Magufuli anasema sana lakini hakumbuki alichosema jana yake

KATIKA miaka takribani mitatu mfululizo, Rais John Magufuli amedhihirika kuwa kiongozi mwenye ndimi mbili kama nyoka. Alianza na sura ya uadilifu, ukali, na umakini. Kuna watu walimwamini. Sasa uadilifu wake umeanza kuhojiwa, ukali wake umegeuka ukatili, na hakumbuki alichosema mwaka jana kwa watu wale wale. Baadhi ya watu makini wameanza kutilia shaka kila anachosema au anachounga mkono.

Mifano ni mingi, lakini hapa tutatoa michache. Alianza kazi kwa kushughulikia watumishi wabadhirifu au wezi, akisema anatekeleza ahadi kwa vitendo. Novemba 6, 2015 –  siku moja baada ya kula kiapo cha urais, alizuia semina na warsha kufanyika kwenye hoteli, alifuta posho za vikao na alizuia safari za nje zisizo na tija. Yeye alipoamua kusafiri alitembelea nchi jirani tu, akianza na Rwanda.

Novemba 9, 2015 alianzisha na kusimamia, bila kujali sura wala cheo, mapambano makali ya kusafisha uoza na kurejesha nidhamu kazini. Aliondoa wazembe, wabadhirifu wa fedha za umma, na waliotumia vibaya ofisi za umma. Haraka haraka akaanzisha mahakama ya mafisadi.

Alifanya ziara za kushtukiza, akasimamisha au kufukuza kazi au kutengua uteuzi wa wakuu wa idara, wakurugenzi, wakuu wa mikoa, wenyeviti na wajumbe wa bodi kadhaa pamoja na watumishi wengine waliotumia vibaya madaraka yao. Fedha “alizookoa” zilielekezwa kwenye miradi ya barabara. Katika kusaka wafanyakazi hewa, alibaini watumishi hewa zaidi ya 16,000.

Walio na haraka ya kutangaza sifa, walimwona kama rais wa mfano. Waliona mkombozi. Waliona mwanamabadiliko. Wengine wakasema huyu ndiye” rais mkali” tuliyemtaka. Waliomjua kwa miaka 20 aliyokuwa waziri, waliotambua hulka yake halisi, walitia shaka.

Sasa imedhihirika. Magufuli yule, si Magufuli huyu. Kimsingi, Rais Magufuli, kwa kujua na kukusudia au kwa mwenendo wake tu, amedhihirisha kauli ya Voltaire, mwanafalsafa Kifaransa na mwandishi wa vitabu, ambaye pia huitwa François Marie Arouet (21 Novemba 1694 – 30 Mei 1778). Katika bidii yake ya kusaka ukweli, haki na uhuru wa kufikiri, Voltaire alisema: “la politique est le moyen pour les hommes sans principes de diriger des hommes sans mémoire,” yaani “siasa ni njia ya wanaume wasio na kanuni kuongoza wanaume (wananchi) wasio na kumbukumbu.”

Mwaka 2016 Magufuli alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani aliwaambia wafanyakazi nchini kwamba asingeweza kuongeza mshahara kwa sababu alikuwa anakamilisha kupitia orodha yao ili kuondoa watumishi hewa.

Ikawa Desemba, ikawa Mei Mosi 2017; akawambia wafanyakazi kwamba kazi ya kuondoa wafanyakazi hewa wapatao 52,000 na wenye vyeti feki ilikuwa imekamilika lakini bado anafanya uhakiki wa watumishi waliopo ili asirudie makosa ya nyuma. Katika miaka miwili hiyo hakuna mfanyakazi aliyeongezewa mshahara au aliyepandishwa cheo – mambo ambayo hayategemei huruma ya rais bali yapo kisheria. Hakuna waliopandisha madaraja, au walioajiriwa.

Ikawa Desemba, ikawa Mei Mosi 2018. Rais ni yule yule Magufuli, na siku ni ile ile Mei Mosi na watu anaozungumza nao ni wafanyakazi walewale na maelezo anayoyatoa ni yale yale yanayothibitisha siasa ni mfumo uliobuniwa na watu wasio na kanuni kwa ajili ya kuongoza watu wasio na kumbukumbu.

Mwaka 2018 katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ambayo kitaifa yalifanyika mjini Iringa, Rais Magufuli amewaambia wafanyakazi kwamba hatawaongeza mshahara kwa sababu “anajenga miundombinu ya uchumi.” Kwamba anajenga reli, barabara, viwanja vya ndege na ananunua ndege lakini atawaongeza nyongeza nono kabla ya kumaliza muhula wake wa utawala.

Mtu yule yule ambaye tangu ameingia madarakani amekuwa akijinasibu kwamba serikali yake sasa inakusanya mapato mengi zaidi kuliko wakati mwingine wowote; ambaye Machi mwaka huu alipofanya ziara Kahama mkoani Shinyanga kuzindua viwanda vya Kahama Oil Mills na vingine vitakavyokuwa vinazalisha bidhaa za plastiki, chuma, mabati na mabomba ya maji, alisema kwa sasa serikali ina fedha za kujiendesha kwa zaidi ya miezi 5 inayokuja, hakumbuki tena kauli yake.

