Kesi ya Mbowe: Uamuzi wa Jaji kukataa pingamizi wageuka faida upande wa utetezi

Kielelezo cha mwaka 2020 chakutwa na maelezo ya mwaka 2021. Shahidi wa mashitaka ajikanyaga 

Kama ilivyowasilishwa na ripota raia BJ leo tarehe 22 Novemba 2021.

Jaji ameingia mahakamani

Wakili wa Serikali Pius Hilla anawatambulisha mawakili wa Jamhuri

  1. Esther Martin
  2. Nassoro Katuga
  3. Jenitreza Kitali
  4. Tulimanywa Majige
  5. Ignasi Mwinuka

Wakili Peter Kibatala anatambulisha mawakili wa upande wa utetezi.

  1. Nashon Nkungu
  2. John Malya
  3. Dickson Matata
  4. Seleman Matauka
  5. Sisty Aloyce
  6. Maria Mushi
  7. Hadija Aron

Jaji anaita majina ya washtakiwa wote wanne. Nao wanaitika.

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Shauri lilikuwa kwa ajili ya kupokea uamuzi na tupo tayari kuendelea na shauri.

KIBATALA: Na sisi pia Mheshimiwa Jaji, shauri lilikuwa kwa ajili ya uamuzi mdogo. Kwa ruhusa yako tupo tayari kuendelea na shauri.

JAJI: Tarehe 18 Novemba Mahakama hii iliahirisha kesi hii wakati shahidi akiwa anatoa ushahidi wake. Mahakama inatoa uamuzi kama ninavyosoma sasa.

JAJI: Wakati wa shauri hili dodo shahidi alikuwa anatoa ushahidi kuhusu kuchukuliwa maelezo ya onyo. Shahidi aliomba kutoa kielelezo ambacho ni Detention Register ambayo alitumia siku anawapokea watuhumiwa namba 2 na namba 3. Walipofikishwa kwake na shahidi namba 1 na shahidi namba 4, kwa maana ya ACP Kingai na ASP Jumanne, wakati anakitoa upande wa utetezi walipinga, kwamba, 1. palikuwa hakuna Disposal Order

  1. Mahakama ilikuwa inazuia kwa sababu ilishakijadili Functus Officio, kwamba jambo ambalo limeshajadiliwa Mahakamani upande wa mashitaka wanazuiwa kurudisha tena mahakamani. Upande wa utetezi waliwakilishwa na Jeremiah Mtobesya na Peter Kibatala. Kwa upande wa mashitaka waliwakilishwa na Abdallah Chavula na Pius Hilla. Kwa kutokurudia Mahakama itazungumzia kwa pamoja hoja zote. Kwa kuanza upande wa utetezi walisema kwamba hakuna Disposal Order.

JAJI: Kwa kupitia kifungu cha 353 wakasema kwamba kwa Mahakama kutoa kielelezo ni kwa njia pekee ya Disposal Order. Na kwamba kielelezo ambacho kinaombwa kuingia kilishatolewa Mahakamami na kwamba Jaji alikuwapo au aliyemrithi hakuna sehemu yoyote ambayo wametoa Mahakamani Disposal Order, na kwamba suala la kutoa
kielelezo Mahakamani linatakiwa kuwa shirikishi na lifuate taratibu za utawala na tatu lazima utoaji wa Disposal Order ufanyike kwenye mwenendo wa wazi. Kwa Naibu Msajili kutoa kielelezo pasipo amri ya Mahakama ni kukiuka misingi na wakaomba basi mahakama isipokee kielelezo, wakasema haitoshi palipaswa kuwa na Register ya DISPOSAL ambapo kwa mujibu wa mwongozo wa Jaji Mkuu unavyosema, na kwamba Mahakama iangalie katika mwongozo katika sehemu ya 4:4.

JAJI: Na hoja ya pili kuhusu Mahakama kuwa Funtus Officio, wakiomba kwamba kwa sababu Mahakama Ilishatoa maamuzi, katika kesi ndogo ndani ya shtaka kubwa, basi Mahakama ione kwamba pale ambapo Mahakama ilishatoa maamuzi haiwezi tena kujadili kuhusu kielelezo hicho. Na kwa sababu Mahakama Ilishaletewa kielelezo hicho na ikakikataa, na kwamba shahidi namba moja alishaletewa na kwa ajili ya utambuzi haijalishi … wakaomba Mahakama irejee kesi mbalimbali, Theresia Zackaria vs Oscar ukurasa wa nne, NBC & IMMA Advocates vs … ya Mahakama ya Rufaa, issue ya Estoppel kwamba waliiomba Mahakama ione kwamba upande wa mashitaka hauwezi kuleta jambo hilo kisheria. Estoppel asili yake ni madai lakini iliingizwa kwenye a kesi za jinai.

JAJI: Kwa kesi Issa Tojo mbele ya Jaji Mkuu wa wakati huo Jaji Samata, alisema kwamba kanuni ya Estoppel ni sehemu za sheria zetu, na wakasisitiza kupitia kesi ya Julius Michael vs Jamhuri ambapo Mahakama … na kufanya maamuzi, ambapo Mahakama iliombwa kurejea ukurasa wa 6 mpaka 9. Waliomba Mahakama ione kwamba suala la … Detention Register lilishajadiliwa na halitakiwi kuletwa tena mahakamani. Lengo la kanuni hiyo ni kufanya mfumo wetu wa jinai kuwa mfumo uliokamilika. Na kwamba mshitakiwa asiitwe tena Mahakamani kulinda heshima ya Mahakama na masuala ya uchumi. Kwa maana hiyo wakaomba Mahakama kuona kwamba kanuni ya Estoppel inazuia kuleta tena mahakamani … Wakaomba Mahakama isipokee Detention Register. Na upande wa mashitaka na wao walianza kwa kupinga.

JAJI: Kwamba suala la upokelewaji wa kielelezo ni vigezo vitatu vinatumika, vya Relevance, Competence and Materiality. Kwa upande wa mashitaka awali walisema kwamba shahidi alisema wazi ni wapi alipotoa kielelezo hicho. Hata maamuzi ya Mahakama ya wakati huo yalihusu shahidi kutokujenga misingi na kwamba kielelezo hicho hakijawahi kutamkwa kwamba ni incompetent. Hoja ya pili ilikuwa ni Detention Register ilikuwa inatolewa kwa ajili ya utambuzi wakati sasa kinatolewa kwa ajili ya kielelezo. Kuhusiana na maamuzi ya kesi ya Oscar na Teresia wamesema hawana shida na maamuzi hayo na kwamba maamuzi hayo kwenye kesi hii ni distinguishable. Kwamba Mahakama iliamua kanuni ya Funtus Officio ni kanuni iliyokuwa inatumika kwenye sheria kesi.

JAJI: Kwamba Mahakama iliamua kanuni ya Funtus Officio ni kanuni iliyokuwa inatumika kwenye sheria kesi kama kesi ya Kamuri vs Jamhuri ambapo kwa maoni yao wanasema mashauri hayo ya natengeneza kanuni kwa jinsi gani kanuni ya Funtus Officio inaweza kutumika ambapo ni mashauri yanayokuwa yamekwishamalizika. Wakaomba turejee kesi ya Theresia kuwa distinguishable, na tukija issue ya Estoppel walikiri kwamba ni kanuni za sheria zetu na wakapinga kwamba ipo tofauti kwenye kesi hii. Wakasema issue ya Estoppel inaweza kutumika pale ambapo kesi iliyopo inafanana kabisa na kesi iliyokwisha.

