Miaka 58 ya Sauti, Migongano na Makali ya Kanisa Mbele ya Mamlaka
Tarehe 10 Agosti 2026, Rais Samia Suluhu Hassan alikaa mezani Ikulu ya Chamwino, Dodoma, na viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Picha zikatoka. Taarifa ya Ikulu ikasema mazungumzo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na TEC, kujadili masuala ya kisiasa, imani na maendeleo, na kuimarisha amani, mshikamano na mustakabali wa Taifa. Rais akawashukuru maaskofu na kuahidi kuendeleza utamaduni wa kushauriana na viongozi wa dini.
Lakini taarifa hiyo haikueleza kwa undani kwa nini maaskofu walikwenda Ikulu, wala nini hasa walimwambia Rais. Sauti Kubwa inafahamu kuwa rais na maaskofu walikubaliana kutojadili undani wa majadiliano yao hadharani.
Watu wazima wakiaminiana kuzungumza na kushauriana juu ya mambo muhimu kwa usiri wa kimaadili na kiutawala, husimamia makubaliano yao. Ndivyo walivyofanya.
Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea na umma ukiendelea kujadili usichojua mitandaoni na vijiweni, wakaibuka baadhi ya makada wa CCM na wanaharakati wakaanza kusimanga maaskofu wa TEC kwamba hatimaye wameufyata mbele ya serikali.
Maswali yakaibuka. Hawa wanajituma au wanatumwa? Kwanini wakubwa wao hawawakemei au kuwazuia kupotosha jambo lililojadilowa kwa faragha ya utu uzima na utawala? Shabaha ya masimango haya inaponya au inaumiza taifa? Kipi kizingatiwe: propaganda au dhamiri ya mazungumzo?
Siku chache baadaye, tarehe 13 Agosti 2026, Katibu Mkuu wa TEC, Padre Dk. Charles Kitima, akatoa upande mwingine wa picha. Akaeleza vyombo vya habari kwamba maaskofu hawakuitwa Ikulu; kwamba wao ndio walioomba kukutana na Rais.
Akasema walikwenda na andiko rasmi la kurasa nne, wakisisitiza umuhimu wa ukweli na msamaha katika kutafuta utulivu wa kweli wa Taifa. Hapo ndipo picha ya Chamwino inapata maana kubwa zaidi.
Haikuwa picha ya Rais na viongozi wa dini pekee. Ilikuwa sura mpya ya mjadala ambao Kanisa Katoliki na Serikali ya Tanzania, katika awamu hii, wamekuwa nao kwa karibu miaka sita sasa – wakati mwingine kwa maelewano, wakati mwingine kwa tahadhari, na nyakati nyingine kwa mgongano wa wazi.
Lakini uhusiano wa aina hii kati ya TEC na Serikali haukuanza juzi.
Tukirudi mwaka 1968, tunagundua jambo muhimu: TEC haikuanza kama adui wa Serikali. Wala historia yake haiwezi kuelezwa kwa kusema Kanisa daima limeipinga Serikali.
Badala yake, historia inaonyesha TEC kama taasisi ambayo mara nyingi imeunga mkono malengo ya Serikali inapoyaona yanaendana na haki na utu wa binadamu, lakini pia imekuwa tayari kukosoa mamlaka inapohisi misingi hiyo imevunjwa.
Kwangu, hiyo ndiyo historia inayotusaidia kuielewa Chamwino ya Agosti 2026. Mkutano wa juzi kati ya rais na maaskofu, ni sehemu ya simulizi ndefu inayorudi nyuma karibu miaka sita.
Katika simulizi hilo, TEC imewahi kuipongeza Serikali. Imeunga mkono sera zake. Imeshirikiana nayo katika elimu, afya na maendeleo. Lakini pia imewahi kuionya, kuikosoa, kuhoji mwenendo wake na, katika nyakati fulani, kutumia lugha ambayo kwa taasisi yenye hadhi na tahadhari kama Kanisa Katoliki inaweza kuitwa kali.
Kwa hiyo, swali la msingi si kama TEC imewahi kuikosoa serikali. Imefanya hivyo mara nyingi.
Swali la kuvutia zaidi ni hili: Makali hayo yamekuaje kutoka awamu moja ya serikali hadi nyingine – na kwa nini? Ili kulijibu, haitoshi kuanzia kwa Samia, Magufuli au hata Kikwete. Tunapaswa kurudi mwaka 1968.

