KUPOROMOKA kwa bei ya pamba, ni moja ya hoja kuu zinazotumiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuonesha udhaifu wa kiuongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kunadi sera mbadala za kuboresha kilimo na biashara ya zao hilo nchini.
Viongozi wakuu wa CHADEMA wamezungumzia zaidi pamba katika mikutano yao ya Oparesheni +255 iliyofanyika kwenye mikoa ya Geita, Mwanza na Shinyanga, na inayoendelea sasa katika mkoa wa Simiyu, wakijenga hoja mbalimbali kuhusiana na anguko la uchumi wa Pamba.
Jana, akihutubia maelfu ya wananchi wa Bariadi, mkoani Simiyu, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama hicho, alisema moja sababu zinazosababisha bei ya kuuzia pamba kuzidi kuporomoka nchini ni kuuliwa, kuuzwa na kubinafsishwa kiholela kwa viwanda vya nguo nchini vilivyoanzishwa na serikali ya awamu ya kwanza, chini ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Wakati wa Mwalimu, pamba ya Wasukuma ilikuwa na thamani sana kwasababu, siyo tu tulikuwa na viwanda vidogo vidogo vya kuchakata pamba (cotton gineries), lakini pia tulikuwa na viwanda saba vya nguo. Hapa Mwanza tulikuwa na kiwanda cha Mwatex, Musoma tulikuwa na Mutex, Morogoro tulikuwa na Morogoro polytex, Arusha tulikuwa na Kilitex, Mbeya tulikuwa na Mbeyatex, Dar es Salaam tulikuwa na Urafikitex, Sunguratex”, alisema Mbowe na kuongeza:
“Tulikuwa tunauza nguo mpaka nje ya nchi. Lakini wakashindwa kuendesha viwanda walivyoachiwa na Mwalimu. Wakavibinafsisha kiholela.Vingi vimekufa au kuanguka katika uzalishaji. Wamesababisha Tanzania kuwa Taifa la wavaa mitumba. Hapa karibu wote tumevaa mitumba. Pamba ya msukuma imeporomoka bei, imekosa soko na wengine wameacha kabisa kulima pamba kwasababu haiwalipi.”
Taarifa zinaonesha kuwa bei ya pamba imeporomoka kutoka Shilingi 2,040 mwaka uliopita hadi kufikia shilingi 1,060 kwa kilo moja hivi sasa.
Aidha, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Magu mjini, mkoani Mwanza, Mwanasiasa huyo alisema, mbali na kuuwa viwanda vya nguo, CCM pia imeuwa benki muhimu za Taifa zilizoanzishwa kwaajili ya kusaidia wakulima na wafanyabiashara.
“Nchi yetu ilikuwa na mabenki. Benki kama CRDB ilianzishwa kama benki ya ushirika ya kusaidia mahitaji ya kilimo ikiwemo kununua pembejeo, lakini serikali zilizofuata baada ya Mwalimu zikabinafsisha. NBC ilikuwa ni benki ya Taifa ya Biashara na NMB ilikuwa sehemu yake. Nazo wakashindwa kuziendesha, wakazibinafsisha. Matokeo yake leo hakuna benki ya uhakika ya kusaidia wakulima” alisema Mbowe.
Mbowe alisema sera ya Chadema ni kufufua na kuanzisha viwanda vyote muhimu vya kuchakata mazao ya kilimo na mifugo ikiwemo viwanda vya nguo.
“Watanzania tupo milioni 64, lakini wengi wanavaa mitumba. Idadi hii kubwa ya watu, ilipaswa kuwa soko la kwanza la pamba yenu mbali na soko la nje. Chadema tutafufua na kuanzisha viwanda vya nguo. Bei ya pamba itapanda, wakulima wataongeza vipato na ajira zitaongezeka,” alisema Mbowe na kuibua shangwe kutoka kwa wananchi waliofurika kwenye mkutano huo.
Kwa upande wake, Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, jana akihutubia wananchi wa Bariadi, alisema sababu nyingine kubwa ya kuporomoka kwa bei ya kuuzia pamba ni kuwepo kwa ‘Genge la Wabunge na Vigogo wa CCM waliojiingiza kwenye mnyororo wa kupanga bei na kununua pamba’, huku akijenga hoja kuwa bei ya pamba haiwezi kupanda kwasababu wabunge waliopaswa kuwatetea wakulima ndiyo hao hao wanaonufaika na bei ndogo ya kununulia pamba.
“Anayenunua pamba hapa Bariadi ni Njaru Silanga, mbunge wa Itilima. Mbunge wa Ushetu, anaitwa Cherehani, ni mnunuzi wa pamba hasa kwa pamba inayotoka wilaya ya Kishapu. Luhaga Mpina, mbunge wa Kisesa, naye ni mnunuzi wa pamba. Halafu Christopher Gachuma, mjumbe wa halmashaur kuu ya CCM (NEC) ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Pamba. Bodi ya Pamba ndiyo inayopanga bei. Sasa unashangaaje bei ya pamba kuporomoka?. Bei ni ndogo kwasababu kuna ‘chain’ (mnyororo), kuna genge la makupe linalo wanyonya wakulima. Ni genge la ma-CCM.Hawawezi kupandisha bei ya pamba kwasababu utajiri wao unategemea umaskini wenu,” alisema Lissu na kushangiliwa na wananchi.
