TUDU LISSU: Mwaka mmoja wa maumivu na matumaini. Nitarudi

IFUATAYO ni kauli ya Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki, leo tarehe 7 Septemba 2018, mwaka mmoja baada ya kupigwa risasi na “watu wasiojulikana” wa serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli.  

UTANGULIZI

Ndugu zangu popote Tanzania na nje ya Tanzania. Nawapa salamu za upendo na furaha kubwa.

Tarehe 7 September, 2017, ni siku iliyobadilisha maisha yangu na, pengine, maisha yetu kama jamii ya Watanzania.

Majira ya saa saba mchana wa siku hiyo, nilitoka kwenye maeneo ya Bunge mjini Dodoma, nilikokuwa nahudhuria vikao vya Bunge, na kuelekea nyumbani kwangu kwenye Eneo D la mji wa Dodoma, kwa ajili ya kupata chakula cha mchana.

Bila mimi kujua, gari yangu ilifuatiliwa kwa nyuma na gari iliyokuwa na vioo vyeusi hadi ndani ya eneo la nyumba za viongozi wa umma. Eneo hili limezungushiwa ukuta na nyaya za miba (barbed wire) na hulindwa na walinzi wenye silaha usiku na mchana.

Na nje ya kila jengo pia, kuna ulinzi usiku na mchana. Mchana wa siku hiyo, walinzi wote, wa geti kuu la kuingilia na wa katika kila jengo, hawakuwepo kabisa. Nje ya jengo ninamoishi, watu wawili wanaume walishuka wakiwa na bunduki za kijeshi na ghafla waliishambulia gari yangu kwa risasi nyingi. Dereva wangu alifanikiwa kuruka nje na kujificha chini ya magari yaliyokuwa jirani.

Mimi sikuweza kuwatoroka. Kwa sekunde chache nilipigwa risasi 16 katika sehemu mbali mbali miguu, kiuno na mikono. Nilipigwa risasi mbili kwenye paja la kushoto zilizotoka nje upande wa pili. Nilipigwa risasi tatu juu kidogo ya kiuno upande wa kushoto zilizopita chini kidogo ya ngozi. Hizi hazikusababisha majeraha makubwa.

Nilipigwa risasi mbili mkono wa kushoto chini ya kiwiko na kwenye kiwiko chenyewe; na risasi moja kwenye mkono wa kulia chini ya kiwiko. Mikono yote miwili ilivunjika. Kwa upande wa kulia, nilipigwa risasi moja kwenye mfupa wa juu ya goti la kulia ambayo iliuvunja mfupa huo vipande vipande. Risasi nyingine ilivunja mfupa wa nyonga.

Baadae hospitalini Dodoma na Nairobi, madaktari walifanikiwa kutoa risasi sita tumboni na moja kwenye kiwiko cha mkono wa kushoto. Risasi moja imebaki chini ya uti wa mgongo juu kidogo ya kiuno.

Majeraha yaliyotokana na risasi hizo yalikuwa makubwa na ya hatari. Kwa mujibu wa Dr. Vincent Mutisso, aliyeongoza jopo la madaktari bingwa wa Nairobi Hospital nchini Kenya walionitibu baada ya kusafirishwa Nairobi kwa ndege ya dharura, nilipoteza sehemu kubwa ya nyama (blocks of muscle) katika sehemu zilizopigwa.

Aidha, nilipoteza mara tatu ya ujazo wa kawaida wa damu yangu, kwa maana kwamba niliongezewa damu robo tatu ya ujazo wa kawaida wa damu yangu. Hadi hapa nilipo, nimekwifanyiwa jumla ya operesheni 21, Nairobi Hospital operesheni 17, na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg, hapa Ubelgiji operesheni 4. Tumboni na kwenye mguu wa kulia pekee, nimefanyiwa operesheni 14.

