SERIKALI ya Tanzania, kupitia vyombo vya usalama, imelazimisha uongozi wa Shule ya Kimataifa ya Moshi (ISM) kukanusha taarifa ya kufungwa kwa shule hiyo kutokana na kukumbwa na ugonjwa wa Corona.
Juzi Jumanne – Januari 19 – uongozi wa shule hiyo iliyopo mjini Moshi, Kilimanjaro, ulijulisha jumuiya ya shule hiyo na wazazi wa wanafunzi wake kuwa inafungwa kwa muda kutokana na mwanafunzi mmoja kupimwa na kubainika ameambukizwa ugonjwa wa Corona.
Taarifa hiyo ya kuwepo kwa mgonjwa huyo ilisambaa katika mitandao ya kijamii na kusababisha taharuki kubwa kwa wananchi, siyo wa mji huo tu, bali maeneo mengi ya Tanzania na nje ya nchi. Shule hiyo yenye wanafunzi wanaofikia 600 (kampasi ya Moshi na Arusha), ni asilimia 20 tu, ambao ni wanafunzi wanaotajwa kufikia 120 ndiyo Watanzania.
SAUTI KUBWA ina taarifa kuwa siku moja baada ya taarifa hiyo kuenea kwa umma, wakuu wa vyombo vya usalama wa Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya ya Moshi walifika shuleni hapo na kufanya mazungumzo ya faragha na mkurugenzi wa shule hiyo, Anna Marsden. Ni katika mazungumzo hayo aliamrishwa kukanusha taarifa yake hiyo.
Katika kutekeleza amri hiyo, mkurugenzi wa shule hiyo, jana aliita waandishi wa habari na kueleza kilichotokea hadi taarifa hiyo ya ndani kufika kwa umma, huku akieleza kwamba masomo katika shule hiyo yanaendelea kama kawaida na wala haijafungwa.
Inaelezwa kuwa mkurugenzi hiyo alielezwa kuwa wenye mamlaka ya kutoa taarifa za kuwepo kwa mlipuko wa magonjwa nchini Tanzania ni “wakubwa” wanne – rais, waziri mkuu, waziri wa afya na msemaji mkuu wa serikali.
Pamoja na mkurugenzi huyo kukanusha, pia Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Rajabu Kundya na viongozi wengine wamekanusha kuwepo kwa mgonjwa huyo na kuwataka wananchi “kupuuza taarifa hiyo.”
Kundya amekuwa akisisitiza kuwa Mji wa Moshi uko alama na kwamba waananchi wasiwe na hofu kwa kuwa kiongozi wan chi, Rais John Magufuli ameema kuwa “Tanzania haina Corona.”
Hata hiyo, katika ukurasa wa taarifa za shule hiyo- website; http://www.uwcea.org (ikijumuisha kampasi ya Arusha), hadi leo saa 9:00 ilikuwa bado imeweka taarifa ya kuwepo kwa tishio la ugonjwa huo, ikiwamo mgonjwa aliyeambukizwa na kwamba shule imefungwa.
Taarifa hiyo inaeleza zaidi kwamba wanafunzi wa kutwa wataendelea na masomo wakiwa majumbani, huku walimu wakifanya kazi zao majumbani kwao pia. Wanafunzi watakaoendelea kuwepo shuleni ni wale wa bweni.
Tanzania ni nchi pekee katika Afrika inayoendelea kuficha taarifa za ugonjwa na kukana kuwepo kwa Corona. Sababu kubwa inayotolewa na serikali hiyo, kwa maelekezo ya kiongozi wake, Rais Magufuli ni kwamba “Mungu amejibu maombi yao kwa kuikimbiza Corona.”