Magufuli ahitimu udikteta uchwara, sasa awa dikteta kamili

Tazama anavyofanana na anavyofuata rasmi nyayo za watawala wakatili wenzake – Mussolini, Hitler, Mobutu na Amini – kama uchambuzi huu unavyoeleza.

Na Mwandishi Wetu

RAIS John Magufuli ni kiongozi safi au fisadi, au dikteta? Katika miaka miwili ya kwanza ya utawala wake, rais mwenyewe amejibu swali hili kwa kauli na vitendo. Kwa msaada wake mwenyewe, sasa dunia inajua vema Rais Magufuli ni nani.

Mwaka 2016 na mwanzoni mwa 2017, aliitwa “dikteta uchwara.” Aliyempa jina hili ni Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki, ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na mnadhimu wa upinzani bungeni.

Wakati huo kulikuwa na kila dalili za udikteta. Lakini kwa viwango vya madikteta wakubwa ambao dunia imewahi kuwashuhudia, Lissu alidhani kwamba Rais Magufuli alikuwa bado anajifunza, anaiga. Akasisitiza: “Tuna rais wa ajabu haijapata kutokea…lazima apingwe na kila mtu mwenye akili timamu.”

Aprili mwaka 2018, Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chadema na kiongozi wa upinzani bungeni, alisema: “mwanzoni tulisema huyu ni dikteta uchwara, sasa tumethibitisha kuwa ni dikteta kamili.” Hiyo ilikuwa baada ya matukio mengi yaliyotia doa serikali, rais mwenyewe na taifa kuhusu watu kupotea, kuteswa, kutekwa, kuuawa, kubambikiwa kesi mbaya, kufungwa gerezani, na kadhalika. Wengi waliokumbwa hayo ni wanasiasa, waandishi wa habari au wanaharakati waliomkosoa rais, au waliopinga jinsi anavyoendesha nchi kwa mabavu na ukatili.

Uchambuzi wa SAUTI KUBWA unaonyesha kuwa Rais Magufuli sasa, ndani ya muda mfupi wa miaka miwili tu, anafanana na madikteta wengine na viongozi katili waliotawala nchi nyingine katika Ulaya na Afrika kwa nyakati mbalimbali. Kwa ajili ya kuweka msisitizo tu, tunafanya ulinganisho fupi kati ya Magufuli na baadhi yao.

 

Magufuli na Benito Mussolini

Mussolini, dikteta na fashisti aliyetawala Italia kuanzia 1922 hadi 1943. Alikuwa na maisha ya utoto na uvulana ambayo watu wanaomfahamu Magufuli wanasema naye alikuwa na utoto na ujana wa aina hiyo. Mussolini alizaliwa katika familia ya kawaida mno, akiwa mtoto wa kwanza. Baadaye, alipokuwa mtu mzima, alijisifu kwamba yeye ni mtoto wa maskini, “mtu wa watu.”

Magufuli naye alizaliwa katika familia masikini, akiwa mtoto wa kwanza. Ingawa kabila lake ni Mzinza, amekuwa anajiita Msukuma kwa kuwa wadogo zake wengine ni wasukuma, naye amelelewa na kukulia usukumani. Ukubwani, hasa katika siasa za kitaifa, amekuwa anasisitiza mara kadhaa kwamba yeye ni “mtoto wa maskini, mtu wa watu,” anayepigania wanyonge.

Utotoni, Mussolini alikuwa mtukutu, mgomvi, na katili. Aliburuza na kuonea watoto wenzake shuleni. Aliwashinda hata walimu wake, wakalazimika kumhamishia kwenye shule ya bweni, ya shirika la watawa wa Salesian, ili aweze kubanwa na kufundwa. Hata hivyo, ukorofi wake uliendelea, hata akamchoma kwa kisu mwanafunzi mwenzake; akamshambulia mmoja wa watawa aliyediriki kumchapa kiboko. Alifukuzwa, akapelekwa Shule ya Giosuè Carducci. Huko nako alifukuzwa, baada ya kushambulia mwanafunzi mwingine kwa kisu. Licha ya ukorofi wake, alishinda mitihani bila shida. Akatunukiwa diploma ya ualimu, akafanya kazi kama mwalimu mkuu kwa muda. Baadaye akagundua kwamba kazi hiyo haimfai.

