Kubeti: Wachina wamiliki, Watanzania mawakala

Hii mashine unavyoiona wamiliki ni Wachina, nimeiweka hapa kwa ajili ya wateja wangu wa vinywaji, wakija hapa wengine wanapata kinywaji, wengine wanacheza kamari maisha yanaendelea.

RAIA wa Jamhuri ya China ndio vinara wa biashara ya mashine za kuchezesha kamari maarufu ‘dubwi,’ mchezo ambao umegeuka jinamizi kwa vijana nchini.

Biashara hiyo ya michezo ya kubahatisha imeshamiri zaidi jijini Dar es Salaam.  Inaendeshwa na raia hao wa China.  Watanzania wanapewa uwakala wa maduka na vituo vya kuendesha kamari kwa ujira maalumu.

Hata hivyo, kuna wasiwasi wa kuwapo biashara haramu nyuma ya michezo ya kamari ikiwa ni pamoja na  uingizaji wa mashine kiholela kupitia njia za panya. Kwa kutokuwa kwenye mfumo rasmi wa usajiri, wanaikosesha mapato serikali.

Uchunguzi uliofanywa na SAUTI KUBWA umebaini kuwa sababu ya kushamiri kwa vituo vya mashine za kuendesha kamari ni ulegevu mkubwa wa utoaji wa vibali na leseni kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) ambao ndiyo wenye mamlaka kwa mujibu wa kifungu cha 7 cha Sheria ya michezo hiyo ya mwaka 2003.

Sheria inaitaka GBT kufanya ukaguzi wa mara kwa mara juu ya ukiukwaji wa sheria, kanuni za uendeshaji wa michezo hiyo, jambo ambalo kwa mujibu wa uchunguzi wetu halifanyiki.

SAUTI KUBWA imezungumza na baadhi ya mawakala wa vituo vya kamari, wamesema hakuna ukaguzi wowote uliofanywa na mamlaka za serikali kuhusu uhalali wa mashine zilizopo mitaani.

Sheria inayoongoza michezo hiyo inataka mtu aliye na leseni lazima mashine zake zisajiriwe na GBT na kuweekewa stika maalum ili kurahisisha ukaguzi. Wanaobainika kukiuka taratibu hizo, mashine zao hutaifishwa na kuteketezwa kwa mujibu wa sheria na  taratibu za Baraza la Mazingira (NEMC).

Kwa zaidi ya miaka miwili sasa, GBT haijafanya ukaguzi wowote wa dharura au endelevu. Jambo hili linadaiwa kuchangia mashine zisizosajiriwa kuzagaa mitaani na kukosa udhibiti.

SAUTI KUBWA imebaini kuwa wafanyabiashara hao wa Kichina wanafunga vifaa au mitambo maalum (GPS) kwenye mashine zao zote kwa ajili ya ulinzi na usalama wa mali zao huku pia wakiweza kufuatilia kila kinachofanyika kwa mawakala wao wa kamari.

Baadhi ya mawakala wameeleza kuwa hawajawahi kuona ukaguzi wowote kutoka taasisi yoyote ya serikali.

Mmiliki wa grocery ambaye ni wakala wa mashine za dubu eneo la Tabata Kisukuru wilayani Ilala jijini Dar es Salaam anayejulikana kwa jina maarufu ‘Master’ alisema amekuwa wakala kwa zaidi ya miaka miwili, lakini hajui kama mashine hizo zinapaswa kukaguliwa na mamlaka za serikali.

 “Hii mashine unavyoiona wamiliki ni Wachina, nimeiweka hapa kwa ajili ya wateja wangu wa vinywaji, wakija hapa wengine wanapata kinywaji, wengine wanacheza kamari maisha yanaendelea.

“Mashine hii ikiharibika nawapigia simu, haraka sana wanafika na kutengeneza wenyewe, hii biashara kwa ujumla inawalipa faida kubwa, hata ikitokea hitilafu yoyote, au umeme kukatika wakati upo kwenye mchezo pesa yote inaondoka, pesa yako ukishaweka hairudi,” anasema.

Kuhusu faida, anasema hana faida kubwa zaidi ya kuburudisha wateja wake, kwani kiasi anacholipwa na wenye mashine ni kidogo mno.

Anasema wenye mashine kila wakija kuchukua fedha zao (coin) ambazo wachezaji wameingiza kwenye mashine yeye hulipwa Shilingi 10,000 kama posho.