Hata hivyo, kama wasemavyo Waswahili, Mungu sio Athumani. Na kama mwanaharakati wa Kenya, Koigi wa Wamwere, alivyosema kwenye kitabu chake ‘I Refuse to Die’, na mimi pia ‘nilikataa kufa.’ Mwenyezi Mungu hakuruhusu mipango ya wauaji na wale waliowatuma kufanikiwa.

Leo ni mwaka mmoja kamili tangu niumizwe kiasi kile, na nimeweza kusimama kwa miguu yangu tena, hata kama ni kwa msaada wa magongo. Majeraha ya sehemu zote za mwili, isipokuwa mguu wa kulia,  yamepona. Na madaktari wangu wamesema mguu wa kulia nao utapona, na nitarudi Tanzania tofauti na nilivyoondoka: nikiwa natembea mwenyewe bila msaada wa mtu mwingine au kifaa. Safari bado ni ndefu kiasi, lakini mwisho wake sasa unaonekana.

Lakini mwaka huu mmoja umeshuhudia mjadala mkubwa, ndani na nje ya Bunge, juu ya mazingira ya shambulio hilo. Kumekuwa na mvutano na mabishano makubwa baina ya watu na taasisi mbali mbali. Leo ni muda muafaka kuyatolea ufafanuzi baadhi ya masuala haya.

KWA NINI WALITAKA NIFE?

Nilitakiwa kufa kwa sababu ya msimamo wangu wa kisiasa, hasa kwa kumpinga Rais Magufuli na kumkosoa hadharani tangu aingie madarakani. Mapema kabisa katika utawala wake, wakati kila mtu anampigia vigelegele, mimi nilimsema, ndani na nje ya Bunge, kwamba ataiingiza nchi yetu kwenye janga kubwa la ukiukaji wa haki za binadamu.

Nilipinga kauli zake tata kuhusu tetemeko la ardhi Mkoa wa Kagera na kuhusu tatizo la njaa mahali pengi nchini. Nilikemea tabia yake ya kubeza na kudhalilisha majaji wetu na kutisha wanasheria na mawakili wa kujitegemea. Nilipinga vikali vitendo vyake vya kukamata mali za wawekezaji wa kigeni bila kujali sheria zetu, mahusiano yetu ya kiuchumi na jamii ya kimataifa na hatari ya kushtakiwa katika Mahakama za kimataifa na kuingizwa hasara kubwa zaidi.

Nilipinga vikali ukiukaji wa haki za binadamu uliokithiri chini ya utawala wake, sio tu kwa kupiga kelele lakini pia kwa kutoa msaada wa uwakilishi mahakamani kwa wale waliokamatwa na kushtakiwa kwa sababu ya kukosoa serikali yake na vyombo vyake.

Serikali ya Magufuli ilipoanza kuingilia masuala ya uendeshaji wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kwa kuingilia uchaguzi wa viongozi wake, nilisimama kidete na nikachaguliwa kwa kura nyingi kuwa Rais wa TLS.

Nilikuwa wa kwanza kutoa taarifa juu ya kukamatwa nchini Canada kwa ndege ya Bombardier iliyonunuliwa na Serikali yake kwa ajili ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), baada ya Magufuli kuvunja mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Bagamoyo na kusababishwa Serikali kushtakiwa na kushindwa kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi.

Kwa sababu ya msimamo wangu kwenye masuala haya, nilianza kutiwa misukosuko mingi. Magufuli hakumaliza hata mwaka mmoja nilianza kusakamwa na Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi (TISS).

Ndani ya takriban mwaka mmoja, nilikamatwa mara nane na kufunguliwa kesi za jinai sita mahakamani. Walifikiri watanitisha na kuninyamazisha kwa manyanyaso ya mapolisi na tishio la magereza. Walipogundua hayo hayanitishi, wakaamua kuninyamazisha milele kwa risasi za bunduki za Kalashnikov. Mungu sio Athumani. Na hilo halikufanikiwa.

