SHIRIKA la Masoko ya Kariakoo, Ofisi ya RAIS, TAMISEMI kutokaguliwa na CAG ni ufisadi

Imeandikwa na Martin Maranja Masese

SHIRIKA la Masoko ya Kariakoo (Kariakoo Markets Corporation) lipo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI. CAG katika taarifa ya ukaguzi 2020/2021 anasema eneo hilo ameshindwa kutoa maoni. Maana yake hakukagua. Je, ni kweli Rais hajui lolote kuhusu Ofisi yake kutofanyiwa ukaguzi na CAG?

Shirika la Masoko ya Kariakoo (Kariakoo Markets Corporation) ni taasisi iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Masoko ya Kariakoo, Na. 36 ya mwaka 1974 (ikafanyiwa marejeo na Sheria Na. 16 ya mwaka 1985) ili kuratibu na kudhibiti soko la Kariakoo, linalopatikana mkoa wa Dar es Salaam

Shirika la Maendeleo la Jiji la DSM (DDC) na Shirika la Masoko Kariakoo ni mashirika ya Umma yanayoongozwa na Serikali kupitia Halmashauri ya Jiji la DSM chini ya Sheria za Makampuni ya mwaka 1971 na Sheria ya Bunge Na. 36 ya mwaka 1974, The Kariakoo Market Corporation Act, 1974

Uongozi wa shirika la Masoko ya Kariakoo unatoa Taarifa zake na kuwajibika kwa Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI). Hivyo, hapa tunajadili udhaifu wa Serikali Kwa Kuhusianisha Muunganiko wa uongozi wa shirika, wizara na Ofisi ya Rais. Tunataka Majibu.

Shirika la Masoko ya Kariakoo kama ilivyo kwa taasisi nyingine za serikali linayo mipango ya Uwekezaji kwa ajili ya maendeleo yake. Katika kipindi chote ambapo limekuwepo kutekeleza shughuli zake kwa mujibu wa Sheria yake, limefanikiwa kutekeleza shughuli kadhaa za kimaendeleo.

Mfano, Usimamizi wa Soko Kuu na Soko Dogo katika Soko la Kariakoo kwamba Masoko haya yote yameendelea kuwepo tangu yalipojengwa na kuanza kutumika katika uingizaji wa mapato. kujenga nyumba saba (7) za kawaida na Ghorofa moja katika maeneo ya Mbezi Beach- Makonde na Tabata Bima.

Pia, Shirika la masoko ya Kariakoo (SMK) limenunua rasilimali ardhi (Viwanja) na kumiliki katika maeneo ya Mbezi Beach Makonde na Tabata Bima, kwa ajili ya kufanya uwekezaji. Ukubwa wa maeneo yote kwa pamoja ni hekta kadhaa. Zote hizi ni mali ya shirika, hazijafanyiwa ukaguzi na mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG)

Pia tulielezwa, Shirika la Masoko ya Kariakoo linamiliki eneo la Soko Dogo ambalo linahitaji Uwekezaji mkubwa kwa kujenga Jengo jipya la Kisasa ambalo litaweza kutoa nafasi nyingi za maeneo ya kufanya biashara, Maegesho ya magari na huduma nyingine za kibiashara. Eneo hili lina eneo lina Mita za Mraba 3,598

Eneo la Mbezi Beach Makonde kuna Mita za Mraba 6,119 na Tabata Bima ni mita za mraba 10,117.14. Tangu Mwaka 2019/2020 tulielezwa na bodo kwamba hatua za awali zimeanza kwa ajili ya kupata Wawekezaji kupitia njia mbalimbali za kiuwekezaji. Hakuna Taarifa iliyotolewa tena shirika la Masoko ya Kariakoo kwa umma na Hakuna Taarifa za ukaguzi

Kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Na.36 ya Mwaka 1974, Shirika la Masoko ya Kariakoo ambalo linayo dhamana ya kupokea mazao yote ya chakula yanayoingia katika mkoa wa Dar Es Salaam, na kwamba ndiyo husimamia shughuli zote zinazoendeshwa katika Soko Kuu la Kariakoo kila siku

Pamoja na usimamizi wa shughuli za kibiashara ambazo hufanywa na Wafanya biashara wa kada mbalimbali. Wafanya biashara wanaofanya shughuli zao sokoni Kariakoo ni wa aina mbili ambao ni Wafanyabiashara wa Jumla (Whole Salers ) na wale Wafanyabiashara wa rejareja (Retail Salers)

Biashara ya mazao ya jumla hufanyika eneo la Shimoni “Basement Floor”. Sehemu hii ya soko la Kariakoo inazo sehemu maalumu za kushushia mazao mbalimbali ambayo huingia Sokoni kila siku kwa ishirini na nne (24). Kariakoo ni soko la kimkakati. Shirika kutofanyiwa ukaguzi ni mzaha

Watumishi wa Shirika hufanya kazi yao ya kupokea mazao ya Wafanyabiashara. Watumishi wa Shirika wanalo jukumu kubwa la kutoza ushuru wa mazao yote ambayo yanafikishwa hapa Sokoni Kariakoo kulingana na viwango ambavyo vimepangwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Shirika

Mazao mbalimbali yakiwemo ya Matunda, Mbogamboga, Nafaka na Mazao ya uvuvi yaani Samaki Wakavu na wabichi huingia Sokoni. Mazao hutoka pande zote za nchi, yaani Tanzania Bara na Visiwani (Zanzibar na Pemba), na hata katika nchi jirani ikiwemo Zambia, Malawi, Kenya na Uganda.