Wakala mwingine wa Tegeta -Wazo wilayani Kinondoni, Denis Rwezaula anasema.

“Kwenye hizi mashine kuna trei ndani ambapo likijaa zile  pesa (coin) ndiyo Wachina wananihesabia kamisheni yangu.

“Naweza kulipwa wastani wa shilingi 10,000 na 20,000  kila wanapokuja kufungua zile mashine kuchukua mapato yao, hii inategemea uzalishaji wa biashara.”

Baadhi ya Wachina wanalipa kamisheni kwa siku, kila baada ya siku tatu au kila baada ya siku 10”anasema wakala huyo.

Mawakala wote waliozungumza na SAUTI KUBWA wanasema michezo yote inayochezwa kupitia mashine  inatumia coin ya shilingi 200.

BIASHARA YA CHENJI                                

Kutokana na kushamiri kwa biashara ya kamari, chenji (coin) za shilingi 200 zimekuwa biashara kubwa kwa baadhi ya vijana, wanawake na hata wafanyakazi wa kwenye mabenki jijini Dar es Salaam.

Uchunguzi wa SAUTI KUBWA umebaini mfuko mmoja wa chenji za shilingi 200 wenye thamani ya Shilingi 200,000 unauzwa kati ya Shilingi 20,000 mpaka 25,000 kwa kampuni za wachina wanaomiliki mashine hizo.

Aidha uchunguzi huo ubebaini kuwapo mtandao mkubwa wa biashara ya chenji katika benki mbalimbali na hata maduka makubwa ya jumla (super markets) ambao huuza chenji hizo kwa wafanyabiashara na kampuni za Kichina.

Aidha baadhi ya kampuni hizo zimeajiri wanawake  ambao huwapatia mtaji wa fedha za noti wazibadilishe na kuwa chenji za shilingi mia mbili kwa ujira wa kati ya Sh 10, 000 mpaka 20,000 kutegemea na kiasi cha chenji wanachokileta kwa siku.

‘Dili’ hilo la chenji limekwenda mbali zaidi kwani maeneo yanayojulikana kuhusisha fedha za chenji mathalani huduma za vyoo vya umma, watoza ushuru sokoni, wauzaji wa kahawa vijiweni nao wanauza chenji hizo kati ya Sh 5000 kwa kila laki moja au shilingi 2500 kwa chenji zenye thamani ya shilingi 50,000.

Mmoja wa wafanyabiashara wa chenji, Hussein Makaranga wa Mbagala Majimatitu aliiambia SAUTI KUBWA kuwa biashara ya chenji imekuwa ikipanda dau kila siku. Anasema mwaka mmoja uliopita alikuwa anapata wastani wa shilingi 30,000 hadi 40,000 kwa siku. lakini kwa sasa anaweza kupata kati ya Shilingi 10,000 hadi 15000.

“Nimejenga nyumba ya vyumba viwili, nina mke na watoto wawili tunategemea biashara hii ya kuuza chenji.

“Awali wauzaji wa chenji tulikuwa wachache sana,  biashara ilitulipa vizuri, benki tulikuwa tunazipata bure, lakini kwa sasa kama hutoi chochote huwezi kuzipata, na Wachina wameajiri watu wa kutafuta chenji mtaani, kwa tunanyang’anyana wateja.

GBT YAKATAA KUTOA MAJIBU

Zaidi ya miezi miwili, SAUTI KUBWA imeandika maswali kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha  (GBT) bila kupatiwa majibu.

Awali mwandishi wa habari hizi alifika Ofisi za GBT na kuonana na mmoja wa maafisa wake aitwaye Zena Simkondo ili kupata ufafanuzi wa maswali kadhaa.

Hata hivyo afisa huyo alikataa kuzungumzia chochote kwakuwa sio msemaji wa GBT, hivyo alimtaka mwandishi kuandika maswali na kuyatuma kwa njia ya email kwenda kwa mkurugenzi mkuu ili yapatiwe majibu.

Hata hivyo licha ya kutuma maswali hayo tangu Agosti Mosi mwaka huu, hayakuwahi kupata majibu hadi tunachapisha habari hii.

KAMARI MARUFUKU CHINA
Wakati mashine za kamari zikishamiri nchini kupitia wafanyabiashara raia wa China, hali ni tofauti kabisa nchini mwao.

