Magufuli amegeuza siku ya wafanyakazi kuwa siku ya rais

DUNIANI kote, siku ya wafanyakazi ni siku yao. Ni ya wafanyakazi. Siku hiyo ni siku ya kukumbushana majukumu yao na wajibu wao katika kutetea maslahi yao. Ni siku ya kuzungumzia changamoto zao. Ni siku ya kumkumbusha mwajiri au serikali wajibu wake kwa wafanyakazi, kumkumbusha na kumdai haki zao kama wafanyakazi.

Hii si siku ya kutoa pongezi kwa waajiri. Mwajiri kuwafanyia wafanyakazi mazuri na kuwalipa haki zao si sifa ya kumpongeza mwajiri siku ya Mei Mosi. Huo ni wajibu wa mwajiri kimkataba. Hauhitaji kutafutiwa sifa mahususi kwenye sherehe za Mei Mosi. Kwa kweli hii si siku ya mwajiri. Zaidi ni siku ya kumlalamikia mwajiri na kumtaka arekebishe upungufu kwenye maslahi na haki za mfanyakazi.

Hata mabango siku ya Mei Mosi kwa ujumla yanatakiwa yaonyeshe upungufu, malalamiko, na maombi kwa mwajiri ili aboreshe maslahi na azingatie mikataba ya ajira au kuiboresha. Hii ndiyo historia na utaratibu wa siku ya wafanyakazi duniani, na kwa kiasi kikubwa ndivyo ilivyokuwa hata Tanzania kwa miaka mingi.

Lakini katika utawala huu wa sasa watu, taasisi na viongozi wamekuwa waoga, wametishwa na kutishika; hata vyama HURU vya wafanyakazi havipo huru tena, viongozi wa vyama vya wafanyakazi wamekuwa na woga. Hawasemi ukweli. Hii ni hatari sana katika kulinda na kutetea maslahi ya wafanyakazi. Hatimaye, wafanyakazi ndio wataumia na kushusha ari na motisha ya kazi na tija sawia.

Tukifika mahali wafanyakazi wanaambiwa nini cha kuweka kwenye mabango ya Mei Mosi na nini kutoandika, tujue tumefika pabaya sana. Sasa mabango ya malalamiko ya wafanyakazi yanakaguliwa na watawala ili yasiyofaa yaondolewe. Mabango mengine yanaandikwa na waajiri (serikali) halafu wanawapatia wafanyakazi wayabebe!

Katika Mei Mosi mwaka huu tumeona mabango mengi ya kusifu serikali hata pale tunapojua kwa hakika kwamba ukweli hauko hivyo. Kwa mfano, wakati hivi karibuni tumesikia malalamiko nchini kuhusu vitabu vya kufundishia darasa la kwanza hadi la nne, Mei Mosi hii tumeona bango lililoandikwa: “Tunashukuru serikali ya awamu ya tano kupitia Taasisi ya Elimu ya kutuletea vitabu vya darasa la kwanza mpaka la nne.” Baadhi ya walimu walikuja na mabango yenye ujumbe wasiouamini mioyoni mwao, kama: “Walimu tumekubaliana na kasi yako…” wakati wako hoi kimaslahi!

Mwaka jana, mkuuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitisha wafanyakazi kwamba angewachapa viboko kama wangebeba mabango ya kulalamikia nyongeza ya mishahara. Mwaka huu, ama kwa woga ama kwa kulazimishwa, wafanyakazi wamekuja na mabango yenye kummwagia sifa hata vitu ambavyo havijatekelezwa: “Tunakushukuru Mheshimiwa Makonda nauli bure na ofisi za walimu DSM zimeongeza ufanisi wa kazi kwa walimu.”

Umuhimu wa kuwekeza katika raslimali watu

Imethibitishwa kwamba nchi zinazowekeza kwenye miundombinu ya vitu kuliko zinavyowekeza kwenye kuendeleza watu wao au nguvu kazi yao, haziwezi kupata maendeleo endelevu kiuchumi.

Kwa mfano, katika andiko lao la kitafiti kuhusu umuhimu wa kuendeleza rasilimali watu walilowasilisha kwenye mkutano wa nchi zinazoendelea na Umoja wa Ulaya, jijini Brussels, Ubeligiji mwezi Machi mwaka huu, wataalam wa masuala ya maendeleo, Brenda King na Eric Osei wameeleza wazi kwamba uwekezaji na uendelezaji wa rasilimali watu katika nchi zinazoendelea una tija na ni kichocheo kikubwa zaidi katika kuinua uchumi wa nchi hizo kuliko uwekezaji kwenye miundombinu ya vitu. Uwekezaji katika rasilimali watu unahusu zaidi uwekezaji kwenye elimu, mafunzo kazini, afya, tija na bei nzuri kwa mazao ya wakulima na maslahi bora ya wafanyakazi.