Magufuli naye vile vile. Waliocheza naye utotoni wanasema alikuwa katili, mkorofi na mwonevu. Waliosoma naye shule ya sekondari wanasema hata kufukuzwa kwake kutoka Seminari ya Katoke, kulitokana na ukatili aliomfanyia mwanafunzi mwenzake. Naye alisomea ualimu, akapata alama ndogo, zikampeleka kusomea diploma chuo cha Mkwawa Iringa. Baada ya hapo alijiendeleza hadi chuko kikuu cha Dar es Salaam. Baadaye alichana na ualimu akajiunga na siasa.

Lakini wanaojadili ukatili wake wanasimulia kituko kilichotokea katika msiba wa baba yake, alipozozana na baba zake wadogo kuhusu jeneza lililopaswa kutumika. Baada ya baba zake wadogo kusisitiza kuwa kaka yao angezikwa katika jeneza walilonunua wao (kabla yeye hajawasili na lake), huku naye akisisitiza kuwa baba yake angezikwa kwenye jeneza alilonunua yeye (Magufuli), wanasema aliingia ndani akatoka na shoka, akapasuapasua jeneza lao mbele yao, halafu akawauliza kwa kejeli: “atazikwa katika jeneza lipi?”

Wote wawili, Mussolini na Magufuli, waliacha ualimu na kuingia katika siasa, na walianza kwa kuungwa mkono na umma kabla makucha yao ya kidikteta hayajachomoza.

Mussolini, baada ya kuingia madarakani, alijitengeneza mazingira awe na mamlaka ya kutawala bila kuingiliwa au kushauriwa. Ndani ya mwaka mmoja, alikuwa amejipatia mamlaka kamili na ameteka bunge kwa kuongeza idadi ya “vijana wake.” Kwa kutojua, Waitaliano wengi, hasa maskini na wa tabaka la kati, walimwamini, wakamuunga mkono; na walifurahia sana kuwa na kiongozi mwenye mamlaka kamili, asiyepingwa, na asiyekosolewa “ili afanye kazi, asikwamishwe na mtu.” Walikuwa wamechoka maandamano na migomo ya wafanyakazi dhidi ya serikali.

Walitamani Mussolini apate mamlaka yote na ayatumie kuchapa kazi ya kuinua uchumi. Walifikiri  ndiyo njia pekee ya kurejesha heshima na utulivu wa nchi yao. Kwa hiyo, walimuunga mkono Mussolini kwa kila hatua aliyochukua. Kwao, Mussolini ndiye mtu pekee aliyeonekana angeweza kurejesha amani na utulivu.  Baada ya kupewa fursa hiyo, Mussolini akafuta mfumo wa vyama vingi. Vyama vya upinzani vikapigwa marufuku. Akabakiza chama chake. Vyama vya wafanyakazi vikapigwa marufuku. Vyombo vya habari huru vikapigwa marufuku. Upinzani ukafa. Akatawala jinsi alivyotaka.

Mussolini akaanza vitisho. Kila aliyehoji agizo lake alitiwa mbaroni. Akaunda makundi ya mashushushu kuvizia na kupeleleza wananchi waliokuwa wanamjadili kwenye baa na vijiwe. Baada ya muda, makali ya Mussolini yakageukia waliomuunga mkono, hasa waliberali, wakristo, na wajamaa wenzake. Mwaka 1924, vijana wake wakateka na kuua Giacomo Matteotti, mmoja wa vinara watetezi wa Ujamaa, aliyejaribu kumkosoa Mussolini.