Mhadhili wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) ambaye ameishi China kwa miaka kadhaa, Edgar Bebwa anasema “nimebahatika kutembea miji mikubwa na midogo nchini China ikiwemo Beijing, Shanghai, Xian, Tianjin, na Chongqing sijawahi kuona michezo ya kamari kwani inakatazwa kisheria.

Nchini China, michezo ya bahati nasibu hupewa leseni na serikali na uendeshaji wake unategemea mfumo wa ufikiaji ulio mkali na uuzaji wa tiketi za bahati nasibu
mtandaoni bila idhini unakatazwa kwa mujibu wa Sheria maalum za udhibiti.

“Kuna bahati nasibu mbili za serikali, ambazo zinaendeshwa na serikali ya China.Bahati nasibu ya kusaidia ilianzishwa mwaka 1987, na Bahati nasibu ya Michezo ilianza miaka saba baadaye.

“Hakuna kabisa mchezo wa kucheza na sarafu za coin kama ilivyo hapa nchini kwetu ijukanayo
kama coin slot machine  ambayo inawekwa kwenye baa, grocery, maduka na kadhalika.
Kwa mujibu wa tovuti ya https://practiceguides.chambers.com/practice-guides/gaming-law-2022/china/trends-and-
developments, watoto wanaruhusiwa kucheza michezo ya video mtandaoni kwa saa tatu kwa wiki.

Mamlaka zinasema watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wanaweza kucheza tu kuanzia saa 12 jioni hadi saa 1 usiku, siku za Ijumaa na mwishoni mwa
wiki. Kampuni za michezo zinalazimika kutekeleza sheria hizi.”
Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, kamari imekatazwa kabisa katika Jamhuri ya Watu wa China tangu mwaka 1935 isipokuwa Hong Kong, Macau, na Taiwan pekee ndizo zimeachwa.

Nchini China shughuli zinazohusiana na kamari zinaweza kusababisha adhabu za utawala na hata
kifungo cha jinai katika kesi kubwa.
Mamlaka husika hususan Wizara ya Usalama wa Umma
wameimarisha utekelezaji kuhusu aina mpya za kamari, kama vile kamari mtandaoni na
kamari za mipaka huku aina yoyote ya michezo inayoweza kuwa kamari pia imezuiliwa kabisa.

Akielezea zaidi, mhadhili huyo anasema michezo inayohusisha kamari ni kama vile michezo ya uvuvi ambayo kawaida ina sifa tofauti, ambayo ni pamoja na mbinu ya kubadilishana pesa kwa “Sarafu za kimagharibi” au vifaa vya mchezo.

Ndani ya mchezo hiyo kuna moduli ya kutoa faida au zawadi kutokana na mchezo; na mwendeshaji wa mchezo hutoa huduma kama vile: biashara au kubadilishana alama za mchezo; au kubadilishana pesa au bidhaa kwa mfumo uliofichwa, mfano, sarafu za
kimagharibi.

Kulingana na sheria, kamari
yoyote katika michezo kama vile kadi inapaswa kufanywa kwa vitu visivyo vya sarafu,
ambavyo ni pamoja na visu. Pia kuna kifungu kinachoitwa ‘burudani ya muda’ kinachoruhusu
michezo ya mahjong kuchezwa wakati wa Mwaka Mpya wa Kichina, lakini matukio kama hayo huwa na muda mfupi kwa asili yake.
UGANDA

Jumuia ya Afrika Mashariki nchi karibu zote zimeruhusu michezo ya kamari.  Nchini Uganda kamari zimeshamiri hususani Jiji la Kampala kama ilivyo Dar es Salaam Tanzania.

Tofuti na hapa kwetu, Uganda wafanyabiashara wamiliki wa mashine na mitandao mingine ya michezo ya kamari ni Wachina na Wahindi.

Nchini Uganda, Sheria ya Michezo ya Kubahatisha ya mwaka 2016 kimaudhui haina tofauti kubwa na Sheria ya Tanzania.

Ibara ya 64 inatoa maelekezo ya adhabu kwa mtu anayechezesha michezo hiyo bila leseni, kuwa anatenda jinai na akibainika anaweza kupata adhabu ya aidha faini au kifungo kisichozidi miaka minne, au vyote kwa pamoja.

Katika suala la uendeshaji wa Casino, kubeti au aina nyingine za michezo hii ya kubahatisha, inaeleza kuwa anayeendesha michezo hiyo bila kuwa na leseni, au kushindwa kutoa zawadi kama ilivyoahidiwa, au anayetengeneza au kusambaza vifaa vya michezo hiyo bila kuwa na leseni pia atapata adhabu kali pale atakapobainika.

