MBOWE: HATUTAKI KUJENGA TANZANIA YA VISASI

Hotuba ya Freeman Mbowe kwa taifa katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

KAMA mjuavyo, nimerejea uraiani toka Gerezani siku nne tu zilizopita. Nawashukuru sana kina Mama wa Chadema kunialika kuja kuwasalimia wakati mkiadhimisha siku yenu maalum.

Ukiondoa kundi dogo sana, tena tuliloliamini lakini likakiasi Chama kwa vipande vya fedha, Wanawake mmekuwa nguzo na Baraka nyingi sana kwa Chama hiki

Usaliti wa wachache haupaswi kuiondoa imani ya Chama chetu kwa Wamawake, bali yapasa kuwa chachu ya kuwafikia, kuwafunda na kutengeneza wanawake wengi zaidi wenye nidhamu, uadilifu na timamu ya uongozi

Mama na Dada zetu, mmetuheshimisha wakati wote kwa uwepo wenu mahali hapa. Ujio wenu toka Majimbo na Mikoa yote ya Tanzania ni kielelezo tosha cha thamani, ujasiri na utayari wenu katika kuipigania nchi yetu kuwa mahali salama zaidi na pa furaha kuishi

Mmewajaza tamaa Wanaume ndani ya Chama chetu. Wanatamani kuwepo kwa Baraza la Wanaume. Huu ni ushindi mkubwa kwa kina mama. Hakika ninyi ni jeshi kubwa. Imejidhihirisha kuwa wanaume ‘hawapindui mbele ya wanawake.

Chama kitawaheshimisha kadiri mtakavyokiheshimisha na kujiheshimisha. Wanawake mnapaswa kuwa kioo cha uaminifu na uadilifu wakati wote.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kati ya mwaka 1958 – 1959, Charles Malik alisema “The fastest and sustainable way to Change Society is to mobilise the women of the world”. Mwisho wa kunukuu. Kwa tafsiri isiyo rasmi, alisema “ Njia ya haraka na endelevu ya kuibadilisha jamii ni kuhamasisha wanawake wa dunia

Naye Mama Hillary Clinton, akitambua hazina kubwa iliyopo kwa wanawake alisema: “Women are the largest untapped reservoir of talent in the world” … kwamba Wanawake ni hazina na mtaji mkubwa wa vipaji ambao haujatumika duniani

Kama mjuavyo, kuanzia July 21, 2021 nilitiwa nguvuni na vyombo wa dola nikiwa Mwanza. Kwa miezi 7.5 au wiki 32 au siku 227, nilikuwa mikononi mwao katika kituo cha Polisi Oysterbay na Gereza la Ukonga, Dar es Salaam, nikishtakiwa kwa kilichoitwa makosa ya ugaidi.

Katika kipindi chote hicho, nilifikishwa mbele ya mahakama ya Kisutu na baadaye kwenye Mahakama Kuu, Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Rushwa, nikiunganishwa na waliokuwa walinzi wangu, Halfani Bwire Hassan, Adam Kasekwa maarufu kama Adamoo na Mohamed Lingwenya hawa wamekuwa kifungoni kwa takribani siku 577, au wiki 82, au miezi 19, au mwaka 1.7.

Ndugu zangu Watanzania, kwa niaba yangu binafsi, walinzi wangu na familia zetu, tunawiwa kutoa neno la shukrani kwenu wote. Wengi walituombea makanisani na wengi misikitini. Wako waliotuombea majumbani, magerezani, mahakamani na kila mahali palipowezekana dua, sala na ibada zenu zilitujaza faraja isiyo kifani. Tuna imani Mungu wetu alizisikia dua na sala zetu. Mbarikiwe sana

Viongozi mbalimbali wa dini zetu, Viongozi wa Vyama vya siasa, Watanzania kwa mamia walitutembelea magereza kututia moyo na kutujaza faraja. Mmetupa na kutufundisha upendo wa ajabu! Asanteni sana

Shukrani za kipekee ziendee Jopo letu la Mawakili. Walidhihirisha pasipo shaka umahiri mkubwa katika fani yao. Walipigana bila kuchoka kwa kipindi chote cha kesi yetu. Mungu wetu aendelee kubariki sana kazi za mikono na akili zao wakaendelee kuwa baraka kwa wengine wenye uhitaji.

Kazi kubwa ya kuhabarisha na kuelimisha dunia ilifanywa na vyombo mbali mbali vya habari vya Tanzania na Kimataifa. Keyboard worriors mbalimbali kupitia makundi na mitandao mbalimbali ya kijamii walifanya kazi ya miujiza na kuufanya mwenendo wa kesi yetu kuwa wazi kwa dunia nzima hatua kwa hatua. Asanteni sana.

