Membe apuuza “machozi ya mamba” ya Musiba

“MACHOZI ya mamba” yanayomtoka mtukanaji wa vigogo, Cyprian Musiba, aliyewahi kutamba na kujiita mwanaharakati huru katika serikali ya awamu ya tano, yatapotea bure, SAUTI KUBWA imebaini.

Taarifa za uhakika ambazo SAUTI KUBWA inazo, zinadai kuwa Musiba amewaendea maaskofu watatu akiwa analia, akaomba wamtetee asilipe Tsh 9 bilioni ambazo mahakama imeamuru alipe baada ya kushindwa shauri lililofunguliwa na Bernard Membe, mmoja wa vigogo waliodhalilishwa na Musiba miaka kadhaa iliyopita.

Chanzo cha habari kimesema: “Musiba anadai kuwa mkewe ni mjamzito, na kwamba alizimia baada ya kusikia hukumu ya mahakama ambayo inampa siku 14 awe amemlipa Membe kiasi hicho, la sivyo mali zake zote zitanadiwa.

“Ndiyo gia yake ya kujinusuru. Ameomba viongozi hao wa dini wamwombee msamaha kwa Membe ili asilipe madai hayo, lakini Membe amegoma akisema hawezi kuingia kwenye mtego wa ujanja wa kutumia dini kulea uhalifu.”

Vyanzo vilivyo karibu na Membe vimesema kuwa Membe amesema kuwa Musiba ana wajibu mmoja kwa sasa – kutubu kwa Mungu na kutekeleza hukumu ya mahakama. 

Amesisitiza kuwa kinachompata Musiba sasa ni adhabu ambayo Mungu ameamua kumpa kupitia kwa Membe, na kwamba Mungu mwenyewe ndiye atatoa msamaha, ambao hauzuii mhusika kulipa anachodaiwa.

Adhabu hiyo, kwa mujibu wa waliomnukuu Membe, haimhusu Musiba pekee bali pia wahalifu wengine walioumiza na kuchafua watu kwa kisingizio cha kutetea rais. Miongoni mwao ni vigogo waliomfadhili Musiba katika harakati hizi za kutukana na kuchafua watu.

“Musiba hakujituma. Alikuwa anafadhiliwa na vigogo. Mmoja alikuwa rais, na mwingine alikuwa katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).  Mmoja kafa, mwingine yupo hai. Huyo aliyekuwa anamtuma na kufadhili uhalifu wake ndiye alimponza, na ndiye anapaswa amlilie badala ya kusumbua maaskofu,” alisema waziri mstaafu aliye karibu na Membe.

Rais anayetajwa ni John Magufuli, ambaye aliaga dunia Machi 17, 2021. Katibu mkuu anayetajwa ni Dk. Bashiru Ali, ambaye wakati Magufuli anafariki dunia alikuwa ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Uteuzi wake ulitenguliwa mara baada ya Rais Samia Suluhu kuingia Ikulu, na kumekuwepo taarifa ndani ya duru za serikali kuwa aliondoka na visasi, na amekuwa anahusishwa na hujuma kadhaa dhidi ya serikali ya awamu ya sita.

Rais Samia alimteua kuwa mbunge, na baadhi ya wafuatiliaji wa mambo ndani ya serikali wanadai kuwa siku moja baada ya kuondolewa Ikulu, Dk Ali alifunga moja ya akaunti zake nono iliyokuwa na mabilioni ya shilingi, akayahamishia “kusikojulikana,” – jambo ambalo limekuwa linachunguzwa.

Wafuatiliaji wake wanadai kuwa sehemu ya pesa hizo ilikuwa inatumika katika kufadhili “matusi ya Musiba.” Mmoja wa viongozi waandamizi wa CCM amesema:

“Dk Bashiru, akiwa katibu mkuu, alitumia magazeti ya Musiba kama ushahidi wa kumfukuza uanachama Membe na kudhalilisha wazee wetu akina (Abdulrahman) Kinana na (Yusuf) Makamba. Ilikuwa dhahiri kuwa Bashiru na mwenyekiti wake ndio walimpa kazi Musiba, halafu wakatumia magazeti yake kumwonea Membe na kumfukuza.

“Sasa ona jinsi Mungu alivyo mkubwa, Magufuli kafa, Bashiru kafukuzwa Ikulu, Membe karudishiwa uanachama na kashinda kesi, na Musiba anatapatapa. Sasa, si aende kwa Bashiru amsaidie? Na tunasikia lile genge lao linamtanguliza Bashiru kubeba ajenda hasi dhidi ya Samia, huku likitumia nguvu kubwa kupenyeza ushawishi ili arejeshwe serikalini kwa malengo ya 2025. 

“Walitesa watu sana, waliiba sana, walidhulumu sana, walikuwa na jeuri sana kana kwamba wamenunua nchi na wanafanya watakavyo. Ghafla, ukurasa ukabadilika. Hawaamini hata haya yanayomkuta kijana wao Musiba, maana hawakuyatarajia.”

Baadaye SAUTI KUBWA imempata Membe. Amesema alikuwa safarini, kwamba asingeweza kuzungumza kwa kuwa alikuwa ndani ya ndege. Lakini amesema kwa kifupi: “Musiba analia machozi ya mamba. Atekeleze hukumu ya mahakama. Alipe, basi!”

Miongoni mwa mali za Musiba ambazo zipo hatarini kupigwa mnada ni magari, mashamba na nyumba zake kadhaa  zilizopo Dodoma, Mara, Pwani na Dar es Salaam, nyingine zikiwa za kifahari. Nyingine ni mitambo aliyokuwa anatumia kuchapisha magazeti yake, ambayo Rais Magufuli aliitaifisha kwa kampuni moja kongwe ya magazeti akampatia Musiba.

Chanzo kimoja kimeieleza SAUTI KUBWA kuwa moja ya akaunti za Musiba imekutwa na pesa taslimu zipatazo Tsh 3 bilioni. 

“Kabla ya Magufuli kuwa rais, Musiba alikuwa lofa tu. Haya yote alipewa kwa kazi maalumu ya kushambulia na kudhalilisha watu kadhaa waliokuwa wanamkosoa Rais Magufuli. Hakuwa mwanaharakati huru bali kibaraka wa Ikulu ambaye alilipwa fedha nyingi za walipakodi na kupewa bure raslimali nyingi za umma. Sasa alipe, hana kisingizio,” amesema waziri mmoja mwandamizi.

Mitandaoni, kumekuwa na mijadala isiyokoma, baadhi ya watu wakihoji sababu ya viongozi wa dini kujiingiza katika utetezi wa Musiba wakati walikaa kimya alipokuwa anadhalilisha watu.

Musiba mwenyewe amegoma kuomba msamaha kwa Membe akidai kuwa hawezi kumpigia magoti kwa sababu hayo yalimpata wakati akiwa “anatumikia taifa.”

Shauri hilo lilidumu kwa miaka minne na nusu, huku Musiba akionyesha jeuri na dharau kwa wadai na hata kwa mawakili wake. Katika hatua za baadaye, aligoma hata kufika mahakamani.

Like