Je, Tanzania inajali ipasavyo uwekezaji kwenye maendeleo ya rasilimali watu? Jibu la swali hilo utalipata katika majadiliano makubwa yanayoendelea nchini kuhusu hali mbaya ya elimu nchini, malalamiko ya wafanyakazi kutopewa mafunzo ya kuwaendeleza wakiwa kazini, bajeti ndogo isiyoakisi mahitaji ya sekta ya afya, malalamiko ya wakulima kuhusu bei ndogo za mazao yao, upandaji wa bei za bidhaa na mafuta, na maslahi hafifu ya wafanyakazi, ambayo ndiyo mada yetu kuu hapa leo.

Uhusiano wa maslahi ya wafanyakazi na tija

Wataalam na watafiti wengi duniani wamethibitisha kwamba mwajiri anapoboresha maslahi ya wafanyakazi, tija inaongezeka. Na wafanyakazi wanapokuwa na malalamiko na kinyongo cha kutolipwa vizuri, tija ya taasisi au nchi hushuka. Kwa mfano, mtafiti mmoja aitwaye James Sherk anasema kwamba maslahi ya wafanyakazi yalipopanda kwa asilimia 78 tija iliongezeka kwa asilimia 81.

Aidha, nchi zote zilizoendelea na ambazo tunazitolea mifano ya uchumi wao kupaa kwa kasi kama China, Korea, Singapore, Malaysia, Thailand, Vietnam n.k. zimewekeza katika kuendeleza nguvukazi na wafanyakazi kwa kuwapa elimu nzuri na maslahi mazuri. Ukipitia historia ya nchi hizo, utaona kwamba wamepata maendeleo hayo kutokana na tija kubwa ambayo nayo imetokana na rasilimali watu iliyoridhika kutokana na maslahi na hali nzuri ya maisha.

Hali ya wafanyakazi Tanzania ikoje?

Kwa bahati mbaya, mikakati ya maendeleo ya serikali ya awamu ya tano Tanzania haionyeshi kuweka umuhimu unaostahili kwenye maslahi na motisha kwa wafanyakazi. Hili ni kosa la kimkakati lenye athari kubwa kwenye uzalishaji na ufanisi, na linaweza kurudisha nyuma dhamira ya serikali tunayoambiwa ya “kukuza nchi kufikia uchumi wa kati.” Wafanyakazi wamekuwa wakilalamikia kutopewa nyongeza ya mishahara kwa takribani miaka minne sasa, kutopandishwa madaraja, kutolipwa madai yao ya likizo, malimbikizo n.k.

Kila mara serikali imekuwa inaahidi kulipa madai yao lakini utekelezaji umekuwa tatizo. Mwaka jana katika sherehe za Mei Mosi, rais aliahidi kuwaongezea mishahara na madaraja wafanyakazi wa serikali katika bajeti ya mwaka huu, lakini Mei Mosi mwaka huu amegeuka ahadi yake na kusema hataongeza mishahara kwa sasa kwa sababu hana hela!

Huku serikali ikijigamba kwamba inafanya vizuri katika ukusanyaji wa kodi, kwamba imepandisha makusanyo kutoka shilingi bilioni 805.6 hadi trilioni 1.3 kwa mwezi, tumeona ikiweka mkazo kwenye matumizi mengine na kupuuzia madai ya wafanyakazi.

Miundombinu kwanza kabla ya maslahi ya wafanyakazi?

Katika utawala huu, serikali imekuwa ikiweka mkazo kwenye ujenzi wa miundombinu kama reli, barabara, ununuzi wa ndege na mengine, huku wafanyakazi wakilalamikia maslahi na mafao yao. Hatusemi kwamba miundombinu si muhimu au isijengwe, lakini lazima ujenzi huo uende sambamba na kuwalipa wafanyakazi maslahi bora na kuwapa haki zao kama nyongeza za mishahara, kupandishwa madaraja na kuwalipa madai yao na mafao wanayostahili.

