KATIKA mkutano wa Rais Samia Suluhu Hassan na wazee wa Jiji la Dar es Salaam unaofanyika leo, washiriki wamelazimika kuvaa barakoa ili kujinga na maambukuzi ya mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19.
Kuvaa barakoa ni moja ya taratibu na kanuni ambazo zimewekwa kwa washiriki wote. Mkutano huo unafanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Hatua ya kuwepo kanuni ya kuvaa barakoa ni tofauti na mtangulizi wake, Rais John Magufuli ambaye hadi anafariki dunia hakuamini kuendelea kuwepo kwa ugonjwa wa Corona, akidai “uliondoshwa kwa Damu ya Yesu.” Pia hakuamini kuvaa barakoa wala kuwepo kwa chanjo dhidi ya ugonjwa huo maarufu kwa jina la COVID-19.
SAUTI KUBWA ambayo inafuatilia mkutano huo utakaorushwa moja kwa moja na baadhi ya vituo vya televisheni na radio, unafanyika mara ya kwanza tangu Rais Samia achukue madaraka ya kuongoza Tanzania. Rais aliapishwa Machi 19, 2021 baada ya mtangulizi wake, Magufuli kufariki dunia Machi 17, mwaka huu.
Hadi sasa haijafahamika Rais Samia atazungumza nini, lakini inadhaniwa na wachambuzi wa siasa nchini kwamba atatumia mwanya huo kueleza umma kuhusu hali ya siasa na huenda akatumia fursa hiyo kueleza yaliyojiri alipokuwa ziarani Kenya mapema wiki hii.
“Hivi karibuni Rais alikuwa Kenya kwenye ziara rasmi, huko alizungumza mambo mengi mazito, ikiwamo kwamba Tanzania sasa imefunguka na mengine mengi,” anasema Thomas Munasa, mchambuzi wa siasa kutoka Dar es Salaam.
Munasa anasema mara nyingi vikao na waze, hasa wa Dar es Salaam vimekuwa vikitumiwa na marais wote waliopita kuzungumza mambo mazito ya nchi, hivyo Rais Samia hatakuwa mbali na watangulizi wake.
Mtangulizi wa Rais Samia, Magufuli alifanya mkutano na wazee wa Dar es Salaam mara moja tu – Februari 13, 2016. Tangu akamate dola ya Tanzania. Alikutana nao katika Ukumbi wa Diamond Jubilee na alizungumza hasa kuhusu “kuukataa umasikini kwa Watanzania.” Pia alizungumzia kile alichozoea kuita “madudu ya ajabu” kutoka uongozi uliopita wa Rais Jakaya Kikwete.
Hata hivyo, kikao hicho cha wazee kilikuwa cha mwisho kwa Rais Magufuli, kwani mara nyingi alikuwa akizungumza na umma kupitia makanisa au maeneo mengine kuwasiliana na umma wa Watanzania.
– SAUTI KUBWA inaendela kukuletea kile kinachojiri katika mkutano huo.