Maridhiano njia panda

Mbowe, Lissu wampa tahadhari Samia

– Washtukia njama za kuchelewesha katiba mpya

MAZUNGUMZO baina ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Serikali, na Chama cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake, yaliyochukua takribani mwaka mmoja, yakijaribu kutafuta muafaka wa kitaifa hususan kwenye suala la katiba mpya, sasa yanaelekea kuwa njia panda, baada ya pande hizo mbili kutofautiana hadharani kuhusu ratiba ya kupatikana kwa katiba mpya.

Wakati serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro, ikisema watatoa kwanza elimu ya katiba ya sasa kwa muda wa miaka mitatu, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti Bara wa Chama hicho, Tundu Lissu, wamepinga vikali ratiba hiyo, huku wakiweka wazi kuwa hizo ni njama za makusudi za kuchelewesha kupatikana kwa katiba hiyo.

Tofauti hizo zimejitokeza, huku kukiwa hakuna taarifa yoyote kuhusu kuwepo kwa mwendelezo wa mazungumzo hayo.

Akihutubia maelfu ya wananchi wa Jimbo la Bariadi, Mbowe, alisema:

“Nilimwambia Rais Samia, kwamba huwezi kuongoza nchi hii kwa kupuuza vyama vingine na kwa kupuuza sauti kutoka nje ya Chama na serikali yako. Tukaingia kwenye maridhiano.

“Tukawapa muda wa kutosha.Sasa wanafikiri sisi ni waoga.Wanataka kuchelewesha katiba mpya. Aliyekuwa waziri wake wa katiba eti anasema wanatoa kwanza elimu ya katiba kwa miaka mitatu. Nani hapa asiyejua haki zake mpaka apewe elimu ya katiba? Jambo hili la kuchelewesha katiba mpya halikubaliki.”

Alisisitiza kuwa kuanza tena kutoa elimu ya katiba ni ufujaji wa fedha za umma, kwani kazi hiyo ilishafanywa na kukamilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba.

“Katiba siyo mali ya Rais, wala hatuhitaji khisani ya Rais kuipata katiba mpya. Sasa wasije wakatulaumu. Tukiamua kukiamsha tunaweza, wala hakuna polisi watakaotosha kuzuia. Ipo siku inakuja…na siku hiyo haipo mbali.Tunataka mchakato wa kupata Katiba Mpya uanze sasa,” alisema Mbowe na kushangiliwa.

Awali, Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Tundu Lissu, alisema, ili kudhibiti uuzaji, ugawaji na ubinafsishaji holela wa raslimali za nchi, ikiwemo bandari, misitu na hifadhi za wanyama pori kama Ngorongoro na Loliondo,
Watanzania wana kazi kuu mbili za kufanya, ambazo ni kuhakikisha katiba mpya inapatikana kuanzia sasa na pili ni kuiondoa CCM madarakani.

Akitoa mfano, alisema katiba ya sasa si tu imemfanya Rais kuwa mdhamini wa ardhi na maliasili za umma, lakini pia imempa kinga ya kutoshitakiwa, hali inayoiweka nchi kwenye hatari ya kushindwa kuiwajibisha serikali.

Like