Nyerere: TEC inaanza kwa kuunga mkono – lakini si kwa kujisalimisha
Mwaka 1967, Serikali ya Julius Nyerere ilitangaza Azimio la Arusha. Tanzania ilikuwa inatafuta mfumo wake wa maendeleo. Ujamaa na kujitegemea vikawa dira ya Taifa.
Mwaka mmoja baadaye, mwaka 1968, maaskofu Katoliki wakatoa waraka muhimu, The Church and Developing Society of Tanzania.
Huu ni waraka muhimu sana kwa kuelewa TEC. Kwa sababu haukuanza kwa kuipiga Serikali. Uliunga mkono kwa kiasi kikubwa maadili yaliyokuwa nyuma ya Azimio la Arusha – usawa, utu wa binadamu, kupunguza pengo kati ya matajiri na maskini, kupinga unyonyaji na kujenga jamii inayowajibika kwa walio dhaifu.
Kwa lugha nyingine, TEC iliona maeneo ambayo Ujamaa wa Nyerere ulikutana na mafundisho ya kijamii ya Kanisa. Hapo ndipo msingi wa uhusiano huu ulipo.
TEC haikujijenga kama upinzani dhidi ya serikali.
Ilijijenga kama sauti ya kimaadili ambayo ingeweza kusema “ndiyo” pale serikali ilipoonekana kwenda katika mwelekeo sahihi, au “hapana” pale mbinu au matokeo yalipoonekana kukiuka misingi iliyokuwa imeungwa mkono.
Na haikuchukua muda kabla sehemu ya pili haijaanza kuonekana. Kadiri sera za Ujamaa zilivyotekelezwa, hususan vijijini, umiliki wa mali, shughuli za taasisi binafsi na nafasi ya dola katika maisha ya wananchi, baadhi ya viongozi wa kanisa wakaanza kuonyesha wasiwasi.
Hapa ndipo tofauti kati ya lengo na njia ilipojitokeza. Kanisa lingeweza kuunga mkono usawa lakini likauliza: usawa unaletwa kwa njia gani? Lingeweza kuunga mkono maendeleo ya vijijini lakini likauliza: wananchi wanashirikishwa kwa kiwango gani? Lingeweza kukubali wajibu wa Serikali katika kujenga Taifa lakini likauliza: mamlaka ya serikali yanaishia wapi?
Mvutano huo ulikuwa mkubwa kiasi kwamba Agosti 3, 1970, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alizungumza na Katibu Mkuu wa TEC wa wakati huo, Padre Robert Rweyemamu, kuhusu shaka iliyokuwa ikitolewa na baadhi ya viongozi wa kanisa kuhusu Ujamaa.
Hii ni hatua muhimu sana katika historia yetu. Kwa sababu miaka miwili tu baada ya TEC kuunga mkono misingi ya Azimio la Arusha, tayari kulikuwa na tofauti kuhusu utekelezaji wake.
Hapo ndipo tunapata DNA ya uhusiano ambao utaendelea kwa miongo kadhaa, yaani ushirikiano bila kujisalimisha.
1970 na kuendelea: Kanisa linaanza kuuliza gharama ya sera
Katika miaka iliyofuata, masuala ya utaifishaji, elimu, huduma za jamii, vijiji vya Ujamaa na nafasi ya taasisi za dini yaliendelea kuleta mijadala. Kanisa Katoliki lilikuwa limewekeza sana katika shule na hospitali. Serikali nayo ilikuwa inapanua wajibu wake katika maeneo hayo.
Hivyo mjadala haukuwa wa kinadharia. Uligusa mali, taasisi, walimu, wagonjwa, wanafunzi na nafasi halisi ya kanisa katika jamii.
Makali ya TEC ya wakati huu hayakuwa sawa na yale tutakayoyaona mwaka 2018 au 2025. Lugha ilikuwa zaidi ya ushauri, tahadhari na mafundisho ya kijamii kuliko “mapambano” ya moja kwa moja.
Lakini mbegu ilikuwa tayari imepandwa – kwamba serikali haiwezi kuwa ndiyo mamlaka pekee ya kuamua kilicho chema kwa jamii.
Mwinyi: TEC inaanza kuzungumza zaidi kuhusu Serikali yenyewe
Rais Ali Hassan Mwinyi alipoingia Ikulu mwaka 1985, Tanzania ilikuwa tofauti.
