SERIKALI YATESA RAIA KWENYE MAENEO YA HIFADHI

Utesaji na kamatakamata ya kionevu vimekuwa vikifanyika katika maeneo zaidi ya moja, mara nyingi vikiacha madhara makubwa kwa wathirika…

Wakili Bahama Nyanduga, Mwenyekiti Mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania. Ndiye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.

MAMLAKA za serikali zimekuwa kichocheo cha ukiukwaji wa haki za binadamu, na zimekuwa zinatumika kutesa na kuua raia wanaoishi kwenye maeneo yaliyo jirani na hifadhi, utafiti mpya umebaini.

Utafiti huo, ambao ripoti yake ilizinduliwa juzi jijini Dar es Salaam, ulifanywa na taasisi tatu zenye dhamana mtambuka za habari, sheria, na haki za binadamu. Ni Centre for Strategic Litigation (CSL) ya Zanzibar, SK Media East Africa yenye makao makuu Nairobi (Kenya), na Media Brains ya Dar es Salaam.

Hafla ya uzinduzi wa ripoti hiyo  – “Conserving our rights: uncovering human rights violations in Tanzania’ conservation sector“- ilishirikisha wanahabari, wanaharakati wa haki za binadamu, wanasheria, waathirika, na wadau wengine.

Deusdedit Rweyemamu ambaye ni Mkurugenzi wa CSL, alisema ripoti hiyo ni maalumu kwa ajili ya kuibua mjadala wa kitaifa wa kuwaleta pamoja watu wa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi kujua changamoto wanazokutana nazo.

Utafiti huo ulifanywa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani kati ya 2022 na 2023.

Ripoti hiyo inaainisha namna haki za makazi, haki ya usalama wa raia, haki za ufikiwaji wa huduma za kijamii zimekuwa zikikiukwa kwa makusudi na zaidi kuwanyima waathiriwa haki yao ya utu.

Rweyemamu alisema katika utafiti huo ambao si wa kisayansi ulilenga kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na watu wa jamii zilizo katika maeneo ya hifadhi, mamlaka za Serikali zikiwamo Mamlaka ya Huduma za Misitu (TFS), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) pamoja na Jeshi la Polisi.

Taasisi hizo zimetajwa kwenye ripoti hiyo kuhusika moja kwa moja katika utesaji, mauaji na ukiukaji wa haki za watu wakati wa utekelezaji wa oparesheni mbalimbali huku wakilenga kulinda haki za wanyama kuliko haki za binadamu.

“Huu si utafiti wa kisayansi lakini ulilenga kuzungumza moja kwa moja na watu wanaoishi karibu na maeneo ya uhifadhi kisheria na namna wanafanyiwa ukatili huku wanyama wakipewa heshima. Nia ya utafiti huu ni kujenga uwiano mwema kati ya uhifadhi na watu wetu,” alisema Rweyemamu.

Ripoti ya utafiti huo iliyofanyika katika mikoa 27 ikijumuisha Zanzibar, iliangalia maeneo 22 ya Hifadhi za Taifa, eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, maeneo 22 Hifadhi za Wanyama, maeneo 27 maalumu ya hifadhi yanayodhibitiwa, maeneo 38 ya uangalizi wa wanyamapori, maeneo matatu ya ardhi chepe, maeneo 465 ya hifadhi za asili za misitu, maeneo 20 ya hifadhi maalumu za misitu na mashamba 24 ya misitu ya Serikali.

Akizungumzia ripoti hiyo, Kamishna Mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu, Wakili Thom Bahame Nyanduga alisema kwa kuangalia historia, utunzaji wa mazingira unazingatia zaidi kumlinda mnyama kuliko binadamu, hivyo kushindwa kutoa majibu ya changamoto za binadamu wanaoishi kwenye maeneo ya hifadhi.

Alisema oparesheni zote ambazo zimewahi kufanyika zikiwamo Oparesheni Uhai na Oparesheni Tokomeza zilisababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ikiwemo uhamishaji wa wananchi unaoendelea katika eneo la Ngorongoro.

Wakili Nyanduga anashauri ripoti hiyo itumike kama nyenzo ya kuwezesha uhifadhi endelevu na linganifu kwa kuzingatia haki za binadamu.

“Maisha ambayo jamii zimeondolewa kwa mabavu katika maeneo yao ya asili yamesababisha uvunjifu wa haki ya makazi, usalama wa raia kwa umoja wao, uwezo wa kupata huduma za afya, maji,barabara na kuwanyima haki ya kuishi kwa uhuru na heshima ya utu.

