Tujadili kwanini Magufuli amejipa kinga ya kupotosha Watanzania

President John Magufuli - file photo

IMEDHIHIRIKA sasa kwamba Rais John Magufuli amekuwa anapotosha Watanzania katika mambo mengi ya msingi.

Upotoshaji wake unakera sana kwenye sekta za afya, uchumi, utawala wa sheria, haki za binadamu, demokrasia na hata elimu. Sekta zote hizi ni nyeti na zinagusa uhai wa taifa.

Kisichojulikana kwa hakika ni chanzo cha upotoshaji wake. Je, ni ujinga wake mwenyewe wa kutojielimisha? Je, ni ujinga wa washauri wake? Je, ni ulevi wa madaraka unaotokana na kile kinachoitwa “Rais hakosei na yuko juu ya sheria?” Je, afya yake ya akili iko sawa sawa wakati wote au ana msongo wa aina fulani unaoathiri mfumo wake wa uamuzi?

Raia wa kawaida akipotosha umma ni kosa la jinai. Iweje upotoshaji unaofanywa na rais uonekane ni kitu cha kawaida?

Rais Magufuli anasema hadharani kuwa chanjo hazina maana!

Huyu ni rais ambaye serikali anayoongoza ina Wizara ya Afya inayotumia karibia asilimia 30 ya bajeti yake kwa shughuli za kinga (yaani chanjo na elimu ya chanjo). Anapambana na wizara yake mwenyewe?

Rais Magufuli anataja orodha ya chanjo “zilizoshindikana kupatikana” duniani na, miongoni mwa hizo, anaitaja chanjo ya kifua kikuu (BCG). Chanjo hii ipo miaka mingi. Kwa hiyo, ama rais anapotosha au anapotoshwa.

Anasema kwa kuwa “wazungu” hawajapata chanjo ya UKIMWI hawawezi kuaminiwa kwa kupata chanjo ya Corona, na kwamba chanjo hiyo haiwezi kuaminika. Ni Magufuli huyu huyu ambaye serikali yake inapokea dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI kutoka kwa “wazungu” hao hao!

Rais Magufuli anarundika tuhuma nzito kwa mataifa ya kigeni – hasa ya Ulaya – kuwa hayatupendi Watanzania na yana nia ovu ya kutuangamiza ili yachukue utajiri wetu. Kwa akili ya Magufuli, ambayo anataka na Watanzania waikubali, Corona ni ugonjwa ambao “wazungu” wameutengeneza kwa ajili ya kuihujumu Tanzania!

Hajui – au anapuuza – ukweli kuwa hao anaowatuhumu ndio wameathirika zaidi, na kwamba Tanzania ni sehemu ndogo sana ya waathirika wakuu wa Corona. Yanayowapata Watanzania ndiyo yanawapata wengine. Tofauti ni kwamba sisi tunasema “hakuna Corona” na hatutaki chanjo hukuwa watu wetu wakifa, wakati wenzetu wanakiri kuwa wana tatizo na wanatumia taarifa zilizopo kutafuta ufumbuzi wa kitaalamu.

Rais Magufuli anaenda mbali zaidi na kudai kuna Watanzania wameenda nje wakapatiwa chanjo ya Corona kisha wakarudi nchini na kuleta “Corona ya ajabu ajabu.” Ni rais huyu huyu ambaye anakaribisha wageni hadi kwake Chato, watalii na wasafiri wengine wengi kutoka mataifa ya nje, na kuwambia watu kuwa “hakuna Corona,” na hivyo kuwafanya wasichukue tahadhari. Wananchi wameeneza ugonjwa kwa mikusanyiko mikubwa tangu wakati wa uchaguzi hadi sherehe za Krismasi na mwaka mpya.

kinachoonekana kusumbua na kuua watu sasa ni matokeo ya uwongo wa rais kwa umma kuwa sala za siku tatu ziliponya Corona, ikafutika Tanzania tangu mwaka jana; kumbe ilikuwa haijasambaa sana, sasa tumeiruhusu ienee kirahisi kwa kutowataka watu wawe makini na kuzingatia ushauri wa kitaalamu.

Mara nyingi, rais amesema mambo haya katika nyumba za ibada, akitumia jina la Mungu kama ganzi. Imewachukua muda hata vongozi wenyewe wa dini kung’amua kuwa tabia yao ya kujipendekeza kwa rais na kumpa mimbari aeneze uwongo wake, itasababisha vifo vya wananchi wengi, hasa kwa kuwa Watanzania wana hulka ya kuamini kauli za wakubwa.