Uwazi kubwa ulisaidia wengi mijini, vijijini na katika jamii ya kimataifa kuamua katika mahakama ya umma kama “Mbowe ni Gaidi au siyo gaidi

Nashukuru Mabalozi na Taasisi nyingi za Kimataifa ndani na nje ya nchi kwa kufuatilia kwa makini kesi yetu ndani ya mahakama na nje ya mahakama.

Juhudi zao za kidiplomasia nina hakika nazo zilisaidia kujenga ushawishi wa kutetea uhuru wetu. Ufuatiliaji wao vilevile, uliipa uzito mkubwa kesi yetu na hivyo kusaidia wengi kuifuatilia.

Nashukuru sana wote waliohudhuria mahakamani kwa nyakati tofauti tofauti. Walifanya kazi kubwa ya kututia moyo na kutujaza matumaini.

Ndugu zangu Watanzania, kwa uzito mkubwa naomba kutoa shukrani za kipekee kwa familia ya Chadema.

Watanzania wenzangu, nguvu yenu wote kwa umoja wenu vilitubariki sana. Mlichangia fedha, vyakula, ushauri wa kisheria, mifugo nguo, nafaka, matunda na kila aina ya msaada uliowezekana. Mungu akazidishe pale mlipotoa pakaongezeke mara nyingi

Nashukuru Mamlaka zote zilizofanya uamuzi wa kutotaka kuendelea na shauri letu Mahakamani. Nina hakika, ziko sababu nyingi zilizopelekea kufikia uamuzi huu. Niendelee kuwashukuru wote walioshiriki kwa njia mbalimbali kuwezesha mamlaka husika kufikia uamuzi huo ulioturejeshea siyo tu uhuru wetu, bali pia haki ya tabasamu kwa familia zetu.

Kwa unyenyekevu mkubwa, naomba nisiingie kwa undani maudhui na mengi yaliyogubika kesi yetu. Natambua kumekuwepo na malumbano mengi maeneo mbalimbali kuhusiana na aina ya mashtaka na mwenendo wa kesi.

“Aidha, pamekuwepo na mchanganyiko wa hofu, mshtuko, mshangao, furaha na taharuki nyingi kwa namna nilivyoweza kukutana na Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan siku hiyo hiyo nilipofutiwa kesi. Taharuki hii nitaijibu katika hotuba yangu.

“Miezi mingi tuliyokaa magereza tuliitumia kusali, kusoma, kuandika na zaidi kutafakari. Changamoto zote tulizopitia, bila kujali ubaya wake, tulizipokea tukiamini kila jambo linalotokea chini ya mbingu ni mpango wa Mungu.

Kipekee, naomba kuwahakikishia Watanzania, changamoto hizi zimeniimarisha sana. Zimeendelea kunipa unyenyekevu mbele za Mungu na kwenu wote. Maandiko yanatufundisha kushukuru kwa kila jambo na kwamba Mungu wetu wa miujiza hutenda kwa wakati wake.

Watanzania wenzangu, wengi mmesikia mara nyingi hata kabla ya kesi hii, nikihubiri kuwa CHADEMA hususan chini ya uongozi wangu kamwe hakitakuwa chama cha visasi.

Niliasisi kauli mbiu ya “NO HATE, NO FEAR, NO FEAR NO HATE” kuelekea mkutano wetu mkuu wa Uchaguzi ndani ya Chama December 2019.. Kwa tafsiri rahisi tulimaanisha hatuna chuki na wala hatuna wogakatika kusimamia tunayoyaamini.

Kauli hii ililenga kuwajengea Ujasiri bila woga wala chuki Wanachadema kwa mamilioni ambao walidhurika kwa njia moja au nyingine na ukatili usio kifani tuliofanyiwa na baadhi ya Viongozi wa Serikali ya awamu ya Tano, vyombo vyake vya Ulinzi na usalama na hata taasisi zake

Pamoja na kuwa watu wetu wameuwawa, wameporwa uchaguzi, wamebambikiwa kesi mbalimbali, wamepigwa risasi, wameporwa mali na mengine mengi, bado tulihubiri kukataa sera za chuki

Watanzania wenzangu, nia yetu njema wakati wote haikuwagusa Watawala, bali walizidisha mikakati ya kujaribu kutufuta katika ramani ya siasa za Tanzania. Uchaguzi Mkuu wa 2020 na yaliyoendelea miezi kadhaa mbele yake ni kielelezo tosha cha nia hiyo.

Vyombo vya dola, vilivyoshiriki kuvuruga uchaguzi ule na kuratibu ukatili mkubwa dhidi ya ubinadamu (crimes against humanity) kwa miaka zaidi ya mitano bado vina ujasiri wa kutuita Magaidi

Pale Wanachadema walipoonekana kupaza sauti kwa kauli kali za kijasiri kuomba angalau haki ya kulia baada ya kuonewa, walipuuzwa, kubezwa na kutwezwa!.