Sheria hiyo nchini Uganda inatoa maelekezo ya namna ya kuendesha michezo ya kubahatisha na kubeti, ikiwemo kuwepo kwa bodi maalumu inayotoa leseni za Casino, michezo ya kubahatisha au ya kubeti na namna vifaa vyote vinavyohusishwa na michezo hiyo vinavyotakiwa kupatikana na kusajiliwa pamoja na masharti mengine ikiwemo idadi ya watu wanaotakiwa kuingia au kuajiriwa katika majengo ya kuchezesha michezo hiyo.

RWANDA

Sheria ya Kusimamia Michezo ya kubahatisha ya mwaka 2011 nchini Rwanda inatofautiana naya Tanzania.

Wakati Tanzania michezo hiyo inasimamiwa na Bodi, Rwanda Ibara ya 4 ya Sheria yao inatoa mamlaka ya usimamizi wa michezo hiyo kwa wizara yenye dhamana husika, ambapo Waziri Mkuu anaelekezwa kushiriki katika uundaji wa mamlaka nyingine za usimamizi.

Ibara ya 32 inaeleza sifa za watu wasioruhusiwa kushiriki michezo hiyo, ambao ni ndugu wa wamiliki wa leseni hizo, watu ambao bado ni tegemezi kiumri na kimajukumu, wenye matatizo ya akili na namna ya kuwashughulikia kupitia mahakama.

Hata hivyo, Ibara ya 33 ya sheria hiyo ya Rwanda inazuia kabisa kurusha matangazo ya kuhamasisha,  kubahatisha kwa namna itakayobainika kuwa ni ya uongo wenye nia ya kuhamamsisha watu kushiriki michezo hiyo.

Katika Ibara ya 18 ya sheria hiyo nchini Rwanda, imeweka masharti ya namna ya kusimamia uagizaji na usambazaji wa vifaa vya kuchezesha michezo hiyo, ambapo inaelekeza kila mashine lazima itambulike kwa namba maalumu za usajili, ikiwemo jina la mtengenezaji, namba maalumu na tarehe za kutengenezwa kwake.

Vifo vya wanandoa

“Siku ya tukio, Mwanahamisi aliniaga kuwa mzazi mwenzake alikuwa amempigia simu wakutane ili ampatie pesa za matunzo ya watoto. Hata hivyo, rafiki yangu alichelewa kurudi nikahisi labda amepitia kwenye ‘mishe mishe’ zake za ususi.

“Baadaye mchana, mmoja wa walioshuhudia tukio hilo ambaye aliishi jirani naye, alinipigia simu kunieleza kuwa Mwanahamisi ameuawa na mumewe, na kwamba wakati mume huyo anatekeleza tukio hilo, alimziba mdomo mkewe kwa kutumia nguo, ili kelele zisisikike.

“Nilichanganyikiwa niliposikia kwamba Mwanahamisi amekutwa kauawa na alikutwa amezibwa tambala mdomoni. Ni simanzi isiyoisha kwa kweli,” anasimulia rafiki wa marehemu Mwanahamisi aitwaye Winifrida Msangi. Anaendelea:

”Wakati tupo kwenye maandalizi ya msiba wa Mwanahamisi, saa 11 jioni tulipigiwa simu kuwa Omary naye kafariki baada ya kujirusha kwenye treni maeneo ya Ubungo Maziwa.”anasema Msangi.

Hivi ni miongoni mwa visa vya kusikitisha vilivyoripotiwa na kuthibitishwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Muliro Jumanne, mwishoni mwa mwezi Juni na mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu.

Omary Herman (39) ambaye alijulikana kwa jina la utani ‘Komi Mjeshi,’ mkazi wa Manzese Tip Top, alimuua mkewe Mwanahamisi Paulin ‘Mwana Mjeshi’ kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali na baadaye akajiua kwa kujirusha kwenye reli wakati treni ikiwa kwenye mwendo.

Watu wa karibu na familia yake wanadai kuwa chanzo cha kifo hicho ni mume kuwa na uraibu mkubwa wa kucheza kamari na kubeti kwa kutumia fedha za mshahara aliokuwa akilipwa kwa kazi yake ya ulinzi katika moja ya vituo vya mafuta huko Mabibo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Wanandoa hao waliishi pamoja kwa miaka tisa, na wameacha watoto wawili, Haiman Omary (7) na Abdulaziz Omary (2).