Walichofanikiwa ni kunivunja vunja viungo vya mwili wangu. Moyo wangu haujavunjika. Nafsi yangu iko vile vile. Na msimamo wangu haujatetereka. Ernest Hemingway, Mwanafasihi wa Kimarekani na Mshindi wa Tuzo ya Fasihi ya Nobel, aliandika – katika fasihi yake ya ‘The Old Man and the Sea’ – kwamba ‘mtu anaweza kuuawa lakini asishindwe.’

‘Kushindwa’ kwa maana ya Hemingway ni kukata tamaa, na kubadili msimamo, na kukubali kumtumikia kafiri ili upate mradi wako. Nimeumizwa vibaya kimwili, lakini bado niko imara kichwani na moyoni. Sijashindwa.

KUHUSU BUNGE NA MATIBABU YANGU

Kumekuwa na mvutano mkubwa kati ya familia yangu na uongozi wa Bunge chini ya Spika Ndugai na Katibu wa sasa wa Bunge, Steven Kagaigai. Mvutano huu unahusu utaratibu wa kulipia gharama zote za matibabu yangu. Huu ni mgogoro wa kutengenezwa na ni aibu kubwa kwa Bunge kama taasisi na kwa Spika Ndugai kama kiongozi wake.

Msimamo wa uongozi wa Bunge chini ya Spika Ndugai na Katibu Kagaigai ni kwamba Bunge haliwajibiki kulipa gharama za matibabu yangu kwa sababu nilikiuka au viongozi wa chama changu bungeni walikiuka taratibu za matibabu ya Wabunge kwa kulazimisha nipelekwe Nairobi badala ya kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwanza.

Kufuatana na maelezo ya Spika Ndugai, Hospitali ya Muhimbili ilitakiwa kutoa mapendekezo ya mimi kupelekwa nje kutibiwa kwa Katibu wa Wizara ya Afya ambaye naye angeunda jopo la madaktari watatu kuchunguza mapendekezo ya Muhimbili.

Endapo mapendekezo ya Muhimbili yatakubalika, basi jopo la madaktari litamshauri Katibu Mkuu ambaye akiridhika, itabidi Bunge liombe idhini kwa Rais Magufuli ambaye naye akiridhika basi pesa ya matibabu itatolewa. Tatizo liko wapi?

Kwanza, utaratibu huu hautambuliki kisheria. Sheria inayohusika na matibabu ya Wabunge ni Sheria ya Uendeshaji wa Bunge, 2008. Sheria hiyo imesema kwa kifupi kwamba kila Mbunge atakuwa na haki ya kutibiwa ndani au nje ya Tanzania kwa gharama ya Bunge. Utaratibu wa kupata kibali cha Muhimbili, au cha Katibu Mkuu Afya, au cha Rais haupo kwenye Sheria hiyo.

Pili, utaratibu unaozungumzwa na Spika Ndugai na watu wake unaliweka Bunge, mhimili huru wa dola na wenye bajeti yake inayojitegemea, chini ya mamlaka ya mhimili wa Serikali, yaani Wizara ya Afya na Ikulu. Hii inaingilia moja kwa moja uhuru, hadhi na heshima ya Bunge na inakiuka kanuni kuu ya Katiba ya mgawanyo wa madaraka.

Tatu, hata kama utaratibu huo ungekuwepo kisheria, haukidhi na usingeweza kukidhi mahitaji ya dharura iliyotokana na kushambuliwa kwangu. Kwa majeraha nikiyokuwa nayo na kwa hali ya kiusalama iliyokuwepo, hakukuwa na uhakika kwamba nikipelekwa Muhimbili nitakuwa salama dhidi ya watu walionishambulia.

