ALIYEKUWA mkufunzi mkuu wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amefutwa kazi dakika chache zilizopita.
Bodi ya klabu ya Manchester united ilikutana baada ya mchezo wa jumamosi jioni kati ya Watford na Manchester United, uliomalizika kwa United kulazwa na viatu kwa kupigwa bao 4-1.Makubaliano ya mkutano huo yalikuwa ni kwamba matokeo hayakuwa yakiridhisha na hivyo hayakubaliki.
Uamuzi huu, unamfanya aliyekuwa mkufunzi msaidizi wa Ole, Michael Carrick kurithi jukumu la ukufunzi mkuu kwenye mchezo wa United dhidi ya timu ya Villarreal siku ya Jumanne.
Gazeti la The Independent limeripoti kuwa Ole mwenye umri wa miaka 48 alikuwa akifahamu kuwa amekalia kuti kavu hasa baada ya kipigo kizito kutoka kwa Watford hapo jana. Viongozi na baadhi ya wachezaji waliamini kuwa mabadiliko yalikuwa yakihitajika klabuni hapo kwa muda sasa.
“Kama walivyo mashabiki, nimeumia pia kwa matokeo haya ya leo, ni aibu kupoteza mchezo kwa namna hii.” Alisema Ole baada ya mchezo dhidi ya Watford ambao ndio umekuwa mchezo wa mwisho kwa Mnorway huyo kuinoa United.