Kikwete alijenga umaarufu wake akabomoa wengine – 007

WANASIASA wetu wamekuwa wanatumia vyombo vya habari kujenga umaarufu wao na kubomoa washindani wao. Wanaficha mengi katika vyombo vya habari. Rais Kikwete alionesha umahiri katika kutumia ukaribu wake na vyombo vya habari kusafisha njia yake na kujilinda. Alipata alichotaka, lakini pia, kwa kufanya hivyo, alitengeneza mazingira ya kuingiza vyombo hivyo katika ushabiki wa kisiasa kuliko wakati mwingine wowote wa historia ya nchi yetu.
Mara nyingi, hakufanya hayo kwa mkono wake, bali kwa kutumia wasaidizi wake. Huu ilikuwa mkakati maalumu ambao uliteka wahariri wengi wenye nguvu, nao wakatumbukia kwenye kampeni na propaganda za Kikwete. Baadhi yao walishirikishwa hata mikakati yake ya kisiasa, na wengine walihusishwa katika hatua ya utekelezaji. Wengine walijipa jukumu la kumwandika vizuri kwa kuathiriwa na wimbi la wenzao waliokuwa ndani ya kile ambacho baadaye kilijulikana kama mtandao wa Kikwete.
Baadhi yao walipewa majukumu ya kushawishi wengine ili wote twende na kauli moja juu ya Kikwete. Siku moja, nilimuuliza mhariri mwandamizi aliyetumwa kwangu anishawishi, “umeingia lini katika mambo haya?” Akajibu, “nimekuwa huko siku zote tangu 1994. Tulijaribu mwaka 1995 tukakosa, tukaanza kujipanga upya.”
Haikuwa rahisi kuona habari yoyote mbali juu ya Kikwete. Miongoni mwa wasaidizi wa Kikwete, yupo mmoja ambaye alipewa jukumu la kuhakikisha habari mbaya za Kikwete haziandikwi kwa gharama yoyote; na zikiandikwa hazifiki sokoni. Hadi 2005 mwanzoni, kila chumba cha habari kilikuwa kama kituo kidogo cha kampeni za Kikwete.
Siku moja, nikiwa mhariri wa Tanzania Daima Jumapili, kabla ya wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM kwenda Dodoma kuteua mgombea mmoja katika majina matatu ya Dk. Salim Ahmed Salim, Jakaya Kikwete, na Prof. Mark Mwandosya, kuna jambo lilitokea ofisini kwangu. Enzi hizo tulikuwa tunatumia disketi badala ya flashi kwenye kompyuta.
Mmoja wa waandishi wangu niliokuwa nawatuma kazi ni Saed Kubenea. Akawa amechukua disketi kuhamishia kazi yake kwenye kompyuta yangu. Alipoichomeka, kabla hajahamisha kazi, akastuka kuona folda inaitwa fataki. Akavutiwa kuisoma. Akaifungua. Ndani yake akakuta folda nyingine inaitwa fataki. Akaifungua. Ndani yake akakuta habari imeshaandikwa ikisimulia jinsi mkutano mkuu wa CCM ulivyokata jina la Kikwete, na hatua ambazo Kikwete alikuwa anapanga kuchukua dhidi ya CCM. Akakuta habari ya pili inayosimulia jinsi Kikwete alivyowapiku wenzake na kuteuliwa kwa kura nyingi. Zote hazikuwa za kweli.
Jambo hili lilimstua Kubenea, akaniita na kunionesha habari hizo za matukio ya kutunga (kwa kuwa wajumbe walikuwa hawajaenda Dodoma), ambayo waandishi waandamizi tuliokuwa nao ofisi moja walikuwa wameziandaa kwa ajili ya kujihami kwa lolote ambalo lingeweza kutokea.