Na hakukuwa na muda mrefu wa kusubiri hali itulie ndio taratibu zinazosemwa zifuatwe. Ilibidi uamuzi ufanywe haraka ili nikapatiwe matibabu katika hali ya dharura ya kiafya na kiusalama iliyokuwepo. Uamuzi wa kunipeleka Nairobi Hospital haukuwa wa Mwenyekiti Mbowe peke yake, hata kama ni kweli kwamba yeye ndiye aliyesisitiza umuhimu wa kwenda Nairobi Hospital badala ya Muhimbili.

Baada ya kukimbizwa Hospitaliya Mkoa wa Dodoma nikiwa nimejeruhiwa vibaya, kilifanyika kikao cha viongozi wa CHADEMA, Bunge na Serikali kuhusu hatua za kuchukua. Upande wa CHADEMA uliongozwa na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mwenyekiti Mbowe na wabunge kadhaa.

Upande wa Bunge uliongozwa na Spika Job Ndugai, Naibu Spika Tulia Ackson  na Katibu wa Bunge wakati huo, Dk. Thomas Kashililah. Kwa upande wa Serikali alikuwepo Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Katibu Mkuu wake Dk. Ulisubisya Mpoki na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba.

Kikao hicho ndicho kilichoamua nipelekwe Nairobi. Ndio maana katika msafara ulionipeleka Nairobi Hospital, alikuwepo pia Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma. Na ndiyo maana ndege iliyonipeleka Nairobi iliruhusiwa kuruka Uwanja wa Ndege wa Dodoma saa sita usiku.

Ningekuwa nimepelekwa Nairobi kwa utaratibu binafsi, kama inavyodaiwa sasa, nisingesindikizwa na Mganga Mkuu wa Mkoa na wala Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) isingeruhusu ndege kuondoka Dodoma saa sita usiku.

Na wala maafisa wa uhamiaji wasingegonga muhuri passport zetu na kuturuhusu kutoka nje ya nchi. Baada ya kuwa nimeshapokelewa Nairobi Hospital na maisha yangu kuokolewa, Spika Ndugai na Katibu wa Bunge Kashililah walikutana na ndugu zangu kwenye Ofisi ya Bunge Dar na kuwashauri waandike barua rasmi ya maombi ili Bunge liweze kutoa fedha za matibabu yangu.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu naye alishauri hivyo hivyo, tena hadharani kwenye mkutano na wandishi habari. Waziri Mwalimu alisisitiza jambo hilo kwa kutoa mfano wa Spika wa zamani wa Bunge, marehemu Samuel Sitta, ambaye inasemekana aliomba msaada wa kutibiwa na Bunge wakati hakuwa Mbunge tena, na tayari alikuwa hospitalini London, Uingereza.

Barua zikaandikwa na ndugu zangu kama walivyoelekezwa na uongozi wa Bunge. Lakini mara Katibu wa Bunge Kashililah akaondolewa madarakani na Rais Magufuli, na Steven Kagaigai akateuliwa kushika nafasi hiyo. Inaelekea Steven Kagaigai alikuja na maelekezo ya Rais Magufuli: Tundu Lissu asipewe pesa yoyote ya matibabu na Bunge.

Spika Ndugai mwenyewe amethibitisha hivyo, tena ndani ya Ukumbi wa Bunge. Spika Ndugai aliliambia Bunge mwezi Juni kwamba sitatibiwa na Bunge kwa sababu Rais Magufuli hajatoa idhini hiyo. Hiyo ndiyo sababu ya mvutano huu. Spika Ndugai amekubali kuingiliwa na kupokwa madaraka ya Bunge kuendesha shughuli zake kama mhimili huru wa dola na mhimili mwingine, Serikali.

Sasa Rais Magufuli ndiye anayeamua nani atibiwe na nani asitibiwe na Bunge. Hii haijawahi kutokea tangu Bunge letu lianzishwe wakati wa ukoloni!!! Kwa upande wetu, njia pekee iliyobaki sasa ni kulipeleka suala hili mahakamani ili Mahakama Kuu itoe tafsiri sahihi ya jambo hili. Maandalizi ya kwenda mahakamani yanaendelea.