Licha ya ukatili wake, nje ya Italia, Mussolini alisifiwa kama mtawala mahiri, mwenye vipawa visivyo vya kawaida. Kila alichofanikisha kilisifiwa mithili ya muujiza. Kwa muda mfupi, alifanikiwa kufanya mambo kadhaa mazuri kiuchumi, yakatumika kudumaza wananchi, na kurejesha matumaini hewa – hasa katika kuboresha mifumo ya kijamii, miundiombinu na ujenzi, akiungwa mkono na wenye viwanda na wamiliki wa ardhi. Kwa hila, alifanikiwa hata kulainisha uongozi wa kanisa, na kuungwa mkono na papa.

Lakini ukweli halisi ulifunikwa na umahiri wake wa propaganda. Migawanyiko ya matabaka iliendelea chini chini, kimya kimya. Misingi ya uchumi ilikuwa imebomolewa. Hakukuwa na amani, bali hofu. Lakini hakuna mtu aliyekuwa na ujasiri wa kumkosoa au kumkemea.

Magufuli naye amefuata njia hiyo hiyo. Mwanzoni, hasa katika miezi ya kwanza ya utawala wake, alifaulu kwa kiasi fulani kuhadaa umma umwone kama kiongozi mwenye kupigania mabadiliko. Alipoona watu wanaanza kumsifu, akaanza kujenga mazingira ya kujipa mamlaka makubwa zaidi. Akafuta matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya bunge. Akapiga marufuku  mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Akapiga marufuku maandamano. Akatoa vitisho kwamba yeye hajaribiwi, na watakaothubutu kumpinga atawavunja miguu.

Akatisha mahakama, vyombo vya habari, wanahabari mmoja mmoja waliomkera, wanaharakati. Baadhi ya waliompinga wakaanza kupotezwa kwa kutekwa. Wengine wakauawa na kutupwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi. Wengine wamepigwa risasi. Katika chaguzi ndogo zilizojitokeza, kumefanywa ukatili wa viwango ambavyo Tanzania haijaushuhudia, ilimradi walazimishe ushindi wa chama cha rais. Amesema mara kadhaa, na ameonyesha kwa vitendo, kwamba anataka kuongoza nchi bila upinzani. Na zimekuwepo jitihada za serikali, kupitia kwa msajili wa vyama, kutafauta mwanya wa kufuta baadhi ya vyama “vinavyomsumbua” rais.

Nchi imegeuka taifa la kipolisi, la mateso na mauaji ya wanaompinga au wanaomkosoa rais. Kama vile Mussolini alivyokuwa na kikosi cha kunyamazisha, kutesa na kuua wapinzani wake, kilichojulikana kama OVRA, Magufuli naye amekuwa anasaidiwa na kikosi cha “watu wasiojulikana” ambao wamekuwa wanatisha, wanateka, wanatesa, na kuua watu wanaomkosoa au wanaompinga Magufuli.

Mussolini alikuwa shabiki mkubwa wa Adolf Hitler, dikteta wa Ujerumani anayesifika kwa ubaguzi wa kikabila, ukatili na chuki  dhidi ya Wayahudi. Mwaka 1938, Mussolini alipitisha sheria ya ubaguzi dhidi ya Wayahudi, akafukuza asilimia 20 ya Wayahudi hao waende Ujerumani kuuawa kwenye kambi za kivita.

Magufuli hajafikia kiwango hicho, kwa kuwa bado hajakaa hata miaka mitatu mdarakani, lakini tayari ameonyesha dalili mbaya. Kwanza, amesema waziwazi kwamba yeye ni shabiki na mwanafunzi wa Paul Kagame,  rais wa Rwanda ambaye ana kashfa ya kufilisi, kufunga, kupoteza na kuua wapinzani na wakosoaji wake. Katika miezi ya karibuni amemnyanyasa binti aliyeonyesha kutamani urais wa Rwanda. Kwanza alimwekea mizengwe asigombee, halafu akamkamata na kumfungulia mashitaka, kabla hajamfilisi yeye na familia yake, na kumweka kizuizini, yeye na mama yake mzazi.

