Mbowe ashitakiwa rasmi kwa ugaidi

HATIMAYE Serikali ya Tanzania, ikiongozwa na chama tawala, CCM, imetimiza malengo yake ya kutesa, kuonea na kudhalilisha wapinzani wake kwa kumfungulia mashtaka ya ugaidi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Mbowe, kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jana alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka mawili yasiyokuwa na dhamana; ugaidi na kufadhili fedha kwa ajili ya kutekeleza vitendo vya kigaidi.

Kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani alifikishwa mahalamani hapo kwa siri, huku mawakili wake wakifichwa. Haifahamiki sababu za usiri huo kwa Mbowe kupelekwa mahakamani.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaa, Jumanne Muliro alipohojiwa na SAUTI KUBWA alisema kupelekwa mahakamani Kisutu kwa Mbowe hakukuwa siri, bali Polisi iliona muda huo ni muafaka na kwamba sheria hailazimishi jeshi hilo kutangazia kila mtu kwamba “wakati fulani linampeleka fulani mahakamani.”

SAUTI KUBWA ilielezwa mpango wa siri wa kumkamata Mbowe, kupata taarifa na kuwa chombo cha kwanza cha habari kuripoti alikofichwa Mbowe; Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam, baada ya Jeshi la Polisi kuficha alipo tangu kukamatwa kwake – kwa nguvu – Jumatano iliyopita akiwa hotelini jijini Mwanza.

Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ester Martine, akisaidiwa na Tulimanjwa Majigo, alisema kuwa mshtakiwa Mbowe alifikishwa mahakamani na kuunganishwa na washtakiwa wengine watatu waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya ugaidi wanayodaiwa kutenda mnamo mwaka 2020.

Washitakiwa wengine wanaotajwa kushirikiana na Mbowe, ambao wako mahakamani kwa mashitaka hayo ni Halofan Bwire Hassan, Adam Hassan Kasekwa – almaarufu Adamo na Mohammed Abdalla Ligwenya. Hawa wote walikuwa walinzi binafsi wa Mbowe.

Kesi hiyo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi, Thomas Simba ambapo katika kosa la kwanza Mbowe anadaiwa kupanga njama za kutenda makosa ya kigaidi kati ya Mei na Agosti 2020 akiwa katika Hoteli ya Aishi Mkoani Kilimanjaro ikiwa ni pamoja na kuwasha vituo vya mafuta na kwenye mikusanyiko ya hadhara kwa kutumia vilipuzi.

Katika kosa la pili Mbowe anadaiwa kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi kinyume cha sheria ya makosa ya ugaidi na kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 5, 2021.

Wakili wa serikali ameiambia mahakama kwamba upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, hivyo tayari kuwasilishwa kwa nyaraka zote katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

Kufunguliwa kwa mashitaka hayo kumeelezwa na idadi kubwa ya watu waliohusika katika utafiti mdogo kupitia ukurasa wa Twitter wa mtetezi wa haki za binadamu, Maria Sarungi, kwamba ni uonevu.

Utafiti huo umeonyesha kwamba kati ya watu 6,138 walioshiriki, asilimia 52 wamesema “wana hasira kali” kwa hatua hiyo ya serikali kumkamata na kumfungulia mashtaka Mbowe.

Asilimia 37 wameeleza “kusikitishwa” na hatua hiyo, asilimia saba wamesema “wamekata tamaa,” huku asilimia tano wakieleza “kufurahishwa” na hatua hiyo ya serikali.

Like