Kabla ya kutengana, walikuwa wakiishi kwenye nyumba ya Kampuni ya kituo kimoja cha mafuta, ambapo mwanamume huyo alikuwa mlinzi. Kwa mujibu wa ndugu na watu wa karibu nao, kutengena kwao kulisababishwa na ugomvi uliotokana na kamari.

Vijana wakiwa nje ya kituo cha kubeti Mwananyamala

Rafiki wa familia hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake aliliambia SAUTI KUBWA kuwa wanandoa hao walikuwa na ugonvi wa muda mrefu ambao ulisababisha wapeane talaka.

“Mwanahamisi alikuwa akilalamika kwa rafiki na ndugu zake kuwa mumewe kila akipata mshahara alikuwa anautumia kucheza kamari na kubeti hadi akawa anashindwa kuhudumia familia.

“Ugomvi kwenye familia hii ulikuwa hauishi. Chanzo ni tabia ya mwanamume kubeti, kucheza kamari na kuvuta bangi hadi kusahau kuhudumia familia hivyo mkewe kufikia hatua ya kuomba talaka.” alisema.

Ashura Mdoe ni mama mkubwa wa Mwanahamisi; alieleza, Wazazi walikwishachoshwa na ugonvi usioisha wa wana ndoa hao. Walikuwa wakisuluhishwa mara kwa mara bila mafanikio.

“Mgogoro wao ulikuwa ni wa muda mrefu. Sisi kama wazazi tulijitahidi kutafuta suluhu lakini tulishindwa. Mwanahamisi alikuwa analalamika kuwa mwenzake anathamini kubeti kuliko familia yake.

“Baada ya suluhu kushindikana watoto wetu hao walipeana talaka na ndipo Mwanahamisi alirudi kwao Ngerengere mkoani Morogoro kabla ya kurejea Dar es Salaam kuendelea na kazi ya ususi.

Mmoja wa marafiki wa marehemu Omary aitwaye Amon Makwega anasema;: “Tulipofika eneo la tukio, walioshuhudia walitwambia kuwa kabla ya kujirusha, alikaa muda mrefu eneo lile (Ubungo Maziwa) na aliweka simu zake pembeni, huku akiwa amechuchumaa na baadaye alijirusha katikati ya behewa la tatu wakati treni ikitembea.

Mwanasaikolojia

Mhadhiri Msaidizi Kitengo cha Saikolojia cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Magolanga Shegembe, amezungumzia kwa undani athari za michezo ya kamari au kubeti kwa jamii.

Aanasema michezo ya kubahatisha ni mambo yenye mtanziko yanapojadiliwa kwa mlengo wa saikolojia kwa kuwa sababu za watu waliojiingiza kwenye michezo hiyo zinatofautiana.

Shegembe ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania, anasema watoto wanaojihusisha na michezo ya kubeti, vijana, wazee, wanawake na wanaume wana sababu  tofauti.

Matangazo ya kubeti katika mazingira ya shule Mwananyamala

Hata hivyo anasema mtoto chini ya miaka 18, kwa namna yoyote ile, hawezi kuhalalishwa kujiingiza kwenye michezo ya kamari kwa sababu umri wao ni wa kutaka kujaribu jaribu vitu hivyo wanahitaji mwongozo wa watu wazima wanaowazunguka.

Uraibu kupindukia

Sheghembe anasema uraibu unaohusiana na michezo ya kubeti ni ile hali isiyokuwa ya kawaida. Mtu ana beti si kwa sababu anafurahia, bali anakuwa na maumivu ambayo anataka kuyatibu.

“Kuna watu ambao wana beti kama sehemu ya burudani, wengine imefikia hatua ya uraibu, yaani kutoka ulevi wa kawaida wa furaha hadi kubeti ili kukwepa maumivu na  kutafuta namna ya kuyatibu.

“Uraibu wa kubeti ni sawa nawa pombe, sigara, dawa za kulevya. Aliyefika kwenye hali hiyo maana yake hawezi kukaa bila kubeti. Asipobeti anajisikia vibaya kwenye akili, mwili na hisia zake. Anabeti ili kuondoa maumivu anayo yapitia.