“Tunatakiwa kuangalia ni namna gani tunaweza kufanya uhifadhi unaoheshimu haki za watu wanaoishi kiasili katika maeneo hayo. Tunatakiwa kuona ni namna gani uhifadhi unaweza kufanyika kwa kulinda haki za raia wanaoishi katika maeneo husika,” alisema Nyanduga.

Kondo Kikunda, mkazi wa Bagamoyo, ni miongoni mwa waathirika wa dhuluma za vyombo vya serikali dhidi ya raia. Alishiriki uzinduzi wa ripoti na kutoa ushuhuda wa mateso aliyopitia.

Maeneo yaliyoguswa.

Ripoti hiyo imegusa baadhi ya maeneo ambayo hayakuwahi kuripotiwa, hasa kuhusu ukiukwaji wa haki za watu ikiainisha ushahidi wa moja kwa moja kutoka kwa waathirika, ikiwemo ukatili ambao umekuwa ukifanywa na Mamlaka ya Huduma za Misitu (TFS), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (Tawa) na jeshi la Polisi.

Inaainisha kuwa matukio mengi ya ukiukaji huo yanatokana na watendaji wa vyombo hivyo kutoheshimu mipaka yao kiutendaji, ambapo wamekuwa wakiharibu mali, zikiwamo nyumba, mifugo na mazao na kuwatesa wanavijiji wanaowatuhumu kuingia katika maeneo yaliyozuiliwa kwa ajili ya kulisha mifugo au kuvuna mazao.

“Utesaji na kamatakamata ya kionevu vimekuwa vikifanyika katika maeneo zaidi ya moja, mara nyingi vikiacha madhara makubwa kwa wathiriwa. Malalamiko ya watu kuondolewa kwenye maeneo yao ya asili bila kulipwa fidia yamekuwa jambo la kawaida na serikali imekuwa haichukui hatua zozote na hata pale ambapo fidia hutolewa, malipo yamekuwa yakicheleweshwa na wakati mwingine yamekuwa ya kibaguzi kiasi cha wengine kukosa kabisa haki zao,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo na kuongeza kuwa matumizi ya nguvu kupita kiasi kinyume cha makubaliano ya Mikataba ya Kimataifa na Kikanda ambayo Tanzania imeridhia yamesababisha maumivu kwa wakazi wa maeneo hayo kwa kuwaondoa kwenye makazi yao ya asili na kuwaacha wakiwa hawana makazi wala pa kwenda.

Ripoti hiyo pia inaainisha baadhi ya matukio ambayo yamekuwa yakisimamiwa na mamlaka za Serikali ikiwemo Tawa na Tanapa, ambayo inaeleza kuwa hayana namna ya kuvumiliwa wala kutetewa kwa kuwa yanafanyika makusudi dhidi ya raia katika maeneo yanayotajwa kuwa chini ya usimamizi wa mamlaka hizo.

Maeneo yanayotajwa katika kadhia hizo ni pamoja na Hifadhi ya Eneo la Igombe, Hifadhi ya Misitu ya Makere Kusini, Hifadhi ya Kilombero na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Mmoja wa wakurugenzi wa Media Brains, Absalom Kibanda alisema ripoti hiyo inayogusa moja kwa moja haki za binadamu ni mnyororo wa matukio ambao lazima ufike mahali usitishwe.

Alisema utafiti wa kadhia hizo, ulifanyika kabla Rais Samia Suluhu Hassan hajaunda Tume ya Haki Jinai ambayo maeneo yaliyoguswa na tume hiyo ni majeshi yanayotumika katika maeneo ya uhifadhi.

“Kati ya mapendekezo yaliyoguswa na Tume ya Haki jinai ni sehemu ya uhifadhi, katika maeneo 333 ambayo yamepelkwa kwa Rais ni pamoja na eneo la uhifadhi. Hawa watu wanavaa sare za kijeshi, yanaitwa majeshi USU, haya ni chanzo kikubwa cha mizozo na uvunjifu wa haki za binadamu katika meeneo yote ya uhifadhi.

Mwandishi mbobevu ambaye ni kati ya wasimamizi ripoti hiyo, Jabir Idrisa alisema ni bahati mbaya matukio ya uvunifu wa haki za binadamu yanatokea katika nchi ambayo imepata uhuru.

“Tunasikitika sana, tuna watu ambao ni walinzi wa raia na mali zao lakini wanakuwa wakatili dhidi ya raia. Haya mambo yafike mahali yakomeshwe kabisa,” alisema Idrisa

BOFYA HAPA KUPATA NAKALA YA RIPOTI YA UTAFITI HUO: Conserving Our Rights -Uncovering Human Rights Violations in Tanzania's Conservation Sector

Like