Soko Kuu la Kariakoo wapo Wafanyabiashara wa rejareja ambao hufanya shughuli zao katika maeneo mbalimbali ya Soko. Eneo la Soko Dogo, Soko la wazi na eneo la mzunguko la Soko Dogo wamepangwa Wafanyabiashara wa rejareja. Aidha eneo la Shimoni pia wapo wafanyabiashara wa rejareja.

Ndani ya Soko kuna maeneo ya maduka ambayo wamepangishwa Wafanyabiashara, Vizimba (Stalls) na Meza, ambapo Wafanyabiashara wote wanaofanya biashara katika Soko hili hutozwa ada mbalimbali ikiwemo Kodi ya pango kwa watu wote wanaofanya biashara kwenye maduka na Vizimba (Stalls).

Eneo la Soko Dogo kuna vizimba vingi ambavyo asilimia kubwa ya wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao huuza aina mbalimbali za Viungo (Spices). Viungo hivi vinazalishwa katika maeneo mbalimbali ya nchi ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, yaani Visiwani Zanzibar na Tanzania Bara

Wafanyabiashara huwauzia wateja katika mkoa wa DSM, wafanyabiashara kutoka Visiwa vya Commoro, Zambia, Malawi hununua na kupeleka katika nchi zao. Wanaofanya biashara kwenye meza hutozwa ada ya kutumia Soko kila siku kwa mujibu wa viwango vilivyopangwa na uongozi wa Shirika.

Yote hayo hayajafanyiwa ukaguzi. CAG anasema ameshindwa kutolea maoni. Rais, kwa kuwa Ofisi ya TAMISEMI ipo katika Ofisi ya, Rais, ni wajibu wako sasa kuwauliza watendaji wako sababu zilizowafanya washindwe kutoa Ushirikiano kwa CAG. Walipa kodi tunataka kuona uwajibikaji.

Sheria ya Bunge namba 36 ya mwaka 1974, The Kariakoo Market Corporation Act, 1974, kifungu cha 21 hadi 23 kinazungumza kwa upana wake uwajibikaji wa shirika katika ukaguzi chini ya the Tanzania Audit Corporation Act, 1968. Itakuwa ni hatari kama Ofisi ya Rais haiheshimu Sheria

Sheria ya Bunge namba 36 ya mwaka 1974, The Kariakoo Market Corporation Act no 36, 1974 Kifungu cha 20 kimetoa Utaratibu unaopaswa kufuatwa na shirika kuandaa vitabu vya Taarifa za mahesabu. Risiti za matumizi, miamala yote ya kifedha ya shirika. Miradi na madeni ya shirika.

Taarifa pia zizingatie mapato na matumizi ya shirika. Pia, ndani ya miezi sita ya Kufunga Mwaka wa fedha, taarifa ya mahesabu ya kifedha ya shirika itakaguliwa na Tanzania Audit Corporation, iliyoanzishwa na Tanzania Audit Corporation Act, 1968

Baada ya taarifa ya kifedha ya shirika Kufanyiwa ukaguzi huo, ndani ya miezi isiyozidi saba, inapaswa Nakala ya Taarifa ya ukaguzi huo na mapendekezo ya wakaguzi inabidhiwa kwa waziri anayehusika na usimamizi wa shirika la Masoko ya Kariakoo ambaye kwa sasa ni waziri wa TAMISEMI

Mtendaji mkuu wa shirika kila baada ya Mwisho wa mwaka wa fedha anapaswa Kuandaa Taarifa ua ukaguzi huo wa shirika na kuwasilisha kwa waziri wa TAMISEMI, Kisha waziri ndani ya miezi 12 anatakiwa kuzisoma Taarifa hizo zote zilizotajwa katika mkutano mkuu. Hayajafanyika!

Rais, utakuwa na nguvu ya kukemea Rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma kwa taasisi nyingine ambazo zipo nje ya Ofisi yako ikiwa taasisi ambazo zipo ndani ya Ofisi yako hazitoi ushirikiano kwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali? Haiwezi kuwa sawa.

Zipo mali na miradi inayomilikiwa na shirika la Masoko ya Kariakoo, zitajwe, zijulikane, hesabu zake ziwekwe wazi. Shirika hili tangu kuanzishwa mwaka 1974 limefanya kazi zake bila tija. Mwaka 2017 shirika lilikuwa na madeni ya zaidi ya Shs. 1.3bn. Zimelipwa au zimeongezeka?

Like