“Nimenusa kwapa la shetani”

HILI NI ANDIKO LA PILI KATIKA MFULULIZO WA MAKALA ZA ndugu Bollen Ngetti KUHUSU KILE ANACHOITA GENGE OVU LILILOTUMIWA NA UTAWALA ULIOPITA KUTESA, KUTEKA, KUFILISI, KUUMIZA NA KUUA RAIA WALIOUKOSOA. YEYE NI MMOJA WA WAATHIRIKA HAO. Endelea.

BADO niko katika ngwe nzito ya kujadili mwenendo wa Mhimili wa Shetani (devil axis) yani lile genge hatari la “Sukuma Gang” lililogoma kuamini kuwa hii ni Serikali Awamu ya Sita na inaongozwa na “Iron Lady” Rais Samia Suluhu Hassan. Bado mawakala hawa wa shetani wanateswa na “hangover” ya utawala wa Pombe.

Genge hili halijafa na kama ni nyoka bado anatikisa mkia jambo ambalo si salama kwa muuaji. Ni lazima lipondwe kichwa kisawa-sawa hadi ujiridhishe kuwa kafa na kisha kumfukia ardhini.

Watoto hawa wa Ibilisi wanafanya kila hila ili tu Iron Lady aonekane amepwaya na hivyo umma umkumbuke Mpita Njia.

Sasa limekuja na injili kuwa ujambazi unarudi kwa kasi jambo ambalo halikuwepo katika Utawala wa Mtwaliwa Pombe Magufuli. Injili hii inakolezwa tofauti na Iron Lady, Rais Samia Hassan alivyolieleza kabla ya kumtoa Mambosasa Dar.

Ninaomba niweke jambo hili sawa (clear). Kwanza ieleweke kwamba si kweli kwamba awamu iliyopita hakukuwa na ujambazi. Ondoeni huo uongo katika historia.

Ni afadhali ujambazi wa mtu binafsi ambao ndio SSH ametaka uondoke kuliko ujambazi unaofanywa na dola. Hivi, kama askari aliyevalia sare za Jeshi anakuja na kuvamia duka lako mchana kweupe (maduka ya kuuzia fedha) huku Arusha na kupora fedha zako huu si ujambazi?

Kama Afisa wa TRA anakwenda kinyemela na kusomba fedha zako kwenye akaunti bila ridhaa yako si ujambazi? Kama wafanyabiashara wanafunga biashara zao na kukimbilia ughaibuni, wanaogopa nini kama si majambazi?

Lakini pia hata kama wangekuwepo majambazi wa watu binafsi ni chombo gani cha habari kingethubutu kutangaza ili ionekane Serikali imeshindwa kazi? Nani angejaribu. Tuliojaribu tulijikuta jela na mateso juu!

Lingine la msingi ambalo nalipasha kwapa hili la shetani ni kwamba, uliona wapi jambazi akimfuata omba-omba fedha barabarani kwa bunduki? Kama matajiri wameporwa fedha zao, wamefanywa kuishi kama mashetani jambazi aende kujambazi nini? Lakini sasa waliopokwa fedha zao wamerudishiwa, wanatumia hadharani, kwa nini jambazi asimshambulie tajiri?

Tumeona kijana mfanyakazi wa Vodacom majuzi amevamiwa na kuuawa na majambazi kwa kuwa alitoka benki kutoa fedha si zaidi ya milioni 5 kwa mujibu wa taarifa za mitandao. Huko nyuma nani angethubutu kutoa hela kiasi hicho bila “kuhojiwa?”.

Siungi mkono ujambazi. Ni lazima udhibitiwe kwa nguvu zote. Kila mtu awe na pato halali si unyang’anyi. Lakini ni dalili kiwa wenye fedha zao sasa wanatumia kwa Uhuru.

Nia ya genge hili ni kutuma salamu kwa wawekezaji walioanza kuingia nchini kuwekeza kwamba, “hali ya usalama si nzuri Tanzania. Ujambazi umeongezeka”. Pumbavu wakubwa! Nia ya ajabu kabisa!

Hili nalo mtashindwa. Iron Lady analisuka Jeshi la Polisi pamoja na TISS wala hamtosikia matukio hayo ya ujambazi. Hadi sasa nchi ni tulivu, Amani imetamalaki, Iron Lady anapiga kazi na tunamuunga mkono 100%. Hakuna wa kumkwamisha maana atakwama yeye!

Kumbukeni enyi uzao wa Shetani. Tunawajua kwa majina. Baadhi yenu mlipewa vitambulisho hewa vya Idara Nyeti ili kuwatisha watu. Ndio mliopewa bakshishi kuimba ule wimbo kichaa wa “tubadili Katiba Mpita Njia aongezewe muda”. Wendawazimu wakubwa.

Kama alivyotoa wito KM wa CCM kwamba chama kinataka kuona umoja na mshikamano wa Watanzania, nami nawapa rai kwamba kubalini kwamba hii ni awamu ya sita na Rais ni Samia Suluhu Hassan, Magufuli hayupo. Njooni tumuunge mkono tuijenge nchi yetu iliyotobolewa na mtangulizi. Acheni hisia za hujuma. Kwa bahati nzuri tunajua njama zenu kabla hamja-apply! Tulieni mpate “chanjo” ya akili. Part II ya andiko hili nitawataja kwa majina yenu na vikao vyenu. Amina!
Maoni: 0683 226539

Like
1