Wakati ule aliposema fedha ipo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi William, Lukuvi naye alidakia: “Tuna fedha nyingi, tunaweza kujitegemea.” Hata hivyo, kauli zao hizo zilipingwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, akasema serikali haina fedha na imekopa zaidi ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge.

Serikali ilimsakama Zitto na hata kumwita majina mabaya, na kwamba kwa kusema serikali haina fedha, hana uzalendo. Kabla hata mwezi mmoja kupita, katika mazingira ya kutafuta jinsi ya kutoongeza mshahara, Rais Magufuli amewambia wafanyakazi na wananchi wote, “nikisema nitaongeza mishahara pesa nitazitoa wapi?” Ni yule yule alisema kuwa serikali ina fedha nyingi.

Huku akitamba kuwa ana fedha za kununua ndege, kujenga reli, barabara, viwanja vya ndege na miundombinu mingine, hajui atapata wapi fedha za kuongeza mishahara ya watumishi. Zimekwenda wapi fedha alizosema zinatosha kwa miezi sita ijayo?

Katika miaka miwili iliyopita amekuwa akitamba kwamba serikali inajenga miundombinu ya barabara na reli kwa fedha zake yenyewe, lakini wiki hii wakati anazindua barabara ya Kidatu-Ifakara ametangazia taifa kwamba fedha zinazotumika kujenga ni za wafadhili Wamarekani, Wajerumani na wengineo.

Ni mtu msahaulifu ambaye wakati bunge linajadili ufisadi wa Escrow nan serikali inasisitiza kuwa hazikuwa mali ya umma, naye alisimama upande wa waliosema hazikuwa pesa za umma. Lakini baada ya kuingia madarakani, amekuwa mwepesi kushughulikia watuhumiwa na ufisadi wa Escrow, huku akiacha watendaji wa TEMESA TANROADS waliokuwa chini yake, na ambao walisababisha ufisadi wa kutisha. Hata waliopoteza Sh 252 bilioni katika wizara ya ujenzi alipokuwa waziri, hawajaguswa.

Ni yule yule ambaye alipokuwa waziri wa ujenzi alizungumzia faida ya safari nyingi za Rais Jakaya Kikwete na umuhimu wa misaada ya Shirika la Changamoto ya Milenia (MCC) ya Marekani. Alikuwa anapaza sauti kuunga mkono juhudi za Kikwete katika kukuza uchumi na kutafuta misaada ya kiuchumi.

Novemba 3, 2012 akizungumza wakati wa ufunguzi wa Barabara ya Minjingu – Babati-Singida, alimtaka Kikwete kuongeza safari za nje kwa sababu zinachochea maendeleo kwa kasi nchini.

“Wapo wanaosema wewe Rais unatembea sana nje ya nchi, lakini bila kutembea kwako tusingepata maendeleo tunayopata. Hivyo tunakuomba uendelee kutembea ili tuendelee kupata maendeleo zaidi,” alisema.

Mara baada ya kuingia Ikulu alizuia safari za nje hadi kwa kibali chake. Novemba 6, 2015 yaani siku moja tu baada ya kuapishwa kuwa rais wa Tanzania, alitangaza kufuta safari zote za nje ya nchi hadi hapo maamuzi mengine yatakapotolewa. Uamuzi huo aliutoa katika kikao kilichojumuisha watendaji mbalimbali wa serikali wakiwemo makatibu wakuu, manaibu makatibu wakuu, Gavana wa Benki Kuu na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Novemba 20, 2015 alipokuwa anazindua Bunge la 11, Rais Magufuli alikosoa vikali viongozi walioendekeza safari za nje akisema baadhi yao walisafiri mara nyingi zaidi kwenda nje kuliko hata walivyokwenda kuwasalimia mama zao, kauli iliyokosolewa na wachambuzi wa siasa.

Rais Magufuli anasema sana, hanamuda wa kusikiliza wengine, lakini hakumbuki alichosema jana yake. Kiongozi wa aina hii kesho anaweza kuibuka na hoja inayopingana na alichosema juzi. Hata mahakama ya mafisadi aliyounda kwa kulenga baadhi ya watu asioshibana nao, haijapata fisadi wa kushitaki wala kuhukumu. Huyu, hata kama angekulazimisha umsikilize, usimwamini. Haaminiki!

Like
3
2 Comments
  1. Mzalendo 6 years ago
    Reply

    Haaminiki na hakubaliki na sio msahaulifu bali ni Muongo na anapenda sifa asizostahili….

    1

    0
    • Jaimee 6 years ago
      Reply

      Hatari

      0

      0

Leave a Comment

Your email address will not be published.