Pale pale, Kubenea akahoji: “Hivi huyu na huyu si wamesomea uandishi wa habari na wana diploma? Na ndio wanaandika mambo haya ya kutunga? Basi, kuanzia leo sitawaheshimu. Kama huu ndio uandishi wa habari waliosomea, bora hata wasiousomea kabisa.” Ndivyo tulivyojua kwamba hata ofisini kwetu kulikuwa na waandishi waandamizi, wahariri, waliokuwa wanafanya kampeni za Kikwete.
Baadaye kidogo nilipata jarida moja linaloheshimika kimataifa, liitwalo Africa Confidential, la Uingereza likiwa na habari mbaya juu ya Kikwete. Lilidai kwamba alikuwa amepata pesa kutoka Uarabuni kwa ajili ya kutafutia urais. Lilihusisha rafiki zake kadhaa wa pande zote mbili za Muungano. Wiki hiyo, mhariri wa habari, Manyerere Jackton, alikuwa amepata dharura. Nikamshikia dawati. Baada ya kusoma habari hiyo na kuona umuhimu wake kwa wasomaji wa Tanzania, niliamua kuichapisha katika Tanzania Daima lakini kwa kuipa sura ya Tanzania, na kwa kumtaka Kikwete mwenyewe atoe kauli kuhusu tuhuma hizo.
Nikamwita Kubenea. Nikampa habari niliyokuwa nimetafsiri kwa Kiswahili, akaisoma. Nikamtuma azungumze na Kikwete, amuulize maswali kadhaa. Nikampa namba ya simu ya Kikwete. Nikamwambia atumie simu ya mezani ampigie. Baada ya dakika kama tatu hivi, Kubenea akarudi mezani kwangu akiwa anahema, huku akitabasamu. Nikamhoji, naye akajibu:
“Umempata?”
“Ndiyo!”
“Amesemaje?”
“Amesema tukiandika habari hii anatushitaki. Amenitisha kwa maneno makali.”
“Umeyaandika maneno hayo makali?”
“Ndiyo. Haya hapa.”
“Haya! Andika hicho hicho alichokwambia…”
Nikampa kompyuta aandike alichoelezwa na Kikwete. Ndani ya dakika mbili, ripota mmoja akaniita kwa sauti ya juu, kwamba kuna simu yangu inatoka kwa Kikwete. Nikaelewa ni kwa sababu ya kile alichokuwa ameulizwa na Kubenea. Nikamwagiza Kubenea apokee simu hiyo wazungumze anachonitakia wakati naendelea na kazi nyingine.
Kubenea na Kikwete walizungumza kwa dakika kama tano hivi. Aliporudi mezani kwangu, akawa anatabasamu; nikamuuliza:
“Anasemaje?”
Akajibu: “Kwanza anaomba samahani kwa maneno makali ya awali aliyonitolea. Zamu hii amezungumza kwa upole. Anaomba tusiandike habari hiyo, kwani ni uwongo mtupu unaotungwa na adui zake wa kisiasa akina Dk. Gharib Bilali. Anasema eti wanamchafua kwa sababu za kisiasa. Lakini amesema kwa gazeti linalojiheshimu kama letu hatarajii liandike uzushi huo. Amesisitiza kuwa tukiandika habari hizo atatushitaki…”
Nikamwambia Kubenea, “andika yote hayo uliyonisimulia.” Akaandika, akanirudishia ili niendelee na jukumu la kuhariri. Katika tafsiri ya Kiswahili ya habari ya jarida, nikaongeza kauli ya Kikwete. Ikawa stori kubwa. Wakati naendelea kuihariri, nikapokea simu kutoka kwa mhariri mkuu kupitia simu ya mezani.
Wakati wote huo nilikuwa sijamshirikisha habari hiyo, kwa kuwa tayari tulikuwa tumepunguza kuaminiana katika habari kubwa kubwa, hasa baada ya kugundua kwamba wenzetu wawili walikuwa katika kampeni za Kikwete. Katika habari nyeti kama hizo, tulikuwa tunashirikishana baada ya kazi yote kukamilika, na kuziba mianya ya kuharibu stori. Matoleo ya Jumatatu hadi Jumamosi yalikuwa na habari nyingi za kumjenga Kikwete. Gazeti la Jumapili lilikuwa na habari za uchambuzi wa kisiasa, zikiwamo makala na habari zilizofanya uchambuzi huru na kumkosoa Kikwete.