JAJI: Kwenye uamuzi wa Mahakama hii wanasema ulijikita katika shahidi kushindwa kujenga misingi, na kwamba shauri linapswa kufika mwisho. Na Kwa shauri hili bado haijafika mwisho na kwamba Detention Register Ilikataliwa kwenye shauri hili hili, na kwamba sababu ya kukataa Detention Register ilikuwa haijafika mwisho na kwamba hakuna namna ambapo shauri dogo litatengenishwa na kesi mama. Issue ya Estoppel kama suala la kisheria linakosa sifa kwa sababu shauri halikufika mwisho. Pia haliwezi kuwepo sababu hata malengo ya kwanini ilikataliwa mara ya kwanza ni tofauti na sasa. Na suala la tatu kuhusiana na Disposal Order kama ilivyokuwa imesemwa na upande wa utetezi.

JAJI: Wamesema kwamba amri ya kuachia kielelezo inatolewa baada ya shauri kufika mwisho, na kwamba kielelezo hakikuombwa kurudishwa kwa wenyewe bali malengo yalikuwa ni kukirudisha mahakamani. Kwamba malengo yake yameandikwa kwenye barua hiyo na Naibu Msajili, na kwamba wanaomba Mahakama ione kwamba kanuni inayohitaji kuwepo kwa amri ya kuachia kielelezo haiwezi kutumika katika shauri hili. Kwa mujibu wa kesi ya Kondo Gede vs Jamhuri, inaelezea kwamba Mahakama inaweza kutumia suala la mdomo, wakaiomba Mahakama ipokee kielelezo kwa sababu ambazo wamezieleza kuhusiana na ukweli kwamba Naibu Msajili hana uwezo wa kutoa kielelezo, shahidi ameeleza namna gani alipata kielelezo. Wakaomba Mahakama imuamini shahidi kwa sababu shahidi anaaminika.

JAJI: Uombwaji wa kielelezo uliomba kwa makusudi ya kurudi Mahakamani na siyo kurudi kwa mwenyewe. Kama rejea ya kesi ya Gandi, Mahakama itumie sheria kesi hii, kwamba maombi yalikuwa ni upokelewaji wa kielelezo. Mahakama ijikite katika kanuni za upokelewaji wa kielelezo ambazo ni Competence, Relevance na Materiality, na kwamba maamuzi ya Mahakama yalisema kwamba kielelezo kinaweza … Kwa upande wa utetezi walipata muda wa kufanya Rejoinder. Wakasema kwamba kesi ndogo iliyopo katika kesi kubwa inajitegemea kabisa kwa sheria na utaratibu uliopo pale ambapo Mahakama inahitaji kufanya kesi ndogo, inaondoka kabisa katika kesi kubwa.

JAJI: Mwenendo wa kesi ndogo katika kesi kubwa ni suala la Factual Exercise, suala la kutafuta ukweli, kwamba suala la kuthibitisha kwamba maelezo ya mshitakiwa yalichukuliwa kwa njia halalali ni wajibu wa upande wa mashitaka na upande wa utetezi wanao wajibu pia. Jambo la tatu ni kwamba Mahakama Ilishawahi kufanya kesi ndogo kwa mshitakiwa wa pili, na kwamba suala la amri kama ambavyo inatajwa katika kifungu cha 353 ni jambo la msingi katika kueleza mnyororo kama ulifuta utaratibu.

JAJI: Waliendelea kueleza tofauti kati ya kesi ndogo katika kesi kubwa ni kwamba tofauti na wakaeleza namna ambavyo mashahidi wanapewa utambulisho tofauti, na kwamba kwa Sababu ni kesi ni tofauti basi waliomba kesi tofauti … Wakaomba Mahakama ifuatilie na kusoma guideline ambayo imewekwa na Mahakama kuhusu kushughulika na kielelezo hicho. Mahakama isome mwanzo hadi mwisho namna ya Mahakama kushughulika na kielelezo hicho.

JAJI: Kwamba quorum ya Exhibit Register inapaswa amri ya Mahakama ione imetolewa na imetolewa na nani, na kwamba kesi ya Dege ni irrelevant. Upande wa mashitaka wamengalia kama jambo la kielelezo tu lakini wao wanaangalia admissibility, na kwamba Mahakama inabanwa kuendelea kushughulika na suala hilo kupitia Funtus Officio.

JAJI: Issue siyo ‘Conclusivity’ ya kesi bali hata jambo ambalo lipo mbele ya Mahakama. Kesi ya Gandhi haihusiani na kutoa kielelezo kinyemela na kesi hiyo ni distinguishable. Kwamba kesi ya Julius Michael na wenzake ndiyo inajielezea yenyewe, Mahakama ione inabanwa na maamuzi yake.

JAJI: Wakaendelea kusema hoja walizoleta kwamba kukosekana kwa amri ya Mahakama, Funtus Officio na issue Estoppel kwa sababu hizo wakaomba Mahakama ikatae kielelezo hicho. Na hizo ndiyo zilikuwa hoja za pande zote mbili. Na hizo ndiyo zilikuwa hoja, na hoja zote zimenisaidia kufikia uamuzi. Siku ya tarehe 19 mwezi Septemba wakati anatoa ushahidi wake Mahakamani aliomba kutoa kielelezo hicho.

JAJI: Maombi hayo yalikuwa yamekataliwa, na hoja zilikuwa kwamba shahidi hakuwa amejenga msingi wa namna gani ambapo kielelezo kimemfikia na namna kilivyotunzwa. Mahakama ilitoa uamuzi wa kukubali pingamizi na kwamba Mahakama iliona kweli shahidi hakuwa amejenga misingi. Na kwamba Mahakama iliona kwamba kielelezo hicho hakikikuwa kimetolewa na utawala na njia nyingine za kuleta kielelezo. Kielelezo hicho kilikataliwa Mahakamani.

JAJI: Kielelezo hicho kilikataliwa Mahakamani ambapo upande wa mashitaka wakaomba kielelezo hicho kwa ofisi ya Naibu Msajili. Naibu Msajili aliwapatia kielelezo hicho. Na kwa sababu Shahidi aliomba kutoa kielelezo ndiyo kikapingwa na upande wa utetezi. Hoja ya Funtus Officio inaweza kuathiri maamuzi ya Mahakama, na kwa sababu hiyo naanza na jambo hili. Kwa sababu hii natazama maamuzi na hoja zilizoletwa na rejea ya mashauri yote yaliyoletwa mbele ya Mahakama.

JAJI: Maamuzi ya Kisopo Medard dhidi ya Waziri wa Ardhi, maamuzi yanakubali kuwa yanatumika katika mfumo wetu wa sheria, Mahakama imeombwa irejee eneo linalosomeka hivi: Kwenye mambo ya Mwenendo wa Mahakama kama maamuzi yalishajulikana basi inazuiwa kuyajadili tena.

Jaji” Na kesi ya Oscar Rwechunugura kama ambavyo nimekwishakusema kwamba Mahakama ilikuwa inazuiwa na kanuni hiyo ya Funtus Officio, kwa hiyo siyo sawa Hakimu Mkazi kukubali kupokea suala hilo katika Mahakama ya Wilaya. Na katika kesi ya Imma Advovcates pia kesi ya Mwiguro Cosmas, pia kesi ya Mahuri dhidi ya Jamhuri.

JAJI: Ambapo iliamua kwamba katika mazingira hayo inajitokeza ni wakati gani hakimu anakuwa Funtus Officio na hawezi kuendelea na shauri mbele yake.