Hakuna aliyekuwa tayari kutusikiliza. Nguvu kubwa ilitumika kujenga nadharia ya amani kwenye Taifa lenye watu wenye kuvuja damu mioyoni mwao. Watawala walihubiri Amani ilhali wakijua wanachowafanyia Watanzania wenzao!.

Chadema ni Chama cha siasa kilichojengwa na kitakachoendelea kujengwa katika ushawishi wa kisera, kimantiki na katika itikadi yenye kutambua demokrasia kama chimbuko la maendeleo.

Hakijawahi kuwa, walahakikusudii kuwa, chama kibaraka wa chama kingine wala dola.Kwa wakati wowote, hakijawahi kuwa chama chenye kusudio la kufikia matumizi ya nguvu katika kuitafuta dola.

Kinajengwa kwa ushawishi wenye kusimama katika madhumuni yake ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ya kupigania Uhuru, Demokrasia, Haki na Maendeleo ya watu wote.

Wajibu huu umetendwa kwa ubunifu mkubwa, kujituma kwa dhati na bidii kubwa ya kazi. Tumekataa katakata wakati wote kukatishwa tamaa.

Tulikataa na hakika tutaendelea kukataa kuwa watumwa wa fedha au madaraka. Wale wenye tamaa hizo miongoni mwetu, hatujawahi kusita, bila kisasi, kuwaacha waende zao.

Tumekataa kuwa chama cha kuongozwa na siasa na mizunguko ya kiuchaguzi (election cycles). Tumekataa kuangalia vidole vyetu vya miguu, na tumeamua kuangalia mbele kwa ujasiri kuiona kesho yenye matumaini, siyo kwetu pekee bali kwa watoto wetu na watoto wa wataoto wetu. Yes, next generation!

Uvumilivu na utayari huu umetujengea kuaminika kwa wananchi. Nguvu hasidi, fitna na propaganda dhidi yetu zimetufikirisha badala ya kutunyongonyeza

Leo, kama Mwenyekiti wa Chama hiki, najivunia kukua kwa Chadema. Tuna mamilioni ya wanachama. Ndani na nje ya nchi. Kila walipo tupo japo hatuna ruzuku ya serikali wala bunduki za utawala.

Nguvu yetu ya umma, ambayo ni ushawishi wa kijamii umekuwa nguzo yetu wakati wote. Tunaheshimishwa kwa nguvu hiyo. Wenzetu kwa muda mrefu wanaheshimishwa na vyombo vya dola na taasisi za kusimamia haki zisizosimamia haki zenyewe.

Watanzania wenzangu, mtakumbuka tarehe 21 April 2021, nilizungumza nanyi katika hotuba ambayo wengi wamependa kuiita “never and never again” ambayo pia inapatikana kwenye mtandao wa youtube.

Katika hotuba ile nilichambua kwa kina hali ya nchi yetu ilivyokuwa wakati wa utawala wa awamu ya tano. Niliamini ukweli ni nyenzo muhimu itakayotujenga katika kuitafuta kesho iliyo bora zaidi

Uchambuzi ule uligusa kwa hisia hasi baadhi ya waliokuwa madarakani wakati wa utawala wa awamu ya tano. Wengine bado wapo hadi leo. Chukizo zito lilijengwa dhidi yangu. Miezi 3 baadaye nilitiwa nguvuni.

Naamini nilichokipitia safari hii, kimechagizwa kwa kiasi kikubwa na hotuba ile. Yote haya namwachia Mungu na kuwaombea msamaha. Hakika nimesamehe na naomba Watanzania wenzangu mnikubalie tuungane katika hili.

Ndugu zangu mtakumbuka, katika hotuba ile nililitangazia Taifa kuwa kwa niaba yangu binafsi na Chama chetu, nimemwandikia Mhe Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa mambo mawili makubwa. Moja kumpongeza kwa wajibu mkubwa aliokabidhiwa na pili kumwomba atenge muda tuweze kukutana naye.

Sikuweza kukutana naye kwa muda ule kabla ya kuingizwa gerezani pamoja na kuwa alijibu barua yetu kuridhia. Ikumbukwe niliomba nafasi ya kukutana na Mhe Rais wa awamu ya tano mara kadhaa ikiwepo mara tatu kwa njia ya maandishi bila mafanikio.