Mhariri mkuu akahoji: “Nasikia una kigongo leo.” Nikakubali. Kabla sijaanza kumsimulia, akanieleza kuwa mheshimiwa amempigia simu, anaomba stori hiyo isitumike. Binafsi nilidhani mheshimiwa aliyekuwa anazungumzwa ni Freeman Mbowe, ambaye siku hiyo alikuwa nje ya nchi. Nikashangaa amejuaje habari hii, na ana maslahi gani nayo! Nikakumbuka si tabia ya Mbowe kuingilia chombo cha habari. Na alishasema tangu mwanzo, na ndiyo mwenendo wake, kwamba kamwe hataingilia wala hatahusika na habari zozote za gazeti. Nikajiuliza, “ameanza lini tabia hii ya kuingilia kazi ya wahariri?”
Nikamuuliza mhariri mkuu, “kwani amejuaje habari hii, na ana maslahi gani nayo? Na mbona yupo nje ya nchi? Na ameanza lini kuingilia kazi za uhariri?” Ndipo mhariri mkuu akanieleza kuwa mheshimiwa anayezungumzwa hapa ni Kikwete. Hapo nikamhoji mhariri mkuu, “kwani Kikwete ndiye anaamua habari gani itumike, na ipi isitumike? Amekuwa mhariri wetu?” Naye akajibu, “Hapana Ngurumo. Anasema tusiitumie leo, kesho tukamuone kwanza, kuna taarifa za ziada ambazo hajampatia Kubenea.” Nikahoji, “habari gani hizo zisizoweza kupenya kwenye simu? Amezungumza aliyokuwa nayo, tutamtendea haki kwenye stori.” Mhariri mkuu akasisitiza kwamba tuiache, tusije kuonekana kwamba tunatumiwa kufanya “kazi za watu.”
Akakata simu. Baadaye kidogo, akapiga tena na kuniambia kuwa hata Rostam Azizi naye amempigia, na anasisitiza tusiitumie. Baadaye akasema amepigiwa tena na mtu mwingine, Lowassa. Nilivyoona wanahangaika kuizima, nikajua kuna ukweli wanaotafuta kuficha. Lakini kwa msisitizo wa mhariri mkuu, kwamba wameomba mimi na yeye tuwaone kesho yake ili tupewe taarifa za nyongeza, nikaamua kupumzisha stori, ili kuwe na amani ofisini, na nikamweleza kwamba mimi sitakwenda kuwaona. Nikamwomba kama ni kufuata hizo taarifa za nyongeza azifuate yeye.
Kesho yake, mhariri mkuu alikwenda mahali walipokuwa wamekubaliana kukutana, Oysterbay, katika Bwalo la Maofisa wa Polisi. Wakati anaondoka ofisini, nilimtahadhalisha kwamba maelezo yoyote watakayompa apokee, lakini ahakikishe kwamba haui stori yetu. Akakubali.
Kwa kuwa siku hiyo mvua ilinyesha asubuhi, alichelewa kwenda kwenye miadi hiyo. Walikuwa wamekubaliana wakutane nasi saa tatu asubuhi, lakini yeye alifika pale mnamo saa saba alasiri. Aliwakuta wakiwa wanamsubiri tangu saa tatu – Kikwete, Rostam, na Lowassa.
Kwa maelezo ya mhariri mkuu aliporejea, ni kwamba alipowasili tu wakamuona, walifurahi mno, kiasi kwamba mmoja wao alijisahau hata akasema, “afadhali umekuja, maana tulipoona hamtokei tulidhani basi mmeamua kuitumia!” Hilo pekee lilinionesha kuwa walikuwa wanatuita ili kuua stori. Akanieleza pia kwamba walimuuliza, “Ngurumo yupo wapi, mbona hujaja naye?” Yeye akawajibu kuwa nimekataa. Nao wakamweleza kuwa walishahisi kuwa nisingekwenda. Eti mmoja wao akamweleza: “Tunajua Ngurumo ni mtu wa Dk. Salim Ahmed Salim.” Ndivyo walivyohisi. Hilo nalo lilinipa picha kwamba watu hawa hawakuwa wamefanya uchunguzi juu yangu. Nikajua kuwa hawanifahamu vema.
