Prof. Baregu kwanini umeondoka kabla hatujamaliza ugomvi wetu?

TANZIA hii imeandikwa na SIMON MKINA, mhariri mtendaji na mmiliki wa gazeti la Mawio. Endelea.

JANA Juni 13 asubuhi, nimepokea taarifa za kifo chako nikiwa bado kitandani; nimejilaza kwa mapumziko na siyo kwa ugonjwa. Mke wangu, Jacqueline akanijuza kuhusu kuondoka kwako hapa juu ya uso wa dunia.

Nilipigwa butwaa na kuuliza – ni Baregu yupi? Wewe Profesa wangu? Wewe uliyenilea kwenye maeneo ya sayansi ya jamii, siasa, utawala na historia; ndani na nje ya vyuo vikuu?

Ni wewe uliyekuwa tukikutana maeneo ya Kunduchi; Dar es Salaam, kwenye bustani, nje kidogo ya nyumba yako na kujadili mambo mengi ya binafsi, nchi na dunia – huku tukipata  kinywaji chetu?

Ni wewe ambaye mara zote nikikusumbua kwa simu kupata maoni yako kuhusu jambo hili ama lile kwa ajili ya kuchapisha gazetini?

Je, ni wewe ambaye hukusita kueleza mawazo yako huru bila woga, bila kujikomba kwa yeyote, bila kumung’unya maneno kwa yale uliyoamini bila kujali nani anayafurahia ama kuyabeza?

Je, ni wewe uliyependa kutunza nywele kichwani na hata zile zinazozunguka kidevu chako? Uliyependa kuvaa bangili mkononi na makubazi?

Maswali yalikuwa mengi mno. Akili yangu iligoma kukubali haraka kwamba unaweza kuondoka kipindi hiki ambacho nchi inakuhitaji zaidi ili kuponya majeraha mengi yaliyoletwa na mazingira ya siasa ya hovyo ambavyo hatukuwahi kuyazoea tangu Tanganyika kupata uhuru wake.

Hakika maswali yalikuwa mengi na itoshe kueleza tu kwamba sikupata majibu yake hadi nilipompigia binti yako Kokuteta, lakini hakupokea simu ila ikapokelea na binti yake, mjukuu wako – Sara na kuthibitishwa kwamba “umenondoka na kwamba tayari wewe ni mgeni wa Mungu.”

Kauli ya Sara ikaleta majibu ya maswali yangu kwamba hakika – Ni wewe.

Ghafla macho yangu yakajaa machozi. Mengine yakitiririka juu ya mashavu na kutengeneza michirizi kuonyesha namna uhai na elimu yako vilivyogusa maisha ya idadi kubwa ya watu; ndani na nje ya Tanzania.

Nilikulilia asubuhi na ninaendelea kulia napoandika makala haya ya tanzia. Kilio changu – nikiamini ni taswira ya kilio cha watu wengine wengi, ambao uhai wako na elimu yako umegusa.

Kilio cha wengi, kama ambavyo nimesoma kwenye mitandao ya kijamii, hasa Twitter, ni dhahiri kwamba maisha yako yaligusa watu wengi na kuwabadilisha. Wengi umewafunza darasani na sasa ni nguzo muhimu kwa maeneo ya nchi yetu Tanzania.

Wapo wengi walioandika kukulilia, lakini hawa wachache ambao ni rafiki zangu, wanawakilisha jumuia kubwa ya watu waliofaidika na uwepo wako hapa duniani.

Mmoja wao ni msaidizi wa Rais wa Awamu ya Nne wa Tanzania – Jakaya Kikwete, Togolani Mavula, ambaye kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika; “ulale mahala pema Prof Baregu, nitaendelea kukumbuka kwa ile dhana uliyonifundisha pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu mlinganyo wa ‘mshiriki, maslahi na mkakati’ katika kuchambua na kutafuta suluhu kwenye mgogoro wowote. Pole sana.”

