Messi anusuru biashara ya Michael Jordan

UJIO wa Messi katika klabu ya Paris Saint-Germain, unatarajiwa kuwa na faida kubwa si tu kisoka bali pia kibiashara klabuni hapo na nje ya klabu.

Hii inakuja kama habari njema kwa mchezaji nguli wa zamani wa kikapu nchini Marekani (NBA) Michael Jordan, aliyetamba na timu ya mpira wa kikapu ya Chicago Bulls, ambaye kupitia kampuni yake inayofahamika kama Nike’s Jordan Brand, aliingia ubia wa muda mrefu na timu ya PSG kuzalisha jezi za timu hiyo kuanzia msimu wa mwaka 2019/20, kwa makubaliano ya kupokea asilimia tano katika kila jezi ya PSG itakayouzwa sokoni.

Tarehe 25, mwezi Machi mwaka huu, gazeti la Chicago Sun Times, liliripoti kuwa kampuni ya Nike’s Jordan Brand, ilipata hasara ya asilimia ishirini na nne ya mapato yake yote, kutokana na athari ya janga la UVIKO-19, huku thamani ya kampuni hiyo ikishuka kutoka dola za Kimarekani bilioni 2.1 mpaka dola bilioni 1.6.

Ujio wa Leo Messi PSG akitokea Barcelona mwanzoni mwa juma lililopita, unatarajiwa luongeza mauzo ya jezi za PSG milioni 2.5 msimu huu, zikiwa na jina la Messi. Mauzo haya yataitengeneza kampuni ya Michael Jordan, kitita kikubwa cha fedha kwani ndani ya wiki moja tu baada ya usajili wa Leo Messi, Michael Jordan ameingiza kiasi cha Euro milioni 6, kutoka kwa PSG ambao ndani ya wiki hiyo, wameuza jezi milioni 120.

Michael Jordan anatarajiwa kupata faida ya mabilioni ya dola, kwani kadri siku zinavyozidi kusonga mbele, mauzo ya jezi yanatarajiwa kuongezeka maradufu kutokana na uhitaji wa jezi hizo kuwa mkubwa sana sokoni.

Like
1