JAJI: Pia Mahakama ya Tanzania Seleman vs SMZ Mahakama ilisema kwamba Mahakama inakuwa Funtus Officio. Maamuzi yote haya ninayoyarejea ni wazi kuwa ni mashauri ambayo imefikisha Mahakama mwisho. Kwa upande wa utetezi wamesema siyo lazima kesi iwe imefika mwisho. Nakubalina nao lakini inategemea ni jambo gani kwa sababu hiyo Mahakama hii inajiuliza kwamba, je, jambo la kuijadili Register ilikuwa inafikisha Mahakama mwisho? Jibu ni HAPANA.

Kielelezo kinaweza kutolewa Mahakamani kwa ajili ya utambuzi, na kinapotolewa kama utambuzi basi ni tofauti inapopokelewa kwa ajili ya ushahidi. Kielelezo kinapoitwa kwa jili ya utambuzi kinakosa hadhi ya Mahakama kutumia akama kielelezo. Katika mazingira mengi ambapo Mahakama imepokea kielelezo anapokuwa shahidi ambaye ni competent anakitumia … Kwamba Mahakama inaona kwamba suala la kutolewa kielelezo na shahidi hakuwa inafikisha Mahakama mwisho.

JAJI: Kwa Sheria Kesi nilizozitaja hapo juu, ili Mahakama iwe Funtus Officio mambo haya lazima yatimie. Mahakama inakuwa Funtus Officio ikithibitika kwamba jambo lililopo mbele ya Mahakama limeshazungumzwa na kutolewa maamuzi. Kwamba jambo hilo linatakiwa liwe limeimaliza kesi kwa kumkuta mshitakiwa ana hatia au kuitisha jambo lolote. Amri hiyo ambayo inakuwa imeinyima Mahakama, inatakiwa iwe na matokeo ya kuifikisha kesi mwisho.

JAJI: Ukiangalia kimantiki kielelezo ambacho kimetolewa baada ya kielelezo hicho kukataliwa kilikuwa katika suala la utambuzi, na kwamba upokelewaji wake siyo wa mwisho, basi hata kupokelewa kwake siyo jambo la msingi. Hoja ya Funtus Officio naitupilia mbali kwa sababu nilizoeleza.

JAJI: Suala zima la Issue Estoppel ni sehemu ya sheria zetu. Nakubaliana na maamuzi ya Mahakama Kuu kwamba ili kusudi ziweze kutumia ya Issue Estoppel lazima mambo haya yawepo. Pale ambapo jambo limeshaamriwa na Mahakama, maamuzi yalifikiwa kwa manufaa ya mshitakiwa, kwamba maamuzi yakifikisha Mahakama mwisho kwa sababu hiyo ndiyo inatengeneza falsafa ya Issue Estoppel. Ni kuhakikisha kwamba mshitakiwa haitwi tena. Pili, kulinda mfumo unaotambulika katika mfumo jinai, kulinda hadhi ya Taasisi na suala la kiuchumi. Kama ambavyo imeelezwa mwanzo. Suala la Detention Register ilishaletwa Mahakamani na Mahakama ikaikataa. Kwa sababu hiyo ilikataliwa…

JAJI: Je, Mahakama inajiuliza baada ya kukata je, Mahakama inazuiwa … Mahakama inazingatia hoja zote za utetezi na upande wa mashitaka. Hakuna ubishi kwamba suala la Detention Register lililetwa kwa ajili ya utambuzi na shahidi alishindwa kujenga misingi ya kielelezo hicho, na kwamba kukataliwa kwake halikuwa imelifikisha mwisho shauri hilo. Kama ambavyo nimeeleza katika Sheria Kesi.

JAJI: Ili Mahakama iweze kufikia maamuzi ili kuona kama Issue ya Estoppel inahusika lazima Mahakama ione kama yanafanana katika context na substance yake. Katika shauri ambalo lipo mbele ya Mahakama hii utolewaji wa kielelezo hicho hata kama kingepokelewa isingefika mwisho. Kielelezo hicho kilikuwa bado lazima kitolewe na shahidi ambaye ni competent. Kama kupokelewa hakuwezi kufikia mwisho wa shauri lake, Mahakama inaona kwamba Issue ya Estoppel haiwezi kuwepo. Suala linalobakia ni kuwepo au kutowepo kwa DISPOSAL ORDER.

JAJI: Mahakama imeelekezwa kutumia kifungu cha 353 na mwongozo wa Mahakama, na kwamba Mahakama imeelekezwa kwamba bila kuwepo kwa DISPOSAL ORDER, basi utolewaji wa barua ya Naibu Msajili hakuwezi kuhalilisha suala hilo. Mahakama imezingatia hoja zote. Mahakama inaona kwamba suala zima la upokelewaji wa kielelezo Mahakamani ni kwa mujibu wa sheria. na baada ya kielelezo kupokelewa unabakia kuwa chini ya Mahakama. Imeelezwa vizuri kwenye mwongozo wa Mahakama.

JAJI: Mahakama imefuata kifungu 353(3) kinasema kwamba, bila kuathiri kifungu cha kwanza … Mahakama ikiona inafaa … Kitu ambacho kimetolewa Mahakamani kitolewe na kurudishashwa Mahakamani kwa ushahidi … Kwa masharti itayokuwaimeweka.

JAJI: Ni wazi kwamba kumbe kielelezo kinapokuwa … ni ya Mahakama. Kwamba pale kielelezo kinapokuwa kinatoka kinapswa kutolewa kwa amri ya Mahakama. Nakubaliana na upande wa utetezi, na kwamba Mahakama inapokuwa imekipokea kielelezo hicho, haihusiki na kutunza kielelezo hicho.

JAJI: Ni jukumu la Hakimu Mfawidhi na Naibu Msajili. Mwongozo unasema kwamba watamteua atakayetunza. Kanuni inampa Naibu Msajili na Hakimu Mfawidhi uwezo wa kudhibiti vielelezo, kwamba Naibu Msajili au Naibu Msajili ana jukumu ya kukagua register ya vielelezo.

JAJI: Ana jukumu ya kukagua register ya vielelezo kwa kusudi la kujiridhisha. Lakini suala la kutoa kielelezo Mahakamani, Sura ya Nne inasema kwamba utoaji wa vielelezo unafanyika mwisho baada ya shauri kufika au rufaa kukata katika shauri hilo. Kama Mwenendo wa Jinai unavyosema. Ni msimamo wa sheria kama ambavyo Mahakama iliamua katika kesi ya Siayo. Vielelezo vinatakiwa vitoke ambapo shauri limefika mwisho. Na kwamba katika Mwongozo sehemu ya nne inasema kwamba, pamoja na kanuni hiyo, kielelezo kinaweza kutoka mapema wakati shauri linaendelea. Kama ambavyo kifungu cha 353 (1) kinasema kwamba Mahakama itatoa amri ya kuachiwa kwa kielelezo, mpaka pale Mahakama itakapokuwa unahitaji kielelezo hicho.

JAJI: Mahakama inaweza kutoa amri ya kutoa kielelezo pale ambapo shauri limefika mwisho au rufaa imefika mwisho. Mahakama katika amri yake inayohusu Disposal Order inahusu kama kielelezo kurudi kwa mwenyewe. Kielelezo kiharibiwe au kurudi Serikalini. Mahakama itasema kwamba ni kielelezo gani kiharibiwe kila mwisho mwezi.

JAJI: Na mwisho ni kwamba pale ambapo kielelezo kinatakiwa kubaribiwa, notisi itolewe siku 30 kabla kwa mshitakiwa, ofisi ya upelelezi, ofisi ya mwanasheria. Hiyo ndiyo namna ambapo kielelezo kinapswa kitolewe. Mahakama hii inakubaliana na upande wa utetezi kwamba Naibu Msajili hana mamlaka ya kutoa kielelezo. Mamlaka yake ni kusimamia pale kuendelea kinapokuwa kwenye chumba cha kielelezo.

