Mwinyi azongwa na aibu ya “urais wa damu”

SASA kuna kila dalili kwamba Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anazongwa na aibu ya kuongoza bila ridhaa ya wananchi. Ameamua kuomba kuungwa mkono na mshindani wake katika nafasi ya urais wa visiwa hivyo, Maalim Seif Sharif Hamad. 

Taarifa za uhakika zinaeleza kwamba Dk. Mwinyi amemuomba Mufti wa Zanzibar, Salehe Kaab, kukutana na Maalim Seif ili kuomba muda wa kukutana na kuzungumza.

Chanzo chetu  kimeeleza kwamba Mufti Kaab tayari ameomba kumuona Maalim Seif, ingawa bado hajapewa majibu kutoka kambi ya Maalim Seif.

Taarifa kutoka ndani ya Ofisi ya Rais wa Zanzibar zinathibitisha hili, ingawa hakuna habari zaidi ya mleta habari kuthinitisha kwa maneno machache: “Zanzibar ni moja, ni nchi yetu, wewe umepata wapi hii habari na je, hupendi amani na maendeleo?”

Inadaiwa kwamba Dk. Mwinyi anataka kuona Zanzibar anayoiongoza ikiwa na maendeleo makubwa ya pamoja na kuondoa Upemba wala Uzanzibari.

Kambi ya Maalim Seif imeeleza kuwa na taarifa hizo, lakini hajui kama aliyetumwa kufikisha ujumbe ni Mjfti Keeb.

Msemaji wa chama cha  ACT-Wazalendo, Salim Bimani  amesema; “taarifa tunazo, lakini hatujajua lini na wapi haya mambo yatafsnyika. Tutatoa taarifa zaidi yakitokea.”

Dk. Mwinyi alitangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwa mshindi wa urais kwa zaidi ya asilimia 76, huku Maalim Seif akiambulia asilimia 19. Haijawahi kutokea katika historia ya uchaguzi na siasa Zanzibar kwani wafuasi na wanachama wa vyama vikubwa vya siasa hukaribiana mno.

Maeneo mengi siku ya Oktoba 27 na 28, wakati wa kupiga kura, kulitokea vurugu zilizoanzishwa na vyombo vya usalama kwa kupiga watu hovyo.  Tayari kuna ripoti za baadhi ya watu kupoteza maisha.

Mashirika ya kimataifa na mabalozi wengi wa nchi za nje Tanzania, wamelaani namna uchaguzi ulivyoendeshwa, huku wakilaani serikali kukiuka haki za binadamu wakati wa kampeni, kupiga kura na hata kutangazwa kwa washindi.

Like