Yanayotokea Rwanda, ndiyo Magufuli anatenda Tanzania, akijaribu kufilisi viongozi wa upinzani, kuwatisha, kuwafungulia kesi na kuamuru wafungwe au wauawe.  Kesi ya viongozi wakuu wa Chadema inayoendelea sasa, kesi na hatimaye kifungo cha mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Sugu), uharibifu wa mali za Mbowe na waziri mkuu mstaafu Frederick Sumaye, ununuzi wa baadhi ya madiwani na wabunge wa upinzani, na mengine ni baadhi ya vielelezo vya kozi aliyofuzu katika somo la udikteta. Wapo viongozi wengi wametendewa ukatili mkubwa na Magufuli kimya kimya.

Magufuli na Adolf Hitler

Hitler aliingia madarakani wakati wananchi wananung’unikia chumi kuharibika, ukosefu wa ajira kwa vijana, na ufisadi uliokithiri. Walitaka mabadiliko na walikuwa na hasira dhidi ya serikali yao. Walifika mahali wakasema wamechoshwa na ufisadi wa watawala katika mfumo wa kidemokrasia, wakatamani apatikane “kiongozi mwenye mkono wa chuma,” kutoka vyama vyenye siasa kali za kikomunisti au za kinazi.

Magufuli naye aliingia madarakani wakati wananchi wanataka mabadiliko. Alijua manung’uniko ya wananchi kuhusu ufisadi, uchumi mbovu, ukosefu wa ajira na kadhalika. Watu walitaka “rais mkali” anayeweza kusafisha mfumo. Mwanzoni, alijitahidi kuzungumza lugha ya wananchi, na kuonyesha dalili za kuwa rais wa aina hiyo. Lakini wanaomjua walisema mapema kuwa sura halisi ya Magufuli haifanani na usafi, uadilifu wala mabadiliko ya kimfumo. Sasa haamini mfumo, na haamini mtu, bali anafanya kila kitu “kwa mikono yake.”

Hitler alifanya jitihada za makusudi kubadili sheria ili apate madaraka kamili yasiyopingwa. Hitler alikuwa mhutubiaji mahiri, mwenye ushawishi wa kufanya watu wamuunge mkono kirahisi. Vyama vya siasa vyenye siasa za kiasi, kwa pamoja, vilikuwa na nguvu kuliko ya chama chake cha Nazi, lakini vilishindwa kushirikiana. Akatumia mwanya huo. Akaanzisha vikosi (Gestapo) vya kushambulia wakosoaji na wapinzani wake. Alitumia propaganda na kauli mbiu mbalimbali ili aungwe mkono. Aliahidi Wajerumani kwamba angeweza kubadili nchi yao na kuwaondolea umaskini kwa “mkono wa chuma.”

Mwanzoni mwa utawala wake, alifanikiwa kuteka wananchi kwa hila, akitumia watu kama Joseph Goebbels, aliyekuwa waziri wa propaganda, Jenerali Franz Halder, na Galeazzo Ciano, waziri mwingine aliyetumika kumpamba Hitler, na kukandamiza yeyote aliyethubutu kumkosoa.

Kwa kifupi, Hitler alianza taratibu. Udikteta wake haukuonekana wazi kwa kila mtu. Alilewa sifa, akatumia “huruma ya wananchi” kuchezea na kubadili sheria. Mkono wake wa chuma ulipoteza mamilioni ya wananchi, hasa waliompinga, au wale ambao yeye alidhani “si binadamu kamili” kama yeye na Wajerumani wengine.

