- Tangu tupate uhuru, kwa sasa miaka sitini,
Mipango tunashukuru, imekuwa milaini,
Kusherehesha uhuru, mjini na vijijini,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Mpango miaka mitano, Nyerere aliiweka,
Mitatu ya mapatano, kuanza kueleweka,
Kwenye mawasiliano, kilimo kuelimika,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Tulianza motomoto, mpaka sitini na nne,
Tukaona mchakato, katika mambo mengine,
Wote kwenda mpwitopwiito, kisomo nazo mashine,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Kuliwekeza viwanda, mkakati wa viwanda,
Kote kujengwa viwanda, tukibomoa vibanda,
Nyerere navyo viwanda, vikashamiri viwanda,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Baada ya Muungano, likafata Azimio,
La Arusha mapambano, Ujamaa azimio,
Kujitegemea nako, yakawa matazamio,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Kuna walioliganga, kuna waloswahibia,
Kuna waliolipinga, kuhama na kukimbia,
Wananchi kwa kuganga, wengi hawakukimbia,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Huo mwaka wa sabini, hadi sabini na moja,
TANU iliishabaini, Uhuru mwongo mmoja,
Mwongozo ulo makini, sote twendwe kwa pamoja,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Hali ya umaskini, mapambano si utani,
Kanisa misikitini, dua hata za ubani,
Watoto wa mashuleni, wakubwa wa vijijini,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Uchumi kutetereka, hadi mwanzo themanini,
Mwalimu alingátuka, Mwinyi yu madarakani,
Uliberali funguka, bidhaa zi madukani,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Mfumuko wa mabei, mapato yakapotea,
Sokoni vitu vya bei, uchumi ukapotea,
Sera kuthibiti bei, zikawa zimekosea,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Azimio la Zanziba, mwaka tisini na mbili,
La Arusha kuliziba, mwaka tisini na mbili,
Ujamaa liliziba, bila kuwasha kandili,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Madeni yalikithiri, nchi ikaelemewa,
Wakadai kwa kiburi, shuruti tukawekewa,
Umaskini kiburi, watu wakaelemewa,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Akaja wetu Mkapa, na sera utandawazi.
Dira ya kwake Mkapa, Ukweli pia Uwazi,
Mali zikabaki kapa, tukauza wawekezi,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Madeni kusamehewa, uchumi nao kukua,
Bei bidhaa kushushwa, ufukara kupungua,
Ilijipenyeza rushwa, na mali wakachukua,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Kikwete alipofika, lake demokrasia,
Uchumi ukifufuka, rushwa ufisadi pia,
Umaskini kufuka, makombo tukilambia,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Likaja litingatinga, Joni Pombe Magufuli,
Dola alishalipanga, akisimamia mali,
Ni yeye tu Tingatinga, kila kitu yake mali,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Akiwa yu peke yake, maamuzi yote yake,
Lawama zikaja kwake, makosa yote ni yake,
Hata Katiba ni yake, avunje bado ya kwake,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Wengi wakilipa kodi, yeye alisha wabinya,
Samia kupiga hodi, wengi alisha wafinya,
Apenda walipa kodi, mitaji aipa mwanya,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Sera zetu nyingi nzuuri, na sheria zetu nzuri,
Kinacho gomba shauri, umasikini hatari,
Tumepambana uzuri, bado mipango mizuri,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Bado mipango mizuri, kulinda raslimali,
Katiba kama ni nzuri, hailindi yetu mali,
Sasa tuiweke nzuri, ilinde raslimali,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Tunautaka usawa, wa kugawana mapato,
Uchumi ukihodhiwa, ni wote tuwe na pato,
Uchumi unaoumwa, Katiba ndiyo kokoto,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Kikwazo chetu Katiba, isiyolinda uchumi,
Dawa yake ni Katiba, ili kujenga uchumi,
Tuandikie Katiba, isiyokuwa UMIMI,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Fursa za kiuchumi, kwa wajuku wetu wote,
Tunaweza kujihami, kwa Katiba yetu wote,
Uwezi jenga uchumi, kwa Katiba bwetebwete,
Imetimia sitini, tangu tupate Uhuru. - Kaditama namaliza, shairi li uwanjani,
Lakini naangaliza, enyi kuweni makini,
Katiba twaimaliza, mpya ilete nyumbani.
Hongera miaka sitini, tangu kupata Uhuru.
(Shairi hili limetungwa na Bravious Kahyoza (CEPA; PhD),
1, Desemba 2021)