Mauaji kwenye hifadhi: Mbowe awa mbogo

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ameitaka serikali ikomeshe mara moja mauaji ya raia yanayofanywa na vyombo vya usalama kwenye maeneo yaliyo jirani na hifadhi.

Mbowe amelaani vikali kile alichokiita mwenendo wa serikali ya CCM wa kuthamini zaidi hifadhi na wanyama pori kuliko uhai wa binadamu, kiasi cha kufumbia macho mauwaji na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na Jeshi la Polisi na askari maalum wa hifadhi nchini.

Akihutubia mamia ya wananchi wa Nkome, jimbo la Geita Vijijini, leo asubuhi, Mbowe alilaani hatua ya askari wa hifadhi ya kisiwa cha Rubondo kukamata na kuua wavuvi wanaovua kwenye maeneo ya Ziwa Victoria yaliyo jirani na hifadhi hiyo.

“CCM na serikali yake wameamua kuthamini hifadhi na wanyama pori kuliko binadamu. Wameamua kuviachia vyombo vya usalama, kama polisi na askari wa hifadhi, wafanye watakavyo na matokeo yake wanajichukulia sheria mkononi na kuwauwa wananchi kwa madai kuwa mnaingilia maeneo ya hifadhi. Ninalaani vikali mauaji, kinyume cha sheria,” alisema Mbowe

Mbali na Rubondo, tuhuma za wananchi kuuwawa na askari wa hifadhi zimekithiri maeneo mengi ikiwemo Serengeti, Ngorongoro na Karagwe.

Akifafanua ukiukwaji wa sheria unaofanyika katika mauwaji hayo, Mbowe alisema:

“Kwa mujibu wa sheria zetu, kuna makosa mawili tu yanayoruhusu adhabu ya kifo ambayo ni kosa la mauaji pamoja na uhaini. Na adhabu hiyo ya kifo ni mpaka itolewe hukumu na mahakama baada ya kesi kufanyika na mtuhumiwa kupewa haki ya kusikilizwa.”

“Hakuna sheria yoyote ya nchi hiii inayokabidhi mamlaka kwa askari wa hifadhi au chombo cha usalama, kuua watu. Wajibu wa askari ni kufanya upelelezi, kukamata watuhumiwa na kuwafikisha mahakamani ili wapewe haki ya kusikilizwa, wajibu mashtaka yao. Si wajibu wa jeshi la polisi wala askari wa hifadhi kujichukulia sheria mkononi na kuua watu,” alisisitiza.

Aliwaomba wananchi wa Nkome kuachana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwani licha ya kuwasababishia umaskini bado kinajali zaidi pesa za utalii wa wanyama pori kuliko uhai wa binadamu.

Familia mbalimbali za wavuvi wa samaki katika Ziwa Victoria,Jimbo la Geita Vijijini, zimeelezwa kubakiwa na wajane tu kutokana waume zao kuuawa na askari wa hifadhi ya Rubondo, huku wengine wakiwa wamenyimwa kabisa hata fursa ya kuzika.

Katika hatua nyingine, mamia ya wananchi wa kata ya Nkome walipiga kura ya wazi iliyosimamiwa na Mwenyekiti huyo wa Chadema, ambapo kwa pamoja wamepinga mkataba wa uwekezaji baina ya serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu uendelezaji bandari na maeneo mengine mahususi ya kiuchumi.

Like