Magufuli amekuwa anatumia watu kadhaa kumsemea kuhusu umuhimu wa kubadili baadhi ya sheria, hata katiba, ili apate nguvu zaidi ya “kusimamia maendeleo.” Mara kadhaa kuna wabunge wamesema kuwa wanatamani kupeleka muswada bungeni ili kubadili muhula wa uongozi kutika miaka mitano hadi saba. Yeye alijitokeza mara moja kukanusha, lakini kanuhso lake linafanana na yale ya Yoweri Museveni wa Uganda na Kagame wa Rwanda – ambao walianzisha kampeni ya kujiongezea madaraka kwa staili hiyo, wakakanusha, baadaye wakaipitisha. Mbunge mwingine wa CCM alitamka bungeni kwamba anatamani Magufuli awe “rais wa maisha.” Huyu alisahau, au hakujua, adha iliyowapa viongozi wote ambao wamewahi kujitangazia urais wa maisha. Lakini wachambuzi wa siasa wanatambua kuwa kauli za namna hiyo hutolewa kimkakati kupima upepo.

Magufuli amenyamazisha vyombo vya habari, na sasa anatumia vyombo vingine vya habari, hasa TBC – shirika la utangazi la taifa – kujifanyia propaganda, kurusha matangazo yake popote anapokuwa, anapoteua maofisa, anapowaapisha, na hata majuzi alipokuwa ananunua mapapai sokoni. Nje ya mfumo rasmi wa serikali, ameunda kikosi cha “wahuni” ambao wamesajili vijigazeti kwa ufadhili wa serikali ili wavitumie kushambulia wapinzani na kumpamba Magufuli. Vijigazeti hivyo ambavyo hata usomwaji wake ni wa kusuasua, vinapewa hata matangazo ya serikali kama sehemu ya fadhila ambayo wengine wanaitafsiri kama rushwa kwa ajili ya propaganda za Magufuli.

 

Shabaha ya propaganda hizo, huku yeye akinyamazisha wanasiasa wengine, ni mbinu yake kufanya wananchi wamsikie na kumuona yeye tu kama mtu pekee anayejua shida zao na mwenye jawabu la kila chagamoto inayowakumbwa. Hata hivyo, utendaji wa serikali yake haufanani na sifa anazojipa, na anazopewa na vyombo vinavyompigania.

Katika hali hiyo, watendaji wengi wa Ikulu na serikali wamegeuzwa mashabiki, watetezi, na mawakala wa Magufuli. Kwa mkono wa chuma ule ule, na kama ambavyo Hitler alitengeneza kikosi cha Gestapo kushughulikia wapinzani, Magufuli ana kikosi chake cha “watu wasiojulikana” ambacho tayari kimeumiza wengi.

Magufuli na Idi Amin

Idi Amini wa Uganda naye alianza kwa kushangiliwa. Alitoa hirruba zenye kutia matumaini. Alizungumzia mabadiliko, hasa kwa aliokuwa wamechoshwa na utawala wa Dk. Milton Obote. Aligusa baadhi ya maeneo yaliyokuwa kero kwa wananchi. Kwa kujua hisia za Waganda, alirejesha Uganda mwili wa Kabaka Mutesa II, uzikwe kwa heshima zote “ulizostahili.” Aliachia huru wafungwa wa kisiasa waliokuwa wamewekwa ndani na Obote. Vile vile, alifumua mfumo wa kikachero uliokuwa unatumika kutesa watu wakati wa Obote. Akatumia vema haiba yake, tabasamu lake hila, na maneno yenye kutia matumaini, akaungwa mkono katika kujenga kile alichoita “Uganda mpya.”

Alitamka wazi: “Shabaha yangu ni kuondoa nchi hii kwenye ufisadi, umaskini, na utumwa. Nikishaondoa madhila haya, nitaandaa mazingira ya uchaguzi wa kidemokrasia, ili Uganda iongozwe kwa utawala wa kiraia.”

Alianzisha “vita ya kiuchumi,” akashushua na hata kufukuza wawekezaji wa kigeni, hasa raia wenye asili ya Kiasia. Akagawa mali zao kwa raia wa Uganda. Alijiimarishia mamlaka  kama kiongozi asiyepingwa, na asiyejaribiwa – akawa dikteta wa kijeshi.

Amin alishabikia matumizi ya polisi na jeshi kudhibiti waliompinga na waliomkosoa.

