MKUU wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, ambaye amekuwa anatuhumiwa na kuhusishwa na matendo kadhaa ya kijambazi, sasa ametuhumiwa kumshambulia Diwani wa kata ya Sombetini, jiji Arusha, Bakari Msangi, Februari 9 mwaka huu. Katika tukio hilo, Sabaya aliambatana na walinzi wake binafsi sita wakiwa na bunduki moja na bastola mbili.
Kwa mujibu wa Msangi na watu walioshuhudia tukio hilo, diwani huyo alishambuliwa baada ya kupigiwa simu na mfanyabiashara mmoja mkoani humo, Ally Asaad Ajirin, anayemiliki duka la mapazia la Shaahidi Stores lililopo Barabara ya Nyamwezi jirani na Soko Kuu, jijini Arusha.
Mfanyabiashara huyo alimpigia Msangi simu akimuomba msaada baada ya vijana wake wa dukani kumtaarifu kuwa Sabaya na vijana wake wamewafungia dukani na wanawapiga.
Sabaya alikuwa anahitaji shilingi milioni 100 kutoka kwa mfanyabiashara huyo, Asaad, akimtuhumu kufanya biashara ya kuuza fedha za kigeni kwa magendo.
Sabaya alitaka apewe fedha hizo, vinginevyo angemfungulia Asaad kesi ya uhujumu uchumi.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Salum Hamduni, Februari 16 mwaka huu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akasema wanaendelea na uchunguzi ingawa hakuwa tayari kulizungumzia kwa kina.
Kikao cha kamati ya ulinzi na usalama mkoa Arusha, ambacho mwenyekiti wake ni mkuu wa mkoa, Iddi Kimanta, kilichokaa Februari 12 mwaka huu, kilimwalika diwani Msangi na kupokea maelezo yake, kisha kikamwagiza RPC Hamduni kuhakikisha anaendelea na taratibu za kipolisi wakati wao wakiendelea na taratibu za kuwasiliana na mamlaka ya uteuzi wa DC Sabaya. Tangu siku hiyo, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.
Siku ya tukio, Sabaya alifika dukani kwa mfanyabiashara huyo majira ya saa 11 jioni akawataka wafanyakazi wake wamweleze alipo Asaad. Walimpigia simu akawa hapokei.
“Waliniambia mpigie simu mjomba wako mwambie tunataka pazia. Mimi nikampigia mjomba simu ikawa inaita tu. Wakatunyang’anya wafanyakazi wote simu tukawekwa chini ya ulinzi,” alisema mmojawao, Norman Jasin, na kuongeza:
“Nilikuwa mimi na mfanyakazi wangu mmoja, ikawa mtu yeyote akiingia dukani anawekwa chini ya ulinzi wanataka kujua ni nani. Machinga waliokuwa wanaona duka linafungwa wanakimbilia kuchukua mali wawapelekee wateja, ilikuwa mtu akiingia wanamwekwa chini ya ulinzi na kipigo juu.”
“Walivuta mlango wakaanza kutupiga kwa kupokezana. Sabaya akawa analazimisha tusema mjomba Asaad alipo, sisi tukawa hatujui, tukipiga simu yake inaita tu. Sabaya akapanda juu akageuza kamera ili wasionekane, lakini ilikuwa imesharekodi.
“Diwani Msangi alipofika dukani hapo akawa anaongea na Sabaya lakini tukashangaa na yeye anapigwa hata kuliko sisi.”
Kwenye tukio hilo, vijana wa duka hilo zaidi ya watatu na wateja wao walipigwa. Kuna waliojisaidia haja kubwa na waliojikojolea.
Baada ya kuwapiga sana, majira ya saa tatu usiku, aliwachukua vijana wawili akawapeleka kwenye kituo kikuu cha polisi na kuagiza wafunguliwe mashitaka ya uhujumu uchumi huku akiondoka na diwani Msangi ambaye walikuwa wamemfunga pingu.
Msafara wa Sabaya ulikuwa wa magari mawili. Gari moja liliwabeba vijana wawili wa dukani na jingine ambalo alikuwemo Sabaya mwenyewe aliingizwa diwani Msangi.
Sabaya ametumia gharama kubwa kuhakikisha habari hii haiandikwi kwenye chombo chochote cha habari. Siku moja baada ya tukio hilo waandishi walianza kuifuatilia.
