“Nenda zako shetani”

UCHAMBUZI HUU MFUPI UMEANDIKWA NA Dk Chris Cyrilo NA KUSAMBAZWA MITANDAONI LEO KAMA SEHEMU YA MJADALA ULIOSABABISHWA NA RAIS JOHN MAGUFULI KATIKA HOTUBA YAKE KWA WAAMINI BAADA YA MISA KATIKA KANISA LA MT. PETRO, DAR ES SALAAM. Endelea.

RAIS Magufuli ana jopo la Madaktari bingwa Tanzania. Wanamzunguka kuhakikisha anabaki katika afya bora. Hiyo ni kawaida dunia nzima, kwamba afya ya viongozi wa nchi inalindwa kwa kadiri inavyowezekana.

Rais Magufuli analindwa na makomandoo waliofuzu medani za juu za mapambano. Makomandoo hao wanaingia naye hadi Makanisani, na Misikitini pindi anapoingia. Hii ni kawaida kwa kiongozi wa nchi. Anapaswa kulindwa kwa ‘udi na uvumba’.

Rais Magufuli analindwa na mitambo ya kisasa yenye teknolojia kubwa kabisa. Nayo anaingia nayo kanisani kumuomba Mungu. Hii pia ni kawaida.

Jambo lisilo la kawaida ni pale Rais anapotuambia tumtumainie Mungu kupambana na janga la Covid halafu anawananga wanaovaa barakoa.

Kuvaa barakoa ni mbinu mojawapo ya kupambana na Covid. Ni sawa na kuambatana na madaktari bingwa wenye vifaa tiba vya kisasa kabisa kila mahala ili kuwa na msaada wa kiafya mara tu unapohitajika. Ni sawa na kuzungukwa na walinzi waliofuzu medani za juu za mapambano. Ni sawa na kuambatana na mitambo ya ulinzi ya kisasa kila mahala.

Je! ikiwa Mungu anaweza kutulinda dhidi ya Covid bila sisi waja wake kuchukua hatua kama kuvaa barakoa, kwanini huyo Mungu asimlinde Magufuli bila madaktari bingwa, bila makomandoo na bila mitambo ya kisasa?

Mungu aliyepo kichwani mwa Rais Magufuli ni Mungu kigeugeu? Ni Mungu asiye na misimamo? Ni Mungu asiyejielewa?

Basi Yesu akamjibu Pilato; kutoka Yohane 18:36-37; akasema, “Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini sasa ufalme wangu si wa hapa.”

Hapo Pilato akamwambia, “Basi, wewe ni Mfalme?” Yesu akajibu, “Wewe umesema kwamba mimi ni Mfalme.

Ufalme wa Rais Magufuli kama ulivyo ufalme wa Wafalme’ wengine ni wa hapa duniani. Ndio maana anajilinda kwa mbinu za kidunia; Madaktari na teknolojia zao, makomandoo na teknolojia zao. Ni Mambo ya kidunia. Yesu hakulindwa na jeshi lolote kwakuwa hakuwa mfalme wa dunia. Yeye hakuwa wa dunia hii (kwa maneno yake mwenyewe). Ndio maana alikamatwa bila ukinzani, akasurubiwa bila ukinzani, akafa bila ukinzani.

Mwanadamu anayeamini kwamba Mungu anaweza kumlinda bila kujichujukulia hatua za kujilinda, atasurubiwa bila ukinzani, na atakufa bila ukinzani. Atakutana na kile alichokutana nacho Yesu, wakati yeye si Yesu.

Rais Magufuli anajua hilo, ndio maana analo jeshi la kumlinda – madaktari bingwa na vifaa tiba vyao, makomandoo na vifaa vita vyao.

Ajabu ni pale anapowashangaa watu wanaovaa barakoa kujilinda na Covid huku akihubiri eti Mungu hashindwi! Ni kweli Mungu hashindwi lakini Mwanadamu anashindwa. Mwanadamu asiyechukua hatua dhidi ya Covid atashindwa kwa sababu anamjaribu Mungu wake. Rais Magufuli anapojilinda dhidi ya hatari za kidunia kwa mbinu za kidunia anafanya sahihi, lakini anawazodoa wanaojilinda na Covid kwa kuvaa barakoa, ni kama anawataka wavue barakoa ili wamjaribu Mungu wao.

Mathayo 4: 5-7
”Kisha Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, mji mtakatifu, akamweka juu ya mnara wa hekalu, akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini; maana imeandikwa: ‘Mungu atawaamuru malaika wake kwa ajili yako; watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe.’” Yesu akamwambia, “Imeandikwa pia: ‘Usimjaribu Bwana, Mungu wako.”

Usimjaribu Mungu wako kwa kutochukua hatua za kujilinda dhidi ya Covid eti kwa imani kwamba Mungu atakuokoa. Yesu alikataa kujitupa chini pamoja na kwamba maandiko yalisena malaika watamuokoa. Alikataa kumjaribu Mungu Baba.

Mathayo 4: 8-10
“Kisha Ibilisi akamchukua mpaka juu ya mlima mrefu, akamwonesha falme zote za ulimwengu na fahari zake, akamwambia, “Hivi vyote nitakupa kama ukipiga magoti na kuniabudu.” Hapo, Yesu akamwambia, “Nenda zako Shetani!

NENDA ZAKO EWE SHETANI. Mnafiki mkubwa shetani. Acha kujilinda kwa mitutu ya bunduki kwakuwa imeandikwa ‘Mungu atawaamuru malaika wake kwa ajili yako; watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe’.

Nawatakia Jumapili njema!

Like
1