Januari 25, 1971, mkuu wa majeshi ya Uganda, Jenarali Idi Amin, alipopindua serikali ya Milton Obote, alisema: “Sina tamaa ya madaraka. Nataka kusafisha serikali na baadaye kuirejesha katika utawala wa kidemokrasia. Nataka kukabidhi serikali iliyo safi kwa kiongozi ajaye… Hii ndio tamaa yangu… Mtashangaa kwamba nitakuwa kiongozi wa kwanza Mwafrika ambaye hang’ang’anii madaraka.”
Kuna watu waliamini kauli hii ya Amin. Waliponzwa na hisia zao hasi dhidi ya Obote, wakadanganywa na tabasamu la Amin na ucheshi wake ulioficha hulka yake halisi ya ukatili na uuaji.
Baada ya wiki moja tu, Februari 2, 1971, Amin alijitangaza rasmi kuwa rais wa Uganda, akajipa na vyeo vingine vya kijeshi ili kujiongezea nguvu, heshima na utukufu.
Miaka sita baadaye, alijitangaza kuwa “rais wa maisha.” Akaongeza: “Mimi ndiye mtu pekee mwenye upeo wa kuongoza na kuendeleza Uganda.”
Amin alianza pole pole, akamaliza kwa kishindo. Alitumia vibaya imani aliyopewa na wale waliomwamini na waliomwogopa. Akatumia hofu yao. Hatimaye, aliingiza nchi katika machafuko, na akaondoka kwa aibu. Miongo minne baadaye, Amin amepata mfuasi kutoka Tanzania. Ni John Magufuli, rais wa awamu ya tano.
Januari 18, 2019, Magufuli alisema: “Changamoto zilizopo tusipozitatua katika awamu ya tano, hazitatatuliwa maishani. Ninawambia ukweli. Kama kuna changamoto zilizobaki, tusipozitatua katika awamu hii, sina uhakika kama atakayekuja atazitatua. Kwa sababu, katika kutatua una-face magumu mengi. Ni mengi mno… ni magumu.”
Hii si mara ya kwanza kwa Magufuli kutamka maneno kama haya. Mwaka 2016, katika ziara yake mojawapo mkoani Geita, alisema kuwa yeye ndiye pekee anayejua matatizo halisi yanayowakabili Watanzania; na ndiye anayeweza kuyatatua. Ameyarudia kwa msisitizo wa pekee. Ni kauli ya ajabu kwa kiongozi wa karne ya 21, na inaweza kupewa tafsiri nyingi.
Raia mmoja wa Tanzania anayefuatilia utendaji wa serikali, anayejua ukubwa wa mikopo yenye riba kubwa iliyochukuliwa na Magufuli, anayejua viwango vya ufisadi vinavyohusishwa na miradi mikubwa inayojengwa sasa, amekubaliana na Magufuli kuwa rais ajaye atapata tabu. Ameandika katika mtandao wa kijamii: “Rais atakayefuata atakuta nchi imefilisika, ina madeni makubwa, na haikopesheki.”
Ni maneno machache yenye ujumbe mzito. Lakini ni mjadala tofauti na kusudio la Rais Magufuli, ambaye kwa maneno yake mwenyewe, ametangazia dunia kuwa hatima ya Tanzania inaishia mikononi mwake.
Anamaanisha kwamba bila yeye hakuna kiongozi mwingine anayeweza kutatua changamoto za Watanzania. Kwa hiyo, wananchi wanapaswa kutambua kuwa awamu ya tano pekee ndiyo inayowafaa. Wasikubali ipite.
Pili, kama anachosema yeye ndicho ukweli, na kama yeye ndiye kipimo cha ukweli, basi kila atakayepingana naye asiaminike. Maana yake ni kwamba wakosoaji wa Magufuli wataitwa waongo, wasaliti, vibaraka wa mabeberu, watu wasioitakia mema Tanzania.
Tatu, kwa kuwa kutatua changamoto ni kazi ngumu inayoweza kutekelezwa tu na mtu anayeweza kukabiliana na “magumu mengi,” na mtu huyo si mwingine bali yeye, Magufuli anatuma ujumbe mzito kwa Watanzania na dunia nzima.
Magufuli ametumia lugha ya mzunguko kusema jambo zito. Kauli yake ni kiashiria kuwa hataki kuondoka madarakani. Hata kama anataka, hawazi kuondoka baada ya kipindi kinachotajwa na katiba ya sasa, yaani asizidi vipindi viwili vya miaka mitano mitano (iwapo atachaguliwa tena).