UCHUNGUZI WA POLISI UMEISHIA WAPI?

Shambulio dhidi yangu limethibitisha jinsi ambavyo Jeshi la Polisi la Tanzania linavyotumika kutekeleza matakwa ya kisiasa ya walio madarakani. Kwa vile aliyeshambuliwa ni mbaya wa Serikali ya Magufuli, Jeshi la Polisi halijahangaika na kufanya upelelezi wa kijinai wa kitendo hiki cha kihalifu.

Hadi ninapoandika haya, hakuna mtu yeyote anayeshukiwa kunishambulia. Hakuna yeyote anayetuhumiwa. Hakuna yeyote aliyehojiwa na wapelelezi wa polisi kama shahidi. Hata wahanga wa shambulio lenyewe, mimi na dereva wangu,  hatujahojiwa.

Lakini ndugu zangu na viongozi wangu wa chama walisema tangu mwanzo: Jeshi la Polisi la Tanzania haliwezi kuchunguza shambulio hili. Linafahamu mpango mzima. Linawafahamu ‘watu wasiojulikana’ na mtu aliyewatuma kuja kuniua. Linawafahamu walioamuru walinzi wote wa majengo nilipokuwa naishi waondolewe ili ‘watu wasiojulikana’ wafanye kazi yao ya mauaji bila ushahidi.

Linafahamu aliyeamuru kamera ya CCTV iliyokuwepo kwenye jengo la makazi yangu iondolewe na wanafahamu ilikofichwa hadi sasa, kama haijaharibiwa ili kupoteza ushahidi.

Marehemu Sipho Sepamla, mshairi maarufu wa Soweto, aliandika shairi linaloitwa ‘At the Dawn of Another Day’, yaani ‘Mawio ya Siku Nyingine’: ‘Tungeweza kuuliza mashahidi, lakini mashahidi wa nini kwa risasi zilizopigwa wakati jua linaangazia macho kitendo chenyewe.’

JE, DEREVA WANGU AMEFICHWA WAPI?

Kuna wajinga wanaoelekea wametumwa na ‘watu wasiojulikana’ kueneza maneno ya kijinga kwamba dereva wangu anafahamu siri za kushambuliwa kwangu. Kwamba alitoroshwa na sasa amefichwa na CHADEMA na Mwenyekiti Mbowe, n.k.

Nimekuwa na dereva huyu tangu mwaka 2002, akiwa kijana wa miaka 19. Katika miaka yote hii, amekuwa ni sehemu ya familia yetu. Ninamfahamu fika. Ninafahamu alivyo mwaminifu kwangu. Hawezi na asingeweza kufahamu njama za kuniua mimi halafu asiniambie.

Mara baada ya kushambuliwa kwangu, ‘watu wasiojulikana’ walianzisha minong’ono ya chini chini kwamba wakimpata dereva wangu basi ‘wamemaliza maneno’ juu ya kushambuliwa kwangu. Watu wetu waligundua hatari kubwa aliyokuwamo dereva kutokana na minong’ono hiyo. Wakaamua kumtoa Tanzania na kumleta Nairobi nilikokuwa nimelazwa mimi.

Hakutoroshwa. Aliondoka na Mh. Godbless Lema na alipitia mpaka wa Namanga. Alipatiwa hati ya muda ya kusafiria na maafisa wa uhamiaji Namanga. Na wala hakufichwa Nairobi. Alikaa na mimi Nairobi Hospital kwa miezi minne.

Jeshi la Polisi la Tanzania lilimjulisha kaka yangu, wakili Alute Mughwai, kwamba litatuma wapelelezi wake kuja Nairobi kutuhoji mimi na dereva wangu. Tuliwasubiri mapolisi hao. Hawakuonekana mpaka wakati tunaondoka Kenya kuja Ubelgiji tarehe 6 Januari ya mwaka huu.

