Mfuko wa Bima ya Afya wachafuka

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Tanzania Mfuko umeingia katika kashfa nzito ya kukata kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwenye madai ya wamiliki wa hospitali binafsi wanaohudumia wanachama wa mfuko huo.

Kutokana na kashfa hiyo, hospitali nyingi binafsi zimefunga kutoa huduma au kukataa kupokea wagonjwa kwa mfumo huo wa bima ya taifa.

Kashfa kubwa ni NHIF kukata kiasi kikubwa cha fedha zinazodaiwa na zahanati na hospitali binafsi baada ya kutoa huduma kwa wagonjwa.

Inadaiwa kuwa mfumo huo wa bima ya afya ulioanzishwa kisheria, umekuwa ukikata kati ya asilimia 25 hadi 50 kwa kila madai yanayotoka kwa watoa huduma. 

Mmiliki wa zahanati moja jijini Mwanza ambaye hakupenda kutaja jina lake amesema baadhi ya watendaji wa NHIF wamekuwa na utaratibu huo ambao unawaumiza wamiliki wa zahanati na hospitali binafsi.

Alisema NHIF chini ya meneja wa mkoa wa Mwanza, Jaralth Mashashu kwa kipindi cha miaka miwili yaani 2019 na 2020, mfuko huo umegeuka “fimbo ya kuumiza wamiliki wa hospitali” kwa kukata kiasi kikubwa cha feha kutoka kwenye madai yao.

Mmiliki huyo alidai kuwa akipeleka madai Sh. milioni 17, NHIF hukata kiasi cha Sh. milioni tatu au zaidi, jambo ambalo linawatia hasara kubwa kuhudumia wananchi wagonjwa.

“Kwa mfano mimi kwa mwezi uliopita (Oktoba, 2020) nilikuwa nadai zaidi ya Shilingi milioni 19, lakini nilikatwa zaidi ya milioni tano, nililia kabisa, hivi nawezaje kuhudumia wagonja kwa hasara kubwa namna hii,” alilalamika daktari huyo.

Daktari huyo anaeleza kwamba hospitali na hata zhanati zinaweza kupeleka fomu za kutibu wagonjwa 1,000, lakini zaidi ya 200 zikakataliwa bila kuwepo kwa maelezo yeyote.

Hatua hiyo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu na watoa huduma; hasa hospitali binafsi, bila kupewa taarifa yeyote.

Mashashu alipohojiwa na mwandishi wa habari hii, alikanusha na kueleza kwamba madai yao hayana msingi kwani shughuli zote za uhakiki wa malipo hufanywa kwa uwazi na penye matatizo wamiliki uhusishwa.
“Hatuna ugomvi na watoa huduma wetu,” alisisitiza.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuthibitishwa na baadhi ya wamiliki wa hospitali mikoa balimbali, unaonyesha kuwa kila wanapolalamika wamekuwa wakipewa vitisho. 

“Hivi sasa wala hakuna anayelalamika, tumekuwa tukitishwa kusitishiwa huduma au kuletewa ukaguzi wa kina na usumbufu mwingine, ni kero,” alisema mmiliki mmoja wa hospitali kutoka Mkoa wa Arusha. Hakupenda kutajwa jina lake kuhofia “adhabu na vitisho.”

Wamiliki hao pia wamekuwa wakilalamikia kucheleshwa kwa malipo hayo na kwamba hukaa muda mrefu zaidi.

Kwamba kila malipo yanapopokewa, huchukua miezi miwili hadi mitano ndipo hulipwa.

“Wanapotucheleweshea malipo, nasi tunapata shida kulipa madaktari, manesi na wahukumu wengine, kununua dawa na mahitaji mengine, kwa kweli ni shida kubwa,” alisema mmiliki wa zahanati moja mkoani Pwani.

Uchunguzi umebaini kwamba kutokana na sababu hizo, baadhi ya wamiliki wa hospitali wamekuwa wakikataa kuwatibu wagonjwa wenye kadi za NHIF na wengine kukataa kutoa baadhi ya huduma, ikiwamo zile zenye gharama kubwa. 