Kila alipoua wakosoaji wake, alitangaza vifo hivyo hadharani kama njia ya kutisha wengine. Inakisiwa kuwa wananchi zaidi ya 5000 waliuawa katika utawala wa miaka minane ya Idi Amin. Miongoni mwao, wamo wanajeshi, viongozi wa dini waliodiriki kumshauri, waandishi wa habari walioandika habari asizopenda, wanasheria, wanadiplomasia, majaji, na wasomi. Lakini vifo hivyo havikuleta amani, wala havikumwezesha atawale nchi kwa kujiamini.

Akiwa na mwonekano wa nje wenye kulainisha uso, tabasamu lililoficha hila na ukatili, na maneno matamu matamu, alifanikiwa kujifanya aonekane “mtu wa watu,” akajisogeza karibu na viongozi wa dini – hasa maaskofu – na kupiga nao picha, huku akisema: “mimi si mwanasiasa, bali askari mwenye hadhi ya profesa.” Tunajua alikoishia.

Magufuli alianza vema kwa kuchukua hatua kadhaa nzuri. Wasio wepesi wa kutafakari wakachokwa kiakili. Amejaribu kujiweka karibu na viongozi wa dini, baadaye walipomshtukia akaamua kuwashughulikia kwa kutumia polisi, mamlaka ya mapato, uhamiaji, na hata mamlaka nyingine zenye kutengeneza mikakati ya kuwagwa au kuwadhalilisha. “Vita ya uchumi” aliyoanzisha, ni kama ile ile ya Idi Amini ambayo haikufaulu kunyanyua uchumi wa biashara za wazalendo, bali kuingia mikataba mipya ya kuficha ufisadi wa mfumo mpya.

Magufuli na Mobutu Seseseko

Mobutu wa Zaire, miongoni mwa miradi yake mingi, alijenga uwanja wa ndege mkubwa kijijini kwake Gbadolite kwa pesa za walalahoi. Leo uwanja huo umechakaa na kugeuka gofu la popo, panya na wadudu.Aliweka makao makuu ya wizara ya maji. Jengo hilo chakavu sasa limegeuka madarasa ya shule ya sekondari. Hoteli kubwa ya kifahari – The Motel Nzekele – imebomoka na kugeuka gofu. Daraja la Gbadolite limebaki nguzo tu. Jumba lake la kifahari lililohudumiwa na watumishi zaidi ya 700 –  askari 300, wapishi, madereva, na wasaidizi katika majukumu mbalimbali – sasa ni gofu lenye magugu ndani likiwa limezingirwa na vichakaa. Ikulu ya Gbadolite imebaki gofu la kifisadi, mabaki ya aibu ya utawala wa kidikteta.

Magufuli tayari ameingia katika kashfa ya ujenzi wa uwanja ndege nyumbani kwao Chato kwa   zaidi ya SH 50 bilioni ambazo hazijaidhinishwa na bunge, na mkandarasi wa uwanja huo ni rafiki yake binafsi ambaye alisoma naye, na ndiye alikuwa mshika fedha katika kampeni zake 2015. Kua miradi mingi inaelekezwa Chato katika kile anachoeleza kwa jeuri ya madaraka kwamba “mikoa mingine isubiri.” Na haya yanatokea wakati ndani ya mwaka mmoja 2016/17 zimepotea Sh 1.5 trilioni, ufisadi ambao haujawahi kufanyika kwa miaka 50 ya uhuru wa Tanzania.

Mwisho mbaya wa madiketa

Uchambuzi huu umegusia kidogo tu tabia ambazo madiketa hawa wamefanana katika maisha hasa katika mfumo wao wa utawala. Kijumla wote walitumia vibaya madaraka kunyamazisha wapinzani, kujiongezea mamlaka, kuteka, kutesa, na kuua wapinzani, kubana vyombo vya habari na kuvitumia kujinadi, kujitangazia usafi, uadilifu na uzalendo, huku wakikwapua raslimali za taifa. Wote, ingawa mwanzoni walishangiliwa, walikuwa na mwisho mbaya.

