Magufuli ahaha kufyatua noti mpya. Azua hofu ya “uchumi wa Mugabe”

BAADA ya uchumi wa nchi kuyumba na maisha ya wananchi kuwa magumu, Rais John Magufuli anahaha kufyatua noti mpya ili kuongeza mzunguko wa fedha.

SAUTI KUBWA inatambua kwamba tayari serikali imeshaanza mradi wa ufyatuaji wa noti hizo.

Hata hivyo, mradi huo umekwama kwa muda kwa sababu ya kugubikwa na sintofahamu kati ya rais na washauri wake; na miongoni mwa kampuni zilizoingia katika mchakato huo.

Kampuni za kimataifa ambazo zimetambulika kuingia katika mzozo huo ni De la Rue International, Oberthur Fiduciare, na M/s Crane Currency.

Vyanzo vinataja ufisadi katika mchakato kama sababu mojawapo iliyosababisha mzozo huo. SAUTI KUBWA inafuatilia habari za kina kuhusu mzozo huo.

Baadhi ya washauri wa serikali wanapinga ufyatuaji wa noti mpya wakidai utaongeza mfumuko wa bei, utashusha zaidi thamani ya shilingi ya Tanzania; na utafanya maisha ya wananchi yawe magumu zaidi.

Baadhi ya wachambuzi na wachumi waliozungumza na SAUTI KUBWA wanasema iwapo serikali itachapisha noti hizo nchi inaweza kukumbwa na mdororo wa kiuchumi kama uliokumba Zimbabwe katika utawala wa Robert Mugabe.

Mchambuzi mmoja amesema: “Itasababisha mfumuko wa bei za kila kitu kwa namna itakayoifanya shilingi yetu isiwe na thamani kabisa.  Hiki ndicho alichokifanya Mugabe miaka ya nyuma baada ya kunyang’anya wazungu mashamba yao na vitega uchumi kutoka nje kukauka.

“Matokeo yake ni kwamba Zimdollar ilipoteza thamani hadi ikabidi ifutwe kabisa. Leo Zimbabwe haina sarafu yake yenyewe, na wananchi wanalazimika kutumia dola ya Marekani na rand ya Afrika Kusini kwa ajili ya manunuzi ya kila aina. Huko ndiko Magufuli anapotaka kupeleka Tanzania. Ataharibu kila kitu kilichobaki.”

Mchumi mmoja anayeheshimika nchini, ambaye SAUTI KUBWA haitataja jina lake, amezungumzia mfumuko wa bei na mzunguko wa fedha. Anasema:

“Mfumuko wa bei uko chini ya asilimia nne (4%). Si mbaya sana. Mzunguko wa hela ni kidogo. Hii ni mbaya. Kuchapisha hela ni uamuzi mbaya kiuchumi. Ujazo wa fedha katika uchumi lazima uendane na kiwango cha shughuli za uzalishaji katika uchumi.  Kuchapisha hela ni njia ya ‘kiswahili’ ya kukabiliana na changamoto ya kiuchumi.”

Uamuzi wa Magufuli kuagiza ufyatuaji wa noti mpya, unaakisi kituko cha Idi Amini (dikteta wa Uganda 1971-1979) ambaye alipoelezwa juu ya upungufu wa fedha katika mzunguko, aliamuru benki kuu: “fyatua nyingi zaidi.”

Akijadili hali hii, mhadhiri wa uchumi anayeishi Marekani, anasema kwa kirefu:

Kwanza, tuanze na kujua sababu za lazima za kuchapa pesa. Hii ni kweli kuwa serikali haina fedha za kuendesha shughuli zake na kulipa madeni.

Pili, ni kwa nini serikali haina fedha? Kwa kawaida, ukiacha misaada, serikali ina vyanzo vikubwa viwili vya mapato: (1) Kodi, (2) kuuza dhamana au bonds.

Kwa hiyo, yawezekana ukusanyaji wa mapato ya kodi umepungua Ila serikali haisemi ukweli ili kijipatia sifa za kijinga.

Pia dhamana za serikali huenda haziuziki kama ilivyokuwa awali.

Mambo yote mawili, kupungua kwa mapato ya kodi na dhamana hutokea iwapo uchumi umesinyaa: hakuna uzalishaji wa kutosha kutokana na kudorora kwa uzalishaji kiuchumi.

Nini hufanyika? Serikali ingeweza kukopa zaidi. Huenda wakopeshaji hawapo tayari kwa kuwa kiwango cha uaminifu wa serikali kimeshuka. Utakumbuka credit rating ya Tanzania imeshuka sana kwa sasa.

Pia, serikali ingeweza kubana zaidi matumizi yake. Lakini hili nalo ni gumu sana kwa sasa kwa kuwa tayari imebana hadi ukomo wake. Kumbuka pia kubana matumizi ya serikali hupunguza ukuaji wa uchumi. Kudorora kwa sekta binafsi ni matokeo ya serikali kubana matumizi.

Nini matokeo ya kuchapa pesa? Uchapaji fedha huwa na madhara hasi kiuchumi iwapo uzalishaji haukui. Yaani, kutakuwa na fedha zaidi kwenye mzunguko zisizo na thamani. Matokeo yake ni mfumuko mkubwa wa bei. Kumbuka kilichotokea Zimbabwe kwa utawala wa Mugabe.

Mfumo wa bei usioendana na kipato halisi cha watu, utapunguza uwezo wa kutumia (purchasing power) na matumizi (consumption). Hapo uchumi utaendelea kuelekea shimoni zaidi.

Like
25

Leave a Comment

Your email address will not be published.