SIKU moja baada ya Serikali kusaini mikataba mitatu ya kutekeleza uwekezaji wa bandari na kampuni ya DP World ya Dubai, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, ametaka mikataba yote mipya iliyosainiwa jana, iwekwe wazi ili umma wote wa Watanzania upate kuiona, kuichambua na kujiridhisha.
Jana, katika hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo, serikali ilieleza kuwa mikataba hiyo imezingatia maoni na ushauri wa wananchi na wadau mbalimbali, vikiwemo vyama vya siasa.
Hata hivyo, akihutubia maelfu ya wananchi wa mji wa Namanyere, Jimbo la Nkasi Kaskazini, jioni hii, Mbowe amesema CCM na serikali yake hawaaminiki kama kweli wamefanya marekebisho ya msingi kuhusu mambo mbalimbali yaliyolalamikiwa katika mkataba wa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Emirati ya Dubai (IGA).
Hivyo, Kiongozi huyo wa Upinzani nchini, amemtaka Rais Samia kuiweka wazi mikataba hiyo hadharani ili umma wote uweze kujiridhisha kama kweli mkataba uliolalamikiwa ndiyo uliorekebishwa na kama kweli maoni ya wananchi na wadau mbalimbali yamezingatiwa.
“Jana tumeona wamesaini mikataba na watu wa Dubai ya utekelezaji wa uwekezaji katika bandari zetu (HGAs). Tulipinga mkataba waliosaini awali ambao haukuwa na kikomo, sasa wanasema mkataba waliosaini una ukomo wa miaka 30.Mkataba ule uliwapa Waarabu bandari zetu zote, lakini wanasema mkataba waliosaini jana unahusu bandari ya Dar-es-Salaam pekee. Mkataba ule uliwapa misamaha (nafuu) za kodi, huu wanasema wawekezaji watalipa kodi zote kwa mujibu wa sheria za nchi. Mkataba huu wanasema tutakuwa na hisa ya asilimia 60. Sasa kupitia mkutano huu, Mbowe nasema CCM hawaaminiki”.
Alisema, msimamo wa Chadema kwasasa ni kutaka mikataba hiyo iwekwe wazi na kwamba Chadema itatoa msimamo wa kina pindi mikataba hiyo itakapowekwa wazi.
“Mkataba ule (IGA) ulikuwa wa siri, lakini kwa bahati nzuri wasamaria wema waliuvujisha. Sasa ninamtaka Rais Samia aiweke wazi mikataba waliyosaini ili tuone kama kweli mkataba ule umerekebishwa au ni kiini macho, kama ambavyo wamekuwa wanafanya siku zote”, alisema Mbowe na kushangiliwa na wananchi.
Pia Mbowe aliwapigisha kura ya wazi wananchi ili kupima mtazamo wao kuhusu msimamo wa Chadema kuhusiana na mikataba hiyo.
Katika kura hiyo ya wazi, wananchi wote waliohudhuria mkutano huo, walinyoosha vidole vyao juu, wakiashiria kuunga mkono msimamo wa Chadema wa kutaka mikataba hiyo iwekwe wazi.
Katika hatua nyingine, Mbowe alimpongeza Mbunge wa jimbo hilo, Aida Kenan (CHADEMA), kwa kuendelea kuwawakilisha vizuri wananchi wa jimbo hilo, licha ya kuwa peke yake bungeni kutokea chama hicho.
“Nampongeza sana Mbunge wenu Aida kwa kuendelea kuwa na msimamo bungeni bila kujali kuwa yupo peke yake. Ninamtaka aendelee kuwa msimamo bila kumuhofia yoyote. Kama ni Rais hata sisi tunazungumza na Rais huyo huyo”, alisema Mbowe.
Awali akitoa salaam zake, Aida, alisema licha ya kuwa mbunge wa jimbo hilo bado yupo yatima, kwani alipata madiwani wanne tu wa Chadema kati ya kata 17 za jimbo hilo.
Aliongeza kuwa hivi sasa amebakiwa na madiwani watatu tu baada ya diwani mmoja wa Chadema kufariki, hali inayofanya azidi kuhujumiwa na kukwamishwa katika maendeleo na madiwani wengi wa CCM wanaongoza halmashauri ya wilaya ya Nkasi.
Hata hivyo, Aida alimuhakikishia Mwenyekiti wake Mbowe, kwamba Chadema Jimbo la Nkasi Kaskazini, imejipanga vizuri kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, utakaofanyika mwakani, ili wapate nguvu zaidi ya kuwaletea wananchi maendeleo.