Prof. Tibaijuka amwangukia Samia juu ya umaskini wa mkoa Kagera

PROFESA Anna Tibaijuka, aliyekuwa Mbunge wa Muleba Kusini (2010-2020) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (2010-2014), amejitokeza “kulilia” mkoa Kagera, akimsihi Rais Samia Suluhu autazame “kwa jicho la huruma.”

Akisisitiza hoja yake, huku akinukuu ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania, Prof Tibaijuka ameieleza SAUTI KUBWA kuwa, “hizi ni facts, si siasa.”

Andiko lake fupi linalochambua hali halisi ya umaskini wa mkoa Kagera, linasema:

Kagera. TWAFA. Tumuombe Rais Samia atuangalie kwa jicho la huruma, la mama mzazi.

 1. Mwaka 1961 tukipata uhuru Kagera ulikuwa mkoa wa pili kwa maendeleo baada ya Kilimanjaro. Sasa hivi miaka 60 baada ya uhuru ni mkoa wa mwisho Tanzania Bara. Nambari 25.
 2. Taarifa rasmi za Benki kuu..(Consolidated Zonal Economic Performance Report) Inaorodhesha pato la taifa kwa kila mkoa kwa kila mwananchi au kichwa (per capita GDP) kwa Tanzania bara.
 3. Kwanza ni Dar es Salaam. Shs 4,678,751. Mwisho namba 25 ni Kagera Shs 1,168,661.
 4. Kwa asilimia kipato cha mwananchi mkoa wa Kagera ni asilimia 44% tu ya kipato cha Taifa.
 5. Na asilimia 25% au robo ya kipato cha wakazi wa Jiji Kuu la Dar es Salaam.
 6. Ukilinganisha na Makao makuu Dodoma (Shs 1,759,347) Kagera ina asilimia 66% au theluthi mbili.
 7. Hali ni tete. Kaya maskini nyingi hata mlo ni wa kubahatisha katika hali ya kawaida. Ukiingiza ukame inakuwa zahama.
 8. Tukubali mkoa slowly but surely umefilisika. Tunahitaji kufanya tathmini ya kina kuona tunajikwamua vipi. Nini kazi ya Serikali? Nini jukumu la WanaKagera. Na kipi Mhe Rais wetu Mama Samia atuwekee nguvu?. Mambo yalipofikia tunahitaji mbinu zote na mikakati mipya kubadilisha hali hii isiyopendeza.
 9. Lazima kumwangalia adui umaskini machoni na kupambana naye.
  Tukikata tamaa au kulaumu hatutafanikiwa.
 10. Kinachohitajika ni utambuzi na uelewa wa pamoja wa sababu za kufilisika kiasi hiki ili kurekebisha mambo. TUNAWEZA. KUJIKWAA SI KUANGUKA. Ila lazima tujipange. Kila mtu kwa nafasi yake.
 11. Baba wa Taifa Mwl Julius Nyerere alisema: “It can be done. Play your part.”
 12. Ninawapongeza waheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kupanga safu ya uongozi upya. Tumeshuhudia maboresho makubwa. Tunawapongeza mawaziri na makatibu wakuu na manaibu wote walioaminiwa na kupewa majukumu ya kuongoza sekta mbali mbali. Ninaomba nao waangalie hii hali tete ya mkoa. Twafaaa… Tunahitaji msaada.

Na wenzetu wa Kigoma nambari 24.( Shs 1,479,389); Singida nambari 23. (Shs 1,622,891) sina budi kuwasemea pia. Kwa ujumla wetu: TWAFAAA.

KAZI IENDELEE katika mwaka huu wa OTAGWISA MUKONO.

Like
2