Si siri kwamba kwa hulka, kauli na vitendo, Magufuli ni kiongozi anayependa mno cheo. Anapenda kusifiwa, na hayupo tayari kukosolewa au kulaumiwa.
Ingawa yeye si mwanajeshi wala hajajipa cheo chochote cha kijeshi, tayari amekuwa anatumia wadhifa wa kikatiba wa Amiri Jeshi Mkuu kuingiza majeshi katika siasa za waziwazi kwa kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa na watangulizi wake.
Taratibu, anaelekea kugeuza jeshi la wananchi kuwa jeshi la rais. Polisi, ambao jukumu kubwa walilonalo kikatiba ni kulinda raia na mali zao, wamegeuka watesaji wa raia, hasa wanasiasa, wanaharakati, na waandishi wa habari. Mifano ni mingi. Shabaha yake ni kutisha watu na kujiimarisha madarakani.
Magufuli anaandaa wananchi waamini kwamba Mungu aliumba mtu mmoja tu mwenye kujua changamoto za Watanzania, na ambaye pekee ndiye awezaye kuzifanyia kazi.
Huu ni ujumbe mzito kwa wanaowaza urais baada ya Magufuli, kwamba “haitawezekana kirahisi,” na kwamba wenye nia hiyo waahirishe kwanza au waachane nayo, wajiunge naye.
Magufuli anapenda mno urais na, kwa kauli yake ya juzi, ni wazi kuwa angefurahi kuwa “rais wa maisha.” Bado tu hajapata ujasiri wa kulitamka. Nitashangaa kama Watanzania watapuuza kauli yake hii, wakidhani ni maneno matupu ya kisiasa.
Aliposema, Februari 5, 2016, kwamba alikuwa anadhamiria kuondoa upinzani kabla ya 2020, wapo ambao walidhani ni maneno ya kisiasa tu. Hawakumwelewa.
Walianza kumwelewa baada ya kushuhudia viwango vyake vya kutumia polisi, idara ya usalama wa taifa, na msajili wa vyama vya siasa, kuvuruga na dhoofisha vyama vya upinzani. Dhamira hiyo imedhihirka zaidi sasa baada ya serikali kupeleka bungeni muswada wa vyama vya siasa ambao maudhui yake ni kufuta siasa na harakati, na kurejesha Tanzania katika mfumo wa chama kimoja.
Wapo ambao walipuuza kauli yake ya Julai 2016 alipojitapa “kuvunja miguu” ya waandamanaji na yeyote ambaye angemjaribu. Walianza kuelewa maana yake kwa uzito mkubwa siku “watu wasiojulikana” walipompiga risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Septemba 7, 2017 – wakamvunja miguu na mikono na “kumtoboa” tumbo.
Waliopuuza kauli yake ya kutaka “matajiri waishi kama mashetani,” na kwamba katika utawala wake “tajiri anaweza kufanywa lolote,” walianza kumwelewa serikali ilipoanza kuumiza wawekezaji, wafanyabiashara na matajiri, wengine wakalazimika kuhamishia mitaji yao nje ya nchi; na mmoja wao, bilionea mdogo kuliko wote Afrika kwa mujibu wa Jarida la Forbes, Mohammed Dewji, akatekwa na “watu wasiojulikana” Oktoba 2018. Juzi juzi wamemnyang’anya baadhi ya mashamba yake.
Waliodhani Magufuli alikuwa anatania pale alipotisha wamiliki wa vyombo vya habari na wahariri (Novemba 2016 na Machi 2017) kwamba asingeruhusu vyombo vya habari viwe na uhuru kuliko anaotaka yeye, wamejikuta hawana kitu cha maana cha kusoma katika vyombo vya habari vya Tanzania, kwani waandishi wa habari wanaishi kwa hofu, na wanalazimika kuchagua moja kati ya mawili haya – kumsifu yeye au kunyamaza kabisa.
Wachache waliokaidi, vyombo vyao vimefungiwa, wameteswa kimfumo na kibiashara, wamenyimwa leseni, wamepelekwa polisi na mahakamani, wametishiwa uhai, na wengine wamepotezwa.
