HUYU (pichani) ndiye Isack Bwire, ofisa usalama ambaye alipigwa risasi katika jaribio la kumvamia na kumteka Peter Zacharia, mfanyabiashara maarufu wa Tarime mkoani Mara. Amepelekwa Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu.
SAUTI KUBWA imeambatanisha picha yake hapa, ikiwa ni mara ya kwanza sura yake kuwekwa hadharani na chombo cha habari tangu alipopigwa risasi.
Vyanzo vyetu vinasema haikuwa mara ya kwanza kwa Bwire na wenzake kumwendea Peter Zacharia, kwani walishamfanya kama mgodi wao wa fedha. Chanzo kimoja kinasema: “Alikuwa amezoea kuchota pesa kwa Peter.” Lakini zamu hii walikwenda kwa jukumu maalumu ambalo watu wanadai kuwa kama Peter Zacharia asingejihami kwa risasi huenda naye angepotezwa kama wengine.
Juni 30 mwaka huu Peter Zacharia alipiga risasi maofisa wawili wa Idara ya Usalama wa Taifa waliomvamia akiwa anatoka ofisini kwake katika kituo cha mafuta anachomiliki mjini Tarime. Baadaye Adam Kighoma Malima, mkuu wa mkoa wa Mara, alidai kwamba maofisa hao walijeruhiwa “wakiwa katika majukumu yao.” Hakufafanua majukumu yao yalikuwa na uhusiano gani na kumvamia Peter Zacharia, mmiliki wa mabasi.
Mara baada ya kuumizwa, walikimbizwa katika hospitali ya mjini Tarime kupatiwa matibabu; lakini sasa mmoja wao amepelekwa Afrika Kusini, wakati Peter Zacharia akiendelea kushikiliwa na kushitakiwa kwa makosa mbalimbali yakiwemo kujeruhi maofisa hao, uhujumu uchumi na kumiliki bunduki na risasi bila kibali.
Kwa mujibu wa Malima, maofisa hao walikuwa watano, walifika kituoni hapo kujaza mafuta kwenye gari lao, na wenzao wawili waliposhuka kukagua gari hilo, Peter Zacharia aliwashambulia ghafla.
Aliwambia waandishi wa habari: “Maofisa wawili walishuka kwenye gari, Zacharia alitoka kwake na kukasikika milio ya risasi. Baadaye ilionekana wale maofisa wawili walikuwa wamejeruhiwa kwa risasi. Hivyo waliobaki kwenye gari waliamua kumdhibiti Zacharia na kumtia nguvuni.”
Hata hivyo, badhi ya watu walioshuhudia tukio hilo, wakiwemo wafanyakazi wa Peter Zacharia, walisema maofisa hao hawakuwa na shida ya mafuta, kwani hata wakati wa tukio kituo kilikuwa kimeshafungwa. Wanasema kilichotokea ni kwamba watu wawili hao walitoka kwenye gari, wakamkamata Peter Zacharia na kumburuza ili wamwingize kwenye gari lao kwa nguvu, akawa anapiga kelele kuomba msaada. Hatimaye alifanikiwa kufyatua risasi zikawapata wawili hao.
Baadaye polisi walikuwa wanafanya jitihada za kuficha utambulisho wao, lakini ilishindikana. Peter Zacharia anashikiliwa na kushitakiwa kwa kuwajeruhi na kumiliki bastola na risasi bila kibali.
Kauli ya kwanza ya mkuu wa mkoa, ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani,, kutambulisha watu hawa kama maofisa wa usalama, ilitosha kwa wananchi kuhusisha tukio hilo na mengine ya raia kutekwa na kupotezwa na “watu wasiojulikana.”
Kwa hamaki na aibu ya jeshi la polisi kuhusishwa na matendo haya mabaya, Kangi Lugola, waziri wa mambo ya ndani, siku chache zilizopita alitoa kauli kuonya wananchi watakaosikika wanahusisha polisi na “watu wasiojulikana.”
Hata hivyo, kauli ya Lugola inaibua maswali badala ya majibu kwani jamii imeshuhudia matukio mengi ambayo polisi na maofisa wa usalama wa taifa wamehusika katika kuteka na kuumiza watu; na hata walipolalamikiwa hakuna hatua iliyochukuliwa, jambo linaloonyesha kuwa huu ni mradi maalumu wa baadhi ya watu wakubwa serikalini kutumia vyombo vya dola kunyamazisha sauti wasizozitaka.
Sababu halisi ya Peter Zacharia, mfanyabiashara na mfadhili wa CCM, kuvamiwa na kundi hili la maofisa, haijawekwa wazi.