Sasa viongozi wa dini wenyewe wameamua kusimamia ukweli wa kisayansi na kuwataka waamini na wananchi wazingatie ushauri wa kitaalamu badala ya kauli za kisiasa. Wamechelewa, lakini, kwa hatua hii, wataokoa roho nyingi ambazo zingepotea kirahisi na kijinga kwa kuamini upotoshaji unaofanywa na rais.

Kwa kuwa rais anasema mambo haya hadharani, tuhuma hii itakuwa ni rasmi sasa, maana yake rais amepewa taarifa za uhakika na si umbea.

Ujumla wa upotoshaji huu unaofanywa na kiongozi mkuu wa nchi unaashiria mambo makuu mawili.

Kwanza, rais anaweza kuwa anaumwa ugonjwa uitwao “Schizophrenia”. Moja ya dalili kuu za ugonjwa huu ni kuishi kwa hofu huku ukijifanya huogopi.

Dalili nyingine ya ugonjwa huu ni kutengeneza maadui wasiokuwepo – nadharia ambazo zinaangukia katika kile ambacho wenzetu wanaita “conspiracy theories.”

Huu ni ugonjwa hatari hasa ukimpata mtu mwenye nafasi na mamlaka ya kufanya uamuzi mzito unaogusa maslahi ya wengi.

Hili si jambo jepesi. Linapaswa litazamwe kwa upana wake.

Pili, Rais Magufuli anaweza kuwa amezungukwa na watu wanaompotosha makusudi ili aonekane kituko mbele ya dunia. Hawa ni watu wanaoishi kwa kumpatia taarifa za kumtisha ili awategemee wao, na wao wapate kula.

Pia wanaweza kumpotosha makusudi ili abaki akifikiria hayo wanayompotosha nayo, na kwa njia hiyo wao wafanye mengine ya kuhujumu taifa letu huku wakilindwa na “mapenzi ya rais.” Ni sawa na kumpa kidoli mtoto mtukutu ashinde anacheza nacho ili mzazi apate nafasi ya kufanya kazi zake.

Msimamo wa rais juu ya ugonjwa wa Corona na uhusiano wa Tanzania na Jumuia ya Kimataifa umejaa upotoshaji. Kwa kiwango kikubwa, unaligharimu taifa uhai wa watu na kuharibu uchumi. Lakini nani atamshughulikia rais hata kama itathibitika kuwa anaongopa? Nani atawajibika juu ya upotoshaji huu ikiwa rais ana kinga kikatiba?

Katika hali ya kawaida, wasaidizi wa rais walipaswa wajiuzuru haraka sana. Kama wakisita, rais mwenyewe alipaswa awafukuze kazi mara moja. Lakini atafanya hivyo tu iwapo naye atafahamu kuwa wanampotosha.

Ndiyo maana Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alimshikinikiza Rais Ali Hassan Mwinyi awachukulie hatua Waziri Mkuu John Malecela na Katibu Mkuu wa CCM Horace Kolimba. Aliwataka wajiuzuru kwa kumpotosha rais, na kumfanya raisbeye apotoshe taifa.

Haishangazi kuona Rais Magufuli kila kukicha anafanya mambo yenye upungufu wa ustaarabu wakati ana wasaidizi.

Kwa mfano, inawezekana vipi rais anafanya uamuzi wa kugawa majina ya watu kwa taasisi za umma bila uchunguzi na mchakato? Inawezekana vipi, licha ya kelele nyingi tika pande, rais aendelee kurundika miradi mikubwa nyumbani kwake Chato wakati wasaidizi wake wapo na hawamwambii athari ya jambo hilo?

Kama wanamwambia anakaidi, wanasubiri nini kujiuzuru? Itawezekana vipi rais ghafla amegeuka kuwa mwekezaji akichukua “mabonge” ya ardhi kila mahali na kuweka vitega uchumi vyake, na haambiwi kuwa baadaye vitamletea mgongano wa kimaslahi na kumomonyoa misingi ya uadilifu na kusimika ufisadi?

Popote, na zaidi kwa Watanzania, rais ni nembo inayotangaza taifa. Matamshi yake yana nguvu kuliko matendo yake.

Lakini, kama ambavyo Wamarekani wamejitahidi kuvumilia vituko vya Rais Donald Trump kwa miaka minne iliyopita, na Watanzania wamejikuta wanalazimika kubeba maumivu ya kauli za ajabu za Rais Magufuli katika miaka mitano iliyopita.

Tusipojihadhari, iwapo tutaendelea kuona mambo haya ni ya kawaida, tutalazimika kuishi na aibu hii kwa miaka mingi ijayo.

Heri Wamarekani wamefanikiwa kuondokana na Trump wao – ingawa naye amewadhalilisha na kuwaachia jina baya duniani.

Like
27