Mimi ndiye rais, Samia aonya makundi

RAIS Samia Suluhu Hassan ameonya makundi ya watu wanaodaiwa kushiriki njama dhidi yake, hasa wanaodharau au kutilia shaka jinsi ya kike katika uongozi wa nchi; akasisitiza kuwa, “mimi ndiye rais.”

“Kwa wale ambao wana mashaka, ‘mwanamke huyu ataweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?’ Nataka niwaambie aliyesimama hapa ni rais… nataka nirudie, aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye maumbile yake ni mwanamke.”

Ametoa kauli hii leo jioni jijini Dodoma wakati akitoa salamu zake kwa umma katika maombolezo ya kitaifa ya John Magufuli, aliyekuwa Rais wa Tanzania.

Mara baada ya Rais Samia kutamka maneno hayo, umati wa waombolezaji ulipiga makofi kwa dakika tatu kushangilia.

Baadhi ya wachambuzi wanasema kauli hii inabeba tafsiri pana, na inaashiria kuwa Rais Samia anatambua kuwa wapo baadhi ya watu ndani ya mfumo ambao wanasemekama kutaka kumhujumu kwa dharau tu na hisia za kijinsia kwa vile yeye ndiye rais mwanamke wa kwanza Tanzania.

Hata kabla Samia hajatangaza kifo cha Rais Magufuli wiki iliyopita, kulikuwepo na tetesi kuwa baadhi ya viongozi wa serikali na hata katika vyombo vya usalama, walikuwa katika mpango wa kuvunja katiba ili kumhujumu asiwe rais.

Zipo taarifa kuwa sehemu ya wapambe wa Magufuli, hasa watokao Usukumani ambao aliwachomeka kwenye nafasi nyeti, hususan katika Idara ya Usalama wa Taifa, walikuwa wanataka nchi iongozwe na “mtu wao” ili kulinda maslahi yao na urathi wa Magufuli.

Kwa upande mwingine, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilisimamia katiba na kutaka Samia ndiye awe rais kama katiba isemavyo.

Wengine waliomtaka Samia ni viongozi waandamizi ndani ya vyombo hivyo na wastaafu katika chama, ambao hawakuwa na sauti wakati wa utawala Rais Magufuli.

Taarifa zinasema hata namna Samia alivyotangaza kifo ilionyesha kasoro kubwa iliyoashiria kuwa alikuwa anawahi kuwapiku waliokuwa wanapanga njama za kuvunja katiba.

Tofauti na kawaida, tangazo lake halikurushwa mubashara bali lilirekodiwa na kutumwa kwenye chombo cha habari. Pili, Samia alikuwa peke yake bila kiongozi yeyote wa serikali au chombo cha dola. Tatu, hata Televisheni ya Taifa (TBC) haikupiga Wimbo wa Taifa kama ilivyo desturi.

Nne, hata baada ya Samia kuwa ametangaza kifo cha Magufuli, mifumo ya mawasiliano haikutangaza siku ya kuapishwa kwake kwa uzito unaotarajiwa, kwani wakati mitandao ya kijamii ilisambaza taarifa hizo siku moja kabla, Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilitangaza kesho yake asubuhi ya siku ambayo Samia alipaswa kuapishwa.

Hata hivyo, kauli hii ya Rais Samia inasisitiza kile alichosema awali siku alipoapishwa, ambacho pia kilirudiwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kuwa, “nchi ipo katika mikono salama.”

Na ujumbe wake huu unasisitiza kuwa uongozi ni karama kwa kufuata katiba, sheria na miongozo, siyo kuangalia jinsi ya mhusika au maumbile yake.

Msomi na mwanaharakati wa jinsia na haki za kiraia, Leticia Mukurasi, amesema: “Ilikuwa lazima akemee chokochoko juu ya uwezo wake kuwa rais ambao unajadiliwa kwenye mitandao mingi; mpaka watu wamediriki kutumia maandiko matakatifu kuhalalisha dhana kuwa wanawake hawastahili kushika nafasi za uongozi. Lugha aliyotumia ndiyo inafaa kwa hali hii, yaani ametumia lugha ya ‘oppressor’ kumkabili ‘oppressor’ mwenyewe.”

Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema kauli ya Rais Samia, akiitoa kwa taifa, mbele ya vyombo vyote vya usalama, marais wa nchi jirani na umma, ni ishara kwamba anapeleka ujumbe kwamba yeye ni amiri jeshi mkuu.

“Ujumbe wa Rais Samia ni sauti ya mamlaka ya mkuu wa majeshi yote, inaonya, inakemea na inatisha wote wenye dharau kwa wanawake,” anaongeza msomi huyo wa fani ya sayansi ya siasa ambaye hakupenda jina lake litajwe na SAUTI KUBWA.

Otela Magele, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Society for Poverty Eradication (Taspe), Dar es Salaam akichambua kauli hiyo ya Rais Samia, anasema kiongozi huyo wa nchi anafikisha ujumbe mapema ili wasaidizi wake wasijaribu kumkwamisha kwa kisingizio kuwa ni mwanamke.

“Hii kauli ni ujumbe wenye makali, huenda anapeleka mamlaka yake kwa wote wanaodhani atashindwa kazi kwa kuwa ni mwanamke, naamini kuna watu anawapa msimamo wake, lazima wajipange,” anasema Otela.

Anasema wasaidizi wa rais, Ikulu, na hata ndani ya baraza la mawaziri, wenye hulka ya kudharau wanawake, wanapaswa kujipanga upya na kufuta “dharau” zao dhidi ya wanawake endapo wanataka kuendelea kufanya kazi na Rais Samia.

SAUTI KUBWA ina majina ya baadhi ya vigogo wanaomdharau Rais Samia tangu akiwa makamu wa rais, na wamekuwa wanasikika wakitoa maneno ya kajeli juu ya uwezo wake wa kuongoza nchi. Kwa sasa tunaifadhi majina yao.

Like
4