Kilichofuata hapo ni simulizi nyingine ndefu. Lakini hatimaye mhariri mkuu alipewa makaratasi ya faksi, yakionesha kuwa Kikwete alikuwa amefungua shauri katika mahakama ya Uingereza kushitaki jarida hilo na kulitaka limwombe radhi au limlipe fidia ya shilingi milioni 20.
Walimpa makaratasi hayo wakidhani ndiyo ingekuwa habari ya kesho yake, na kumweleza kuwa waliogopa kama ingeandikwa jinsi ilivyokuwa awali, ingeleta hisia kwamba Kikwete anafadhiliwa na magaidi wa Osama bin Laden. Kulikuwepo na ubishi mkali kati yangu na mhariri mkuu juu ya namna ya kuiweka habari hiyo – kama tuzungumzie tuhuma au shauri la mahakamani, Hatimaye, tuliandika habari yetu, tukatenda haki kwa pande zote, tukaingiza kila kitu tulichopata kwa Kikwete tangu jana yake.
Mnamo saa tatu usiku, nilipokea simu kutoka kwa Kubenea akiuliza, “nimeambiwa na Shaban Londa, Meya wa Kinondoni, eti wameua stori yetu, haitoki tena?” Nilimjibu, “hakuna mtu wa kuua stori hiyo. Soma gazeti kesho.” Kesho yake gazeti lilitoka na habari hiyo, lakini magazeti mengine yote yalikuwa na habari ya Kikwete kushitaki jarida – jarida ambalo hata wasomaji walikuwa hawajaliona, wala hawajui limefanya nini. Nilihisi kuna mchezo mbaya ulikuwa umechezwa, na kwamba kama tusingeshtuka, nasi tungetoka na stori ya Kikwete kushitaki jarida!
Baadaye nilipata habari kwamba kuandikwa kwa habari hiyo kulimletea shida mhariri mkuu wangu, kwani akina Kikwete walikuwa wamemuomba isitumike. Hakuweza kuizuia kwa kuwa haikuwa mikononi mwake, na tulishakubaliana tangu awali kwamba hatutaua stori.
Mwaka mmoja baadaye nilikwenda masomoni Uingereza. Kwa muda wote niliokaa kule, nilipeleleza kuhusu shauri hilo. Hakujawahi kuwa na shauri kama hilo mahakamani. Ilikuwa geresha tu ya kutisha wahariri na kuokoa jina la Kikwete kwa kuzima stori mbaya iliyomhusu.
Baadaye, wakati bado anaendelea kutafuta uteuzi ili awe mgombea urais kupitia CCM, waendeshaji wa kampeni zake waliandaa “kura za maoni” kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu. Kura hiyo iliratibiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), chini ya Tido Mhando.
Wapambe na mashabiki wake wakapeana jukumu la kutuma meseji kwa watu wao kwa wingi ili watume meseji wenyewe mara kadhaa kumuunga mkono Kikwete apate kura nyingi zaidi za kufanyia propaganda. Bahati mbaya, baadhi ya meseji za simu walizokuwa wanatumiana zilikwenda hata kwa washindani wao, na wengine wasiohusika kabisa. Na sisi wengine tulizipata.
Baada ya matokeo ya kura hizo za maoni, walidai kwamba hayo yalikuwa matakwa huru na ya haki ya wananchi walio wengi waliopiga kura. Na hawakuishia hapo. Ziliandaliwa bahasha za khaki zikatembezwa kwenye vyombo vya habari, zikilenga wahariri. Waliziita ‘zawadi ya sikukuu kutoka kwa mheshimiwa.’
