Nyota ya kinda Kingazi wa Azam FC yaanza kuwakia Uingereza

NYOTA ya mchezaji wa timu ya vijana chini ya miaka 20 (U—20) wa Azam FC, Shaban Kingazi, inaendelea kung’ara na huenda akaonekana akisakata kabumbu katika viwanja vya soka England hivi karibuni.

Shaban ambaye kwa sasa bado yuko kwenye majaribio, akiwa chini ya kituo cha kulea na kukuza vipaji vya soka kwa vijana, kinachomilikiwa na nyota wa zamani wa klabu ya Chelsea na timu ya Taifa ya Uingereza, Dennis Wise.

Dennis, maarufu kwa jina la Taxi alipokuwa uwanjani, akimzungumza uwezo wa Shaban anaeleza kwamba kijana huyo kutoka Tanzania ni msikivu na mwenye tamaa ya kuona anacheza timu kubwa hasa za England.

“Mara zote amekuwa akieleza kwamba anapenda kubaki hapa England ili kusakata kabumbu kwenye timu kubwa, hasa zinazoshiriki ligi kubwa na timu zenye heshima,” anaongeza Dennis.

Jana kinda huyo wa Azam FC, aliyepelekwa London, Uingereza kwa ajili ya kujiunga na kituo hicho, timu ya vijana inayumiwa zaidi na kituo alichojiunga, Combine, ilicheza na timu ya vijana ya Man City. Timu ya Shaban ilifungwa mabao 3-1.

Baada ya mechi kumalizika, Shaban alipongezwa kwa kuwa nyota wa mchezo huo, kwa kufanikisha “kuwalisha” washambuliaji wa timu yake, lakini hawakuweza kumalizia vyema.

Taarifa zinaeleza kwamba kinda huyo amekuwa kiungo mzuri na mwepesi wa kutoa pasi kwa washambuliaji na anatajwa kuwa na kipaji “cha pekee.”

Shaban alifika London, Uingereza Desemba mwaka jana na amekuwa katika majaribio ambayo yanaelezwa na Wise kuwa ya mafanikio makubwa.

Akiwa katika kituo hicho kwa mafunzo ya soka, Shaban atakuwa akishiriki katika mechi nyingi za kirafiki – “akijishikiza” kwenye timu mbalimbali za vijana.

Like
1