WACHEZAJI watatu wa timu ya soka ya taifa ya England, kwa siku tatu mfululizo, wameendelea kutukanwa, kudhihakiwa na kudharauliwa – kwa rangi ya ngozi yao – wakisakamwa kwamba “wameikosesha ushindi timu yao katika fainali za Kombe la Ulaya 2020 (Euro 2020).
Katika fainali za kombe hilo – michuano maarufu ya soka baada ya Kombe la Dunia – wachezaji wenye asili ya Afrika; Marcus Rashford, Jardon Sancho na Bukayo Saka, walikosa penati, hivyo England kukosa kombe dhidi ya Italia.
Mashabiki wengi, kutoka Uingereza, hasa Wazungu, wamekuwa wakiandika katika mitandao ya kijamii; Twitter, Facebook na Instagram wakiwalaani wachezaji hao, huku wakiwataja kuwa ni “nyani wasiofaa.”
Wachambuzi wa soka na wafuatiliaji wa mchezo huo wanaeleza kwamba wanaowatukana na kuwadhalilisha kwa kuwa na nasaba za Waafrika, wanasahau kwamba ni wachezaji haohao aliosaidia England kufikia fainali baada ya kushindwa kuingia hatua hiyo kwa miaka 55 mfululizo.
Tayari Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amelaani ubaguzi wa rangi uliojitokeza katika mitandao ya kijamii dhidi ya wachezaji hao na kueleza kwamba wanaofanya hivyo hawana ustaarabu.
Polisi nchini Uingereza imeanza kuchunguza matusi na maneno ya ubaguzi wa rangi yaliyoandikwa katika mitandao ya kijamii dhidi ya wachezaji hao.
Wachezaji hao walipoteza mikwaju ya penalti baada ya Italia na England kutoka sare bao 1-1 usiku wa Jumapili- Julai 11, 2021, mechi iliyochezwa katika uwanja wa Wembley mjini London mbele ya mashabiki 60,000.
Kupitia mikwaju hiyo ya penalti Italia iliibuka na ushindi kwa mabao 3-2 na kutwaa kombe hilo.
Katika mvutano uliokuwa na mashambulizi ya mara kwa mara wengi waliamini kwamba England ingeweza kushinda mechi hiyo, kwani walifanikiwa kupata bao la mapema kabisa dakika ya pili kupitia kwa beki kushoto wa Manchester United, Luke Shaw. Mbali na bao la mapema, England walikuwa na kikosi chenye uwezo mkubwa wa wachezaji wake, Harry Kane, Sterling, Marcus Rashford, Jason Sancho na wengine ikilinganisha na Italia ambayo kikosi chake kilikuwa na wachezaji wasiokuwa maarufu.
Katika hali ambayo haikutegemewa, Italia iliweza kurudisha bao dakiza ya sabini kupitia beki wa Juventus Leonardo Bonucci na kuwapa hofu mashabiki wa England.
Rekodi zinaonyesha kwamba England haiwezi “kufua dafu” dhidi ya Italia, kwani imekuwa ikipata shida kuifungwa kila wanapokutana uwanjani.
Kutokana na England kusubiri finali hizo kwa muda mrefu bila kufika finali, wengi waliamini wakati wa zamu yao kubeba kombe hilo ulikuwa umefika, kumbe haikuwa hivyo.
Moja ya picha ya mchezaji wa Manchester United, Rashford iliyochorwa katika kuta kama ishara ya kuenzi juhudi na msaada anayotoa kwa watoto wenye uhitaji Uingereza, iliandikwa matusi na maneno mengi ya kibaguzi juu yake.
Hata hivyo, baadhi ya watu wanaopinga vitendo hivyo vya kibaguzi na udhalilishaji walifunika matusi hayo kwa stika za picha zenye alama ya upendo pmoja na maneno ya faraja kwa nyota huyo.
Katika ukurasa wake wa Instagram, Rashford aliandika – “Sikutegemea kama ningeweza kukosa penati hasa penati muhimu kama ile ambapo tumesubiri miaka 55 kucheza finali. Nimekuwa nikifunga penati hata ndotoni, sasa inakuwaje nakosa hii ambayo ni muhimu zaidi? Pengine ni uwoga kwani nilikuwa na msimu mbaya na klabu yangu na ule uwezo wa kustahimili uwoga sikuwa nao. Naombeni mnisamehe sana sana”
Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limesema linalaani na kwamba linafanya uchunguzi kwa watu wanaohusika na ubaguzi huo kwa njia yoyote ile ili kuona namna nzuri ya “kuwashughulikia.”