Ujamaa ulikuwa unapoteza nguvu yake ya kiuchumi. Uchumi ukaanza kufunguliwa. Masharti ya taasisi za fedha za kimataifa yakaingia. Baadaye mfumo wa chama kimoja ukaondoka na vyama vingi vikarejea mwaka 1992.
Lakini pamoja na uhuru zaidi wa kiuchumi na kisiasa, matatizo mengine yakawa yanaonekana. Rushwa. Pengo la matajiri na maskini. Maadili ya viongozi. Migogoro ya kidini. Zanzibar. Na swali la namna Tanzania mpya ya vyama vingi ingeongozwa.
Hapa TEC ikaanza kupanua lugha yake.

1992: True Human Development
Mwaka 1992 maaskofu walitoa waraka True Human Development.
Hapa TEC ilikuwa inarudisha hoja ya maendeleo kwenye msingi mmoja muhimu: maendeleo si takwimu za uchumi peke yake.
Maendeleo lazima yamhusu binadamu. Utu wake. Uhuru wake. Haki yake. Mahitaji yake ya msingi. Na uwezo wake wa kushiriki katika uamuzi unaohusu maisha yake.
Ni muhimu kwamba waraka huu ulitokea wakati Tanzania ilikuwa inabadilika kutoka mfumo wa chama kimoja kwenda vyama vingi.
Kwa hiyo TEC ilikuwa, kwa namna yake, ikiweka kipimo cha kimaadili juu ya Tanzania iliyokuwa inazaliwa upya kisiasa.
1993 – 1994: Dini, Zanzibar na Serikali
Kisha mjadala ukawa mkali zaidi. Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Tanzania ilikumbwa na mvutano wa kidini.
Kulikuwa na malalamiko ya viongozi wa Kikristo kuhusu mahubiri na vitendo vilivyoonekana kudhalilisha Ukristo. Kulikuwa pia na mjadala mkubwa kuhusu Zanzibar na Organization of Islamic Conference (OIC).
TEC na taasisi nyingine za Kikristo zikaonyesha wasiwasi. Serikali ya Mwinyi ikajikuta katikati ya mjadala wenye hatari kubwa: dini, Muungano na siasa.
Rais Mwinyi akakutana na viongozi wa Kikristo.
Hapa tunaona mwelekeo ambao utarudi tena miaka mingi baadaye: Kanisa linatoa malalamiko hadharani, hali ya kisiasa inakuwa tete, Ikulu inaingia, viongozi wanakutana.
Lakini kipindi cha Mwinyi kinaonyesha pia ongezeko la makali ya TEC. Sasa haizungumzi tu kuhusu falsafa ya maendeleo. Inazungumzia mwenendo wa Serikali, ulinzi wa haki, rushwa, dini na uadilifu wa mamlaka.
Mkapa: Kutoka maadili hadi uwajibikaji wa dola
Rais Benjamin Mkapa alipoingia madarakani mwaka 1995, rushwa ilikuwa mojawapo ya matatizo makubwa yaliyokuwa yakizungumzwa nchini.
Mkapa mwenyewe alikiri tatizo hilo na kuunda Tume ya Jaji Joseph Warioba kuchunguza mianya ya rushwa. Kwa TEC, hili lilikuwa suala la kimaadili.
Katika kipindi hiki, ujumbe wa Kanisa uliendelea kusisitiza uongozi wa maadili, matumizi ya haki ya rasilimali, kupunguza umaskini, wajibu wa viongozi na haki za wananchi.
Lakini jambo jingine lilikuwa linatokea. Mageuzi ya kiuchumi yalikuwa yanaanza kubadilisha Tanzania.
Mashirika ya umma yalibinafsishwa. Sekta ya madini ilipanuka. Wawekezaji wa nje wakaongezeka. Lakini wananchi wengi waliendelea kuwa maskini.
Hapo Kanisa likauliza swali ambalo litaendelea kulirudia katika awamu zinazofuata: Maendeleo haya ni kwa ajili ya nani?
Hili ndilo daraja kati ya TEC ya Nyerere na TEC tutakayoiona baadaye katika mjadala wa rasilimali, bandari na DP World. Hoja yake ya msingi haikubadilika sana. Kilichobadilika ni mazingira.
Uchaguzi na dhamiri ya mpiga kura
Katika kipindi cha mfumo wa vyama vingi, TEC pia ilianza kutoa mwongozo wa mara kwa mara kuelekea uchaguzi.
Maaskofu walihimiza waamini na wananchi kupiga kura kwa dhamiri, kuchunguza tabia na uwezo wa wagombea na kutokubali rushwa ya uchaguzi.
