Makosa ya uteuzi kumgharimu Magufuli

TANGU aingie madarakani, Rais John Magufuli amefanya teuzi nyingi kana kwamba anaunda mfumo wa taifa jipya lililopata uhuru mwaka juzi. Katika kufanya hivyo, mambo matatu yamejionyesha wazi.

Kwanza, ni ameonyesha upeo mdogo sana na ulimbukeni wa hali ya juu kuhusu mifumo ya kiserikali. Pili, ana tabia ya kulipa visasi, kukomoa na kujionyesha alivyo mbabe na kwamba yuko juu ya sheria. Tatu, anaonyesha kuwa marais waliotangulia hawakufanya lolote, ni mafisadi na waliharibu taifa hili.

Uteuzi wa hivi karibuni katika wizara ya mambo ya ndani – kwa jinsi alivyomwondoa Mwigulu Nchemba na kumweka Kangi Lugola – unaangukia katika kundi la kwanza. Magufuli ana hulka ya kutumia vyombo vya dola bila uangalifu wa kutosha. Mathalani, kuna maofisa wa vyeo vya juu katika majeshi, ambao ukitaka kuwagusa inabidi utumie sheria na kanuni za ndani za vyombo hivyo. Yeye hajali kanuni wala sheria.

Alipomteua Jenerali Venance Mabeyo kuwa Mkuu wa Majeshi (CDF), alikuwa na majenerali 5 juu yake waliomtangulia kiwadhifa. Hivyo, rais alipowaacha na kumchukua mdogo wao, Mabeyo, kwa sababu ambazo wachambuzi kadhaa wanasema ni za kikabila tu, hakujua kuwa alitakiwa kuwaondoa wote waliokuwa juu yake, kwa sababu kimsingi hawapaswi kutii na kupigia sauti “mdogo wao.”

Wajuzi wa masuala haya walimwendea rais na kumwambia kuwa uteuzi wa Mabeyo umevunja misingi na unajenga mazingira ya uasi jeshini. Baada ya ubishi na ubabe ulioambatana na ujuaji, rais alikubali kuwaondoa, akawateua kuwa makatibu wakuu wa wizara, wakuu wa mikoa na mwingine akapewa ubalozi. Hilo lilikuwa doa la kwanza.

Alipoletewa maneno ya kimajungu kuhusu DCI wa Polisi Kamishna Diwani Athuman yakimhusisha na rushwa ya majangili, alikurupuka na kumfukuza bila kuomba ushauri. Baadaye alishtuliwa na wajuzi wa mambo hayo, kwamba hawezi kufukuza mtu wa aina hiyo halafu akamwacha hivi hivi mitaani.

Kwa shingo upande, alilazimika kumpa ukatibu tawala wa Mkoa wa Kagera (RAS). Baadaye alikuja kujutia uamuzi wake wa papara alipogundua kuwa alidanganywa na kina Daudi Albert Bashite na kundi lake.

Juzi juzi alimtumbua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa taifa Robert Msalika akamteua kuwa RAS mkoani Tabora. Watangulizi wawili katika nafasi hii walipoondolewa walipewa ubalozi. Pamoja na kwamba uhusiano wa Msalika na Bashite na matokeo ya ushirikia huo yalifahamika na yakikuwa na idhini ya bwana mkubwa, wajuzi wa mambo wanadai kwamba kumwacha mtu kama yule akifanya kazi za ukarani huko Tabora ni kuidhalilisha idara hii nyeti katika uhai wa taifa.

Amefanya makosa yale yale katika kumfukuza kazi Mwigulu na kumteua Kangi Lugola. Kumtoa mtu aliyekuwa na dhamana ya kuongoza vyombo vya usalama kunahitaji umakini na maadili ya hali ya juu. Na wajuzi wa masuala haya wanasema ukishamwondoa, katika mazingira kama haya yaliyopo, unamwita unamlisha kiapo cha kutunza siri, na unamweka mahali pengine kimya kimya.