JAJI: Kusimamia utolewaji au kuharibiwa kwa kielelezo hicho. Kwa namna hiyo basi ni kweli kwamba kielelezo hakiwezi kutolewa pasipo amri ya Mahakama. Hata hivyo, Mahakama inatakiwa ijielekeze katika sheria kesi hiyo. Mahakama inatakiwa kusema kwamba kielelezo kirudi kwa mwenyewe, au kiharibiwe, au kurudishwa Serikalini. Mahakama haina mamlaka ya kutolea amri nje ya kazi hizo …

JAJI: Barua ilivyoandikwa kwa Naibu Msajili haikuwa imeeleza mambo hayo hapo juu. Mahakama ina maoni kwamba halikuwa muafaka kwa kutolea amri ya kuteketeza. Lakini Naibu Msajili ametajwa kwamba ana uwezo wa kutunza kielelezo, na kwamba kielelezo kinachotakiwa kwa kesi zaidi ya moja au mahakama zaidi ya moja. Kutokana na hali hiyo basi ni wazi siyo kila wakati kwamba kila wakati kielelezo kinapokuwa kinatumika kinatakiwa kiwe na amri ya Mahakama.

JAJI: Kwamba kinaweza kutumika kwa kesi au mahakama zaidi ya moja bila amri ya Mahakama. Kielelezo siyo lazima pawe na amri ya mahakama. Nimeona kwamba siyo lazima kielelezo hicho kuwa na amri ya Mahakamani.

JAJI: Kwa sababu hiyo natupilia mbali sababu zote tatu za mapingamizi ya kuzuia kielelezo hicho. Natoa AMRI.

Mawakili wa pande zote mbili wanasimama na kukaa.

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Mheshimiwa Jaji, kufuatilia maamuzi ya Mahakama naomba sasa shahidi aruhusiwe kuendelea kutoa ushahidi wake.

JAJI: Upande wa utetezi kuna hoja yoyote?

KIBATALA: Hakuna. Endelea!

JAJI: Kwa mujibu wa utaratibu, kielelezo kinatakiwa kisomwe.

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Tunaomba sasa tupewe P2 ili shahidi aweze kusoma. Tunaomba shahidi asome maeneo ambayo ni relevant tu.

JOHN MALLYA: Sawa tu.

WAKILI WA SERIKALI: Kwenye ushahidi wako wako umesema tarehe 7 Agosti 2020 ulipokea watuhumiwa walioletwa na Kingai na ACP Jumanne. Twende kwenye eneo ulilowaingiza na utusomee.

(Shahidi anapekua … Anaanza kusoma).

(Shahidi amemaliza kukifafanua kitabu)

WAKILI WA SERIKALI: Mtu huyu aliyetolewa alirejea saa ngapi?

SHAHIDI: Saa tano na dakika sita.

WAKILI WA SERIKALI: Anaonekana namba ngapi?

SHAHIDI: Namba 401.

WAKILI WA SERIKALI: Wakati anaingia hii mara ya pili?

WAKILI WA SERIKALI: Wakati anaingia hii mara ya pili alikuwa na hali gani?

SHAHIDI: Physical condition ni good.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kuingia tarehe 7 Agosti 2020 saa tano, ni lini tena alitoka?

SHAHIDI: Alitoka tena tarehe 8 Agosti 2020, majira ya saa nne na dakika tano asubuhi.

WAKILI WA SERIKALI: Nani alimtoa?

SHAHIDI: Inspector Mahita.

WAKILI WA SERIKALI: Sababu za kumtoa?

SHAHIDI: Nje kwa upelelezi.

WAKILI WA SERIKALI: Mtu mwingine uliyepokea ni nani?

SHAHIDI: Adam Kasekwa.

WAKILI WA SERIKALI: Anasoma entry namba ngapi?

SHAHIDI: Namba 393.

WAKILI WA SERIKALI: Aliingizwa saa ngapi?

SHAHIDI: Tarehe 7 Agosti 2020, saa 12 na dakika tisa.

WAKILI WA SERIKALI: Baada ya kumwingiza ni lini alitoka tena?

SHAHIDI: Tarehe 7 Agosti 2020 saa 11 na dakika 11.

WAKILI WA SERIKALI: Sababu?

SHAHIDI: Nje kwa mahojiano.

WAKILI WA SERIKALI: Ni lini tena alirejea?

SHAHIDI: Tarehe hiyo hiyo saba Agosti 2020 … Kwa entry namba 396.

WAKILI WA SERIKALI: Alikaa mahabusu hadi lini?

SHAHIDI: Alikaa Mahabusu mpaka tarehe 8 Agosti 2020 majira ya saa 4 na dakika 15 asubuhi.

WAKILI WA SERIKALI: Nani alimtoa?

SHAHIDI: Inspector Mahita.

WAKILI WA SERIKALI: Sababu za kumtoa?

SHAHIDI: Nje kwa upelelezi.

WAKILI WA SERIKALI: Kwa mujibu wa kitabu hicho kuwa na entry ya ‘ration’?

SHAHIDI: ‘Ration’ supply anatakiwa apewe asubuhi mchana na jioni.

SHAHIDI: Kwa mujibu wa kitabu mtuhumiwa amepewa chakula asubuhi, mchana na jioni.

WAKILI WA SERIKALI: Hizo taarifa za kwenye kitabu ni taarifa za kituo gani?

SHAHIDI: Taarifa za Central Dar es Salaam.

WAKILI WA SERIKALI: Watu hao uliowapokea hapa mahakamani wapo?

SHAHIDI: Wapo kwenye kizimba cha washitakiwa.

WAKILI WA SERIKALI: Ifahamishe Mahakama yupi ni yupi.

SHAHIDI: Hawa wawili wa katikati.

SHAHIDI: Wa pili kutoka kulia ni Adam na huyu mwingine ni Mohammed Abdilah Ling’wenya.

WAKILI WA SERIKALI: Uliwapokea wapi?

SHAHIDI: Dar es Salaam Central.

WAKILI WA SERIKALI: Lini?

SHAHIDI: Tarehe 7 Agosti 2020.

Anaamka Wakili Nashon Nkungu.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji hatuna swali lingine kwa shahidi. Tumemaliza examination in chief.

NASHON: Shahidi unafahamu kwamba washitakiwa wanasema kwamba hawajawahi kuonana na wewe na hawajawahi kufika Central Da es Salaam?

SHAHIDI: Sifahamu kama wanasema hivyo.

NASHON: Unafahamu kuhusu Station Diary?

SHAHIDI: Ndiyo nafahamu.

NASHON: Na ni Duty ya CRO?

SHAHIDI: Sahihi.

NASHON: Mheshimiwa Jaji naomba kupatiwa Exhibit P2.

NASHON: Ni sahihi kabisa kwamba askari anayekuja na anayetoka lazima wasainishane kwenye Station Diary?

SHAHIDI: Ni sahihi.

NASHON: Ni sahihi kwamba inatajwa kwamba nimemkabidhi … pamoja na silaha na majina ya mahabusu?

SHAHIDI: Nafahamu kwamba ni takwa la kisheria.

NASHON: Na kutaja watuhumiwa na mali?

SHAHIDI: Kwenye suala la watuhumiwa sijafahamu.

NASHON: Huoni kwamba Station Diary, huoni kwamba ingekuwa ya muhimu kuwepo Mahakamani?

SHAHIDI: Siyo ya umuhimu.