Hili linaweza kuonekana jambo la kawaida leo. Lakini lina maana kubwa. Kwa kufanya hivyo, Kanisa lilikuwa limekubali kwamba ubora wa uongozi wa kisiasa ni suala la kimaadili.
Hapo ndipo mlango ulifunguliwa zaidi. Kwa sababu ukishasema wananchi wachague viongozi waadilifu, lazima uwe tayari pia kusema nini kinatokea viongozi wanapokosa uadilifu.
Kikwete: TEC inakaribia zaidi kiini cha mamlaka
Rais Jakaya Kikwete aliingia madarakani mwaka 2005 akiwa na umaarufu mkubwa. Lakini kadiri miaka ilivyopita, mijadala kuhusu rushwa, ufisadi, rasilimali, uwajibikaji na Katiba ikawa mikubwa. TEC nayo ikawa sehemu ya mijadala hiyo.
EPA, Richmond na maadili ya uongozi
Kipindi cha Kikwete kilikumbwa na kashfa kubwa zilizotikisa serikali. Richmond ilisababisha Waziri Mkuu Edward Lowassa kujiuzulu mwaka 2008. EPA ikawa mjadala mkubwa wa fedha za umma.
Kanisa na viongozi mbalimbali wa dini wakazidi kusisitiza uwajibikaji, kupinga rushwa na kulinda mali ya umma.
Hapa makali ya TEC yalikuwa yanaingia hatua nyingine. Haikutosha tena kusema: “Viongozi wawe waadilifu.”
Sasa mazingira yalikuwa yanailazimisha jamii kuuliza: “Kiongozi asipokuwa mwadilifu, nani anamwajibisha?”
2010: TEC na uchaguzi
Katika maandalizi ya uchaguzi wa 2010, TEC ilitoa mwongozo uliosisitiza wajibu wa wananchi kuchagua viongozi wenye uwezo, uadilifu na kujali maslahi ya Taifa. Waraka huo ulizua mjadala mkubwa wa kisiasa.
Baadhi ya watu waliona Kanisa linaelimisha wapiga kura. Wengine wakahisi lugha yake ingeweza kutafsiriwa kama “kuelekeza uchaguzi.”
Hapa ndipo tatizo ambalo TEC itaendelea kukabiliana nalo linapoonekana wazi, kwamba unawezaje kutoa mwongozo wa kimaadili kuhusu uchaguzi bila kuonekana unachagua upande wa kisiasa?
2014–2015: Katiba Mpya
Lakini moja ya hatua muhimu zaidi za TEC katika awamu ya Kikwete ilikuwa Katiba. Mchakato wa Katiba Mpya ulianza kwa matumaini makubwa.
Tume ya Jaji Joseph Warioba ikakusanya maoni ya wananchi. Rasimu ikatolewa. Bunge Maalumu la Katiba likaingia. Mgogoro ukazuka.
Mwaka 2015, maaskofu Katoliki wakatoa waraka uliosainiwa na maaskofu 34. Walikuwa na mashaka makubwa kuhusu mchakato ulivyokwenda. Walizungumza kuhusu uadilifu wa mchakato, ushirikishwaji na namna maoni ya wananchi yalivyoshughulikiwa.
Hili lilikuwa jambo kubwa. TEC haikuwa tena inazungumza pembeni ya mfumo. Ilikuwa inazungumza kuhusu sheria mama inayounda mfumo wenyewe.
Makali yalikuwa yameongezeka – kutoka “Ujamaa utekelezwe kwa haki” kwenda “viongozi wawe waadilifu;” hadi “wananchi wachague kwa dhamiri.”
Na sasa imekuwa “mchakato unaounda Katiba yenyewe lazima uwe wa haki na uaminifu.”
Magufuli: TEC inataja dalili za kuvunjika kwa demokrasia
Rais John Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015, alianza kwa nguvu kubwa ya kisiasa.
Kwa wengi wasiojua mambo ya ndani ya serikali, alionekana anapambana na ubadhirifu. Alifukuza watumishi. Alitembelea taasisi kwa kushtukiza.
Akasisitiza nidhamu na ukusanyaji wa mapato. Wananchi wengi wakampokea kama “rais wa vitendo.”
Lakini kadiri muda ulivyopita, sura nyingine ya Magufuli ilianza kujitokeza. Mikutano ya kisiasa – hasa ya wapinzani – ikabanwa. Vyombo vya habari vikakabiliwa na shinikizo – vikatishwa na kufungiwa.
