DC na mbunge wa zamani CCM ajiunga Chadema

– Asombwa na mafuriko ya Mbowe Meatu
– Ni Rosemary Kirigini aliyewahi kuwa mbunge Viti Maalumu

MAELFU ya wananchi wa mji wa Mwanhuzi, wilayani Meatu, mkoani Simiyu, wamehudhuria kwa wingi katika mkutano wa hadhara wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalum mkoa wa Simiyu na Mkuu wa Wilaya (DC) za Meatu na Maswa, Rosemary Kirigini, akitangaza kuachana na Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga rasmi na CHADEMA.

Mbowe akimkabidhi kadi mwanachama mpya Rosemary Kirigini

DC mstaafu Kirigini, akiwa amevalia vazi rasmi la CHADEMA, almaarufu kombati, aliwasili dakika chache katika mkutano huo na kushiriki mapokezi ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Akimpokea Kirigini, Mbowe alimtaka aombe msamaha kwa dhambi zozote za kisiasa alizowahi kuzifanya akiwa CCM na kueleza sababu iliyomsukuma kujiunga CHADEMA.

Kirigini alieleza kuwa ameamua kujiunga CHADEMA kwasababu ni haki yake ya kikatiba na kisheria kujiunga na chama chochote, lakini zaidi ameamua kujiunga na chama chenye dhamira ya kweli ya kusimamia demokrasia na maendeleo ya Watanzania wakiwemo wananchi wa Meatu, ambako ndiko nyumbani kwao anakotokea.

“Ndugu zangu msishangae. Tambueni kuwa inawezekana kutoka CCM na kuhamia CHADEMA. Hakuna asiyenifahamu, hapa ni nyumbani kwetu. Nimeamua kujiunga CHADEMA ili tushirikiane kuisaidia Meatu na Tanzania nzima. Nipo tayari kutumika mahali popote pale kupitia chama hiki. Mimi mnajua nilikuwa CCM na mnajua mimi ni bulldozer, najua CCM tulikuwa tunashindaje. Kwa hiyo, msiwe na wasiwasi, nipo tayari tuijenge Meatu yetu. Na wana CCM msione kwamba kama amewaacha, bado nitaendelea kuwa nanyi kupitia CHADEMA,” alisema Kirigini na kushangiliwa na wananchi.

Alihutubia wananchi hao, Mbowe, aliendeleza ujumbe wake mkuu kwa wananchi wa mikoa ya kanda ya ziwa, kwamba CCM imekuwa ni pango la walanguzi wa maliasili na raslimali za nchi.

Kwamba, pamoja na utajiri mkubwa wa raslimali za madini, ziwa Victoria na mazao ya biashara hususani Pamba, bado Meatu na maeneo yote ya kanda ya ziwa yapo kwenye umaskini mkubwa wa kipato na huduma duni za kijamii.

“Ukanda mzima wa ziwa victoria na serengeti, ikiwemo wilaya ya Kishapu, Maswa, Meatu na mikoa yote tuliyopita, kuna umaskini mkubwa wa kipato. Maji hakuna wakati ziwa Victoria lipo karibu hapa. Wananchi ni maskini pamoja na uwepo wa madini na kilimo cha pamba. Nataka mtambue kuwa miaka 62 ya uhuru, CCM imekuwa ni pango la walanguzi, wanagawa raslimali zetu kiholela kwa wageni na kuwaacha kwenye umaskini. Asilimia zaidi ya 90 ya dhahabu yetu yote, almasi na madini yetu yote tayari yalishawekwa chini ya umiliki wa wageni kiholela.

“Wameuza mashirika ya umma, wamegawa migodi, vitalu vya mafuta na gesi asilia, wakagawa maeneo ya hifadhi za Ngorongoro na Loliondo. Sasa wameona haitoshi wamegawa na bandari zetu. Njia pekee ya kunusuru raslimali zetu, ni kuiondoa nchi hii mikononi mwa CCM,” alisema Mbowe na kushangiliwa.

Rosemary Kirigini akisalimia wananchi

Katika hatua nyingine, umati wote wa wananchi wa Mwanhuzi walioshiriki mkutano huo, ulipiga kura ya hapana kupinga mkataba wa uendelezaji bandari na maeneo mengine mahsusi ya kiuchumi, mkataba ulioingiwa baina ya serikali ya Tanzania na Dubai.

Mwishoni mwa mkutano huo, maelfu ya wananchi walimsindikiza Mbowe na msafara wake mpaka katika hoteli aliyofikia mjini Mwanhuzi.

Like
1