Serikali za Mitaa, Vijiji zashitakiwa kwa Mbowe

SERIKALI za mitaa na vijiji ambazo karibu zote zipo chini ya Chama cha Mapinduzi (CCM), zimelalamikiwa na wananchi kwa kutosoma mapato na matumizi wala kuitisha mikutano mikuu ya wananchi.

Kwa mujibu wa sheria, mikutano mikuu ya mitaa na vijiji, inayoshirikisha wananchi wote wa eneo husika,inapaswa kuitishwa kila baada ya miezi mitatu, sawa na mara nne kwa mwaka, huku moja ya ajenda ya lazima ikiwa ni kuwasomea wananchi mapato na matumizi.

Leo asubuhi, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Taifa, Freeman Mbowe, akihutubia wananchi wa Kata ya Lalaga, Jimbo la Kishapu, pamoja na mambo mengine amepokea malalamiko ya wananchi kuhusu kutosomewa mapato na matumizi na kutoitishwa kwa mikutano mikuu ya vijiji vya kata hiyo, hali inayowanyima taarifa, haki na wajibu wa kuamua hatma ya maisha yao na kuzisimamia serikali zao.

Katika kuhakikisha hali hiyo, Mbowe aliuliza kama serikali za vijiji zinasoma mapato na matumizi, basi waseme ukweli kwa kunyoosha mikono yao juu, lakini hakuna mwananchi hata mmoja aliyenyoosha mkono wake juu.

Hata hivyo, alipouliza kama hawasomewi mapato na matumizi, wanyooshe mikono yao juu, ambapo wananchi wote walinyoosha mikono yao juu kuthibitisha tatizo hilo.

Jana, Mbowe na msafara wake, wakiwa katika kata ya Didia, jimbo la Solwa, wananchi walithibitisha pia kutoitishwa kwa mikutano ya vijiji na kutosomewa mapato na matumizi, huku wakilalamia pia ukandamizaji unaofanywa na serikali ya kijiji cha Didia, wa kuwatoza Shilingi 10,000 kila mwananchi anapokwenda kupata huduma ya kiofisi katika serikali ya kijiji.

Mbali na malalamiko ya wananchi wa mkoa wa Shinyanga, maelfu ya wananchi wa vijijij na mitaa iliyopo kwenye majimbo yote ya mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma (Kanda ya Magharibi); Kagera, Geita na Mwanza (Kanda ya Victoria) pia wamekuwa wakithibitisha tatizo la serikali za mitaa na vijiji kutoitisha mikutano wala kusoma mapato na matumizi.

Akizungumzia suala hilo, Mbowe alisema chanzo cha tatizo hilo ni kuvurugwa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji wa mwaka 2019 ambapo karibu wagombea wote wa vyama vya upinzani walienguliwa kwa makusudi na kuacha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa.

“Tatizo hili la tumekutana nalo kwenye mikutano yote, kwenye mikoa na majimbo yote. Mikutano ya vijiji haifanyiki, mapato hamsomewi, kwasababu mnaongozwa na watu ambao hamkuwachagua, na wao hawajali, kwasababu walipachikwa,” alisema Mbowe.

Ili kukomesha serikali za vijiji na mitaa, zisizowajibika wala kuheshimu wananchi, Kiongozi huyo amewaomba Watanzania kuzidi kujiunga kwa wingi CHADEMA na kujipanga kuiondoa CCM madarakani kwa kuanzia na uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji na baadaye uchaguzi mkuu.

Alisema mbali na kutoitishwa kwa mikutano ya vijiji, wananchi wengi wa jimbo la Kishapu wanaishi katika umaskini mkubwa katikati ya kilimo cha pamba ambacho kingetosha kuwaondolea umaskini kama serikali ya CCM ingewajali na kuwawezesha kufanya uzalishaji mkubwa na kuvutia wanunuzi wa zao hilo kwa bei inayowalipa.

Bei ya kuuzia pamba imeporomoka kutoka shilingi 2,040 mpaka 1,060 kwa kilo, na kuathiri vipato vya wananchi wengi wa mkoa wa Shinyanga, Mwanza na Geita, wanaotegemea zao hilo.

Like