NASHON: Pale kituo cha Central Police Dar es Salaam palikuwa na askari wengine wakati akina Kingai wanatoka Moshi?

SHAHIDI: Ndiyo. Palikuwa na askari wengine.

NASHON: Je, ulimwambia Mheshimiwa Jaji kwamba katika askari waliokuwepo kituoni hapakuwa na askari wengine ambao wangewachukua maelezo watuhumiwa?

SHAHIDI: Sikusema.

NASHON: Je, ulipata kufahamu kama kuna ndugu au wakili waliokuwepo wakati wanachukuliwa maelezo?

SHAHIDI: Hapana.

NASHON: Je, kuna ndugu au mawakili walikuja kuwatembelea washitakiwa?

SHAHIDI: Hakuna.

Anaingia Wakili John Mallya.

MALLYA: Kwamba kwa madai yako ulikuwa Central siku ya tarehe 7 Agosti 2020?

SHAHIDI: Ndiyo.

MALLYA: Kwamba wakati huo ulikuwa umefanya kazi kwa muda gani?

SHAHIDI: Mwaka 2014 mpaka 2020.

MALLYA: Pale CRO ulikaa mara ngapi?

SHAHIDI: Sikumbuki.

MALLYA: Kwa hiyo ulishawahi kufanya kazi za General Duties mara kadhaa.

SHAHIDI: Sahihi.

MALLYA: Kwa huo mwezi wa saba pia ulikaa pale CRO?

SHAHIDI: Ndiyo, lakini sikumbuki mara ngapi.

MALLYA: Umesema umeshawahi kufanya kazi Central? Nitafutie sehemu nyingine kwenye hicho kitabu ambapo ulishawahi kufanya majukumu hayo.

SHAHIDI: Tarehe 2 Agosti 2020.

MALLYA: Mheshimiwa Jaji, utaangalia wakati unafanya uamuzi kwenye Serial Number 184.

MALLYA: Wakati unaandika wakati wa kumtoa mtu, sababu inakuwa kweli au la?

SHAHIDI: Wakati amemtoa.

MALLYA: Interest yangu entry inayomuhusu mshitakiwa wa pili. Wakati anamtoa aliandika nini.

SHAHIDI: Nje kwa upelelezi.

MALLYA: Jumanne anasema kwamba alimtoa kwa sababu ya mahojiano. Wewe umeandika sababu ya upelelezi.

SHAHIDI: Ndiyo. Mahojiano ni sehemu ya upelelezi.

MALLYA: Kwa hiyo ni kitu kimoja hicho?

SHAHIDI: Ndiyo.

MALLYA: Soma hapa na hapa.

SHAHIDI: Nje kwa upelelezi, nje kwa mahojiano.

MALLYA: Sasa nikitu kimoja?

SHAHIDI: Hapana. Upelelezi ni broad na mahojiano ni specific.

MALLYA: Kwa uelewa wako wewe maana yake nini?

SHAHIDI: Mchakato unaotumika kuanzia kesi imefunguliwa mpaka pale inapofikishwa Mahakamani.

MALLYA: Walikwambia wanawatoa kwa jambo gani?

SHAHIDI: Mmoja kwa ajili ya upelelezi na mmoja kwa ajili ya mahojiano.

MALLYA: Aliyemtoa mshitakiwa wa tatu ni nani?

SHAHIDI: Inspector Mahita.

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Objection! Kuhusu utaratibu. Unapomrtejea mtu basi inukuliwe maneno sahihi. Wakili azuiliwe kuweka maneno kwa shahidi ambaye hayupo huku.

KIBATALA: Objection! Tulishawahi kuweka utaratibu humu kwamba objection itafanyika kwa majibu siyo maswali

JAJI: Una kifungu cha sheria kinachokataza hilo?

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Naomba dakika moja.

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Sijakipata kifungu moja kwa moja ila Mheshimiwa Jaji unapokuwa unamhoji shahidi kwamba fulani alishasema kifu fulani hairuhusiwi na wewe unajua hilo.

JAJI: Kanuni za cross examination inasemaje?

MALLYA: Maswali ambayo yanamdhalilisha shahidi, maswali anayoulizwa shahidi hapa hayamlengi shahidi.

MALLYA: Sababu alizomtoa shahidi mahabusu Central ni pamoja na kwenda kumpiga?

SHAHIDI: Hapana. Ni kwa ajili ya upelelezi.

MALLYA: Ulikutwa na diary hapa Mahakamani, na Jaji akasema wewe ni violator.

SHAHIDI: Mheshimiwa Jaji, entry namba 396 sababu ya kumtoa, tarehe na muda na mtu aliyemtoa mtuhumiwa no. tofauti na kalamu iliyotumika au mwandiko wangu uliotumika kumwingiza mtuhimiwa.

MALLYA: Ulipata kueleza Mahakamani? Vifupi vya maneno kwenye Detention Register mnandika wenyewe au ni kwa mujibu wa sheria?

SHAHIDI: Kwa mujibu wa PGO.

MALLYA: Ngoja nikuonyeshe PGO. Naona Dar es Salaam kwamba CDS ni nini?

SHAHIDI: Inawekezakana ni Chuo Cha Polisi.

MALLYA: Haya. Nakuonyesha vituo vya polisi vyote Tanzania na vifupi vyake. Nionyeshe walipoandika CENTRAL ni CD.

(Shahidi anakodoa macho kwa muda mrefu kidogo).

MALLYA: Miye nimetafuta tangu jana sijaona. Sijui kama utapata muda wa kutosha.

SHAHIDI: Mimi sijaona humu.

MALLYA: Sasa sisi ili tuamini kwamba hiki kitabu kimetoka Dar es Salaam Polisi Central tulitaka tuone kiandikwe ni ‘POLICE CENTRAL DAR ES SALAAM’ au kifupi chake. Kwa sababu kwenye PGO hakuna, kimoja hakipo sahihi.

SHAHIDI: Detention Register ipo sahihi.

MALLYA: Miye nataka nijue kipi hakipo sahihi.

JAJI: Sasa kati ya PGO na Detention Register ni kipi kipo sahihi?

SHAHIDI: Mheshimiwa Jaji siwezi kusema kwamba PGO haipo sahihi.

JAJI: Swali ni kwamba kipi hakiko sahihi?

SHAHIDI: Hakuna ambacho hakipo sahihi.

MALLYA: Sasa kuna diary yako ulikamatwa nayo Mahakamani.

SHAHIDI: Kwanza sijakamatwa nayo. Niliandika siku ya kwanza kuja kutoa ushahidi tarehe 20 Septemba.

JAJI: Ndiyo siku uliyoandika.

SHAHIDI: Hapana. Kabla ya siku ya kuja kutoa ushahidi.

MALLYA: Kwa uwezo wa pale Central na rasilimali zake ukoje?

SHAHIDI: Hayo sasa wanatakiwa kuzungumzia watu wa utawala.

MALLYA: Kwa ufahamu wako wewe ulishawahi kuishiwa karatasi pale Central za kuandikia maelezo?

SHAHIDI: Hapana.

Anaingia Wakili Dickson Matata.

MATATA: Nitakuhoji maswali machache kutokana na maelezo uliyoyatoa hapa Mahakamani. Kutokana na wateja wetu kupinga kwamba hawakuwahi kuandika maelezo na hawajawahi kufika Central Dar es Salaam. Shahidi ulisema kituo chako cha kwanza kuanza kazi ni wapi?

SHAHIDI: Msimbazi.

MATATA: Msimbazi ipo wapi?

SHAHIDI: Wilaya ya Kipolisi Kariakoo.