Inaelezwa sababu kubwa kwa baadhi ya hospitali kushindwa kutoa huduma au dawa zenye gharama kubwa ni NHIF kugoma kulipa huduma hizo wanapopelekewa madai.

Kwamba madai hayo halali, hutolewa katika orodha ya malipo kwa maelezo kwamba “hakukuwa na sababu kwa hospital kuwapa wagonjwa dawa au huduma hizo.”

“NHIF kuna shida, madai yenye huduma za gharama kubwa hukataa kulipa kwa madai kwamba mgonjwa au wagonjwa hawakupaswa kupewa, hivyo mara nyingi inakuwa hasara kubwa kwetu,” anaeleza mmoja wa wamiliki wa hospitali moja wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Mmiliki huyo anaeleza kwamba NHIF imekuwa ikilazaimisha wagonjwa wapewe ‘antibiotic’ za bei ndogo, hata kama hazina uwezo wa kutibu mgonjwa, hatua ambayo hulazimiha wamiliki kuifata ili kuepuka hasara, lakini mgonjwa haponi.

Chama cha wamiliki wa hospitali binafsi nchini (APHFTA) kimekuwa kikiungana na wanachama wake kulalamikia hali hiyo, lakini taarifa zilizopatikan kwa SAUTI KuBwA zinaeleza kwamba wamekuwa hawasikilizwi, hatua ambayo inawakaisha tamaa.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Benard Konga (pichani juu), alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa adai hayo, alikiri kukumbana nayo, lakini akaeleza wengi wanaolalamika hukosea kufuata masharti na taratibu za makubaliano ya mkataba baina ya mfuko na wamiliki binafsi wa hospitali.

Kuhusu vitisho, Konga alisema ni kosa kwa mtumishi wa NHIF kutoa vitisho vya aina yoyote kwa watoa huduma na kwamba mfuko una sheria kali za kushughulikia na tuhuma hizo.

“Sababu kubwa nyingine ni kutofuata mkataba wa utoaji huduma, ambapo ndani yake kuna orodha ya bei ya dawa na huduma zingine za afya, lakini wapo wasiofuata na wao huanza kulalamika bila sababu za msingi,” aliongeza.

Pia alieleza kuwepo kwa udanganyifu kwa baadhi ya watoa huduma, kiasi kwamba madai yao yanapokataliwa huanza kulalamika na kwenda kwenye vyombo vya habari kuwa wameonewa. Konga aliteuliwa kushika wadhifa huo mwaka 2017.

Taratibu za kumpatia huduma mwanachama zinaonyesha kwamba watoa huduma hulazimika kumuhakiki mwanachama kupitia mfumo wa kutoa namba ya uhakiki kabla ya kuanza kupatiwa huduma, ikiwa namba hiyo haijapatikana, hakuna huduma inayoeza kutolewa. Na endapo itatolewa na madai kupelekwa NHIF, basi mfumo hukataa kupitisha malipo kwa anayedai.

Uchunguzi uliofanywa na SAUTI KUBWA umebaini kwamba hadi kufikia Desemba mwaka jana, NHIF ilikataa malipo ya Sh. bilioni 4.46 kutoka madai ya gharama za matibabu, uchuguzi na dawa kutoka zahanati, vituo vya afya, hospitali na hopitali za rufaa katika mamlaka za serikali kutokana.

Sababu zilizoelezwa na NHIF ni makosa ya kujaza taarifa za wagonjwa pamoja na kutozingatia taratibu kama vile idhini batili, kutozingatia miongozo ya matibabu, kutoonesha vipimo vya utambuzi na kuingizwa kwa huduma ambazo hazikuwa katika mfuko.

Katika hatua nyingine, NHIF ni miongoni mwa taasisi za umma ambazo hazikuwasilisha taarifa zake kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Umma (CAG), hatua ambayo ililazimu Spika wa Bunge kuamru kuwasilishwa kwa sababu za kutofanya hvo kupitia Kamati ya Bunge ya Fedha za Umma (PAC).

Ripoti ya CAG ya mwaka 2018/19 ilionyesha kwamba NHIF ilikuwa na upotevu wa fedha unaofikia Sh. bilioni 3, ambazo hazikuwa na maelezo ya kuridhisha.

Like