Lakini rais alifukuza waziri, halafu akasimama hadharani akamsimanga na kumwaga hadharani kile alichodai ni udhaifu wake. Rais hajui kuwa uhusiano wa  wasimamizi wa vyombo vya ulinzi na Amiri Jeshi Mkuu ni sawa na ndoa ya mke na mme.

Wanapofikia kuachana inabidi kila mmoja akae kimya kwa kulinda hadhi na unyeti wa vyombo vya ulinzi. Wachambuzi wanasema kuwa katika hali ya kawaida, kudhalilisha mtu mwenye kiapo kinachomzuia kukujibu ni uonevu uliopitiliza mipaka.

Hali hii inawaweka shakani wakuu wote wa vyombo vya ulinzi. Hawajui ni lini Amiri Jeshi Mkuu atamwaga hadharani baadhi ya siri kuu, tena za hatari, kuhusu mambo mazito yanayohojiwa.

Mathalani, taifa linahitaji kupewa majibu ya uhakika kuhusu kupotea kwa Ben Saanane, shambulio la risasi dhidi ya Tundu Lissu, kupotea kwa Azory Gwanda, mauaji ya kutisha huko Rufiji na Kibiti, na upotevu wa fedha shilingi trilion 1.5, na kadhalika.

Licha ya propaganda za serikali kujaribu kuficha masuala haya, watu wenye akili timamu wanajua kuwa, masuala haya na mengine yametendeka mikononi mwao, na si siri kwa makamanda na mawaziri wa vyombo husika. Ndiyo maana waziri mpya ameingia na “mkwara” wa kuzuia wananchi kuhusisha jeshi lake na “watu wasiojulikana.” Bila kujua, waziri alikuwa anatuhumu jeshi lake. Yeye na wao wanajua mambo haya.

Na bado wananchi wanataka maelezo. Wanajua kuwa rais anajua, mawaziri wanajua, wasimamizi wa vyombo wanajua – maana serikli ina mkono mrefu. Wote wana mikono iliyojaa damu. Kwa hiyo, hata wanapotofautiana, kwa kawaida, wanapaswa watengane kwa kujengeana mazingira yanayowalinda wote.

Kwa kuwa rais hajui na hataki kujifunza, kwa kwa anadhani anajua kuliko wenzake, anafanya atakavyo; na sasa yeye na wapambe wake wanahaha kufunika makosa yake kwa kujaribu kunyamazisha au kuondoa baadhi ya wale aliokosea utaratibu wa “kuwatumbua.”

Kwa miaka mwili sasa, idara ya usalama wa taifa imemeguka vipande viwili, ikiwa na idara mbili zinazofanya kazi za usalama  sambamba; na wakati mwingine kwa mgongano. Idara moja imekuwa inahusika na kuteka, kutesa, na kuua.

Zipo habari za uhakika kuwa baadhi ya wateule wake, kwa nyakati kadhaa bila kujua wala kuhusishwa, wamejikuta wanatumia polisi kukamata watesaji hao na hatimaye wao wakaishia kuamriwa wawaachie mara moja.

Kamanda mmoja mzoefu katika idara ya upelelezi ndani ya jeshi la polisi amedai hali ya mauaji na utesaji inatisha. Anasema: “Hata hawa mnaosikia wamefia mikononi mwa polisi, wanaletwa na kikosi hicho wakiwa taabani,”.

Kosa la uteuzi wa Kangi Lugola ni kubwa, na linaweza kurekebishwa ama kwa kumtumbua au kwa kumbadilisha wizara. Pamoja na kwamba ni yeye askari polisi mstaafu, ni mdogo kwa wengi anaowaongoza; na haiingii vizuri katika taratibu za polisi kuwafanya makamanda wenye vyeo vya juu kuliko alichokuwa nacho alipostaafu, walazimike kumpigia saluti.

