SERIKALI YAAHIDI KUFANYA MAPINDUZI KATIKA SEKTA YA HABARI

“Na ndiyo maana tukasema sasa kabla ya kwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na baadaye Uchaguzi Mkuu mwakani, sheria zile ambazo zilikuwa zinatumika kwenye uchaguzi na zinawabinya sana waaandishi wa habari kuripoti habari za uchaguzi zirekebishwe,”

SERIKALI inakusudia kushirikiana na sekta binafsi kufanya mabadiliko na maboresho makubwa kwenye sekta ya habari kwa kutunga na kuhuisha sera, sheria, miongozo inayosimamia sekta za habari, mawasiliano na teknolojia ya habari.

Serikali pia inakusudia kuimarisha huduma za mawasiliano ya simu na posta kote nchini kwa kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza na kuimarisha biashara mtandao nchini, kuimarisha miundombinu itakayowezesha utekelezwaji wa uchumi wa kidigitali, kuimarisha ulinzi na usalama wa anga.

Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba ambaye alimwakilisha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye leo Juni 27,2024 kwenye kongamano la uhuru wa kujieleza na sheria za vyombo vya habari lililoandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC).

Msemaji huyo wa Serikali amesema mwaka 2024/2025 Wizara imepanga kukamilisha uhuishwaji wa sera mbalimbali ikiwamo sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 na kutunga Sera mpya ya Taifa ya Tehama.

“Nyingine ni kufanya mapitio ya sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 ili iendane na wakati wa sasa na pia iweze kujumuisha masuala ya kumlinda mtoto dhidi ya ukatili wa mtandaoni na masuala ya ughaidi mtandaoni.

“Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa kituo cha kuhifadhi data mkoani Dodoma na Zanzibar pamoja na kuanzisha kituo kimoja cha usalama wa mawasiliano cha Taifa na kuendelea na taratibu za kuanzisha Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, Baraza Huru la Habari na Mfuko wa mafunzo kwa wanahabari,” amesema Makoba.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa amesema wakati sheria zingine zinaendelea kupitiwa ni muhimu pia sheria zinazosimamia waandishi wa habari kwenye uchaguzi zirekebishwe.

Mtetezi huyo wa haki za binadamu, amesema mwaka 2019 wakati wa Uchaguzi wa serikali za mitaa na baadaye uchaguzi mkuu mwaka 2020, waandishi wa habari walikuwa na hali mbaya kutokana na sheria kuwabana kuhusu kuandika habari.

“Na ndiyo maana tukasema sasa kabla ya kwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na baadaye Uchaguzi Mkuu mwakani, sheria zile ambazo zilikuwa zinatumika kwenye uchaguzi na zinawabinya sana waaandishi wa habari kuripoti habari za uchaguzi zirekebishwe,” amesema Ole Ngurumwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Gulumwa, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Kongamano la Kitaifa la kujadili Uhuru wa Kujieleza kwa Vyombo vya Habari na Sheria ya Habari nchini lililoandaliwa na mtandao huo na kushirikisha viongozi wa serikali, waandishi wa habari na washirika wa maendeleo. Kongamano hilo limefanyika Jijini Dar es Salaam Juni 27.2024 . (PICHA: Fidelis Felix)

Naye Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Michael Battle amesema wakati Tanzania inaendelea kukuza demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari, Serikali yake imetenga Dola za Kimarekani milioni 250 sawa na zaidi ya (Shilingi milioni 600 za Tanzania) ili kuwezesha waandishi wa habari nchini kufanya tafiti, kuandika habari za kuelimisha jamii.

Katika hatua nyingine, Balozi huyo ameipongeza Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassani kwa kuruhusu vyombo vya habari kufanya kazi zake kwa uhuru.

Hata hivyo amesema hatua hiyo bado haitoshi kusema kuna uhuru kamili hivyo, kuna ulazima wa kuboresha hatua hiyo kwa kuondoa vitisho kwa wanahabari ili wawe huru zaidi kufanya kazi zao.

Meneja Uendeshaji wa Jumuia ya Wanahabari wa Mitandao ya kijamii Tanzania (JUMIKITA), Dr. Bravious Kahyoza amesema mijadala kuhusu uhuru wa habari inayoendelea ni matokeo ya mifumo ya Katiba iliyopo ambayo muundo wa Serikali hauwezi kutoa uhuru kwa vyombo vya habari.

”Kuna vitisho vya kitaasisi, vyombo vya habari vina changamoto kubwa sana, kwa mfano ingawa JUMIKITA ina wanahabari nchi nzima, lakini hawaonekani niwa muhimu katika masuala muhimu ya kitaifa isipokuwa yale ya ku push tu. Hata Rais akiwa anasafri au akiwa na shughuli za kiserikali waandishi hao wa mitandao hawashirikishwi, umuhimu wao hauonekani, hili ni tatizo” amesema Dk. Kahyoza

 

 

Like