Samia akerwa na porojo Bungeni

RAIS Samia Suluhu Hassan amekerwa kuona baadhi ya wabunge wanaacha kujadili ajenda za kitaifa zenye maslahi mapana kwa umma, badala yake wanatumia muda mrefu kujadili porojo na kusifia viongozi.

Porojo anazoeleza Rais Samia ni wabunge hao kuacha kupanga na kupitisha bajeti, badala yake wanamlinganisha yeye na mtangulizi wake, hayati John Magufuli, rais wa awamu ya tano aliyefariki dunia Machi 17, 2021 jijini Dar es Salaam.  

“Inasikitisha sana kuona watu wanapiga ngoma mitandaoni, lakini ngoma ile inachezwa bungeni na inachezwa kwa kudemka vizuri sana, mnademka vizuri sana; kulinganisha watu, siyo kulinganisha agenda za kitaifa, agenda ya kitaifa ni (imekuwa) moja, mnalingansha Magufuli na Samia, hawa watu ni kitu kimoja, alisema Rais Samia.

Akaedelea: “nimekuwa nikifuatilia mijadala yenu bungeni, mijadala ambayo haina afya kwa taifa letu, naomba sana, kipindi hiki ndugu zangu wabunge, tunatakiwa kupitisha bajeti za sekta mbalimbali, bajeti ya serikali kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu, nawaomba sana mjikite huko. Naomba tufanye sana kazi kama bunge linavyotakiwa kufanya kazi.”

Akizungumza Jumapili, 18 Aprili 2021, jijini Dodoma, Rais Samia alisema yeye na Magufuli ni kitu kimoja kwa sababu anaendeleza kazi iliyoanza kufanywa na mtangulizi wake.

Alikuwa akizungumza wakati wa kongamano la kitaifa lililandaliwa na viongozi wa dini mbalimbali nchini kuombea taifa na kujadili “namna ya kuenzi” mchango wa hayati Magufuli.

Rais Samia alitoa mwito kwa wabunge kuanza kujadili masuala yanayohusu ajenda ya maendeleo ya kitaifa.

Hivi karibuni, wabunge kadhaa wamekuwa wakijadiliana juu ya namna ya kuenzi kazi za hayati Magufuli kwa kujikitita katika kuangalia “nguvu na udhaifu wa serikali ya awamu ya tano dhidi ya awamu ya sita.”

January Makamba, Mbunge wa Bumbuli, mkoani Tanga, aliunga mkono wazo la kukosoa serikali ya awamu ya tano kama njia ya kutengeneza njia ya maboresho yatakayofanywa na serikali ya awamu ya sita.

“Hayati Rais Magufuli ni kama mshonaji ambaye alitutengenezea vazi zuri. Ikiwa vazi hili lina nyuzi zinazojitokeza, ni jukumu letu kuzikata na ikiwa kuna kifungo kilicholegea, lazima tukiimarishe. Lakini kufanya hivyo haimaanishi kukataa kazi nzuri iliyofanywa na mshonaji,” Makamba alisema akisisitiza kuwa sifa zote za ubora zitabaki kwa mshonaji.

Makamba aliungwa mkono na Nape Nnauye, Mbunge wa Mtama huku akipingwa vikali na Joseph Kasheku Musukuma mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini.

Kwa upande mwingine, Spika wa Bunge hivi karibuni alikosoa uamuzi wa serikali ya awamu ya tano kukataa mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo akisema kuwa, “serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli ilishauriwa vibaya.”

Wakati wa semina hiyo, Rais Samia alibainisha ajenda zake kuu za kitaifa ambazo zinajumuisha mambo yafuatayo; kukuza na kuimarisha maadili ya kitaifa, kulinda amani, umoja, usawa, uhuru, na undugu; kuimarisha uchumi jumla ili kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa njia hiyo; kupambana na ufisadi; kushughulika na wahujumu uchumi, kupambana na biashara ya dawa za kulevya.

Vipaumbele vingine vilivyotajwa na Rais Samia ni kuimarisha nidhamu ya wafanyikazi wa umma na kuboresha maslahi yao; upatikanaji wa elimu bora; kuimarisha mafunzo ya ujuzi-kazi; kusaidia kupatikana huduma bora za afya; kuboresha huduma ya maji safi na salama; kuimarisha utawala wa sheria; kudumisha uhuru wa kujieleza; na kuendeleza utawala wa kidemokrasia.

Pia aliahidi kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati hadi kukamilika kwake; kuboresha mazingira ya biashara, kuvutia mitaji kutoka nje ya nchi; kukuza ustawi wa wafanyabiashara na kuboresha uhusiano wa kimataifa.

Pia kuheshimu msingi ya serikali isiyofungamana na dini yoyote na kufanya kazi vizuri na taasisi za kidini katika kukuza imani ya jamii na jamii ya amani, pia ni vipaumbele cya serikali ya awamu ya sita.

“Vipaumbele hivi vilikuwa vya serikali ya awamu ya tano na bado ndio vipaumbele vya serikali ya awamu ya sita kama ajenda moja ambayo nimekula kiapo kuisimamia na kuiboresha kwa kutumia uwezo wangu kama Rais wa awamu ya sita,” alisisitiza.

Kongamano la kitaifa iliandaliwa na viongozi wa dini nchini Tanzania, ikiwa ni njia ya kuliombea taifa na kumshukuru Mungu kwa maisha ya hayati John Pombe Magufuli.

Like