Mbowe apokea mashitaka ya umma dhidi ya Bashe, NFRA

Kutoka Ileje, Momba na Kwela

MAMIA ya wananchi wa majimbo ya Ileje na Momba, mkoa wa Songwe na Kwela, mkoa wa Rukwa, wameilalamikia Wizara ya Kilimo, inayoongozwa na Waziri, Hussein Bashe, pamoja na Wakala wa Ghala la Taifa la Chakula (NFRA), ilio chini ya wizara hiyo, kwa kuwakopa mahindi yao na kukaa kwa muda mrefu bila kuwalipa mpaka sasa.

Pia wananchi hao wamelalamikia kukatazwa kuuza mazao yao kwenye nchi jirani ya Malawi, ambako wamedai wangeweza kuuza kwa bei nzuri na ya kulipwa papo hapo badala ya kukopwa mahindi yao na NFRA.

Wananchi wao wametoa malalamiko hayo mbele ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, katika mfululizo wa mikutano ya hadhara ya Oparesheni +255, ya kuimarisha Chama hicho, inayoendelea katika Kanda ya Nyasa, inayoundwa na mikoa ya nyanda za juu kusini.

Bashe amewahi kunukuliwa mara kadhaa, ndani na nje ya bunge, akisema serikali haijakataza wananchi kuuza mazao yao nje ya nchi, lakini Oparesheni +255 ya Chadema, iliyofanyika kwenye mikoa Kigoma, Tabora, Katavi, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, na sasa ikiwa imeingia mikoa ya nyanda za juu kusini, imeendelea kukutana na maelfu ya wakulima wanaolalamikia udhibiti wa soko pamoja na kukithiri kwa kamata kamata ya wakulima wanaojaribu kuuza mazao yao nje ya nchi.

Akiwa kata ya Isongole na Chitete, jimbo la Ileje, Mbowe aliwapa wananchi fursa ya kueleza kero na matatizo yao, ambapo suala la kutolipwa fedha za mahindi yao na NFRA, liliibuka kama lalamiko kuu la wananchi wengi, huku wananchi wengine wakilalamikia kukamatwa kila wanapojaribu kuuza mazao yao Malawi.

Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa wakati debe la mahindi lenye ujazo wa kilo 18 mpaka 20 linauzwa kwa shilingi 11,000 Ileje, mahindi hayo hayo yanaweza kuuzwa kwa zaidi ya shilingi 15,000 kwenye nchi jirani ya Malawi, inayopakana na wilaya hiyo.

Katika mkutano uliofanyika Laela, jimbo la Kwela, mwanasiasa machachari, Daniel Naftari, na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, kupitia Chadema, akizungumzia tatizo hilo, alisema wakulima wa Kwela waliuza mahindi yao kwa NFRA kuanzia mwezi wa nane mwishoni na mwezi wa tisa, lakini mpaka sasa bado hawajalipwa.

Akizungumzia changamoto hizo, Mbowe alisema sera ya Chadema, si kuwadhibiti wananchi wasiuze mazao yao nje ya nchi wala kutegemea NFRA pekee inunue mazao yote ya wakulima, bali ni kuleta soko huria litakalowaruhusu wakulima kuuza mazao yao popote pale wanapotaka na kwa bei nzuri.

Alisema sera ya CCM ya kudhibiti wakulima wasiuze mazao yao nje ya nchi ni ya makusudi kwasababu inawapa nafasi vigogo wa CCM na serikali yake ya kujichomeka katikati na kuwalangua wakulima mazao yao kupitia vyama vya msingi (AMCOs) na kuuza kwa faida.

Mbowe alimuagiza Katibu wa Chadema, Kanda ya Nyasa, Gwamaka Mbughi, kuwasilisha kero hiyo pamoja na kero nyingine za wananchi hao katika mamlaka zote za kiserikali ili ziweze kupatiwa ufumbuzi, huku akiwataka wananchi hao kujiunga na Chadema na kuing’oa CCM madarakani, kwani huo ndiyo ufumbuzi wa msingi wa matatizo mengi yanayowakabili.

Like