MATATA: Kuna sehemu yoyote ulitaja kiongozi uliyewahi kufanya naye kazi pale Msimbazi?

SHAHIDI: Sijazungumzia.

MATATA: Ukiachana na kutaja majina yako na Force Number zako, kuna ushahidi wowote umeonyesha kwamba uliwahi kufanya kazi Central Police Dar es Salaam?

SHAHIDI: Ndiyo. Nimeleta Detention Register yenye mwaandiko wangu mimi hapa.

MATATA: Kuna kitu chochote umeleta Mahakamani ambacho kwa kuangalia DR tunaweza kusema huu ni mwandiko wako?

MATATA: twende sasa kwenye DR, Mheshimiwa Jaji namwomyesha kuanzia entry namba 393.

MATATA: Nenda tarehe saba. Kuna sahihi yako hapo kwenye hizo entry?

SHAHIDI: Hakuna.

MATATA: Kuna sehemu yoyote yenye Force Number yako hapo?

SHAHIDI: Hakuna.

MATATA: Nikisema mtu yoyote anaweza kuandika kilichoandikwa hapa nitakuwa nakosea?

SHAHIDI: Utakuwa unakosea.

MATATA: Kuna kitu kingine chochote kinachoonyesha kwamba Detention Register imetoka Polisi Central Dar es Salaam na siyo Mbweni?

SHAHIDI: Kitu pekee ni hiyo CD.

MATATA: Ni sahihi kwamba mwaka huu ndiyo umeanza kufanya kazi Oysterbay Polisi?

SHAHIDI: Ndiyo. Mwaka huu.

MATATA: Pale Central mmesema mnatumia CD, je Oysterbay mnatumia nini?

SHAHIDI: OB.

MATATA: Hiyo OB inatokana na nini? PGO namba 05 ndiyo inazungumzia vifupisho vya vituo vya polisi. Hebu soma hapa.

SHAHIDI: Oysterbay inasema ni OYB.

MATATA: Kuna kitabu au mwongozo umekuja nao hapa unaoonyesha Oysterbay ni OB?

SHAHIDI: Hapana.

Anaingia Wakili Peter Kibatala.

KIBATALA: Ile diary uliyokuwa nayo kwenye kizimba, sehemu mahususi ambazo zinahusika na kesi hii zimeingia kama kielelezo cha Mahakama namba 1.

SHAHIDI: Sikumbuki.

KIBATALA: Siku hiyo ulikuwa wapi?

SHAHIDI: Sikumbuki nilikuwa wapi.

KIBATALA: Je, unafahamu kwamba vitu vilivyochukuliwa kwenye diary yako vinahusiana na kesi hii na ushahidi wako?

SHAHIDI: Ndiyo vinahusiana.

KIBATALA: Na unafahamu kwamba Mahakama imechukua kurasa kwenye diary yako kabla ya wewe kuja kutoa ushahidi leo?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Je, ulifafanua kwa Mheshimiwa Jaji wakati wa kuongozwa na wakili wa Serikali kwamba kuna kidhibiti namba moja mule kuna 1,2,3 na maana yake ni nini?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Kwa sababu hujafafanua, je unafahamu kwamba ulifafanua wakati wa re-examination?

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Basi kama hufahamu, mkijaribu tutasimama.

KIBATALA: Shika kielelezo namba P1 mwonyeshe Mheshimiwa Jaji ni wapi pameandikwa CENTRAL POLICE STATION DAR ES SALAAM.

SHAHIDI: Hakuna.

KIBATALA: Kwa hiyo ili Mahakama ijue kwamba kielelezo hiki ni cha Central lazima iingie kwenye details za ndani?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Mojawapo ya vifaa kazi vya utambuzi ni PGO.

SHAHIDI: Ndiyo PGO.

KIBATALA: Kingine ni kipi?

SHAHIDI: Kuna mwongozo ya Jeshi la Polisi huwa inatolewa.

KIBATALA: Ni lini umefahamu kwamba unakuja kutoa ushahidi wa kesi ndogo ya Mohammed Ling’wenya?

SHAHIDI: Sikumbuki tarehe, ila kama siku 13 nyuma.

KIBATALA: Toka unapokea summons, ni lini ulifanya maandalizi ya kuleta mwongozo?

SHAHIDI: Sijaleta mwongozo.

KIBATALA: Kuna mtu yoyote alikuzuia kuleta?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Kingine ni kitu gani?

SHAHIDI: Police Auxiliary Act.

KIBATALA: Kifungu gani?

KIBATALA: Katika kielelezo P1 hapo Katika ni nini hicho?

SHAHIDI: Mheshimiwa Jaji ni pini iliyodondokea hata kwa bahati kama ukurasa unaowahusu washitakiwa hawa hakuna.

KIBATALA: Ulifafanua kuhusu hiyo pini?

SHAHIDI: Sikufafanua.

KIBATALA: Hiyo tarehe 7 Agosti 2020 ulipokea zamu kutoka kwa nani na nani?

SHAHIDI: Aliyepokea zamu ni Afande Fatuma.

KIBATALA: Kwa hiyo wewe humfahamu hata askari mmoja kati ya wale uliowapokea?

SHAHIDI: Siwakumbuki.

KIBATALA: Ulipotoka duty uliwakabidhi askari nani na nani?

SHAHIDI: Aliwakabidhi Afande Fatuma, miye siwajui.

KIBATALA: ‘Imakama’ maana yake nini?

SHAHIDI: Miye sikumbuki.

KIBATALA: Kuna mpango kazi unaonyesha askari fulani anakaa wapi na nani anaenda wapi?

SHAHIDI: Ndiyo. Upo.

KIBATALA: Na wewe mpaka unakuja kutoa ushahidi, hujaleta sehemu ya mpango kazi.

KIBATALA: Unamfahamu mtu anaitwa Lembrus Mchome?

SHAHIDI: Simfahamu.

KIBATALA: Anasema kwamba mwaka jana mwezi wa tano ulimpokea Oysterbay Polisi ukiwa CRO.

SHAHIDI: Simkumbuki.

KIBATALA: Ana sababu gani za kukusingizia?

SHAHIDI: Simfahamu.

KIBATALA: Hiyo siku ya tarehe 7 Agosti 2020, wakati unampokea Mohammed Abdilah Ling’wenya alikuwa na karatasi yoyote?

SHAHIDI: Sikumkuta na chochote.

KIBATALA: Wakati unaongozwa ulipata kuzungumzia kuhusu Seizure Certificate?

SHAHIDI: Sikuongozwa.

KIBATALA: Je, exhibit zinatunzwa wapi kama mtu akikutwa navyo?

SHAHIDI: Kwa mtunza vielelezo.

KIBATALA: Walikuongoza kuzungumzia kuhusu vielelezo vya Mohammed Ling’wenya.

KIBATALA: Mtunza vielelezo anaitwa nani?

SHAHIDI: Sikumbuki. Ni siku nyingi sana.

KIBATALA: Ulisema kwamba Mohammed Ling’wenya alichukuliwa maelezo kwenye ofisi ya OCS, je, umesema kwa Jaji nani alifungua mlango?

SHAHIDI: Sikusema.

KIBATALA: Ulimweleza Mheshimiwa Jaji kuwa OCS alikuwapo wapi?

SHAHIDI: Sikusema.

KIBATALA: Nani alikuwa custodian wa Detention Register?

SHAHIDI: Mimi.

KIBATALA: Wakati unasema ulimsindikiza ASP Jumanne, ulisema Detention Register ulimuachia nani?

KIBATALA: Kuna sehemu nilisikia unasema kwamba ulitambua barua ya Naibu wa Msajili kwa sababu ya sahihi yake. Wewe unaifahamu sahihi ya Naibu Msajili?