Sabaya alipopata taarifa majira ya saa 2 usiku waandishi hao wakiwa wameweka kambi polisi, aliwasiliana na mmoja wao, kisha akawatumia kiasi cha shilingi laki nne kwenye simu ya mwandishi mmoja.
Hata hivyo, alipata taarifa kuwa bado kuna waandishi wengine wanne wanafuatilia habari hiyo aliwasiliana na mmoja wao akawaita ofisini kwake Hai, akawapa fedha, laki moja moja.
Baada ya hapo, alikuwa akijipongeza kuwa suala hilo limekwisha, akiwaeleza watu wake wa karibu kuwa suala hilo lingekuwa gumu kulimaliza endapo vyombo vya habari vingeandika, ila kwa hatua iliyopo anajua namna ya kulimaliza.
Hata hivyo, amekuwa akiendelea na jitihada za kumshawishi diwani Msangi wayamalize, na yuko tayari kumpatia hata fedha milioni 20, lakini imeshindikana.
Sabaya amekuwa akizunguka mara kwa mara jijini Arusha huku akilazimisha wafanyabiashara wampe fedha, vinginevyo atawafungulia kesi za uhujumu uchumi.
Amekuwa akizunguka na magari yake binafsi matatu ambayo hubandika namba za usajili tofauti tofauti ikiwemo za umoja wa mataifa (UN) na ya Miradi inayofadhiliwa na watu kutoka nje ya nchi, (DFP) ambapo huwa na mabaunsa kati ya watatu na sita na hupenda kufikia hoteli za kitalii za Tulia, Mount Meru, Orlando Garden na Lush garden.
Sabaya amekuwa akitumia muda mrefu jijini Arusha wakati yeye ni Mkuu wa wilaya ya Hai, jambo ambalo limekuwa likiibua maswali mengi kutoka kwa wananchi na wafanyabiashara ambao ndio wahanga wa matukio yake ya kitapeli.
Mwaka 2019 Sabaya alikusanya zaidi ya milioni 300 kutoka kwa wafanyabiashara jijini hapa akiwaahidi kuwatafutia fursa ya kuwa miongoni mwa wafanyabiashara watakaoshiriki kikao cha Rais John Magufuli na wafanyabiashara jijini Dar es Salaam.
Taarifa hizo zilipofika Ikulu, Sabaya aliitwa na alishikiliwa kwa siku tatu ili atoe maelezo, lakini yeye mwenyewe anasema kilichomsaidia wakati ule ni hoja kuwa alikuwa akizitumia kununua madiwani na viongozi wa Chadema Jimbo la Hai.
Sabaya, ambaye huongea kwa kujidai na kujiamini mbele za watu, anasema kuwa alimweleza Rais Magufuli kuwa ni kweli alichukua fedha na ndizo alikuwa anazitumia kutekeleza mpango huo, na amemhakikishia Rais Magufuli kuwa atazitumia kumng’oa Freeman Mbowe kwenye ubunge jimbo la Hai, rais akamsamehe.
Sabaya amekuwa akitumia mamlaka yake ya ukuu wa wilaya kuwatisha wafanyabiashara kwenye mikoa ya kilimanjaro na hasa Arusha huku ambapo kwa wenye vituo vya mafuta hutumia mabavu kulazimisha magari yake matatu anayozunguka nayo yajazwe mafuta.
Hata hivyo tayari baadhi ya wafanyabiashara hao wameamua kutoa taarifa kwa mkuu wake wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mugwira ndipo akapunguza kuwatisha.
Sabaya amekuwa na kawaida ya kuongozana na mabaunsa wake na amekuwa akionekana kwenye maeneo mbalimbali ya starehe ila amekuwa na tabia ya kutokulipa bili mara baada ya kuanya matumizi.
“Sabaya akiingia hapa kila mtu hataki kumhudumia. Huwa anakunywa na kula lakini halipi. Unashangaa wanaanza kuondoka mabaunsa wake halafu yeye anakuwa wa mwisho kuondoka akiwa anaongea na simu hata ukimfuata mpaka kwenye gari anaendelea kuongea na simu huku gari inaondoka,” alisema mhudumu wa bar moja iliyopo maeneo ya Sakina.
Hadi tunaenda mitamboni, Sabaya hakupatikana kujibu hoja na tuhuma zinazomkabili. SAUTI KUBWA inaendelea kumsaka.