Hata ofisini kwangu bahasha hizo zilifika. Siku moja alikuja mgeni mmoja wa kike ofisini kwangu akiwa na bahasha. Akajitambulisha kuwa yeye ni mfanyakazi wa ‘mheshimiwa’ na ametumwa aniletee mzigo. Nikaupokea mzigo na kuufungua. Nikakuta katarasi nyeupe yenye maandishi. Ilikuwa ni habari iliyoandikwa na kuhaririwa kikamilifu, kwamba JK amewapiku washindani wake wote katika kura za maoni ya BBC. Iliwekewa hata kichwa cha habari. Kilichohitajika ni kuipachika gazetini jinsi ilivyo.
Nilimshukuru aliyeileta. Tukaagana. Akaondoka. Sikutumia “habari” hiyo ya mwandishi maalumu maana sikutaka kutumia gazeti langu kama bango la njama na kampeni la kundi fulani ndani ya CCM. Lakini matukio haya yalinipa fursa ya kutambua kuwa wenzetu hawa walikuwa wameamua kudhalilisha taaluma yetu, nikaanza kugundua kisa cha Kikwete kuwa kipenzi cha wanahabari kiasi cha kupewa sifa asizokuwa nazo.
Kesho yake, magazeti yote, isipokuwa Tanzania Daima, yalikuwa na habari hiyo hiyo ukurasa wa mbele; ikiwa na kichwa cha habari kile kile, na imeandikwa vile vile – neno kwa neno, sentensi kwa sentensi na aya kwa aya. Ni matokeo ya bahasha ya khaki! Umma ulilishwa uchafu wa propaganda za kampeni za mmoja wa wagombea urais ndani ya CCM.
Kwa hiyo, umaarufu wa Kikwete haukuja tu. Ulijengwa kwa mbinu nyingi, na kwa kutumia vyombo vya habari na watu mwashuhuri. Kwa wanaojua, hii ilikuwa ni sehemu ndogo tu ya mbinu zao nyingi walizotumia kumuuza Kikwete mwaka 2005.
Lakini hawakuishia hapo. Hata alipokuwa rais, aliendelea kutumia vyombo vya habari kujijenga na kujitangaza. Septemba 2009, alifanya igizo jingine, zamu hii kupitia Televisheni ya Taifa (TBC), akitumia watu wale wale aliowatumia walipokuwa BBC, na wengine wa Ikulu.
Walianzisha kipindi (hakikudumu) cha wananchi kuuliza maswali kwa rais moja kwa moja kwenye kipindi cha televisheni. Wengine tuliona kwamba majibu yake katika televisheni si dawa ya matatizo yaliyokuwa yanakabili taifa. Ilikuwa njia ya kuahirisha matatizo na kupoza hasira za wananchi walioona serikali inashindwa kazi yake; na ulikuwa mkakati wa kulainisha wananchi na kumwombea rais kura mwaka 2010.
Walijua kuwa kinachokosekana serikalini si ujuzi wa rais kuhusu matatizo ya wananchi, bali dhamira ya kutekeleza majukumu yake bila woga wala upendeleo. Kama rais angekuwa mtu wa vitendo, asingehitaji kujitokeza kwenye televisheni kuonyesha umahiri wake wa kukwepa maswali au kuficha majibu, huku akitetea udhaifu wake wa ziada hadharani.
Na hata pale alipokuwa anatoa majibu yasiyoridhisha, mwongoza kipindi, Tido Mhando, angeweza (na alipaswa) kumrudisha katika mstari na kumtaka rais atoe majibu makini, ya kina yanayolenga moja kwa moja maswali anayoulizwa – swali linalohusu Kigoma lisijibiwe kwa maelezo ya Lindi!
Lakini Tido tuliyemjua kwa maswali makini, magumu na yenye king’ang’anizi akiwa BBC, si huyu aliyekuwa mwenyeji na mwongozaji wa kipindi cha Kikwete. Alikuwa mnyonge kwa sababu alishajeruhiwa tangu miaka mingi iliyopita.