SHAHIDI: Siyo familiar sana.

KIBATALA: Wakati barua hii inasainiwa ulikwepo?

SHAHIDI: Sikuwepo.

KIBATALA: Wakati mnapeana barua hii sisi tulishirikishwa?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Mwambie Mheshimiwa Jaji sehemu gani katika hii barua umesaini kwamba ulipokea wewe.

SHAHIDI: Sijasaini.

KIBATALA: Nilisikia kwamba kuna sehemu walikusainisha. Je, umekuja na hicho kitabu ulichosaini?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Soma hii barua ilivyoandikwa kwa Naibu Msajili, je, kuna jina lako?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Sasa Naibu Msajili alijuaje wewe unahitaji kielelezo?

SHAHIDI: Sijui yeye.

KIBATALA: Sisi kwenye kesi ya Adamoo hakutukuwahi kuwa na kielelezo TP1 bali P1.

SHAHIDI: Sikumbuki.

KIBATALA: Soma kwenye barua. Mlipeana kielelezo gani?

SHAHIDI: TP 1

KIBATALA: Unafahamu kwamba kwa mujibu wa Jaji Mkuu, vielelezo vyote vinatakiwa kuanza na P na siyo TP? Unajua kwanini tulipinga hii barua kupokelewa? Tulipinga Mahakama kuitwa kama shahidi.

KIBATALA: Kwa ruhusa ya Mahakama, kesi inayomuhusu Mohammed Ling’wenya, alitolewa nje kwanini?

SHAHIDI: Kwa upelelezi.

KIBATALA: Eleza sasa ni wapi ulifafanua kwamba nje kwa upelelezi inamaanisha nini.

SHAHIDI: Sikumbuki.

KIBATALA: Nje kwa upelelezi na nje kwa mahojiano ni sawa?

SHAHIDI: Hazifanani lakini ni kitu kimoja.

Kibatala:* Unafahamu kwamba kidhibiti kinatakiwa kijielezeee chenyewe?

SHAHIDI: Nafahamu.

KIBATALA: Kuna PPR namba. Mweleze Mheshimiwa Jaji maana yake nini. Je, nakala ya Ling’wenya ya Seizure Certificate for na fall kwenye PPR namba.

SHAHIDI: Sifahamu.

KIBATALA: Ulitoa ufafanuzi hapa kwenye kitabu kuna dash kwenye PPR namba.

SHAHIDI: Ndiyo ipo.

KIBATALA: Ulitoa ufafanuzi kwa Mheshimiwa Jaji?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: Ulimwambia Mheshimiwa Jaji kwamba hii Detention Register inaishia lini?

SHAHIDI: Tarehe 12 Agosti.

KIBATALA: Kama mke wa Ling’wenya alikuja Polisi Central Station alikuja Polisi Station, kwa kitabu hiki angeambiwa yupo wapi?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Kame mke wa Ling’wenya alikuja Central na hakumwona kwenye daftari itakuwa nini?

SHAHIDI: Sijui.

KIBATALA: Nimesikia kwamba mnaulizana na Mallya kuhusu mwandiko. Je, ulitoa kitu kingine chenye mwandiko wako tuweze kulinganisha?

SHAHIDI: Hapana.

KIBATALA: physical condition ni sawa na health conditions?

SHAHIDI: Si sawa. Ni tofauti

KIBATALA: Wakati unaweka entry za Ling’wenya wakina Kingai na timu yake walikuwepo?

SHAHIDI: Kingai alikuwa mbali ila timu yake walikuwepo.

KIBATALA: Wakati wamefika upekuzi maungoni Ling’wenya?

SHAHIDI: Ndiyo.

KIBATALA: Nani alikuwepo?

SHAHIDI: Afande Fatuma.

KIBATALA: Kwa hiyo ni ushahidi wako kwamba ulifanya upekuzi wako mbele ya afande Fatuma?

SHAHIDI: Ndiyo nilifanya.

KIBATALA: Shahidi wako mwingine ni nani?

SHAHIDI: Timu nzima iliyokuwa CRO.

KIBATALA: Majina ya Ling’wenya uliyapata kutoka kwa nani?

SHAHIDI: Kwa wao wenyewe.

KIBATALA: Ulimwambia Mheshimiwa Jaji kwamba kulikuwa na Alternative Facilities za kuwasiliana na ndugu zake Ling’wenya?

SHAHIDI: Hapana. Sijamwambia.

KIBATALA: Unaifahamu Station Diary?

SHAHIDI: Ndiyo PF 51.

KIBATALA: Umetoa hapa Mahakamani?

SHAHIDI: Sijaja na Station Diary.

KIBATALA: Ulitaja kwa Mheshimiwa Jaji kwamba nani alikupa DR?

SHAHIDI: Sikutaja.

KIBATALA: Ulitaja mtu aliyekupa?

SHAHIDI: Sikutaja.

KIBATALA: Ulitaja muda wakati unapewa?

SHAHIDI: Sikutaja.

KIBATALA: Kwani hii ni mali yako au mali ya Jeshi la Polisi?

SHAHIDI: Mali ya Jeshi la Police.

KIBATALA: Entry ya Ling’wenya ipo wapi?

SHAHIDI: 392.

KIBATALA: Na imeacha kutumika lini?

SHAHIDI: Tarehe 12 Agosti 2020.

KIBATALA: Fungua entry namba 208. Kibatala tarehe ngapi?

SHAHIDI: Hapasomeki.

KIBATALA: Miye nakwambia ni mwaka 2021.

SHAHIDI: Hapana. Hapasomeki.

KIBATALA: Fungua tena entry 114.

SHAHIDI: Tarehe 30 July 2021.

KIBATALA: Fungua entry 113.

SHAHIDI: Haisomeki.

KIBATALA: Fungua entry namba 156.

SHAHIDI: Tarehe 3 Agosti 2021.

KIBATALA: Na unafahamu kwamba hiki kielelezo kinapimwa pia kwa uongo wake?

KIBATALA: Nakuonyesha entry inayomhusu Ling’wenya. Aliingia saa 06:07hrs wakati anatoka 08:10. Kuna hours au hakuna hours?

SHAHIDI: Hakuna hours.

KIBATALA: Ulifafanua wakati unaongozwa na Hila? Ulifafanua?

SHAHIDI: Sikumbuki.

KIBATALA: Katika entry ya Ling’wenya kuna dole gumba. Mwambie Mheshimiwa Jaji kama ulifafanua kuwa dole gumba ni la nani.

SHAHIDI: Sikufafanua.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji sina swali lingine. Naomba kurudisha kielelezo namba P2.

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Tumekaa mfululizo tangu asubuhi. Ikikupendeza tunaomba tupate health break.

JAJI: Utetezi?

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji sisi tunapinga. Tunapinga tunahisi muda huo utatumika kumfundisha majibu shahidi.

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Hoja iliyotumika ni tuhuma.

JAJI: Kasema anawasiwasi tu.

WAKILI WA SERIKALI: Basi tunaomba tupate health break.

JAJI: Wote tulikuwepo humu ndani na hasa mimi sitoki.

JAJI: Na mimi napata ugumu kumfungia sehemu asifundishwe majibu. Wakili Mallya tusaidie.

MALLYA: Najitolea kukaa naye na nitakula naye.

JAJI: Basi naelekeza Hilla, Malya na shahidi mkae pamoja.

Pius Hilla: Hatujawahi kula pamoja.

JAJI: Na kama watachukua nusu saa basi break iwe lisaa lizima.

Jaji anaondoka kwenye chumba cha mahakama.