Wanasiasa na wanaharakati wakosoaji wakakamatwa. Baadhi ya watu wakashambuliwa, wakatekwa, wapotea au wakauawa. Hapa TEC ikabadilisha sauti.
Waraka wa Kwaresima wa 2018
Hili ni mojawapo ya matamko muhimu zaidi katika historia ya TEC baada ya mfumo wa vyama vingi. Maaskofu wote 36 waliweka majina yao katika waraka uliogusa hali ya kisiasa nchini.
Walizungumzia hofu. Walizungumzia uhuru wa kujieleza. Walizungumzia uhuru wa vyombo vya habari. Walizungumzia mazingira ya vyama vya siasa.
Walizungumzia watu waliokuwa wakipotea au kushambuliwa. Walizungumzia haki na wajibu wa Serikali kulinda wananchi. Hapa lugha ya TEC ilikuwa imeendambali sana na 1968.
Mwaka 1968, kanisa lilikuwa likizungumza kuhusu namna ya kujenga jamii ya Ujamaa yenye haki. Mwaka 2018 lilikuwa linauliza kama mfumo wa kisiasa wenyewe ulikuwa unaheshimu haki za msingi za wananchi.
Haya ndiyo “makali ya TEC” tunayotafuta katika historia hii. Hayakutokea ghafla. Yalikua hatua kwa hatua.
Serikali yajibu
Waraka huo haukupokelewa bila msuguano. Kulikuwa na mjadala mkali kuhusu kama viongozi wa dini walikuwa wamevuka mpaka na kuingia katika siasa.
Barua iliyodaiwa kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani kuhusu TEC na KKKT ilisambaa na kuzua taharuki, ingawa serikali baadaye iliikana.
Lakini jambo kubwa zaidi lilikuwa tayari limetokea: TEC ilikuwa imeweka hadharani wasiwasi ambao ulikuwa unasikika sehemu nyingine za jamii. Na Serikali ilikuwa imelazimika kujibu.
Ni katikati ya mvutano huu, Katibu Mkuu wa TEC, Pd. Raymond Saba, alivuliwa uraia, akanyang’anywa pasipoti. Ndipo TEC Ikamteua Dk. Charles Kitima. Baadaye Padri Saba akafariki dunia katika mazingira yenye utata.
2020: Uchaguzi Mkuu unaongeza makali
Kadiri uchaguzi mkuu wa 2020 ulivyokaribia, maswali kuhusu mazingira ya kisiasa yaliongezeka. Viongozi wa dini wakasisitiza amani, haki, uchaguzi wa kuaminika na wajibu wa taasisi za uchaguzi.
Baada ya uchaguzi, kulikuwa na malalamiko makubwa kutoka upinzani na mashirika mbalimbali kuhusu mchakato. Wakasema uchaguzi haukufanyika. Wakauita “uchafuzi.”
Hapa pia Kanisa lilikuwa katika mazingira magumu. Lilitakiwa kuhubiri amani. Lakini amani yenyewe ilikuwa inahitaji haki.
Hili ndilo jambo ambalo baadaye litakuwa muhimu sana katika lugha ya TEC chini ya Samia, kwamba “amani si ukimya” na kwamba msingi wa amani ni haki.

Samia: Kutoka maridhiano hadi DP World, uchaguzi na Oktoba 29
Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani Machi 2021, alirithi nchi iliyokuwa na migawanyiko mikubwa ya kisiasa. Tanzania ilijawa na hofu kila mahali.
Hatua zake za mwanzo zilitoa matumaini. Mazungumzo yakaanza. Baadhi ya vizuizi vikalegezwa. Mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa baadaye ikaruhusiwa.
Neno maridhiano likawa sehemu ya lugha ya kisiasa ya Taifa. Wananchi wakampa rais jina jipya – “mama.”
Lakini TEC haikuacha jukumu lake la kukosoa.
2023: DP World
Mwaka 2023, mjadala kuhusu makubaliano ya Tanzania na Dubai kuhusu bandari ulilipuka. Kelele zikapigwa kila kona. TEC ikaingia moja kwa moja.
Maaskofu walitaka serikali kusikiliza zaidi wananchi na wakatoa tahadhari kuhusu makubaliano hayo ya DP World.
Hii ilikuwa hatua kubwa kwa sababu bandari si suala la ibada. Ni uchumi. Ni uwekezaji.Ni mamlaka ya Serikali. Ni mikataba ya kimataifa. Ni rasilimali ya Taifa.
