FREEMAN MBOWE, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ameguswa na utaratibu wa wanachama wa Chama hicho, Kata ya Kasunzu, jimbo la Buchosa, mkoani Geita, wa kusaidiana na kufarijiana wao wao pamoja na chama chao.
Utaratibu huo unaojulikana kama “Chadema Family” unahusu wanaChadema kusaidiana katika nyakati za shida na raha ikiwemo kuchangiana na kushirikiana katika misiba, ugonjwa, sherehe na kuendesha miradi ya pamoja ya kusaidiana wao kwa wao kiuchumi na kijamii, ikiwa ni pamoja kuchangia chama chao.
Chadema Family inatajwa kuwa imara katika baadhi ya majimbo nchini ikiwemo jimbo la Nyamagana mkoani Mwanza na Ukonga Dar-es-Salaam..
Leo asubuhi, akizindua mradi wa pikipiki ya miguu mitatu (Guta), ya kubebea mizigo, iliyonunuliwa kwa michango ya wana Chadema Family wa kata ya Buchosa, pamoja na mradi wa ujenzi wa ofisi ya Chadema ya kata hiyo, Mbowe, aliwapongeza na kutoa tamko kuwa wamepata funzo kubwa la kuanzisha mfumo wa Chadema Family nchi nzima.
“Ahsanteni kwa mapokezi mazuri na mema yote mliyonifanyia mimi na msafara wangu. Hongereni kwa kununua chombo cha usafiri kwaajili ya kunyanyua mapato yenu wanachama na ofisi zetu za Kazunzu. Hongereni kwa utaratibu huu wa kupendana, kufarijiana, kujaliana kusaidiana mnapopata misiba, maradhi, sherehe na kuchangishana kwaajili ya mambo ya kiuchumi na kijamii, utaratibu huu mzuri tunauita Chadema Family,”
alisema Mbowe na kuongeza:
“Sisi ni viongozi wa kitaifa, lakini tumepata funzo kubwa kutoka kwenu. Yale mazuri tutayachukua ili tuweze kujenga Chadema Family nchi nzima. Ahsanteni na Mwenyezi Mungu awabariki na kuwazidishia.”
Katika mkutano huo, Mbowe, alizungumzia umaskini mkubwa wa kipato unaowakabili wananchi na pamoja huduma duni za kijamii, ikiwemo afya na maji, ambapo aliwahakikishia kuwa Chadema inao uwezo wa kutosha wa kuwaletea mabadiliko ya kimaendeleo kwa kutumia vizuri mapato ya serikali na raslimali nyingi zilizopo nchini.