Kesi yetu ilipofutwa, nilipokea ujumbe wa Mheshimiwa Rais kutaka tuonane haraka iwezekanavyo. Kwa sababu mbalimbali, niliridhia. Kwanza binafsi na chama changu kimetafuta fursa hiyo tangu awamu iliyopita bila mafanikio

Tuna mengi tumeyatunza mioyoni mwetu na tuliamini na bado tunaamini, Rais kama Mkuu wa nchi ndiye mwenye ufunguo wa vikwazo vingi vinavyosababisha simanzi ya muda mrefu kwa taifa letu

Kamwe sikuruhusu uchungu na maumivu binafsi vinitie upofu wa kutokuiona heshima niliyopewa. Wakati wote nikiwa gerezani nilimwomba sana Mungu atoe kibali cha kuliponya Taifa letu. Nilikiona kibali hiki kupitia kwa mwaliko wa mapema wa Mhe.

Sasa basi, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kunipa nafasi ya mapema baada ya kutoka gerezani. Aidha nimshukuru kwa pole alizinipa.Namshukuru pia kwa namna mazungumzo yetu yalivyokwenda. Asante kwa kufungua milango ya mashauriano.

Mama amekuwa Rais wa kwanza wa nchi yetu baada ya ujio wa pili wa vyama vingi mwaka 1992, kusimama hadharani na kutamka nia njema ya kukiri kutanguliza haki katika kuijenga Tanzania mpya yenye amani endelevu. Nawaomba Watanzania wenzangu wote waridhie msingi huu

“Haki ni dhana pana sana. Tulikubaliana kuwa haki hizi haziwezi kupatikana kwa tukio la kikao kimoja. Tulikubaliana kikao kile kiwe cha kuweka msingi imara wa kuanza kujenga kuaminiana na isiwe kwa maneno tu bali kwa matendo

Ndugu zangu, taharuki iliyozuka kwa wengine ni ushuhuda tosha wa namna tulivyo na viwango vya juu vya kutokuaminiana katika Taifa letu.

Njia sahihi na ya kidemokrasia ya kutafuta haki katika Taifa hujengwa kwanza kwa kuwepo nia ya kweli ya kisiasa (political will). Kisha ni mchakato wa majadiliano ya kutengeneza mifumo ya kutekeleza azma hiyo. Huku ndiko mazungumzo yetu yalipojikita

Wengi wanahisi pengine CHADEMA itaacha harakati zake za kuitaka katika mpya au Tume huru ya uchaguzi. Hofu hii si kweli. Naamini kupitia mazingumzo hatua kwa hatua patapatikana njia bora ya kulitunza jambo hili.

Kukosekana kwa maelewano ya pamoja ndiko kulikwamisha mchakato wa kwanza wa katiba. Lazima tutibu majeraha haya. Lazima tuheshimiane. Lazima tupunguze tofauti zetu

Maelewano hayawezi kupatikana bila makundi yanayohasimiana kukubaliana kwa kukaa pamoja na kutafuta njia bora kwenda mbele

Nina imani muda utasema. Naheshimu vikao vya chama chetu vitakaa mapema iwezekanavyo na kutafakari na kufanyia kazi makubaliano yangu na Rais.

Natamani chama chetu kifuate nyayo za mwanaharakati Martin Luther King Jnr. Nimesoma harakati zake nyingi namna alivyofanikiwa kuongoza mapambano dhidi ya ubaguzi wa watu weusi katika Taifa la Marekani hadi mauti ilipomfika mwaka 1964 kwa kuuwawa na mahafidhina.

Alisema pia, “Returning hate for hate multiplies hate, adding deeper darkness to a night already devoid of stars. Darkness can not drive out darkness, only light can do that. Hate can not drive out hate, only love can do that Alihubiri msamaha, upendo na uvumilivu katika kuyafukia malengo ya haki sawa kwa wote.

Waheshimiwa Wanachadema na Wana Bawacha, asanteni sana kwa kukilinda chame chetu. Muda wote nikiwa Gerezani nimejulishwa kazi kubwa mliyoendelea kuifanya ya Chadema digital pamoja na Join the Chain Movement

“Kazi hizi tuziendeleze kwa wivu mkubwa. Lazima tujenge uwezo wetu wa ndani. Kujitegemea ndiyo njia ya heshima itakayowezesha kukipeleka chama hiki kwenye malengo yake

Wanawake ninyi ni jeshi kubwa. Nawashawishi mkukue challenge ya kuunganisha kwenye chain wanawake milioni moja watakaochangia shilingi 1,000 tu katika kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo. Zoezi hili litakusanya shs bilioni moja zitakazokwenda moja kwa moja kwenye uimarishaji ..wa demokrasia katika nchi yetu!

Watanzania wenzangu, leo sikusudii kutoa hotuba ndefu. Bado nina kamba za magereza na tutazungumza mengi baada ya vikao muhimu vinavyotegemewa kukaa siku za hivi karibuni

Kwa Mama zetu mliosafiri umbali mrefu na mfupi, nawatakia kheri ya kurejea makwenu salama. Tupelekeeni salama zetu kwa familia nzima ya Chadema na watanzania wenzetu wote.

Like
1