Kwa wakosoaji wa TEC, hapa Kanisa lilikuwa limeingia katika eneo ambalo lilipaswa kuachiwa serikali na wataalamu.
Lakini kwa TEC, suala lilikuwa na “dimension” nyingine; kwamba mali ya taifa inasimamiwaje kwa maslahi ya wananchi?
Ukirudi nyuma hadi kipindi cha Mkapa na mijadala kuhusu rasilimali, utaona mwendelezo. TEC ilikuwa inapanua matumizi ya mafundisho yake ya kijamii hadi kwenye usimamizi wa mali ya umma.
2024 – 2025: Lugha inakuwa nzito zaidi
Kadiri mazingira ya uchaguzi mkuu wa 2025 yalivyoanza kujengwa, TEC ilizidi kuzungumzia haki, amani na mazingira ya kisiasa.
Hapa ndipo tunafikia hatua ambayo “makali” yake hayawezi tena kupimwa kwa waraka mmoja. Ni mlolongo. Matamko. Mahubiri. Tahadhari.Sala. Wito wa mazungumzo. Na kisha matukio halisi.
Aprili 30, 2025, Katibu Mkuu wa TEC, Padri Charles Kitima, akavamiwa na kushambuliwa katika makao makuu ya TEC Kurasini.
Tukio hilo lilikuwa na uzito mkubwa kwa sababu sasa mtu aliyekuwa mmoja wa sauti zinazotambulika zaidi za kanisa katika masuala ya taifa alikuwa ndiye mwathirika wa shambulio.
TEC ikataka uchunguzi. Na baadaye ikaonyesha kutoridhishwa na kasi ya uchunguzi huo.
Juni 2025: Sala na kufunga kwa ajili ya Taifa
TEC ikaitisha sala na kufunga kwa ajili ya haki na amani kuelekea uchaguzi.
Kwa nje hili linaweza kuonekana jambo la kidini kabisa. Lakini katika muktadha wa wakati huo, ujumbe wake ulikuwa mzito.
Kanisa lilikuwa linasema taifa lina tatizo ambalo haliwezi kutatuliwa kwa taratibu za uchaguzi pekee. Linahitaji haki. Linahitaji ukweli. Linahitaji dhamiri.
Oktoba 29, 2025: mstari unakatika
Kisha ukaja uchaguzi mkuu. Na vurugu. Na vifo. Hapa ndipo historia ya matamko ya TEC inapofikia kilele chake.
Baada ya matukio ya Oktoba 29 na yaliyofuata, TEC haikutoa tu wito wa kawaida wa amani. Maaskofu walitaka uchunguzi huru.
Walizungumza kuhusu mauaji. Walitaka waliofungwa katika mazingira ya uchaguzi waachiwe. Walitaka haki. Walirudisha hoja ya Katiba Mpya.
Hii ilikuwa tofauti muhimu katika harakati na mchakato mzima.
Katika historia ya TEC, tumetoka mwaka 1968 ambapo maaskofu walikuwa wanajadili namna Ujamaa unavyoweza kujenga jamii ya haki. Sasa, mwaka 2025, maaskofu walikuwa wanauliza Serikali kuhusu damu ya wananchi.
Huwezi kuelewa makali ya tamko hili bila kuona safari nzima. 1968: maendeleo yenye haki. 1992: maendeleo yanayomheshimu binadamu. Miaka ya 1990: rushwa, dini na haki. Miaka ya Mkapa: maadili, umaskini na uwajibikaji. 2010: dhamiri ya mpiga kura. 2015: uadilifu wa mchakato wa Katiba. 2018: demokrasia, hofu, uhuru na watu kupotea. 2023: rasilimali na DP World. 2025: uchaguzi, vurugu, vifo na uchunguzi huru.
Huo ndio mstari wa makali ya TEC.
2026: Kutoka tamko hadi mezani
Mwaka 2026, TEC haikufunga mjadala. Katika Mkutano Mkuu wake wa 87, maaskofu walirudia hoja za haki, rasilimali, mazungumzo na uponyaji wa Taifa.
Halafu wakafanya jambo muhimu. Wakaomba kumuona Rais. Agosti 10, wakaenda Chamwino. Ikulu ikatoa picha na taarifa.
Lakini siku chache baadaye Padri Charles Kitima akaeleza jambo ambalo linabadilisha namna ya kuutafsiri mkutano ule: Maaskofu hawakuitwa. Wao ndio walioomba kukutana na Rais.
