Mafuriko ya Chadema Buchosa

– Wananchi wakataa mkataba wa bandari

WAWEZA kusema ni “mafuriko” kwa namna maelfu ya wananchi walivyojitokeza katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jimbo la Buchosa, mkoa wa Mwanza.

Akihutubia wananchi hao leo katika eneo Nyehunge, Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, alifanya uchambuzi wa mkataba baina ya Tanzania na Dubai unaohusu uwekezaji wa bandari na maeneo mengine mahsusi ya kiuchumi, na kujenga hoja kuwa unahatarisha maslahi ya taifa, hususani ya upande wa Tanganyika.

Mbali ya kuchambua mkataba huo, Mbowe
aliongoza kura ya wazi iliyowapa wananchi fursa ya kuukubali au kuukataa mkataba huo.

Mbowe aliwaeleza wananchi jinsi watu wengine mashuhuri wakiwemo makada wa CCM walivyopinga mkataba huo, akiwemo Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, mbunge mstaafu wa Muleba na Waziri wa zamani, Profesa Anna Tibaijuka na mwanazuoni wa taaluma ya sheria, Profesa Issa Shivji.

“Profesa Anna Tibaijuka alisema CCM ni chama changu lakini mkataba huu hapana, unauza nchi, unauza uhuru wa nchi, wao wakamsema kuwa anamuonea wivu mwanamke mwenzie kwa kuwa Rais. Haya, Warioba pia aliwaambia kwamba CCM ni chama changu, lakini mkataba huo hapana, haufai, unaumiza nchi, lakini naye wakampuuza wakamwambia wee Mzee unazeeka vibaya”, alisema Mbowe na kuibua vicheko uwanjani.

Akianza na wale wanaokubaliana na msimamo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa mkataba huo ni mzuri na hauna, tatizo, Mbowe aliuliza, yeyote anayekubaliana na CCM anyooshe mkono wake juu, lakini hakuna mwananchi yeyote aliyeonyesha ishara ya kuunga mkono mkataba huo.

Hata hivyo, uwanja mzima ulipunga mikono juu kuunga mkono msimamo wa Chadema wa kupinga mkataba huo.

Aidha, Mbowe aliwaongoza wananchi kushika vichwa na kupiga ukunga kulaani hatua ya serikali kuingia mkataba huo, aliosisitiza kwamba unahatarisha maslahi ya nchi kwani umekabidhi bandari zote 54 za Tanganyika ziwe chini ya kampuni ya Dubai milele kutokana na mkataba huo kutokuwa na ukomo.

“Ukomo wa mkataba huu ni mpaka maji yote ya bahari na maziwa yakauke. Na mkataba unahusu mpaka bandari zenu zote za ziwa Victoria. Unapompa mgeni bandari zote za ziwa maana yake ziwa linakuwa sio letu tena. Kwa mkataba ule, Rais hatoweza kufanya chochote kwenye bandari zetu mpaka kwanza apata kibali cha Dubai,” alisema.

Mikutano ya Chadema ya Operesheni +255 yenye ujumbe wa Katiba Mpya: Okoa Bandari Zetu, inaendelea katika mikoa ya kanda ya ziwa, huku Mbowe akinadi zaidi misingi mikuu ya serikali itakayoongozwa na Chadema ambayo ni Haki, Uhuru, Demokrasia na Maendeleo ya Watu.

Mbali na mikutano inayoongozwa na Mbowe, mikutano mingine ya Operesheni hiyo inaongozwa na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu

Like