaka mingi tangu Uhuru na bado somo linafundishwa katika ngazi mbalimbali za elimu, lakini bahati mbaya limejaa “propaganda za utawala” hivyo huenda haya yakajirudia.
“Mimi naamini kinachotafutwa hapa siyo kufundisha watoto wetu historia. Kinachotafutwa ni namna ya kurudisha propaganda ya kisiasa ya watawala wetu wa sasa kwa kuiita historia,” alisema Lissu.
Alisistiza kuwa ni muhimu kufundisha jamii yetu historia ya nchi yote katika maeneo mbalimbali ya maisha, siyo ya watawala tu, na kwamba ili somo hilo lifanikiwe, ni lazima kufanyike utafiti na kuandika vitabu, majarida na maandiko mengine ya kitaaluma na kuwafundisha wanafunzi, na si kukurupuka kama inavyoonekana sasa.
Aliongeza: “Somo la historia, siyo propaganda, kila nchi imekuwa ikihakikisha wanafunzi wake wanalielewa vyema ili kuwa na utambuzi wa nchi imetoka wapi, inakwenda wapi na namna nzuri ya kuishi na kuitumikia.”