Na hawakwenda mikono mitupu. Walikuwa na andiko lao. Kwa hiyo picha ya Chamwino haikuwa mwisho wa matamko ya TEC. Ilikuwa mwendelezo wake kwa njia nyingine.
Baada ya kusema hadharani, kanisa lilikwenda kusema moja kwa moja kwa mwenye mamlaka.
Je, TEC imekuwa kali zaidi?
Ukiangalia miaka 58 kwa pamoja, jibu ni ndiyo – lakini linahitaji maelezo.
Si kwamba maaskofu wa leo wana hasira zaidi kuliko wa 1968. Ni kwamba masuala wanayokabiliana nayo yamebadilika.
Nyerere alikuwa anajenga mfumo mpya wa maendeleo. Mwinyi alikuwa anafungua uchumi na mfumo wa kisiasa. Mkapa alikuwa anakabiliana na rushwa na mageuzi ya uchumi. Kikwete alikabili mjadala wa Katiba na uwajibikaji.
Magufuli alikabili maswali kuhusu uhuru wa kisiasa na haki za kiraia. Samia anakabili urithi wa masuala hayo yote pamoja na jeraha la uchaguzi wa 2025.
Kwa hiyo lugha ya Kanisa imekuwa kali kadiri mada yenyewe ilivyokuwa nzito. Ni tofauti kuzungumzia sera ya maendeleo na kuzungumzia kifo cha mwananchi.
Lakini TEC si Serikali mbadala
Hapa lazima kuwe na tahadhari. Historia hii isitufanye tuiweke TEC juu ya ukosoaji.
Kanisa nalo linaweza kukosea katika tathmini yake ya kisiasa. Linaweza kukosa taarifa ambazo serikali inazo. Lakini matamko yake yanapimwa katika dhamira ya kanisa kwenye muktadha wa utume wa maaskofu. Yanabeba sauti ya ufalme, ukuhani, na unabii.
Baadhi ya kauli zake zinaweza kutafsiriwa na wananchi kwa maana tofauti. Na ikumbukwe kuwa Wakatoliki wenyewe hawana msimamo mmoja wa kisiasa.
TEC si Bunge. Si mahakama. Si chama cha siasa. Na haiwezi kuchukua nafasi ya taasisi hizo.
Lakini pia si sahihi kusema: “Viongozi wa dini wabaki madhabahuni.” Kwa sababu historia yenyewe inakataa hoja hiyo.
Kanisa limekuwa mshirika wa serikali katika elimu, afya na maendeleo kwa miongo mingi. Kama lina wajibu kwa ustawi wa mwili wa mwananchi hospitalini, linawezaje kukosa wajibu wowote kwa utu wake anapodhulumiwa?
Hapo ndipo msingi wa hoja ya TEC ulipo.
Serikali nayo ina hoja
Serikali ina wajibu wa kulinda taifa lisigawanywe kwa misingi ya dini. Ina haki ya kutaka viongozi wa dini wasigeuze madhabahu kuwa majukwaa ya kampeni.
Ina haki ya kujibu hoja ambazo inaamini hazina taarifa kamili. Na haiwezi kutekeleza kila pendekezo la maaskofu kwa sababu tu limetolewa na kanisa.
Lakini mamlaka yenye nguvu haihitaji ukimya wa wakosoaji wake ili ithibitishe nguvu yake. Inaweza kusikiliza. Inaweza kujibu. Inaweza kukataa. Inaweza kurekebisha.
Huo ndio ukomavu wa taasisi.
Ndiyo maana Chamwino ni muhimu
Mkutano wa Agosti 10, 2026 una maana kubwa zaidi ukiwekwa mwisho wa mfululizo huu wa hatua za maaskofu
TEC haikufika Chamwino kutoka ombwe. Ilibeba historia. Ilibeba 1968. Ilibeba mijadala ya Ujamaa. Ilibeba miaka ya Mwinyi.
Ilibeba maadili na uwajibikaji wa miaka ya Mkapa. Ilibeba Katiba ya Kikwete. Ilibeba waraka wa 2018. Ilibeba DP World.
Ilibeba kifo cha Padri Saba. Ilibeba shambulio la Padri Kitima. Na zaidi ya yote, ilibeba Oktoba 29 – uchaguzi wenye utata na vifo vya raia.
Kwa hiyo, swali baada ya mkutano wa juzi Ikulu si kama rais na maaskofu walitabasamu.