Sababu kujiingiza kwenye kamari

Mtaalam huyo wa sikolojia ya binadamu anasema; zaidi ya miaka 20 sasa, tafiti mbalimbali kuhusu michezo hiyo zinaonyesha kuna vinasababishi kadhaa ikiwa ni pamoja na marafiki, makundi rika pamoja na mazingira yanayowazunguka wahusika.

Sababu nyingine ni kufurahia, kusisimua sehemu ya ubongo huku wengine wakibeti ili kufurahisha watu wengine, kubungua bongo, hasa kwa mchezo kama karata, pool table, bao, na michezo mingine ya ushindani.

Baadhi ya watu wanabeti kwa lengo la kukabiliana na changamoto za kiuchumi au msongo wa mawazo.

“Wengine wameweka maisha yao kwenye ‘betting’, hawawezi tena kujizuia. Hii inachangia upotevu wa pesa, kuweka rehani uhusiano, familia, urafiki au hata kazi kwa sababu ya kubeti.

Kamari ni ugonjwa gani?

Daktari Saldin Kimangale wa Somedics Poliyclinic Health Centre ya Upanda Dar es Salaam

Anasema “Kwa mujibu wa Kitabu cha muongozo wa utambuzi wa magonjwa ya akili ukurasa wa 358 chini ya kichwa cha Habari “Gambling Disorder”  (Bahati nasibu). Mwenye kujihusisha na kamari anaweza kupata uraibu kwa ile shauku ya kupata zaidi na yale maumivu ya kupoteza.

Kwa kuwa amepata akili inajenga hisia kuwa atapata zaidi na kwa sababu ya kupata anajisikia raha. Anataka kujisikia raha zaidi. Na pale anapopoteza anajisikia maumivu ya kupoteza, hivyo inamjia shauku ya “kulipa kisasi” kwa hivyo anawekeza muda na pesa zaidi.

Tabia hii ikidumu kwa muda mrefu utamuona muhusika akipata huzuni, hasira, kukosa utulivu, kukosa kumakinika kwenye kazi, kukosa usingizi, hamu ya kula nakadhalika.

Muhusika pia anajenga tabia ya kuuza vitu, kudanganya, kuiba, kutapeli, na tabia nyinginezo ili tu apate ufumbuzi wa kwenda kucheza kamari.

Mtu akishapata ugonjwa wa kucheza kamari anakuwa tegemezi, hata pale anapopata madhara kama vile kufukuzwa kazi, kugombana na marafiki, kupoteza familia, kupoteza fedha na muda, bado ataendelea kufanya.

Ugonjwa wa kubeti unatibika?

Dk Kimangale anasema ingawa ugonjwa wa akili unaotokana na kubeti unatibika kama magonjwa mengine, kuna changamoto kadhaa hususan kwa muhusika kukubali kushiriki matibabu kwa sababu ya zile hisia za kupoteza na kutaka kujaribu tena ana tena.

“Mara nyingi tunatumia tiba inayohusiana na mabadiliko ya tabia (Behavioural Change) na uhamasishaji. Katika hatua za mabadiliko ni pamoja na kumwezesha mhanga ajenge utayari wa kuibadili tabia (Contemplation stage). Iwapo anaweza kushiriki matibabu vizuri anaweza kubadili tabia yake na kupona kabisa.

Amewahi kutibu waraibu wa kubeti?

Dk Kimangale anakiri amewahi kutibu wagonjwa wa akili waliotokana na kubeti kupitia wale waliofanikiwa kubadili tabia ingawa kuna walioshindwa kukamilisha matibabu yao, hivyo hawezi kusema kwa sasa wanaendeleaje.

Daktari huyo anasema Tanzania hakuna takwimu za idadi kamili za wagonjwa waliotokana na kubeti kwa sababu  tatizo hilo linafanywa lionekane ni kawaida.

“Michezo ya kamari inaratibiwa na mamlaka za serikali, inatangazwa kwenye vyombo vya habari, imefanywa rahisi sana kufikika, kwa hivyo haionekani kuwa ni tatizo.”anasema Dk Kimangale.

Anasema kwa mtu mmoja mmoja au familia ambao wamekumbana na tatizo la kamari wanaelewa ukubwa wa tatizo na namna linavyotesa familia.

Anaainisha kuwa licha ya kutokuwepo takwimu sahihi za wagonjwa wa akili waliotokana na kubeti; uzoefu wa kimazingira unatuonesha tatizo ni kubwa kwa sababu wanaocheza ni wengi na vyombo vingi vinaendesha mchezo huo.

