Makonda ajimilikisha “kijiji kizima” ukubwa wa viwanja 15 vya soka

PAUL Makonda, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, amemvua nguo Rais John Magufuli katika vita ya ufisadi.

Siri zake zimeanza kuvuja na imeanza kudhihirika kuwa hasira zote na bidii ya kunyamazisha bunge, wapinzani, wakosoaji, na vyombo vya habari ni mbinu ya kuwezesha wajanja kuvuna wasikopanda na kujilimbikizia mali kwa kutumia ofisi ya umma.

Shaka ya wananchi juu ya sababu za rais kudekeza na kumpendelea Makonda, ambaye kwa kutambua kuwa ni kipenzi cha Rais Magufuli amekuwa anatumia cheo chake na ukaribu wake na rais kupora mali na kujimbilikizia mali zisizo na maelezo ya kutosha, imeanza kupata majibu.

Mali nyingi alizonazo hazijulikani kwa tume ya maadili ya viongozi, na haziendani na kipato chake.

SAUTI KUBWA inaanza na viwanja vya ardhi sita vikubwa vinavyomilikiwa na Makonda katika mkoa wa Dodoma pekee.

Viwanja hivi sita anavyomiliki Dodoma vipo katika eneo linalojulikana kama Iyumbu New Town Centre, katika block R na S, vikiwa na ukubwa wa mita za mraba kati ya 5,000 na 40,000 kwa kila kiwanja.

SAUTI KUBWA inasema pasipo shaka kuwa katika ujumla wake, viwanja vyote sita vya Makonda vinachukua eneo la mita za mraba 92,341.

Mchambuzi mmoja anasema: “Kwa ukubwa huo wa viwanja, kama mita ya mraba moja iliuzwa kwa Sh. 3,500, Makonda alilipa Sh. 323,193,500 kununua viwanja hivyo.

“Kama mita moja ya mraba iliuzwa kwa Sh. 5,000,  Makonda alilipa Sh. 461,705,000 kununua viwanja vyote. Na kama mita ya mraba iliuzwa kwa Sh.15,000, alilipa Sh. 1,385,115,000 kumiliki viwanja vyote. Waliofungua mahakama ya mafisadi, kama wanataka waaminike, waanzie hapa.”

Eneo hilo ni sawa na hekta 9.23 au ekari 22.3 za ardhi, ambazo ni sawa na ukubwa wa viwanja 15 vya mpira wa miguu (soka). Ni sawa na kijiji kidogo.

Viwanja hivyo, ambavyo vielelezo vyake vimeambatanishwa hapa, havijulikani kwa tume ya maadili ya viongozi.

Katika block R kuna viwanja vinne namba 1, 28, 32 na 33. Kiwanja namba 1 kina mita za mraba 40,973, na kinalipiwa kodi na riba ya Sh. 2,581,300.

Kiwanja namba 28 kina ukubwa wa mita za mraba 18,210 na kinalipiwa kodi na riba ya Sh. 1,147,250.

Kiwanja namba 32 kina ukubwa wa mita za mraba 13,080 na kinalipiwa kodi na riba ya Sh. 824,050.

Kiwanja namba 33 kina ukubwa wa mita za mraba 9,932 na kinalipiwa kodi na riba ya Sh. 625,750.

Katika block S, Makonda anamiliki viwanja viwili, namba 17 na 18.

Kiwanja namba 17 kina ukubwa wa mita za mraba 5051, na kinalipiwa kodi na riba ya Sh. 318,250. Kiwanja namba 18 kina ukubwa wa mita za mraba 5,095, na kinalipiwa Sh. 321,000.

Kwa mujibu wa vielelezo ambavyo SAUTI KUBWA inavyo, hadi tarehe 21 Mei 2018, viwanja hivyo vilikuwa vimehakikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma. Ingawa mmiliki ni Makonda, vyote vinaonekana vimesajiliwa kwa ajili ya taasisi.

Suala la viwanja vya Makonda linaibuka wakati kuna sintofahamu juu ya makontena 20 bandarini ambayo Makonda anagoma kuyalipia kodi, huku Mamlaka ya Mapato Tanzania ikiamuru yapigwe mnada kuokoa kodi ya serikali.

Makontena hayo, ambayo awali Makonda aliyakana, yameandikwa jina lake, naye anadai kwamba vifaa vilivyomo ni kwa ajili ya shule ambazo hata hivyo hazijulikani.

Hata huko Marekani anakodai vilichangwa, kuna utata juu ya watu wanaodaiwa walivichanga. Hapo hapo kumezuka hoja kwamba ndani ya makontena ya makonda kuna vifaa vingi zaidi ya samani za shule, na kwamba samani hizo zimetumika kufunika “mzigo” halisi.

Tayari kuna maelezo kuwa Makonda aliingiza makontena hayo kwa ajili ya miradi yake binafsi kwa kutumia ofisi ya serikali. Ubabe aliotumia kushambulia wanaohoji kuhusu makontena hayo, huku akitumia jina la rais, ni baadhi ya mambo yanayoleta hisia kwamba kati ya Makonda na rais kuna biashara ambayo wananchi hawajaijua.

Baadhi ya wachambuzi wa siasa wameiambia SAUTI KUBWA kuwa uswahiba uliopitiliza kati ya Makonda na Rais Magufuli una harufu ya ufisadi.

Wanasema hata mabavu ya rais na Makonda kutumia vyombo vya dola dhidi ya raia wanaokosoa utawala wake ni mazalia ya ufisadi mkubwa utakaoibuka taratibu, hasa baada ya Rais Magufuli kuondoka madarakani.

Chanzo kimoja kimeiambia SAUTI KUBWA: “Usidhani Magufuli hajui uchafu wa Makonda. Anamlinda kwa sababu wana mradi wao. Makonda ni mtoto wa baba, ni mmoja wa viongozi wapendwa wanaojua dili chafu za baba; ndiyo sababu ya ushirika wao kunyamazisha wakosoaji.”

“Kama Watanzania walidhani Magufuli ni mwadilifu kama anavyojitapa mbele yao, walikosea sana; huyu anajulikana kwani katika wizara zote alikopitia, kulikuwa na kelele na mbwembwe nyingi za takwimu, lakini ufisadi ulitamalaki. Ataacha leo kwa vile yupo Ikulu?,” kimehoji chanzo kingine, na kuongeza:

“Hawa jamaa wana majengo na viwanja nchi nzima. Wanajimilikisha nchi utadhani dunia inaisha kesho au wanamkomoa mtu. Si uliona hata majuzi rais akiwa Mwanza, baada ya kumtembelea dada yake hospitalini, alisimama pale Nyerere Road kuzindua kwa siri jengo lake linaloitwa Nyerere Plaza, akajidai anazungumza na wananchi. Ni mali yake ile.

“Tutajua mengi sana kadiri muda unavyokwenda, na watu watashangaa. Hili la Makonda limeshamchafua rais, nasikia anajipanga kujifanya anamtumbua kwa lawama za juu juu kama njia ya kuficha uchafu wao. Hata akitumbuliwa leo ni geresha tu. Utasikia Makonda ametokea mlango mwingine.

“Hata huyu mhuni (Cyprian) Musiba ameagizwa kurusha mashambulizi dhidi ya Makonda kwa malengo maalumu maana wote ni kambi moja. Ni sanaa inachezwa kuzuga wananchi, kumsafisha rais.

Like
40

Leave a Comment

Your email address will not be published.