Ndiyo maana alishindwa kujizuia kumsifu Rais Kikwete kwa sekondari za kata, ambazo baadaye Kikwete mwenyewe ‘alizikandia’ akijua hisia halisi za wananchi kuhusu hadhi ya shule hizo ambazo serikali yake na chama chake wanajivunia katika orodha ya “mafanikio ya Kikwete!”
Katika uchambuzi wangu wiki iliyofuata, niliandika hivi: “Kipindi kimeisha, lakini wananchi makini bado wanauliza: Je, kipindi hiki kilimjenga au kilimbomoa Kikwete? Kwa viwango gani? Je, waandaaji waliweza kuepuka kishawishi cha kuandaa na kupandikiza waulizaji (kama ilivyo kawaida yao na) kama walivyofanya kwenye kura za maoni ya BBC mwaka 2005?
Je, maswali yaliulizwa pale pale au teknolojia ilitumika kuyarekodi kabla na kuyacheza katika kipindi kama vile yanaulizwa moja kwa moja? Na baada ya kumsikiliza rais, wananchi wameridhika kwamba ana majibu ya maswali yao, na ana nia na uwezo wa kuyaweka majibu yake katika vitendo? Na kwa kuwa maswali yote yaliyoulizwa hayakuwa mapya, rais alikuja na kipya gani kwenye televisheni? Au alionyesha kipya gani katika majibu yake – ambacho viongozi wengine wa CCM hawajawahi kusema?
Na katika suala la mafisadi papa, hasa baada ya yeye kukiri kwamba ‘ni wanjanja hawakamatiki’, rais aliondoka kwenye televisheni akiwa na sura ya mpambanaji shujaa au majeruhi mteteaji wa mafisadi au kiongozi asiyejali uzito wa kauli zake na athari zake kwa umma? Na kama anajitapa kwamba ameshughulikia mafisadi, huku wananchi wakiendelea kumkomalia kwa maswali ya ziada (au yale yale), inampa tafsiri gani ya maoni na imani ya wananchi juu ya utendaji wake? Inaonyesha wameridhika na majibu yake au wanamuona kama kiongozi, mtetezi na msemaji wa mafisadi?
Anadhani mbinu hii mpya ya kutangaza udhaifu wake kwenye televisheni itakomesha maswali ya wananchi? Na anadhani maswali yataisha kwa sababu ya kuulizwa sana au kwa sababu ya kujibiwa vizuri? Au anadhani ufumbuzi wa shida ya wananchi ni majibu yake kwenye televisheni si hatua kali za kiuongozi? Kama rais anachukua jukumu la kuwa ‘katibu mwenezi’ wa serikali, wasaidizi wake (hasa wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na Idara ya Habari MAELEZO) watafanya nini? Na yeye atatekeleza lini majukumu yake kama rais mtendaji? Na iwapo majibu ya rais hayataridhisha, ni nani atakuwa amebaki atakayeweza kuwaridhisha wananchi kwa majibu makini?”
Novemba 4, 2016, Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilialika wahariri iliowataka katika mahojiano maalumu na Rais John Magufuli kuhusu mwaka wake mmoja Ikulu. Sikualikwa. Nilifuatilia tukio zima kupitia luninga nikiwa mjini Dodoma. Baada ya kusikia maswali yao na majibu ya rais, hasa baada ya kukosa maswali ya nyongeza kwa maswali ambayo rais aliyajibu vibaya au aliyakwepa, niliamini mbinu za watawala wetu ni zile zile, na mchezo ni ule ule. Niligundua kwamba vyombo vya habari navyo bado vinahitaji kukombolewa kama tunataka kuleta mabadiliko ya msingi. Na baadhi ya wahariri bado wananywea mbele ya rais. Badala ya kumuuliza maswali magumu, wanabaki kuchekacheka, wanamwachia anateleza kama kambale! Anawatoroka. Wanakosa stori.

ITAENDELEA…

Like
13

Leave a Comment

Your email address will not be published.