Viongozi wa dini

Askofu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Tanga, Askofu Steven Munga anasema kamari ni mfumo uliorasimishwa kuwaibia wananchi na kuwafanya mafukara katika uchumi dhaifu wa jamii kama tulionao. Wananchi dhaifu kiuchumi, wananunulika kirahisi na ni rahisi kuwatumia.

 Aidha Imamu wa Msikiti wa Kichangani Magomeni jijini Dar es Salaam, Mursarina Ally Mavere, anasema kamari kwa watoto, vijana hata watu wazima linahitaji nguvu ya pamoja ya Serikali, wazazi, walimu, wadau wa maendeleo kwa sababu ilikofikia  ni pagumu sana.

“Tusipokaa imara tutapoteza kizazi hiki, watoto ambao wanakuzwa na fikra za kamari hawana mwisho mwema”anasema Imamu huyo na kuongeza.

“Tunahitaji nguvu ya pamoja, wazazi, walimu, serikali na viongozi wa dini tukae pamoja tutafakari jambo hili. Kamari ipigwe vita sambamba na kampeni ya uvunjifu wa maadili kwa jamii yetu. Naamini elimu hii ikiambatana na kampeni nyingine zinazopiga vita mmomonyoko wa maadili kwa kwa watoto na vijana wetu inaweza kutusaidia kupunguza kasi hii inayoendelea sasa.

“Kwa mfano sisi kwenye Uislam kamari pamoja na riba ya aina yoyote haikubaliki katika vitabu vyote vinavyozungumzia Uislam na Waislamu tumeonywa kuhusu jambo hili.

Kamari na uchumi

Mmoja wa wachumi waliozungumza na SAUTI KUBWA, Donald Bubelwa, anasema kamari imekuwa kimbilio la vijana wengi ambao kwa namna moja au nyingine wanaitegemea kama chanzo cha kujikwamua kiuchumi.

 “Hali ya ajira ni ngumu duniani, na pia tukubaliane kwamba si kila kijana anaweza ujasiriamali; na wanaoweza pia wanakumbana na vikwazo na changamoto za mitaji n.k. Hali hii husababisha vijana wengi kujiingiza katika wimbi hili.

Mbali na kodi inayokusanywa kupitia leseni na vibali mbalimbali, bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/2024 imeongeza ushuru wa asilimia 20 katika mashine za michezo ya kubahatisha.

Watoto wakiwa kwenye kituo cha kamari

Hasara za kiuchumi

Mbali na faida hizo za jumla, kuna hasara za kiuchumi zitokanazo na kamari. Kwa mujibu wa mchumi huyo, hasara hizo ni pamoja na  kupungua kwa shughuli za uzalishaji mali wa bidhaa viwandani, kupungua kwa uwekezaji na biashara, na hivyo kushusha pato la Taifa (GDP) kwa sababu nguvu kazi yote inakuwa kwenye kamari.

Vyombo vya habari

Kushamiri kwa michezo ya kubahatisha hapa nchini imekuwa ni neema kwa baadhi ya vyombo vya habari Tanzania ambavyo vimenufaika kutokana na matangazo ya kampuni mbalimbali zinazoendesha michezo hiyo.

Huku kila kampuni ikiwa na matangazo yenye kuvutia kama vile “maokoto,” “tatu mzuka,” “mchezo supa,” “bingo,” “tusua mapene,” “daka mkwanja,” vyombo mbalimbali vya habari, vimenufaika kiuchumi.

Mmoja wa mameneja wa Kituo cha runinga maarufu (jina tunalo) anasema matangazo ya michezo ya kubahatisha yamewainua kimapato:

“Sitaki kwenda mbali zaidi kwa kutoa siri za kampuni, lakini matangazo ya bahati nasibu yametusaidia sana.”

Mhariri wa redio inayojulikana kuwa ya burudani zaidi aliiambia SAUTI KUBWA kuwa matangazo ya michezo ya kubahatisha yamekuwa mkombozi katika uendeshaji wa kituo hicho.

“Unajua redio kama hizi zetu ambazo tunaegemea zaidi burudani zina wasikilizaji wengi vijana. Hivyo, hii michezo ya kubahatisha ndiyo mahala pake. Matangazo ya betting yametuongezea ‘maisha.” anasema.

Mhariri mwingine wa gazeti aa kila siku (jina tunalo) anasema matangazo ya kubahatisha yamechagizwa zaidi na udhamini wa vilabu vikubwa vya soka nchini.

Like