Kwa hiyo, yeyote atakayependa kupuuza kauli yake ya juzi, atakuwa ameshindwa kujifunza haraka kutokana na mwenendo wa utawala wa Magufuli katika miaka mitatu iliyopita.
Na katika hili la “urais wa maisha,” Magufuli hatakuwa wa kwanza. Wala hatupaswi kusubiri alitamke kama walivyofanye wengine. Ni ajabu tu kwamba katika karne hii, naye anaweza kujiingiza katika jambo la kijinga lililotesa na kudhalilisha akina Kamuzu Banda (Malawi), Idi Amin (Uganda) na Mobutu Seseseko (Zaire).
Labda anatafuta fursa ya kukaa muda mrefu kwa kufuata nyayo za akina Yoweri Museveni (Uganda) na Paul Kagame. Na kwa kuwa Magufuli hana msingi mzuri katika historia na siasa za dunia, yawezekana haoni hatari inayomnyemelea kwa matamshi yake haya.
Na kwa kuwa amefanya mambo kadhaa makubwa na mabaya, wananchi wakakaa kimya, anaweza kudhani kwamba anaongoza watu mbumbumbu, waoga, wasioweza kufanya lolote asilotarajia.
Jambo la msingi hapa ni kwamba mawazo yake haya yakiachwa yakatamalaki, yatahatarisha mustakabali wa kisiasa wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika, hasa Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ni vema aambiwe mapema kuwa tamaa au hisia za “urais wa maisha” si neema kwake wala kwa Tanzania.
Aambiwe kuwa mawazo ya aina hii ni mwanzo wa upotevu wa amani ya kijamii na kisiasa tuliyojivunia kwa muda mrefu. Ni msingi wa mtikisiko wa kitaifa unaoweza kumomonyoa uimara wa kisiasa uliofanya Tanzania kuwa jabali na kimbilio la majirani kila walipotetereka.
Ni chanzo cha mtikisiko unaoweza kuleta machafuko ya kisiasa na kijamii, na hata vita ya wenyewe kwa wenyewe. Watu wenye akili timamu na wazalendo wa kweli wamwambie mapema, na wafanye hivyo sasa wakitambua hekima ya wahenga kuwa kuzuia ni bora kuliko kuponya.
Kama ana washauri – bila kujali kama anawasikiliza au la – wachukue hatua sasa ili kuepusha balaa hili. Na hapa ndipo tungependa kuona uimara wa Idara ya Usalama wa Taifa. Badala ya kukubali rais aipe majukumu ya “kimgambo” ya kuwinda wanasiasa wa upinzani na wanaharakati wanaomkosoa, inapaswa kutambua kuwa taifa ni kubwa kuliko rais, na kwamba kuna nyakati fulani hata rais mwenyewe anaweza kuwa tishio la usalama wa taifa.
Magufuli asaidiwe kujifunza kwa Mwalimu Julius Nyerere. Mwaka 1985, Mwalimu Nyerere alishinda vishawishi vya wapambe wake waliomlilia asiondoke madarakani wakisema, “hakuna mwingine anayeweza kuwa rais.”
Aliwakatalia kwa lugha kali. Katika moja ya hotuba zake baadaye, Mwalimu Nyerere alisema kuwa aliona vema aondoke madarakani akiwa bado “ana akili timamu.”
Nataka kuamini kwamba Rais Magufuli bado ana “akili timamu” za kumwezesha kukataa badala ya kutamani urais wa maisha. Lakini kwa kauli yake hii, itakuwa vigumu kwake au wafuasi wake kukatalia wanaohisi kuwa ndiye anamtuma Juma Nkamia, mbunge wa Chemba, kuibua hoja ya kubadili katiba ili rais aongoze kwa miaka saba badala ya mitano.
Anaweza kukataa au kukubali, lakini tumeyaona yakitendeka Uganda kwa Museveni na Rwanda kwa Kagame, kwa jinsi hii. Hapa tulipofikia, Magufuli asiachwe kuamua. Msimamo wake umeshajulikana. Asaidiwe mapema kuusitisha.
Badala yake aonyeshe ushujaa kwa kutatua baadhi ya changamoto za msingi kama kujenga mfumo imara wa utawala – katiba mpya, kutoingilia mihimili mingine ya dola, kuheshimu misingi ya haki za binadamu, kuheshimu uhuru wa watu, kupiga vita ufisadi badala ya kulipiza visasi, kuruhusu uhuru wa maoni na uwazi katika utawala wa nchi.