Tunarejea mahakamani sasa.

Jaji ameshaingia Mahakamani. Kesi namba 16 ya mwaka 2021 ya Jamhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe inatajwa tena.

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Ikupendeze Mheshimiwa Jaji, uwakilishi upande wa Jamhuri una marekebisho kidogo. Tungeomba Mahakama iridhie kuwaingiza kwenye ‘quorum’ wakili wa Serikali Robert Kidando na wakili wa Serikali Abdallah Chavula. Wengine tupo kama tulivyokuwa awali.

KIBATALA: Kwa upande wa utetezi ‘quorum’ ipo kama tulivyokuwa awali na tupo tayari kuendelea.

(Jaji anainama na kuandika kidogo wakati mahakama imetulia).

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Shahidi sasa nitakuuliza maswali kwa ajili ya ufafanuzi kufutiwa na yale waliyokuuliza mawakili wasomi. Shahidi umeulizwa kwamba washitakiwa wanakana kwamba hawajafikishwa Central. Hebu fafanua hufahamu nini?

SHAHIDI: Sikuwa nafahamu kama …, Lakini mimi ndiye niliyewapokea na nikawa- detain.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji naomba kuwa supplied na kielelezo cha Mahakama.

WAKILI WA SERIKALI: Shahidi uliulizwa swali hukusiana na hawa watuhumiwa kutolewa nje kwa mahojiano na kwa upelelez. Ifafanulie Mahakama uliposema kwamba mahojiano ni sehemu ya upelelezi.

SHAHIDI: Upelelezi unajumuisha kuwa mtuhumiwa alitolewa atahojiwa, atarekodiwa na ninavyo fahamu mimi mahojiano ni pale mtuhumiwa anapotolewa nje specific kwa kwenda kuhojiwa.

WAKILI WA SERIKALI: Ukasema kwa kusoma kuna utofauti, je utofauti wake nini?

SHAHIDI: Kwamba mahojiano ni tofauti na upelelezi lakini mahojiano ni sehemu ya upelelezi.

WAKILI WA SERIKALI: Kuna swali Mallya alikuuliza kwamba Mahita aliwatoa watuhumiwa kwenda kuwapiga, ukasema siyo kweli. Je ulimaanisha nini?

SHAHIDI: Kwa sababu Afande Mahita hakumtoa kwa sababu ya kupigiwa na kupiga siyo sehemu ya upelelezi.

WAKILI WA SERIKALI: Uliulizwa maswali mengi mengi kuhusiana na abbreviation CDS na CD ukaonyeshwa na PGO, ukasema DR haina makosa na PGO haina makosa. Je, kule Central CD ni kifupisho cha neno gani?

SHAHIDI: CD Kifupisho cha CENTRAL DAR ES SALAAM. Haipatikani kwenye kifupisho cha kituo chochote pale Tanzania nzima.

WAKILI WA SERIKALI: Uliulizwa pia kuwa kituo chako cha kazi Msimbazi na pia kitu gani kinathibitishwa kwamba ulifanya kazi Central.

SHAHIDI: Kwa hapa ni DR ambayo kifupisho chake huwezi kukipata sehemu yoyote Tanzania na kwamba mimi ndiye niliyejaza.

WAKILI WA SERIKALI: Pia ulionyeshwa specific kwenye entry namba 393 ukasema kwamba hakuna sahihi yangu wala jina langu. Je, ni kitu gani kitaonyesha wewe umewahi kufanya kazi Central?

SHAHIDI: Entry inaonyesha mtuhumiwa alichukuliwa na Afande Kingai.

WAKILI WA SERIKALI: Nini kinaonyesha kwamba ulikuwepo siku ile?

SHAHIDI: Uwepo wa mwandiko wangu.

WAKILI WA SERIKALI: Kwenye swali hilo hilo hujafafanua kwamba siyo mtu yoyote anaweza kuandika hicho kitabu.

SHAHIDI: Siyo watu wote waweza …

WAKILI WA SERIKALI: Jikite kwenye entry namba 393.

SHAHIDI: Siyo mtu yoyote anaweza kupata namba ya kesi, kupata details za watuhumiwa.

WAKILI WA SERIKALI: Uliulizwa swali hapa kuhusiana na PIN kukutwa katikati, ukajibu kwamba haikuwepo. Ifafanulie Mahakama haikuwepo wakati gani?

SHAHIDI: Wakati natoa ushahidi mara ya kwanza.

KIBATALA: Objection! Awali lilikuwa alifafanua au hakufafanua.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji nilisikia jibu la ‘pin’ haikuwepo na nataka kufafanua.

JAJI: Alitoa hilo jibu lakini wakili akasema halitaki.

WAKILI WA SERIKALI: Uliulizwa swali ukasema hukufafanua, kwa kuwa ‘pin’ ndiyo umeonyeshwa, ieleze Mahakama ni pini ya namna gani?

SHAHIDI: Mheshimiwa Jaji, ni kipande cha stapler pin ipo Katikati katika ukurasa wa Mohammed Ling’wenya. Ndiyo maana nikafafanua haikuwepo.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji naomba kupewa P1 (barua), Mheshimiwa Jaji naomba kumwonyesha shahidi.

WAKILI WA SERIKALI: Kwa mujibu wa hiyo barua ni kitu gani unaitambua?

SHAHIDI: Nilikuwa nakabidhiwa Detention Register.

WAKILI WA SERIKALI: Kwa hiyo shahidi ulichokuwa unakabidhiwa kwa mujibu wa hiyo barua ni kitu gani?

SHAHIDI: Ni Detention Register.

WAKILI WA SERIKALI: Lipo swali lingine uliulizwa kuhusiana na Physical Condition na ukasema hakuna entry ya Health Condition. Ukasema kwenye D. R hakuna sehemu ya Health Conditions. Ulikuwa unamaanisha nini?

SHAHIDI: Sehemu tulyiokuwa tunatumia physical condition kuandika kwenye Detention Register.

WAKILI WA SERIKALI: Aliuliza wakili kwamba mtu aliye kutishia akiwepo atakuwa na hofu.

SHAHIDI: Ndiyo aliuliza kwamba mtu aliyekutishia akiwepo tishio linaendelea? Nikajibu NDIYO.

WAKILI WA SERIKALI: Uliulizwa kuhusu D. R ukasema DR ni mali ya Polisi. Ulimwambia kuwa unamanisha nini?

SHAHIDI: Nilienda kumuomba mkuu wa kituo, kwamba natakiwa kutoa ushahidi. Akanisainisha kwenye Station Diary.

WAKILI WA SERIKALI: Mheshimiwa Jaji, hatuna tena maswali.

JAJI: Shahidi nakushukuru kwa ushahidi wako. Kuna shahidi mwingine?

WAKILI WA SERIKALI: (Pius Hilla) Kwa leo hatuna shahidi Mheshimiwa Jaji ambaye tupo tayari kuingia kwenye kizimba cha ushahidi. Tunaomba usikilizwaji uahirishwe kwa leo hadi kesho tarehe 23 Novemba 2021 ambapo tutaleta shahidi mwingine.

JAJI: Utetezi?

KIBATALA: Hatuna pingamizi Mheshimiwa Jaji ukizingatia na muda.

JAJI: Kufuatia maombi ya kuomba ahirisho, Mahakama naahjirisha mpaka kesho tarehe 23 saa tatu asubuhi. Upande wa mashitaka wanaelekezwa kuleta mashahidi, na watuhumiwa wataendelea kuwa chini ya Magereza mpaka kesho asubuhi saa tatu.

Jaji anaondoka mahakamani.

Like
3