Polisi Dar washikilia vichanga 21 kwa ‘mafundisho ya imani kali’

WATOTO wadogo 21 wenye umri wa kati ya miaka mitatu (3) na 11, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, Dar es Salaam, Tanzania kwa kukutwa ndani ya nyumba moja jijini Dar es Salaam, wakipewa mafunzo yanayodaiwa kuwa ya “imani kali ya Dini ya Kikristo.”

Gazeti la SAUTI KUBWA liligundua kuwepo kwa idadi kubwa ya watoto wanaoingia na kutoka katika nyumba moja Mtaa wa Kivule, Kata ya Majohe, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam na kufuatilia kwa mwenyekiti wa mtaa huo ambaye naye kwanza hakuwa na habari za kinachoendelea ndani ya nyumba hiyo.

Jana mwenyekiti wa mtaa huo, Ally Mzava Daudi, alifika katika nyumba hiyo na kuomba kuonana na mwenye nyumba, lakini alizuiwa na mtu mmoja aliyejitambuisha kuwa ni Lyimo, akieleza kwamba watu wasiojulikana kwake au kwa familia yake, hawaruhusiwi kuinga ndani.

Daudi alisisitiza kwamba ana mamlaka ya kujua nini kinaendelea katika nyumba hiyo kwani yeye ni mwenyekiti wa ulinzi na usalama wa eneo hilo, na kwamba ana shaka na shughuli zinazofanyika ndani ya nyumba hiyo – kwa kuwa siyo shule wala chuo kinachotambulika ofisini kwake.

Baada ya mabishano ya muda wa zaidi ya nusu saa, Lyimo na watu wengine wawili, waliojitambulisha kwau walimu wa dini, walimruhusu kuingia na ndipo ndani alikuta watoto hao wakiwa ‘darasani.’

Kiongozi huyo alihoji wanachofundishwa watoto hao na kama ni shule, kwanini haijasajiliwa na kupewa uhalali na serikali, lakini Lyimo alimjibu kwamba hapo ni shule ya watoto wanaofunzwa imani halisi ya Mungu.

“Hapa wanafundishwa imani ya kweli ya Yesu Kristo, tena Yesu alivyoagiza ndiyo tunafundisha, hatutaki raha za shetani ambazo zinaleta maangamizi kwa binadamu,” alisema Lyimo.

Lyimo alisema kwamba wanawafunza watoto kujiandaa na safari ya eneo alilolitaja kuwa ni mbinguni ambako watakutana na mtu aliyemtaja kuwa ni Yesu.

Alisema yeye na wenzake na Watoto hao hawafuati mapokeo ya dhehebu lolote, isipokuwa wana kanisa lao maalum linalopigania ukombozi wa Dunia na mapenzi ya Yesu linaloitwa; Jumuia ya Kristo.

“Madhehebu mengine yote ni ubatili na yanaungana na shetani kuangamiza watu, ndiyo maana kila kitu niwe kanisani, maofisini na hata kwenye familia, maisha yametawaliwa na yule mwovu mwenye alama ya 666 kichwani kwake,” alisema Lyimo na kuongeza kwamba matumizi ya umeme, simu, dawa za hospital ni ushetani na chukizo kwa Mungu.

Katika nyumba hiyo, SAUTI KUBWA imegundua kwamba haina umeme, walimu wake wala mmiliki, hawana simu.

Baada ya kupata maelezo haya “yaliyomuogopesha”, kiongozi wa Mtaa wa Kivule, Ally Mzava Daudi, aliita Jeshi la Polisi ili kufuatilia zaidi. Polisi wa Kituo cha Sitakishari walifika jana hiyohiyo na kuwachukua watoto hao, mmiliki pamoja na walimu wawili.

Polisi waliwahoji watoto, walimu wao pamoja na Lyimo, ambao waliendelea na msimamo wao kwamba wanafundisha watoto utayari na ruhusa ya kufika “mbinguni kwa Yesu.”

Jeshi la Polisi lilianza mchakato wa kuwapata wazazi wa watoto hao, lakini ni wachache waliojitokeza, hivyo uamuzi wa kuwanza watoto hao hapo kituoni ulitolewa.

Leo, Jeshi la Polisi limeendelea kuwaita wazazi hao na kuwahoji sababu za kuruhusu watoto wao kujiunga na kundi la mafunzo “yasiyoeleweka rasmi.”

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alipohojiwa  na SAUTI KUBWA alisema kwamba, pamoja na kwamba haijamfikia rasmi, ana imani upelelezi unaendelea na kuwa endapo atapokea taarifa rasmi, basi umma utajulishwa.

Kundi hilo la “imani Kali ya Kikristo,” linataka kufanana na kundi jingine lililokuwa likijiita Dhehebu la Waadventista Wasabato Masalia, katika Jiji la Dar es Salaam, lilikuwa na imani Kali kwamba wafuasi wake hawapaswi kukaa Tanzania na kuwa makazi yao ni Marekani na lilikuwa likijiandaa kwenda nchini humo bila kuwa na viza wala nauli ya ndege.

Kundi hilo la Wasabato Masalia, lilikusanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kuweka kambi kwa siku nne – kuanzia Septemba Mosi hadi 3, 2008, huku wakisali na kuomba kuanza safari ya Marekani bila mafanikio hadi walipotimuliwa na Jeshi la Polisi.

Like
2