Bandari: CCM yapata Kura Moja Geita Vijijini

  • HATIMAYE Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepata kura moja katika Jimbo la Geita Vijijini, inayounga mkono msimamo wa chama hicho unaokubaliana na mkataba wa uwekezaji wa bandari na maeneo mahsusi ya kiuchumi ulioingiwa baina ya serikali ya Tanzania na Dubai, dhidi ya msimamo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) unaopinga mkataba huo.

Kura hiyo ya CCM imepatikana hivi punde katika Kata ya Nzera, Jimbo la Geita Vijijini katika zoezi la kupiga kura ya wazi ya wananchi inayopima misimamo ya wananchi kuhusiana na mkataba huo.

Hata hivyo, ukiondoa kura hiyo moja iliyokwenda CCM, mamia ya wananchi waliofurika kwenye mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, katika kata ya Nzera mchana huu waliendeleza wimbi la kupiga kura nyingi zinazounga mkono wa msimamo wa Chadema, unaoupinga mkataba huo.

Aidha, katika mikutano mingine iliyofanyika leo asubuhi kwenye kata za Nkome, Nyawilimilwa, Kakubilo, za Jimbo hilo hilo la Geita Vijijini, maelfu ya wananchi waliohudhuria mikutano hiyo walipiga kura inayounga mkono msimamo wa Chadema unaopinga mkataba huo.

Pamoja na uchambuzi wote uliofanywa kuhusu vifungu vya mkataba huo swali la kwanini mkataba huo umehusisha tu bandari za upande wa Tanganyika na kuziacha bandari za upande wa Zanzibar, ndilo lililoonekana kugusa na kuteka zaidi hisia za wananchi, huku wengi wao wakisikika wakilalamikia kile walichokiita “kuuzwa kwa Tanganyika”

Mbowe, amekuwa akiendesha kura hiyo ya wazi kupitia mikutano ya hadhara ya Operesheni +255 yenye ujumbe wa Katiba Mpya: Okoa Bandari Zetu, inayoendelea katika mikoa ya ukanda wa ziwa Victoria.

Tayari kura hiyo imeshapigwa katika majimbo ya Bukoba Mjini, Nkenge, Karagwe, Kyerwa, Biharamulo, Muleba Kaskazini, Bukoba Vijijini, Muleba Kusini na Ngara (mkoa wa Kagera); majimbo ya Buchosa na Sengerema (mkoa wa Mwanza) na majimbo ya Chato, ya mkoa wa Geita, ambako Chadema ilijizolea maelfu ya kura kutoka kwa wananchi waliofurika kwenye mikutano hiyo.

Mikutano zaidi ya Chama hicho inayoongozwa na Mbowe anayetumia usafiri wa Helcopter, inaendelea katika jimbo la Nyang’wale na Geita Mjini, kwa ratiba itakayohitimisha jumla ya mikutano saba kwa kutwa nzima ya leo.

Like
1