Rafiki yangu mwingine, Zitto Kabwe, Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo anamuelezea Prof Baregu; “Msiba wa Prof. Mwesiga Baregu ni mzito sana. Hakika mchango wake mkubwa katika ujenzi wa demokrasia ya nchi yetu na haswa katika mchakato wa Katiba ambayo yeye alikuwa Mjumbe wa Tume ya Katiba, utakumbukwa daima. Alikuwa Mwanazuoni wa mmma na mhadhiri mahiri! Huzuni.”

Mwingine aliyemlilia Prof. Baregu ni John Elijah wa Dar es Salaam, ambaye anasema; “Prof Baregu alielewa haswa wapi tupo katika siasa za nchi hii. Alielewa pia mwelekeo unaotakiwa kufuatwa ni upi ikiwa kweli tuna dhamira njema ya kisiasa ya kujenga taifa lisilomilikiwa na dola. Safiri salama Profesa Baregu.”

Pamoja na kilio cha hawa Rafiki zangu, binafsi nitakulilia zaidi Prof. Baregu kwa kuwa umeondoka kabla hatujamaliza ugomvi wetu. Ni ugomvi wa hoja. Ni ugomvi wa kutokubaliana kukubaliana.

Kwamba tukiwa darasani – Chuo Kikuu cha St. Augustine, Kampasi ya Dar es Salaam, wakati wa mafunzo ya shahada ya uzamili, Prof. Baregu ulitoa zoezi kwa kila mwanafunzi kuunda serikali yake. Kila mmoja baada ya wiki alipata fursa ya kuwasilisha mbele ya darasa. Ilipofika zamu yangu nilijongea mbele ya wenzangu na kuanza kuwasilisha.

“Nchi yangu itaitwa X (tamka Eksi); haitakuwa na jeshi; haitakuwa na polisi; haitakuwa na magereza; haitakuwa na benki. Atakuwepo rais, waziri mkuu na mawaziri sita. Kila waziri atakuwa ndiye mkuu wa mkoa na Ofisi ya Ikulu atakuwepo rais na waziri mkuu,” wakati nikiendelea, Prof. Baregu ulinikatiza. Ukasema; “sijawahi kusikia nchi kama hii, wewe subiri utakuwa wa mwisho kuwasilisha.”

Nilisubiri hadi walipomaliza wote nikajongea mbele kuelezea na kufafanua zaidi kuhusu nchi nitakayounda.  Maswali yalikuwa mengi kuhusu nchi X na haukubaliana na muundo wa nchi hiyo pamoja na kwamba ulinipa alama za juu zaidi kuliko wengine.

Baada ya darasa, uliomba lifti kweye gari yangu kwa kuwa njia unayopita ndiyo naitumia kila mara ninapokwenda kwenye mihangaiko yangu.

Tukiwa ndani ya gari uliendelea kushikilia msimamo wa kutokubaliana na muundo wa nchi X. Nami sikushawishika kwa hoja zako. Hivyo basi, nchi X ikabaki kuwa somo la kwanza kila napokutana nawe.

“Wewe Simon Martha Mkina, hiyo nchi yako haiwezi kuwepo, achana nayo. Unda nyingine,” hii ndiyo ikawa salamu yangu kila unaponiona kijana wake; iwe kanisani, kwenye vijiwe, migahawani na popote.

Naamini hata huku ulipo sasa, tukikutana, utalianzisha tu. Nami sitakubali kubadilika. Kila mmoja abaki na lwake.

Ewe mwalimu wangu – Profesa Mwesiga Baregu; mwanazuoni mahiri, msomi uliyeelimika, mwerevu na mfuasi-mchambuzi wa imani za Karl Marx, Thomas Hobbes, Frederick Angels, John Locke, Marchieveli na wengineo lala salama sasa. Tutaonana baadaye!

·Mwandishi anapatikana kwa namba +255754 020 880.

Like
1