Serikali isipofanya hivyo, wafanyakazi hawatakuwa na tija na ufanisi, kwani watapoteza ari na motisha ya kazi, na kama tulivyoona bila kuwekeza kwenye kuendeleza rasilimali watu uchumi wa nchi utadorora.

Majuzi siku ya Mei Mosi tumemsikia Rais Magufuli akiwaambia wafanyakazi kwamba hawezi kuwaongeza mishahara hadi akamilishe kujenga reli ya kisasa, anunue ndege zaidi, akamilishe mradi wa umeme wa Stigler Gorge na miradi mingine mikubwa ya miundombinu.

Kauli hii haiwezi kufurahiwa na wafanyakazi hata kidogo, lakini pia ni kauli ambayo inaweza kushusha morali na tija ya wafanyakazi na kupunguza kasi ya kukua kwa uchumi wa nchi. Kwamba wafanyakazi wangojee hadi 2020 au kabla Rais Magufuli hajatoka madarakani ili kupata nyongeza za mishahara? Kwani nyongeza ya stahiki zao ni hisani ya rais au matakwa ya kisheria?

Kuna mtaalam mmoja amewahi kusema: “When the employer pretends to pay the employees, the latter also pretend to work. As a result, whatever progress was expected will come to a halt.” Kwa tafsiri rahisi ni kwamba mwajiri asipomlipa vizuri mfanyakazi au akijifanya anamlipa, mfanyakazi naye atajifanya anafanya kazi kumbe hafanyi na, hatimaye, tija na maendeleo havitapatikana.

Lakini pia tuulizane maswali muhimu. Miradi hiyo mikubwa inayojengwa na serikali ya awamu ya tano inajengwa kwa fedha za mishahara ambazo wangelipwa wafanyakazi? Tunavyojua, sehemu kubwa ya miradi hii inajengwa au inategemea kujengwa kwa mikopo toka nje ya nchi na si bajeti inayotakiwa kwenda kwenye nyongeza za mishahara ya wafanyakazi.

Aidha, tutaaminije kwamba miradi hii ya muda mrefu ikikamilika wafanyakazi hawataambiwa wasubiri hadi serikali ikamilishe kulipa mikopo iliyotumika kujengea miradi hiyo? Na marejesho ya mikopo hiyo yatakamilika mwaka gani? 2050?

Uhuru wa Vyama vya Wafanyakazi umeminywa

Kwa ujumla, vyama huru vya wafanyakazi nchini Tanzania kwa sasa havipo huru. Viongozi wa vyama hivyo wanafuata na kusikiliza wanachotaka viongozi wa serikali, na si wafanyakazi waliowaweka madarakani ili wawatetee. Serikali inataka vyama na viongozi wao wawe dhaifu. Chama cha Walimu (CWT) kwa mfano, ambacho huko nyuma kilikuwa na nguvu ya utetezi wa wanachama wake, kimekuwa dhaifu na kimekuwa kama idara ya Serikali huku kikiwanyonya wanachama wake kwa kuwatoza ada kubwa.

Ingawa sheria inaruhusu vyama vingi kuanzishwa kwenye sekta moja na kuna walimu wengi wasioridhika na uendeshaji wa CWT, juhudi zao za kutaka kuanzisha chama kingine cha walimu zimegonga mwamba kwa mbinu za CWT ikishirikiana na serikali, kinyume kabisa na utashi wa sheria ya vyama vya wafanyakazi.

Ni kwa muktadha huo tunaweza kusema uhuru wa vyama vya wafanyakazi nchini Tanzania uko kifungoni kama ulivyo uhuru wa kufanya siasa, uhuru wa habari na hata uhuru wa mihimili mingine kama Bunge na Mahakama. Taifa lipo kifungoni, na serikali inajidanganya kuwa inapendwa.

Uchambuzi huu umefanywa na Dk. Milton Mahanga, mtaalamu kwenye masuala ya fedha, ununuzi na uendeshaji wa nyumba mijini. Amekuwa mhadhiri kwenye fani za uhasibu, ununuzi na ugavi, mbunge kwa miaka 15, na naibu waziri kwa miaka 10 katika wizara kadhaa za Tanzania, ikiwemo miaka saba katika wizara ya kazi na ajira. Ni mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala, na  mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema.

Like
3
1 Comment
  1. Mzalendo 6 years ago
    Reply

    Nchi inaangamia kw kukosa kiongozi anaejielewa….

    0

    0

Leave a Comment

Your email address will not be published.