WILLIAM Ruto, Makamu wa Rais wa Kenya, amesema katika kuwania uongozi wa nchi hiyo mwakani hatapigana “vita vya nyama,” bali atazidisha maombi na sala kwa Mungu.
Ruto ameeleza haya leo kupitia ukurasa wake wa Twitter ikiwa ni njia ya kujibu mapigo ya Rais Uhuru Kenyatta ambaye ameweka wazi kwamba hatampigia kampeni msaidizi wake huyo kuwa kiongozi mkuu wa Kenya.
Kenya inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu mwaka kesho 2022. Rais Kenyatta hatagombea kwa sababu anang’atuka baada ya kuwa rais wa Kenya kwa mihula miwili. Katiba ya nchi hiyo inaeleza kwamba rais wake hawezi kugombea nafasi hiyo mara tatu mfululizo.
Akiambatanisha gazeti la The Star toleo la leo, Juni 15, 2021 katika kujibu msimamo wa Kenyatta kupitia Twitter, Ruto amesema: “…. sawa tu, tutajipanga na support ya Mungu.”
Katika habari yake kuu leo, gazeti hilo limeandika kwamba Rais Kenyatta atamuunga mkono na kumpigia kampeni mgombea yeyote atakayepitishwa na muungano wa vyama vya upinzani (NASA) dhidi ya Ruto.
Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, uhusiano wa Rais Kenyatta na Ruto umekuwa wa kutegeana, kuviziana na kupigana vijembe hadharani.
Hata katika shughuli za kiserikali, kila mmoja amekuwa akimwepa mwenzake, hata pale walipotarajiwa kuwa pamoja.
Kiini cha ‘ugomvi’ wao hakiko wazi, lakini wachambuzi wa siasa wanaeleza kuwa wawili hao walitofautiana mara tu Uhuru alipoanza kushirikiana na Raila Odinga, kiongozi wa upinzani ambaye kwa zaidi ya miaka mitatu sasa amekuwa kama ndiye mkono wa kuume wa Rais Uhuru.
Inavyoonekana, Odinga, ambaye Wakenya humwita “baba” – jina la utani kisiasa – bado ana nia ya kugombea tena urais kupitia NASA, na zipo dalili kwamba Rais Uhuru anajipanga kumpigia debe.