Kwao, kwa kawaida, ni rahisi kumpigia saluti waziri raia kuliko waziri askari mwenye cheo cha chini yao. Hata Lugola anafahamu jambo hilo. Ndiyo maana anatumia misuli kuwaamuru ili kuwaonyesha kuwa siasa ina nguvu kuliko taratibu za jeshi.

Kwa muundo wa jeshi la polisi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), hawajibiki kwa waziri. Anawajibika kwa rais moja kwa moja. Rais, licha ya kuwa amiri jeshi mkuu wa majeshi, ndiye mwenyekiti wa baraza kuu la usalama wa nchi.

IGP ni mjumbe ni mjumbe wa baraza hilo; na waziri wa mambo ya ndani si mjumbe. Kwa mantiki ile ile, mkurugenzi mkuu wa usalama wa taifa hawajibiki kwa waziri wa utawala bora.

Hata hii tabia ya Lugola na rais kutumia vyombo vya habari kutoa amri kwa watendaji badala ya kutumia utaratibu wa ndani wa kiserikali, ni ushamba na maonyesho ya ubabe uliojaa ulevi mbaya wa madaraka.

Kama waziri anataka kukutana na IGP ofisi kwake, kuna haja gani, kwa mfano, kwa waziri kumwita IGP kupitia vyombo vya habari, kama alivyofanya Lugola majuzi? Lakini kwa kuwa anasoma tabia ya mkubwa wake, na anajua hayo ndiyo anapenda, anafanya bila kujali sheria wala utu wa huyo anayeitwa.

Matamshi ya Lugola kulazimisha makamanda kutembea na ilani ya chama tawala, sambamba na maagizo ya rais kutesa wafungwa, yanaingiza taifa katika giza kwa minajiri ya utawala wa sheria ulioliliwa na majaji wakuu wastaafu hivi karibuni.

Kuingiza watumishi wa serikali katika siasa za vyama ambazo sheria inawazuia kufanya, ni dharau dhidi ya katiba na raia wengine wasio wanachama auu wasio na wanachama tawala.

Hali kadhalika kejeli ya Lugola kuwa wafungwa walimie meno huku rais akiagiza wapigwe mateke na kufanyishwa kazi mchana na usiku, ni ukiukwaji wa haki za wafungwa na binadamu kwa ujumla.

Ikumbukwe kuwa Rais Jakaya Kikwete aliwahi kumfukuza kazi mkuu wa wilaya mbabe aliyetumia bakora kuchapa mwalimu aliyechelewa kuingia darasani. Hata JPM kabla ulevi wa madaraka haujapanda kichwani, aliwahi kumfukuza RAS wa Mwanza aliyepigana na mkuu wa mkoa. Hiyo yote inaonyesha kwamba kuchapa mtu ni kutweza utu wake, na ni kinyume cha sheria.

Kuna haja ya kuchunguza kwa makini historia ya JPM ili kubaini asili ya ukatili wake na ukosefu wa uvumilivu. Baadhi ya wasaidizi wake wa karibu wanasema haogopi kumwaga damu iwapo kwa kufanya hivyo anafanikiwa kuondoa ubishi wowote dhidi yake au kuwanyamazisha kabisa wasimkosoe.

Na kadiri siku zinavyokwenda, ubabe wake unazidi kuongezeka. Lakini kinachotia moyo ni kwamba wananchi wanaona na wanasikia. Ndiyo maana utafiti wa juzi wa TWAWEZA ulionyesha kuwa ndani ya miaka miwili umaarufu wa rais umeshuka kutoka asilimia 96 hadi 54.

Hili si jambo dogo kwa kiongozi ambaye kwa miaka miwili mfululizo ameziba wengine midomo, na anazungumza peke yake na kuzunguka nchi nzima akifanya mikutano ya hadhara, huku vyombo vya habari vikitangaza matukio yake yote moja kwa moja. Wananchi ni wakimya, wana hofu, lakini wanajua wasichotaka.

Like
15

Leave a Comment

Your email address will not be published.