Mussolini alitimuliwa madarakani na wale wale waliokuwa wamemshangilia. Alipothubutu kupuuza nguvu ya umma, walimkamata, wakamweka jela, katika kisiwa cha Ponza. Baadaye alihamishiwa katika kisiwa kingine, pwani ya Sardinia, na hatimaye akatoroshewa Ujerumani. Alipouawa kwa risasi Aprili 28, 1945, maelfu ya wananchi walishangilia kwa kuondokewa na dikteta waliyemlea wenyewe, mkono wa chuma na maneno matamu, uliodhaniwa kuwa kiongozi mwema. Hatimaye demokrasia ilirejea Italia. Hitler naye aliishia pabaya. Hakupata hata bahati ya kuzikwa na ndugu zake.

Licha ya utajiri aliojikusanyia kwa wizi akiwa madarakani akishrikiana na rafiki zake, Mobutu alifia uhamishoni Morocco, akiwa maskini, akazikwa na watu wachache mno katika kijiji kidogo. Amin naye, baada kutimuliwa na majeshi ya Tanzania, alikimbia nchi hatimaye akafia na kuzikwa Uarabuni akiwa maskini hohehahe.

Kijumla, kwa juu juu, wote walifaulu kutumia mabavu kuanzisha na kukamilisha baadhi ya miradi ya kimaendeleo. Lakini kwa kuwa ilitekelezwa kwa gharama ya damu ya raia wema, miradi hiyo nayo haikudumu. Walikuwa wababe, wakatili, wapenda mamlaka, wasiojaribiwa, matajiri, wenye majeshi na ulinzi mkali; lakini kila majaribio halisi yalipojitokeza, hakuna dikteta aliyebaki salama.

Wachambuzi wanasema kwa vigezo hivi, ingawa ni katika kipindi kifupi tu, Magufuli amefaulu kuwa dikteta   kamili, na kwa sababu hiyo, amejiondoa katika orodha ya viongozi safi na waadilifu. Na bado hawajui kwanini ameamua kufuata njia hiyo ya maangamizi.

Like
17
6 Comments
 1. makaveli 6 years ago
  Reply

  Tanzania has never had a free, fair and credible presidential elections.Since the first multiparty elections were conducted in 1995 ccm has riged every election in there favor through unorthodox means.A riged democratic system has replaced one dictator with another only this time many people have been caught by surprise by how president magufuli has taken it to a whole new level,in only his second year in office politcal assassinations have been on the increase,opposition members of parliament have faced jail terms, journalists and human right activists have dissappeard,everyone can now see who he really is even those who were skeptical or given him the benefit of a doubt have now seen him for who he really is .Like any other dictator,magufuli is bound to fail .it is very important for us as citizens of this great nation to come together and prevent this juvenile dictator from failing us all.

  5

  0
  • Kipye 6 years ago
   Reply

   We said and is true. Let us keep praying for God has never forgotten his people. God loves Tanzania.

   2

   0
 2. charles 6 years ago
  Reply

  good analysis

  3

  0
 3. Mtanzania 6 years ago
  Reply

  Magufuli uses the methods other dictators did. Unfortunately many Tz close their eyes for fear or negligance.

  5

  0
 4. Mbongo 6 years ago
  Reply

  Huyu dikteta ni mtu hatari sana kwa mshikamano wa Taifa letu. Yeye na genge la wahuni wenzie wanaiharibu sana Tanzania na kuwashangaza Watanzania wengi, Waafrika na hata Walimwengu wengi duniani ambao kwa miaka mingi walikuwa wanafahamu sifa nzuri ya Taifa la Tanzania ambayo sasa inachafuliwa na hili genge la wahuni.

  4

  0
 5. Sikulumbusya 6 years ago
  Reply

  Ni Hatari Tupu huyu dikteta Maana Ndg zetu wamepotezwa kwa Sababu tuu Hataki kupingwa.

  3

  0

Leave a Comment

Your email address will not be published.