Swali ni: Nini kitabadilika? Je, kutakuwa na ukweli kuhusu yaliyotokea? Je, kutakuwa na uwajibikaji? Je, waliofiwa watapata majibu?
Je, uchunguzi utakuwa na kiwango cha uhuru kinachoweza kujenga imani? Je, waliojeruhiwa kisiasa na kijamii watasikilizwa?
Je, Katiba Mpya itarudi mezani? Je, Serikali itayaona maridhiano kama mchakato wa kubadilisha mazingira au kama mkutano wa viongozi?
Na TEC yenyewe itafanya nini kama mambo ambayo iliwasilisha kwa Rais Samia hayatatekelezwa? Hapo ndipo hatua inayofuata ya historia hii ilipo.
Miaka 58 ya kusema ukweli mbele ya mamlaka
Ukiweka matamko haya pamoja, jambo moja linaonekana. Makali ya TEC hayakuzaliwa mwaka 2025. Hayakuanza na Samia. Hayakuanza na Magufuli. Wala hayakuanza na DP World.
Yamejengwa polepole katika historia ya taifa. TEC ya 1968 ilisema maendeleo lazima yawe ya haki. TEC ya miaka ya Mwinyi ikasema maendeleo lazima yamheshimu binadamu na Serikali iwajibike katika mazingira mapya.
TEC ya Mkapa ikaendelea kuunganisha uongozi na maadili, umaskini, rushwa na matumizi ya rasilimali. TEC ya Kikwete ikaingia hadi katika uadilifu wa uchaguzi na Katiba.
TEC ya Magufuli ikasema wazi kwamba uhuru, demokrasia na usalama wa wananchi viko ndani ya eneo la dhamiri ya Kanisa.
TEC ya Samia ikaenda hatua nyingine: rasilimali za taifa, uchaguzi, mauaji, uchunguzi huru, Katiba, ukweli na maridhiano.
Huu si mstari ulionyooka. Wakati mwingine TEC imekuwa kimya, wakati wananchi wengine wakitaka izungumze. Wakati mwingine imezungumza, na baadhi ya watu wakaona imechelewa.
Wakati mwingine imeonekana ipo karibu sana na Serikali. Wakati mwingine imeonekana mbali sana nayo.
Hilo lenyewe linastahili uchambuzi. Lakini katika miaka 58, msingi mmoja umeendelea kujitokeza: TEC imekataa kukubali kwamba utii kwa mamlaka unamaanisha ukimya mbele ya mamlaka.
Na Serikali zote, kuanzia Nyerere hadi Samia, kwa namna tofauti, zimelazimika kuishi na ukweli huo.
Kwangu, hiyo ndiyo maana kubwa ya picha za Chamwino. Si picha za serikali na kanisa ambazo ghafla zimeamua kuwa marafiki.
Ni picha za taasisi mbili ambazo zimekuwa zikishirikiana, zikivutana, zikikosana, zikijibu, zikionya na kurudi mezani kwa zaidi ya nusu karne.
Na pengine hapo ndipo Tanzania inaweza kupata somo kubwa zaidi. Taifa lenye afya halihitaji kanisa linaloogopa serikali. Wala halihitaji kanisa linalotaka kuwa serikali.
Linahitaji taasisi yenye uwezo wa kusema: “Hapa tumekubaliana nanyi.” Na inapobidi: “Hapa hatukubaliani nanyi.”
Serikali yenye afya nayo haihitaji kuona kila anayeikosoa ni adui. Inahitaji uwezo wa kusikiliza bila kupoteza mamlaka, kujibu bila kutisha na kurekebisha inapobidi bila kuona marekebisho kama udhaifu.
Mwaka 1968, TEC iliingia katika mjadala kuhusu Tanzania iliyokuwa inajengwa. Agosti 10, 2026, ikaingia Ikulu kujadili Tanzania iliyojeruhiwa na namna ya kuijenga tena.
Kati ya matukio hayo mawili kuna miaka 58 ya historia. Na ukifuatilia matamko yake moja baada ya jingine, unaona kitu ambacho picha moja ya Chamwino haiwezi kuonyesha:
Kadiri maswali ya Taifa yalivyokuwa mazito, ndivyo sauti ya TEC ilivyozidi kuwa kali.
Sasa swali si kama TEC itasema nini tena. Swali kubwa zaidi ni kama, baada ya miaka 58 ya kusema, mamlaka itasikia nini.