Dereva wangu hakutoroka Kenya kuja Ubelgiji. Ili aweze kusafiri kutoka Kenya kuja Ubelgiji, alihitaji passport ya Tanzania na visa ya Ubelgiji. Hakuwa navyo. Hivyo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Serikali ya Ubelgiji ilimpatia hati maalum ya kusafiria na kuingia Ubelgiji. Wakati mimi na mke wangu tulisafiri kwa passport za Tanzania; dereva wangu alisafiri kwa passport maalum ya Serikali ya Ubelgiji.

Hapa Ubelgiji anaishi mji mmoja na mimi. Amekodishiwa nyumba na anaishi kwa gharama za Serikali ya Ubelgiji, sio za CHADEMA au Mwenyekiti Freeman Mbowe au za kwangu mwenyewe. Anasomeshwa na Serikali ya Ubelgiji.

Bado anaweza kuhojiwa na wapelelezi kuhusiana na jaribio la mauaji dhidi yangu. Utaratibu wa kufanya hivyo upo kisheria, kwa mujibu wa Sheria ya Kusaidiana Katika Masuala ya Jinai iliyotungwa na Bunge la Tanzania. Lakini Jeshi la Polisi la Tanzania halitaki kufanya hivyo. Linafahamu mpango mzima wa ‘watu wasiojulikana.’

Huu ujinga unaosambazwa na vijigazeti vya Jamvi la Habari na Tanzanite ni kazi ya ‘watu wasiojulikana’ wanaofamika vyema. Ni aibu kubwa kwa nchi yetu, kwa Jeshi la Polisi na kwa Serikali ya Magufuli.

HITIMISHO

Naomba nimalizie ujumbe huu mrefu. Nataka niwe muwazi. Huu mwaka mmoja umekuwa mrefu na mgumu sana kwangu sio kwa sababu ya majeraha ya mwili. Ni kwamba pia nimei-miss sana Tanzania na nimewa-miss Watanzania.

Nime-miss sana Bunge, licha ya matatizo yote ya Bunge la Spika Ndugai. Nimewa-miss sana watu wangu wa Jimbo la Singida Mashariki na mikutano yetu ya hadhara. Nime-miss sana kazi zangu za chama na nimewa-miss viongozi wenzangu, wanachama wetu na wafuasi wetu katika mamilioni yao.

Nime-miss sana mapambano ya utetezi wa haki za watu wetu ndani na nje ya mahakama. Nimewa-miss mawakili wa Tanzania Bara walionipa heshima ya kuwaongoza katika kipindi kigumu sana katika historia ya TLS.

Mshairi Sipho Sepamla aliandika shairi lingine liitwalo ‘The Exile’, yaani ‘Uhamishoni.’ Shairi hilo linaelezea machungu ya kuishi uhamishoni kwa kulazimishwa wakati wa utawala wa kibaguzi wa makaburu wa Afrika Kusini.

Katika huu mwaka mmoja wa kulazimishwa kuwa nje ya nchi; wa kutokuonana moja kwa moja na watu wetu, familia, ndugu, jamaa, majirani na marafiki zangu; wa kufuatilia mapambano ya kudai haki na demokrasia mitandaoni badala ya kuwa mshiriki kwenye uwanja wa mapambano, sasa ninaelewa maana hasa ya kuwa ‘uhamishoni.’

Baada ya kushindwa na Wajapan kwenye Mapigano ya Bataan nchini Ufilipino mwaka 1942 wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kamanda wa majeshi ya Marekani katika Bahari ya Pacific ya Magharibi, Jenerali Douglas MacArthur, alitamka: ‘I Shall Return.’ ‘Nitarudi.’ Na mimi nawatamkia Watanzania: ‘Nitarudi!!!’

Like
6

Leave a Comment

Your email address will not be published.