Akirejea historia ya kilimo cha pamba, Lissu alisema wakati wa ukoloni wafanyabiashara hasa wa wa asili ya Kihindi, walikuwa wakiwanyonya wakulima kwa kununua pamba kwa bei ndogo.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa jamii ya kisukuma wakiongozwa na Paulo Bomani wakaamua kuanzisha Shirikisho la Vyama vya Ushirika lililoitwa Victoria Nyanza Federation, na shirikisho hilo likaanza kufanya kazi ya kuwezesha wakulima wa pamba kwa kuwapatia pembejeo na kununua pamba yao kwa bei nzuri inayowalipa.
Alisema shirikisho lilifanya kazi kubwa ya kunyanyua uchumi wa pamba ikiwemo kujenga shule mbalimbali zilizosaidia watoto kutoka familia za wakulima wa pamba kupata elimu bora.
“Malampaka, Maswa, Luguru, kote kulikuwa na gineries (viwanda vidogo vya kuchakata pamba). Walijenga mashule kila mahali. Pamba ndiyo ilikuwa mkombozi wa usukumani,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa Paulo Bomani, kupitia Shirikisho hilo la wakulima wa Pamba, ndiye aliyetoa fedha zilizomwezesha Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kusafiri kwenda umoja wa Mataifa (UNO) kupigania uhuru wa Tanganyika, kwani Mwalimu hakuwa na fedha maana alifukuzwa kazi ya ualimu mwaka 1955 kwasababu ya kujihusisha na siasa.
Hata hivyo, alisema, Shirikisho hilo lilivunjwa na Nyerere mwaka 1966 na kuanzishwa Bodi ya Pamba, bodi ambayo alisema imekuwa haifanyi vizuri kwasababu ya kuendeshwa na watu aliowatuhumu kuwa wanajali tu mishahara yao na maslahi yao binafsi badala ya kusaidia wakulima.
Lissu amewaomba Watanzania wa mikoa yote ya kanda ya ziwa, kuachana kabisa na CCM na kujiunga Chadema, huku akiahidi kuwa Chadema itafanya mageuzi makubwa ya kuboresha kilimo na biashara ya mazao yote ya biashara ikiwemo pamba, kahawa na tumbaku.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chadema upande wa Tanzania Bara, Benson Kigaila, akizungumzia Pamba, katika mikutano mbalimbali iliyofanyika kwenye jimbo la Maswa Magharibi na Itilima, mkoani Simiyu, alisema sababu nyingine ya wakulima wa pamba kulipwa pesa kidogo wanapouza pamba yao, ni kuwepo kwa makato mengi, yakiwemo ya pembejeo za kilimo, ada kwa vyama vya msingi (AMCOS), pamoja na tozo na ushuru, ambavyo kwa pamoja, hufikia makato hayo ni zaidi ya Shilingi 1,000 kwa kila kilo moja ya pamba.
Kigaila alisema makato yote hayo yanamuumiza mkulima kwa kufanya apate shilingi 1,060 tu hivi sasa kwa kila kilo moja ya pamba, wakati angeweza kuuza kwa zaidi ya shilingi 2,000.
Akifafanua zaidi alisema makato hayo si halali, bali ni mbinu tu ya serikali kujipatia fedha kwa kumnyonya mkulima.
Kigaila alifafanua zaidi akisema:
“Kwa mfano, wanawakata Shilingi 300 kwenye kila kilo moja ya pamba, wanadai ni makato ya kuwaletea mbolea na pembejeo za kilimo. Wanapowakata Shilingi 300 kwa kilo, maana yake, kwa tani 3 za Pamba, kila mkulima anakuwa amekatwa shilingi 600,000. Na kwa tani 10 za Pamba, kila mkulima atakuwa amekatwa Shilingi Milioni Tatu.Je, kuna pembejeo mkulima anapewa zinazofikia gharama ya Shilingi Milioni Tatu? Hakuna eeh
“Serikali ya CCM inawaibia fedha zenu za Pamba. Huu ni wizi..Wanawaibia kwenye Pamba na wanawaibia kwenye mradi wao wa kumvalisha kila ng’ombe hereni kama wasichana. Ni wezi. Achaneni kabisa na CCM. Tunawaomba mjisajili kwa wingi kuwa wanachama wa Chadema ili muweze kujikomboa kwa kuiondoa CCM madarakani na kukomesha wizi huu,” alisema Kigaila.
Mbali na kuporomoka kwa bei, kilimo cha pamba kinakabiliwa na tatizo la kuwa na tija ndogo ya uzalishaji, ambapo kwa wastani wakulima huvuna kati ya kilo 200 mpaka 300 kwa ekari moja.
Uzoefu wa nchi nyingine kama Brazil unaonesha kuwa wanavuna mpaka kilo 3,000 kwa eneo la ekari moja, tija ambayo ni kubwa kwa zaidi ya mara kumi ya Tanzania.
Tija ndogo katika uzalishaji inasababishwa na huduma duni za ugani na wakulima kukosa pembejeo stahiki za kilimo, husani kukosa mbegu bora na mbolea, huku ruzuku ya mbolea inayodaiwa kutolewa na serikali, ikiwa haifikii walengwa wengi wala kukidhi haja ya malengo yao ya kilimo.